Abdullah ibn Abbas (r.a.) amesema kuwa baada ya kumaliza Hajj ya mwisho (mwaka
wa 10 Hijriyyah), Mtume Mtukufu s.a.w.w. alisimama mbele ya mlango wa Ka'aba
Tukufu, akiwa ameshikilia komeo ya mlango, huku akiwauliza ma-Sahaba wake:
"Je, nikuambieni dalili za siku ya QIYAMA?" Salman Farsi (r.a.)
ambaye alikuwa karibu naye, alisema:"Ndiyo, Ewe Mtume wa Allah swt."
Mtume Mtukufu s.a.w.w. akasema, "Hakika,miongoni mwa dalili za saa, ni kuwa
(1) watu watapuuza sala, (2) watafuata matamanio yao wenyewe (3) wataelekeza
kujipendelea wao wenyewe, watawaheshimu matajiri, (4) na watauza Dini yao
kwa manufaa ya kidunia (5) wakati huo roho na moyo wa Muumin itayayuka (kwa
huzuni) kama chumvi inavyoyayuka katika maji, kwa sababu ataona mambo
yaliyoharamishwa na hataweza kuyabadili."
Salman akasema: "Haya yatatokea, ewe Mtume wa Allah swt?"
Mtume Mtukufu s.a.w.w. akasema: "Ndiyo, naapa kwa Aliyonayo roho yangu mkononi
mwake."
"Ewe Salman, (6) wakati huo watawala watakuwa wadhalimu (7) Mawaziri watakuwa
waasi, (8) na wadhamini (wale waliopewa amana kwa kuaminiwa) watafanya hiana,
(9) hakika wakati huo maovu yatakuwa mema na mema yatakuwa maovu, (10) wale
wafanyao hiana wataaminiwa na waaminifu watafikiriwa kuwa si waaminifu;na
mwongo atasadikiwa,na msema kweli atahesabiwa mwongo. (11) Wakati huo kutakuwapo
na utawala wa wanawake, (12) Masuria watashauriwa, (13) na watoto watakaa
juu ya mimbar, (14) udanganyifu utahesabiwa kuwa ni uerevu (15) na Zaka itakuwa
ni kama kutozwa faini;na mateka ya vita (yaani mali ya ummah) yatakuwa kama
ni mali ya mtu binafsi; na mtu atakuwa mjeuri kwa wazazi wake na atakuwa
mwema kwa marafiki zake, (16) na wakati huo kutatokea na nyota zenye mikia
(comets)."
Salman akasema: "Haya yatatokea, ewe Mtume wa Allah swt?"
Mtume Mtukufu s.a.w.w. akasema: "Ndiyo, naapa kwa Aliyonayo roho yangu mkononi
mwake."
"Ewe Salman! (17) wakati huo mwanamke atakuwa mshiriki wa mumewe katika biashara,
(18) na mvua itakuwa moto sana (19) na watu wema watabaki katika huzuni;
na masikini hawata heshimiwa; na wakati huo masoko yatakaribiana, (20) Tena
huyu atasema,"Mimi sikuuza chochote, na yule atasema, "Mimi sikupata faida
yoyote." Kwa hivyo hutamkuta mtu yeyote asiyemlalamikia Allah swt.
"Ewe Salman! (21) tena itatokea iwapo watu watawazungumzia watawala wao,
watawaua, na ikiwa watanyamaza kimya, watanyang'anywa mali yao, watanyimwa
heshima zao, watamwaga damu yao na mioyo ya watu itajaa woga;kisha hutamwona
mtu yeyote ila atakuwa mwoga,mwenye khofu, ametishika na ameshstushwa"
"Ewe Salman! (22) Bila shaka wakati huo mambo fulani yataletwa kutoka Mashariki
(23) na mambo fulani yataletwa kutoka Magharibi, (24) Basi ole kwa watu walio
dhaifu (wa imani) katika Ummah wangu kutokana na hayo; Ole ya Allah swt iwe
kwa hayo. Wao hawatakuwa na huruma juu ya wadogo wao, wala hawatamsamehe
yeyote aliyefanya kosa. Miili yao itakuwa ya wanadamu, lakini mioyo yao itakuwa
ya mashetani."
"Ewe Salman! (25) Wakati huo wanaume watawaashiki wanaume, (26) na wanawake
watawaashiki wanawake; (27) na watoto wa kiume watapambwa kama wanawake;
(28) na wanaume watajifanya kama wanawake(29) na wanawake wataonekana kama
wanaume; (30) na wanawake watapanda mipando (31) Hapo tena patakuwepo laana
ya Allah swt juu ya wanawake wa Ummah wangu."
"Ewe Salman! (32) Bila shaka wakati huo Misikiti itapambwa (kwa dhahabu n.k.)
kama inavyofanywa katika masinagogi na makanissa, (33) na Quran zitapambwa
(kwa nakshi na rangi za kupendeza n.k.) (34) na minara (ya misikiti) itakuwa
mirefu; na safu za watu wanaosimama katika sala zitazidi, lakini nyoyo zao
zitachukiana na maneno yao yatatofautiana."
"Ewe Salman! (35) Wakati huo wanaume watatumia mapambo ya dhahabu; kisha
watavaa hariri,na watatumia ngozi za chui."
"Ewe Salman! (36) Wakati huo riba itakuwako, (37) na watu wata-fanyia biashara
kwa kusemana na rushwa (38) na dini itawekwa chini, na dunia itanyanyuliwa
juu."
"Ewe Salman! (39) Wakati huo talaqa zitazidi (40) na mipaka ya Allah swt
hayatasimamishwa (41) Lakini hayo hayatamdhuru Allah swt."
"Ewe Salman! (42) Wakati huo watatokea wanawake waimbaji, (43) na ala za
muziki (44) na wabaya kabisa watawatawala Ummah wangu."
"Ewe Salman! (45) Wakati huo matajiri katika Ummah wangu watakwenda Kuhiji
kwa matembezi, na walio wastani kwa biashara, na masikini kwa kujionyesha.
(46) Hivyo basi wakati huo watakuwapo watu ambao watajifundisha Quran si
kwa ajili ya Allah swt na wataifanya Quran kama ala ya muziki. (47) Na watakuwapo
watu ambao watasoma dini si kwa ajili ya Allah swt (48) na idadi ya wanaharamu
itazidi (49) watu wataiimba Quran, (50) na watu watavamiana kwa uroho wa
kidunia."
"Ewe Salman! (51) Haya yatatokea wakati heshima zitakapo- ondoka,na madhambi
yatatendwa (52) na watu waovu watakuwa na uwezo juu ya watu wema, (53) na
uongo utaenea na mabishano (matusi) yatatokea (54) na umasikini utaenea,
(55) na watu watajiona kwa mavazi yao (56) na itakuwepo mvua wakati si wake
(57) na watu watacheza dama, kamari na Ala za muziki, (58) na hawatapenda
kuhimizana mema wala kukatazana maovu (59) na kwa ajili hali itakavyokuwa
hata itafikia wakati huo kuwa Muumin atakuwa na heshima ndogo kuliko hata
mjakazi (60) na wanaosoma na wanaotumia wakati wao katika kumwabudu Allah
swt watalaumiana. (61) Hao ndio watu watakaoitwa wachafu na wanajisi katika
Ufalme wa mbinguni."
"Ewe Salman! (62) Wakati huo matajiri hawataogopa chochote isipokuwa mtu
masikini; hadi kwamba masikini wataendelea kuomba kati ya ijumaa mbili, na
hawatamwona mtu yeyote wa kutia chochote mikononi mwao."
"Ewe Salman! (63) Wakati huo itazungumzwa Ruwaibidhah."
Salman akauliza: "Ni nini Ruwaibidhah ? Ewe Mtume wa Allah swt, baba na mama
yangu wawe fidia kwako."
Mtukufu Mtume s.a.w.w. akajibu: (64) "Watu fulani watazungumza kuhusu mambo
ya watu ambayo hayakuwahi kuzungumzwa namna hii zamani. (65) Tena baada ya
muda mchache machafuko yatatokea duniani, na kila nchi itafikiri kuwa machafuko
yapo katika nchi yao tu."
(66) "Watabaki katika hali hiyo kwa muda ambao Allah swt atapenda wabaki;
(67) kisha ardhi itatapika vipande vya moyo wake dhahabu, fedha na madini
mengineyo; (Hapo Mtume s.a.w.w.) alinyosha kidole chake penye nguzo, na
akasema:"Kama hizi (kwa ukubwa), lakini siku hiyo dhahabu wala fedha
hazitamsaidia mtu yeyote. Na hii ndiyo maana ya maneno ya Allah swt
'Hakika dalili Zake zimekuja.'
Zipo habari zingine zilizoelezwa katika vitabu vinginevyo kwa kupitia Jabir
Ibn Abdullah Ansari, ambavyo ninazitaja:
"Ewe Salman! Wakati huo (1) Wazee watajitumbukiza katika mambo ya ushirikina
na uchawi, (2) ghiba ndiyo itakuwa mazungumzo yenye kupendeza, (3) mali
iliyopatikana kwa njia za haramu, itachukuliwa kama ndiyo neema, (4) wazee
hawatakuwa na mapenzi ya wadogo na vile vile wadogo hawatawajali wazee na
kuwaheshimu (5) Islam itabakia kwa jina tu kwani wafuasi wake hawatakuwa
wakifuata maadili na maamrisho yake, (6) Kimbunga kikubwa cha rangi nyekundu
kitatokezea mbinguni na kutaanguka mawe kutoka mbinguni (7) nyuso zitakuwa
za kuchukiza (8) kutakuwa na mitetemeko na kuporomoka kwa ardhi kila mara.
Hapo Sahaba walimwuliza Mtume s.a.w.w., "Ewe Mtume wa Allah swt, je lini
yatakapotokea hayo yote?" (pamoja na nishani na dalili za hapo juu, baadhi
zimeongezeka hapa chini)
Mtume s.a.w.w. aliwajibu: (1) "Watu watakuwa watumwa wa shahwa au matamanio
yao, (2) watu watakuwa walevi wa kupindukia kwani matumizi ya ulevi utakithiri
na utakuwa ukipatikana kwa udhahiri bila ya watu kuona aibu ya aina yoyote,
(3) Wanaume watakuwa wakiwatii wake zao, (4) jirani atakuwa wakiwaudhi na
kuwatesa majirani wenzake, (5) Wakubwa hawatakuwa watu wenye huruma, mioyo
yao itakuwa imejaa kwa maonevu, (6) vijana hawatakuwa na heshima (7) watu
watajenga majumba imara na marefu mno, (8) wafanyakazi watadhulumiwa haki
zao, (9) ushahidi wa kiuongo utachukuliwa kuwa wa kawaida, (10) ndugu atakuwa
akimwonea wivu ndugu yake halisi (11)watu watakaokuwa wakifanya biashara
kwa ushirika, basi watakuwa daima wakifikiriana mbinu za kumdhulumu mwenzake,
(12) mambo ya zinaa yatakuwa kama kawaida kwani yatatendeka na kusikika pia.(13)
ile mioyo ya kutaka kusaidia watu wengine itakuwa imetoweka, (14) Maasi na
dhuluma itaongezeka kupita kiasi, (15) matumbo ya watu itachukuliwa kuwa
ndiyo miungu yao,kwani hawatajali kiwevyo, ilimradi wapate chochote kile,
(16) wanawake watakuwa wakitawala akili za wanaume na watakuwa wakiwaendesha
wanaume vile watakavyo wao, (17) kutatokea Maulamaa au wanazuoni waovu kabisa
kwani watajionyesha kuwa ni wacha Mungu na wenye ilimu, ambapo kwa hakika
watakuwa waroho wa mali ya dunia tu."
Hapo Mtume Mtukufu s.a.w.w.liwaonya: "Kumbukeni,wakati kama huo utakapokuja,
basi Allah swt atatumbukiza watu katika balaa za aina nne, (1) kutawaliwa
na watawala dhalimu (2) ukame na vitu vya matumizi ya kila siku kuwa bei
ghali yaani kupanda kwa maisha, (3) dhuluma za watawala (4) kuabudu miungu."
Sahaba waliposikia hayo walishtushwa na kuuliza: "Ewe Mtume wa Allah swt!
Je kweli kuwa Mwislamu atakuwa akiabudu miungu na masanamu?"
Mtume s.a.w.w. aliwajibu: "Naam! Kwao mapesa yatakuwa kama miungu kwani watakuwa
wakiziabudu kupindukia kiasi."
Kwa hakika sisi tunayashuhudia haya yote yakitokea ambayo Mtume s.a.w.w.
amekwisha bashiri karibu karne kumi na nne zilizokwishapita. Imam Ali a.s.
katika khutba yake ijulikanayo kama Al-Bayan anaelezea ubashiri kwa undani
zaidi. Wasomaji wenye kutaka kupata habari zaidi wanaweza kutazama (1)
Yanabi-ul-Muwaddah (2) Basharat-ul-Islam, Sayyid Mustafa Ali-Sayyid
Haider al-Kazami, chapa ya Baghdad.
.
A / Alaikum brother Muslim men and women either after greetings are you ignorant of blogs this is Islam referencing everything apply Islam and Muslims problems all questions feedback analysis of various topics and highlights from our religion of Islam but God is the one most skillful Insha'llah to comment questions do not hesitate to write abdulmohamedy23@gmail.com or +255762084268 inshallah
No comments:
Post a Comment