Wednesday, 24 December 2014

mambo atakayoulizwa mja siku ya qiyama

Mambo manne utayoulizwa siku ya Qiyama

Yawmul QiyaamahKutoka kwa Abu Barzah Al-Aslamiyy ambaye amesema: Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Nyayo za mja hazitoondoka [Siku ya Qiyaamah] mpaka aulizwe juu ya umri wake alivyoumaliza, elimu yake alivyoifanyia, mali yake ameichuma kutoka wapi na ameitumia kwa mambo gani, na mwili wake aliutumia kwa kazi gani)).
  Mafunzo Na Hidaaya:
  1. Hima ya Muislamu kutumia umri wake katika yale yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى).
  1. Mambo manne hayo ni miongoni mwa neema nyingi za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa mja, anapaswa kushukuru kwa yakini, kauli na vitendo, na ataulizwa kuhusu neema hizo.
ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴿٨﴾
Kisha bila shaka mtaulizwa siku hiyo kuhusu (kila) neema (mmezitumiaje duniani?)
  1. Kuwa na ikhlaasw katika ‘amali azitendazo Muislamu. [Al-Kahf 18: 110].
  1. Himizo la kuchuma mali kutoka njia za halali na kuitumia katika yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى) pamoja na kuitolea Zakaah na sadaka na tahadharisho la chumo la haramu. [Al-Baqarah 2: 168, Twaahaa 20: 81].
  1. Kuuhifadhi mwili usitende yaliyo haramu na kuutiisha pamoja na kuutumikia katika utiifu wa Allaah (سبحانه وتعالى), na kufanya ‘Ibaadah kwa wingi.
  1. Kujifunza elimu iliyo na manufaa na aifanyie kazi kwa ikhlaasw anufaike nayo na anufaishe wengineo.
  1. Mambo manne hayo ni majukumu ya kila mtu Siku ya Qiyaamah. Hakuna atakayeondoka mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) bila kuulizwa.
  1. Hadiyth hii ni tahadharisho la kujirekebisha kwa mtu anayekwenda kinyume na yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى) duniani.
  1. Uhai na maisha ya dunia ni kama madrasa anayosoma mtu na kufanya juhudi, kisha mtihani wake na malipo ni Siku ya Qiyaamah. Atakayefanya kinyume chake, atapata khasara Aakhirah kwenye maisha ya milele [Ash-Shuwraa 42: 20].
مَّن كَانَ يُرِيدُ الْعَاجِلَةَ عَجَّلْنَا لَهُ فِيهَا مَا نَشَاءُ لِمَن نُّرِيدُ ثُمَّ جَعَلْنَا لَهُ جَهَنَّمَ يَصْلَاهَا مَذْمُومًا مَّدْحُورًا ﴿١٨﴾ وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾ كُلًّا نُّمِدُّ هَـٰؤُلَاءِ وَهَـٰؤُلَاءِ مِنْ عَطَاءِ رَبِّكَ ۚ وَمَا كَانَ عَطَاءُ رَبِّكَ مَحْظُورًا ﴿٢٠
Anayetaka ‘aajilah (starehe za kupita kwa haraka za dunia) Tunamharakizia humo Tuyatakayo, na kwa Tumtakaye. Kisha Tutamjaalia (Moto wa) Jahannam auingie (na) kuungua hali ya kuwa mwenye kushutumiwa na kufukuziliwa mbali (kuwekwa mbali na Rahmah ya Allaah). . Na anayetaka Aakhirah na akaifanyia juhudi inayostahiki kufanyiwa, naye ni Muumin, basi hao juhudi zao ni za kushukuriwa (na kulipwa thawabu na Allaah). Wote (wanaotaka dunia na Aakhirah) Tunawakunjulia – hawa na hawa- katika neema za Mola wako. Na hazikuwa neema za Mola wako zenye kuzuiliwa (zisimfike Amtakaye Allaah)
  1.  Umuhimu wa kufanya kazi, na mtu achunge sana kazi atakayofanya, kwa sababu chumo la haramu litampeleka mtu pabaya.
  1.  Muislamu anatakiwa na shari’ah achume chumo la halali na alitumie kwa njia za halali.
  1.  Katika riwaya nyengine ya at-Tirmidhiy badala ya mwili inataja ujana umetumiwa vipi kumaanisha kuwa kipindi hicho ni muhimu sana katika maisha ya mwanaadamu na ni wakati wa kuchuma mema mengi.
Kwa hisani ya Alhidaayah

No comments: