Waislamu
 sote tunakiri na kutamka kwa ndimi zetu kwamba Muhammad (Swalla Allaahu
 ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mtume wa mwisho, naye ni mbora wa 
viumbe, mwenye tabia bora za kupigiwa mfano na sisi tunawajibika 
kuzifanyia kazi.
	Hata 
hivyo, juu ya hikmah zake, cheo na daraja alichonacho, hatustahiki hata 
kidogo kumuomba Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa 
sallam) katika lolote tunalohitajia kuliomba. Wala hatuwajibiki kuamini 
kwamba du’aa isiyopita transit
 kwake, haikubaliwi. Hilo sio sahihi katu, kwani Muhammad (Swalla 
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa malaaikah wala jamii 
isiyokuwa yetu sisi. Ni mwenzetu, mwenye maumbile sawa na sisi, 
kilichobadilika kutoka kwake ni kupokea wahyi tu.
	Mola wetu, Anasema kwamba tumuombe Yeye, kwani Ndiye Anayezisikia du’aa zetu na malalamiko yetu:
	{{Na
 waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi Nipo 
karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie 
Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.)) [Al-Baqarah:186]
	Pia Amesema:
	{{Na Mola wenu Anasema: Niombeni nitakuitikieni.}} [Suratul-Ghaafir: 60]
	Kwa 
upande wake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema 
kwamba tusimtukuze kama walivyomtukuza Manasara kwa Nabii ‘Iysaa hadi 
kumpa daraja na cheo sawa cha Uungu:
	((Msinitukuze
 (kwa kunipandisha cheo kama cha Allaah) kama walivyomtukuza Manasara 
‘Iysaa mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja, kwa hiyo semeni mja wa 
Allaah na Mjumbe Wake.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
	Wala 
hawa Manasara hawakuishia hapo, nao pia wakajitukuza na kujipachika vyeo
 vya Unabii na Utume, na kujidai kuweza kuombwa na wanaadamu wenzao 
pamoja na kusamehe madhambi. Hayo kwetu yatabakia ni uzushi mkubwa na ni
 shirki iliyo wazi.
	Kwa 
hapa, tunaomba tuzingatie kwamba du’aa yoyote inatakiwa kuelekezwa moja 
kwa moja, kiroho na kimatamshi kwake Muumba wala sio kwa Mtume. Tunaona 
ndani ya jamii zetu za Kiswahili, mtu anapojitoka, anapotokewa na tatizo
 la ghafla au mfano wa hayo; basi kauli ya mwanzo linalomjia mdomoni ni 
la kishirikina: Mtume! na mfano wa hayo.
	Ewe 
ndugu yangu Muislamu, umesahau ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi 
wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti. Naye Mtume (Swalla Allaahu 
‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti, asiyeweza hata kusikia 
maombi yetu, seuze kuweza kutuombea kwa Mola. Sasa iweje leo neno lako 
la mwanzo unapotokezewa na shida liwe Mtume!?
	Na 
wengine wapo waliochupa mipaka, wakawapatia vyeo wanaowaita masharifu, 
mashekhe, mamufti, maqadhi, mawalii na kadhalika, wakawatumia 
kuzipitisha du’aa zao kwao. Ni ushirikina na uzushi ulioje. Utakuta 
kwenye du’aa zao wakisema: Kwa kuhudhuria Sayyiduna Muhammad, mawlaana, sharful-anbiyaa, wa shuyukhina, al-faatihah!
 Ujahili ulioje huu, Mola wetu yupo karibu kuliko mapigo ya mioyo yetu, 
ya nini kupata taabu kuzipitisha du’aa kupitia kwa viumbe vinavyotegemea
 rahmah zake?
	Tunamalizia
 kwa kuzinasihi nyoyo zetu na za Waislamu wote, kuachana na aina hii ya 
shirki, kwani tutakuwa tunamuomba kiumbe badala ya kumuomba Muumba.
 
	
 
1 comment:
1- A.alykum mimi nauliza kuhusu tawasul sheikh
2- Allah ameahidi kulitukuza jina la Mtume SAW hadi kuwekwa kuwa swala bila kumswalia Mtume haikubaliki. Pia inasemekana dua unapoianza na kumswalia Mtume SAW ni maqbul.
Hili unasemaje sheikh
Post a Comment