Alichokifanya
Nyerere baada ya uhuru
Kilichofuata baada ya kupatikana uhuru ilikuwa
ni kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kuhamishwa kwa masheikh na Waislamu
wengine waliodhaniwa kuwa wanapinga utawala wa Nyerere.
Mashuhuri miongoni mwao walikuwa: Abdillah Schneider
Plantan, Sheikh Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi
Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sharff Hussein Badawiy,
Shariff Mwinyibaba na Shariff Adnan
Wengine ni Bilali Rehani Waikela, Sheikh Jumanne
Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh Hashim Haji Abdallah, Sheikh
Nurdin Hussein, Salum Abdallah Popo, Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al
Amin Maftah, Rajab Kiguu cha Mbuzi na wengine wengi.
Lakini ukweli ulikuwa kwamba si wote katika wale
waliokamatwa na kuwekwa kizuizini walijihusisha na siasa. Baadhi yao walikamatwa
kwa sababu tu walikuwa wakishirikiana na wale waliodhaniwa ni wapinzani
wa Nyerere.
Maalim Matar na Shariff Adnan walifungwa jela
kwa sababu tu walihusika na msikiti wa Badawiy mjini Dar es Salaam ambako
Sheikh Hassan bin Amir, wakati huo akichukuliwa kuwa ndiyo roho ya waumini
wa Tanganyika, alikuwa ikiendesha madrasa yake kila magharibi pale msikitini.
Shariff Hussein na nduguye Mwinyibaba walihamishiwa
Kenya, walikotoka si kwa sababu walikuwa wamejishughulisha katika harakati
za kuipinga serikali, ila lakini kwa sababu walikuwa waangalizi wa msikiti
wa Badawiy.
Sheikh Mzee Ali Comorian alitiwa kizuizini kwa
sababu kila mara alikuwa akifuatana na Sheikh Hassan bin Amir kama vile
alikuwa kivuli cha sheikh. Huenda kile kilichomfanya Nyerere kuwatia kizuizini
masheikh na wengine kuhamishwa ni kufuata ule msemo wa Biblia usemao, 'yule
ambae hayuko nasi basi ni dhidi yetu'.
Jinsi siasa na za Tanzania zilivyobadilika na
jinsi Nyerere alivyoanza kuonesha uadui dhidi ya Waislamu kulimsikitisha
sana Abdulwahid. Alishindwa kuelewa uhasama huu ulikuwa unatoka wapi. Alihisi
kuwa anahusika na yale yaliyokuwa yanawapata Waislamu. Mawazo haya yalimzonga
kama jinamizi. Kwa ufahamu wake alikuwa akidhani matatizo yote ya udini
walikuwa wameyashinda toka miaka ya 1950. Mwaka 1953 Abdulwahid akiwa Muislamu
na akiungwa mkono na Al Jamiatul Islamiyya aligombea kiti cha urais wa
TAA na Nyerere, Mkatoliki.
Abdulwahid alishindwa uchaguzi ule. Waislamu hawakuuchukulia
uchaguzi ule kama uchaguzi kati ya Muislamu na Mkristo. Kilichotazamwa
ni uwezo wa wagombea.
Nyerere alikuwa amemzidi Abdulwahid na kwa ajili
hii alichaguliwa kuiongoza TAA. Abdulwahid alikumbuka ugomvi wa Sheikh
Suleiman Takadir wakati ule Mwenyekiti wa Baraza La Wazee wa TANU. Sheikh
Takadir aliwaonya Waislamu wachukue tahadhari kwani Nyerere atakuja kuwapendelea
Wakristo wenzake pale atakaposhika madaraka. Kama walivyofanya Waislamu
wengi, Abdulwahid alimuunga mkono Nyerere na kumpinga Sheikh Takadir.
Wakati ule Abdulwahid aliamini kama Waislamu wengi
walivyoamini kuwa Sheikh Takadir alikuwa anataka kuleta siasa za kibaguzi
ambazo alikuwa anaziegemeza katika dini. Abdulwahid aliona udini aliokuwa
anataka kuuleta Sheikh Takadir lilikuwa jambo ambalo lingeiletea hatari
Tanganyika.
Abdulwahid alikufa mwaka 1968 wakati nchi ikiwa
imegubikwa na hasama za chinichini kati ya Waislam dhidi ya serikali ya
Nyerere ambae sasa alikuwa amehodhi madaraka yote katika serikali.
Umoja wa kitaifa, moja ya maadili ambayo yeye(Abdulwahid
) aliyapigania katika maisha yake yote katika siasa ulikuwa unahatarishwa.
Halikadhalika umoja wa Waislamu ulikuwa unaelekea kuvunjika. Kulikuwepo
na kuwekwa kizuizini kwa masheikh chini ya Preventive Dentation Act
of 1962.
Baadhi ya masheikh waliotiwa gerezani walikuwa
watu waliomuunga yeye mwenyewe mkono wakati anaunda TANU. Baadhi yao aliwashawishi
kumuunga mkono Nyerere na TANU katika kile kipindi kigumu cha harakati
za kudai uhuru. Mwanakamati wa Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA, Mufti Sheikh
Hassan bin Amir, kiongozi wa ngazi ya juu kabisa kwa Waislamu alikuwa amekamatwa
na kuondolewa nchini na kurudishwa kwao Zanzibar kwa amri ya Nyerere. Sababu
iliyotolewa ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan bin Amir ilikuwa alikuwa ati
'akipanga njama ya kupindua serikali'.
Sheikh Hassan bin Amir alikuwa kati ya Waislamu
wachache ambao walithubutu kusimama kidete dhidi ya serikali na kutoa mawazo
yake kuhusu jinsi serikali ilivyokuwa ikiwakandamiza Waislam. Kabla hajafa
Abdulwahid alikuwa akifikiwa na habari kuwa Nyerere alikuwa alikuwa akiendesha
kampeni makini sana ndani ya chama kuwafuta Waislamu ndani ya TANU.
Abdulwahid alikuwa anafahamu matokeo ya kuvunjika
kwa umoja wa Waislam. Yeye alikuwa anajua vyema nguvu ya umoja wa Waislamu
wakati walipokuwa wanapigania uhuru wa Tanganyika.
Abdulwahid halikadhalika alikuwa anafahamu nguvu
ya wale waliokuwa nyuma na njama zile za kuwagawa Waislamu katika makundi
hasimu. Vilevile alikuwa anatambua hofu na watu wote waliokuwa nyuma ya
njama zile.
Alifahamu kuwa wale aliowapokea na kuwatia katika
harakati za kudai uhuru sasa walikua na hofu na Uislam. Kama Uislamu ulitumika
kuwaondoa wakoloni Uislam hautashindwa kuwatoa wao madarakani. Uislam ikiwa
itkadi ya kupinga ukoloni sasa ilikuwa ni tishio kwa Ukristo katika Tanzania
huru.
Kabla hajafariki dunia Abdulwahid alifanya mazungumzo
na Nyerere. Mazungumzo haya baina ya Abdulwahid na Nyerere yalifanyika
katika miezi ya mwisho ya mwaka 1968 wakati mashekhe na Waislamu mashuhuri
wanasombwa na kutupwa gerezani. Abdulwahid na Nyerere walikuwa wametoka
mbali. Watu hawa walikuwa marafiki wa zamani. Huenda kama isingelikuwa
kwa msaada wa Abdulwahid historia ya TANU na ya Nyerere mwenyewe zingechukua
mkondo tofauti.
Mazungumzo haya yalikuwa muhimu kwa Abdulwahid
kwa sababu kwa kiasi fulani alihisi anahusika na yale yaliyokuwa yakiwasibu
Waislamu, wale kutoka Dar es Salaam. Taarifa za Waislamu kukamatwa usiku
na kuwekwa kizuizini zilikuwa zikimfikia karibu kila siku. Abdulwahid hakuweza
kujifanya kuwa haathiriki na matokeo yale. Baadhi ya watu ambao Nyerere
alikuwa anawatupa gerezani walikuwa watu ambao yeye Abdulwahid binafsi
walimuunga mkono wakati anaanza siasa na watu ambao aliwashawishi wamkubali
Nyerere wakati wa kuundwa TANU.
Abdulwahid alimwambia Nyerere huenda yeye akawa
hana hisia wala uhusiano wowote na watu ambao yeye anatia sahihi wakamatwe
na kutupwa gerezani. Lakini kwake yeye hao ni jamaa zake anaokutananao
ama msikitini au mitaani. Yeye kama mtu anayeishi miongoni mwa Waislamu
na zile familia zao alikuwa anaelewa majonzi yao.
Abdulwahid alimwambia Nyerere kwamba watu wale
wanajua kuwa yeye, Abdulwahid ndiye aliyesamsaidia Nyerere wakati akiwa
mgeni mjini Dar es Salaam, watu wakamjua na kumkubali na hivyo kuja kuweza
kufika hapo alipofika.
Abdulwahid alimwambia Nyerere kuwa ndugu na jamaa
za wafungwa wale wanamjia wakimbembeleza amsihi Nyerere awatoe ndugu zao
jela. Abdulwahid alimwambia Nyerere kwamba kule kuwatia watu kizuizini
ni uonevu kwa sababu wale watu hawana uwezo wa kupindua serikali yake.
Kwa sauti ya masikitiko Abdulwahid alimaliza maelezo
yake kwa kumwambia Nyerere 'Naondoka hapa nikiwa nataka kuamini kuwa wewe
Julius Nyerere, leo hujatugeuka.' Kwa maneno hayo Abdulwahid aliaga na
kuondoka.
Alichosikia Nyerere kuhusu Abdulwahid baada ya
maneno yale ilikuwa taarifa ya kifo chake jioni moja Jumamosi tarehe 12
Oktoba, 1968. Mkewe Mama Maria Nyerere, alizirai aliposikia habari zile
za msiba. Alikuwa Abdulwahid ndiye aliyewapokea yeye na mume wake mara
ya kwanza walipokuja Dar es Salaam.
Mazishi ya Abdulwahid Sykes yalifanyika siku ya
Jumapili tarehe 13 Okrtoba. Mazishi yake yalikuwa makubwa yasiyo kifani.
Ukitoa mazishi ya mwaka 1950 ya Sheikh Idrissa bin Saad, muasisi na Khalifa
wa Tariqa Askariya na mazishi ya Sheikh Kaluta Amri Abeid mwaka 1963, Dar
es Salaam ilikuwa haijapata kushuhudia mazishi kama hayo. Gerezani yote
ambako Abdulwahid aliishi katika utoto wake na mahali ambapo alianza harakati
zake dhidi ya Waingereza ilikuwa kama vile imesimama hakuna kinachoendelea
ila maziko ya Abdulwahid. Hii ilikuwa pamoja na sehemu nyingine zilizozunguka
Kariakoo kama Misheni Kota na Kisutu.
Gerezani kwa hakika ilikuwa na mwito wa pekee.
Ilikuwa ni kutoka Gerezani ndipo walipotoka wanaharakati wa mwanzo waliounda
TANU ukimtoa John Rupia. Siku hiyo Gerezani ilikuwa imekuja kumzika shujaa
wao. Watu walianza kukusanyika nyumbani kwa mama yake, Abdulwahid Bibi
Mluguru bint Mussa mapema asubuhi ambako maiti ilipokuwa imepelekwa. Ilipofika
adhuhuri ikawa kama vile Dar es Salaam nzima imekusanywa pale. Chifu wa
Unyanyembe Abdallah Said Fundikira, ambae Abdulwahid alisomanae darasa
moja katika shule ya serikali mjini Dar es Salam katika miaka ya 1930 na
mtu ambae walikwenda wote kuhiji Maka alikuja Dar es Salaam kwa ndege kutokea
Nairobi kuja kuhudhuria mazishi.
Inasemekana Nyerere hakutaka kuja kwenye mazishi
ya Abdulwahid kwa kuwa wakati ule ndiyo kulikuwa na lile tatizo la EAMWS
na masheikh walikuwa wakikamatwa nyakati za usiku na kutupwa jela. Usalama
wa Taifa unasemekana ulimshauri Nyerere kwa usalama wake kutohudhuria mazishi
yale kwa sababu mazishi ya Abdulwahid yatahudhuriwa na Waislamu wengi.
Chuki za Waislamu dhidi ya Nyerere kwa wakati ule zilikuwa juu sana.
Rashid Kawawa aliyekuwa Makamo wa Rais alipopata
habari zile kuwa Nyerere hatofika mazishini haraka alimwendea Nyerere na
kumwabia kuwa kabla hajachukua uamuzi wa kutokwenda yeye atakwenda kuangalia
hali ya mambo yalivyo pale msibani kisha atarudi kumpa habari kamili.
Aliporudi kwa Nyerere Kawawa alimwambia Nyerere
kuwa umma uliokuja kumzika Abdulwahid haujapata kuonekana. Chifu Fundikira
amekuja kutoka Nairobi kuja kumzika Abdulwahid. Watu wa Dar es Salaam hawatamwelewa
kama yeye Nyerere yupo Dar es Salaam na ashindwe kwenda kwenye mazishi
yake. Watu wa Dar es Salaam wengi wao wanakumbuka kwa mara ya kwanza kumuona
Nyerere akiwa amefuatana na Abdulwahid na wanafahamu hisani aliyomfanyia
Nyerere. Nyerere aliona busara ya Kawawa na palepale ikatoka amri kuwa
ulinzi katika mazishi ya Abdulwahid uimarishwe na Nyerere atakwenda kumzika
rafiki yake aliyempokea na kumuunga mkono wakati ule wa kipindi kigumu
cha kuasisi TANU.
Rais Nyerere akawa mmoja wa watu waliokwenda kuomboleza
kifo cha Abdulwahid. Akitembea kwa miguu Nyerere alilifuata jeneza la Abdulahid
nyuma kutoka Mtaa wa Lindi, Gerezani hadi Msikiti wa Kitumbini maiti ilipokwenda
kuswaliwa swala ya jeneza kama ilivyo ada ya Kiislamu.
Pale Kitumbini, Nyerere alisimama nje ya msikiti
pamoja na Wakristo na wananchi wengine kungojea maiti ilitolewe nje. Mfanyabiashara
mmoja wa Kiasia kuona rais amesimama wima, kwa ajili ya heshima alileta
kiti na kumuwekea Nyerere akae. Nyerere alikataa kukaa na akawa amesimama
pamoja na watu wengine. Kutoka Kitumbini msafara wa maziko ulielekea makaburi
ya Kisutu kwa ajili ya mazishi.
Chifu Fundikira alikuwa mmoja wa watu walioingia
kaburini kuupokea mwili wa Abdulwahid. Wakati huu wote wakielekea makaburini,
Nyerere alikuwa nyuma ya jeneza kichwa chake amekiinamisha na kila wakati
alionekana akifuta macho yake na kitambaa.
Nyerere alikuwa analia. Ilikuwa mwaka 1952 Abdulwahid
alipofahamiana na Nyerere na yeye Abdulwahid akamjulisha kwa watu mashuhuri
wa Dar es Salaam Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir,
Mwinjuma Mwinyikambi, Mohamed Jumbe Tambaza, Omar Londo, Rajab Diwani,
Mshume Kiyate, Bibi Tatu bint Mzee, Bibi Asha Ngoma, Bibi Titi Mohamed,
Bibi Hawa bint Maftah, Bibi Khadija bint Kamba, Said Chamwenyewe na wengi
wengine. Ilikuwa na kutokana na msaada wa Abdulwahid na Waislam hawa ndiyo
uliomuwezesha Nyerere kuwa katika siasa na kuchukua uongozi wa nchi miaka
tisa baadae.
Hakuna aliyeweza kukisia ni mawazo gani yalikuwa
yanapita katika fikra za Nyerere. Lakini ni wazi kuwa alikuwa akimfikiria
Abdulwahid na jinsi pamoja walivyoweza kuanzisha harakati za kudai uhuru
wa Tanganyika. Ilikuwa miaka kumi na tano iliyopita katika Ukumbi wa Arnatouglo,
si mbali na pale alipokuwa, Nyerere aligombea urais wa TAA na rais aliyekuwa
madarakani, Abdulwahid Sykes. Abdulwahid akiwa na umri wa miaka thelathini
na Nyerere akiwa na miaka thelathini na mbili.
***
Tarehe 27 Aprili, 1985 Julius Kambarage Nyerere,
sasa akijulikana kama Baba wa Taifa,294 katika sherehe kubwa
katika viwanja vya Ikulu, alitoa jumla ya medali 3979 kwa Watanzania waliochangia
katika maendeleo ya taifa. Kati ya wale ambao walipewa medali hizo alikuwa
Sheikh Abdallah Chaurembo.
Wazalendo waliotajwa ndani ya kitabu hiki ambao
walipigania uhuru wa Tanganyika, hakuna hata mmoja wao aliyekuwa katika
orodha ile ya heshima. Baada ya siku chache kupita, Nyerere kama mtu aliyegutuka
alimualika Dossa Aziz Ikulu. Dossa Aziz, wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika
alikuwa mtu maarufu, mwenye nafasi, na kujiweza sana. Sasa Dossa baada
ya miaka kupita hakuwa akifahamika tena na ule umaarufu na utajiri wake
ulikuwa umetoweka. Alikuwa akiishi maisha ya kawaida kijijini Mlandege,
maili chache nje ya Dar es Salaam. Katika sherehe ya faragha Nyerere alimtunukia
medali Dossa Aziz, rafiki yake wa zamani. 295
Ule Mkutano wa Tabora ulikuwa umeacha kovu lake
katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Huenda kama si yale masharti ya
uchaguzi wa kura tatu, historia ya TANU na kwa hakika ile ya ukoloni Tanganyika
isingekuwa hivi ilivyo sasa. Yamkini kusingekuwepo na mgawanyiko katika
TANU wala Zuberi Mtemvu asingeunda ANC, na Mashado Plantan - AMNUT; wala
suala la udini katika siasa za Tanganyika lisingewekwa katika agenda, jambo
ambalo kwa miongo mitatu baada ya uhuru ngurumo zake bado zinasikika na
zinatishia utengemano na uthabiti wa nchi. Waislam wanamlaumu Nyerere na
Wakristo waliokabidhiwa madaraka ya kutawala nchi kwa msaada mkubwa wa
Waislam. Waislam wanadai kuwa wamesalitiwa. Kwa hivi sasa Waislam wako
katika mwelekeo wa kujitambua kwa mara ya pili na historia yao yenye mengi
sana. Wanaamini majibu ya baadhi ya matatizo yao ya hivi sasa yamo katika
historia yao ya zamani.
***
Mjini Dar es Salaam katika msikiti wa Kitumbini
hawli husomwa kila mwaka katika mwezi wa Oktoba kumkumbuka Abdulwahid Kleist
Sykes. Hii ni hafla ya kifamilia ikihudhuriwa hasa na wana-ndugu. Ukiachia
mbali ule wajibu wa Waislam kurehemiana kama ilivyo kawaida katika Uislam,
Abdulwahid hufanyiwa hafla hii pale msikitini kwa sababu nyingine. Katika
umri wake mfupi, Abdulwahid alikuwa akiswali pale msikitini na katika msikiti
ule ndipo aliposwaliwa swala yake ya mwisho kabla ya kupelekwa kuzikwa.
Abdulwahid alikuwa mtu mashuhuri katika jamii ya Waislam Dar es Salaam.
Alifanya shughuli nyingi chini ya Al Jamiatul Islamiyya. Halikadhalika
alikuwa katibu baadae rais wa TAA. Ingawa historia ya Tanzania bado haijamtambua
mchango wake ni wazi kuwa Abdulwahid ndiye aliyekuwa bongo katika kuasisi
TANU chama ambacho kilikuja kuwaunganisha wananchi wa Tanganyika katika
kudai uhuru wao kwa Waingereza.
Marika ya Abdulwahid bado wa hai na baadhi yao
wanaswali pale msikitini. Huwa wanafurahishwa na kumbukumbu hii ya kumrehemu
mwenzao. Karibu walio wengi ni maveterani wa TANU ya miaka ya 1950. Hivi
sasa wao ni wazee na kwa uchungu hawana haja na siasa. Ukiacha ndugu wa
marehemu Abdulwahid (sasa hivi wanajumuika na wajukuu zake), marafiki wa
karibu na wanachama wa zamani wa TANU, hakuna hata mtu mmoja katika Chama
cha Mapinduzi (chama kilichorithi nafasi ya TANU) anaemkumbuka. Jina la
Abdulwahid halitajwi kabisa katika historia ya kudai uhuru wa Tanganyika
au katika historia ya kuasisi TANU. Juu ya haya yote Abdulwahid ndiye aliyewasha
cheche za kuanzisha harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.
Jopo la wana-historia wa Chama Cha Mapinduzi waliopewa
jukumu la kutafiti na kuandika historia rasmi ya TANU, hakuna hata sehemu
moja waliyotaja jina la Abdulwahid katika kitabu kizima.296
Dhana inayojaribiwa kuenezwa katika kitabu kile ni kuwa kabla ya kutokea
kwa Julius Nyerere mwezi Aprili, 1953, alipochaguliwa kuwa rais wa TAA,
chama hicho hakikuwa na mwelekeo wowote wa siasa. Kitu cha ajabu ni kuwa
kitabu hicho wala hakielezi huo urais wa TAA, Nyerere aliupataje au aliuchukua
kutoka kwa kiongozi gani wa wakati ule. Kitendo hiki kimeondoa hadhi na
heshima ya wazalendo wengi waliopigania nchi hii na halikadhalika kimeiondolea
TAA heshima ya kuitwa chama cha siasa. Wanahistoria wazalendo pamoja na
wanasiasa wa sasa hawataki kabisa kuipa TAA hadhi ya chama cha siasa. Kambona
aliiita African Association chama cha majadiliano:
Sasa inakaribia mwaka mmoja toka iundwe Tanganyika
African National Union na katika kipindi hiki chama kimekua kikipata nguvu
siku hadi siku, wakati mwingine chini ya upinzani mkubwa. Kama mnavyofahamu
chama hiki ni badala ya Tanganyika African Union ambayo ilikuwa sawasawa
na chama cha majadiliano.297
Ulotu anaieleza TAA kuwa ilikuwa chama cha ustawi
wa jamii.298 Wengine wameieleza TAA kama taasisi ya jamii: Nyerere
(1976), 299 halikadhalika Japhet na Seaton (1966).300
TAA wakati mwingine inaelezwa kuwa ilikuwa chama cha vuguvugu za upinzani
dhidi ya ukoloni, lakini upinzani wake haukuwa dhahiri: Kaniki (1974),
301 Nyerere (1953) 302 aliieleza TAA kama chama cha
vuguvugu la siasa lakini si za dhahiri. Julius Nyerere alipohutubia Baraza
la Udhamini la Umoja wa Mataifa, New York, tarehe 7 Machi, 1955 alisema:
Tanganyika African National Union kwa mtazamo
mmoja ni chama kipya, lakini kwa mtazamo mwingine ni chama kikongwe. TANU
imechukua nafasi ya Tanganyika African Association ambayo ilianzishwa mwaka
1929, kama chama cha kijamii. Tanganyika African National Union, chama
kilichochukua nafasi ya African Association miezi kumi iliyopita ni chama
kipya kwa maana ni chama cha siasa, wakati TAA ilikuwa chama cha siasa
nusunusu.
Wasomi wengine wameishusha TAA kufikia daraja
la kuwa klabu: Mwenegoha (1976) anaandika: 'Mwaka 1954, baada ya miaka
ishirini na tano ya kutoweza kufanya lolote, Nyerere aliigeuza TAA kutola
chama cha kijamii kuwa chama cha siasa chenye kuogopwa kilichoitwa Tanganyika
African National Union'. 303
Abdulwahid ambae alitoa mchango wa pekee katika
kuunda TANU alikuwa anaiona TAA kama chama cha siasa (1951).
304
Katika kundi la waandishi na wasomi walioandika kuhusu African Association
kisha wakabadili mawazo yao kuhusu nini hasa chama kile kilikuwa, ni Nyerere
na Hatch ndiyo waliobadili misimamo yao ya awali. Nyerere alipoandika barua
kwa Gavana wa Tanganyika, Edward Twining tarehe 10 Agosti, 1953 alieleza
kuwa TAA ni chama cha siasa. 305
Lakini baadae alibadili msimamo na kusema kuwa
TAA kilikuwa chama cha starehe. Kauli hii ilitawala hotuba za Nyerere na
maandishi yake kwa kipindi kirefu. Katika miaka ya hivi karibuni amesikika
akisema kuwa TAA kilikuwa 'chama cha siasa kisichokuwa na katiba ya siasa'.
Hatch (1976) ameieleza TAA kama chama cha starehe 306 sehemu
moja na chama cha siasa sehemu nyingine.307 John Kabudi ameieleza
African Association kama 'chama cha watu binafsi wananchi kilichokuwa na
mwelekeo wa kitaifa'.308 Ieleweke kuwa hata viongozi wa TAA
hawathaminiwi kama wanasiasa. Kaniki, kwa kukosa neno la kuwatambulisha
waasisi wa TAA, amewaita wanasiasa na kuwawekea quatation mark:
Nyerere, kabla ya hapo akiwa hajulikani na 'wanasiasa'
wengi katika Tanganyika, alikuwa mwalimu katika shule ya Mtakatifu Francis,
Pugu, jirani na Dar es Salaam, na alikuwa amechaguliwa rais wa (TAA) mwaka
uliopita.309
Kwa mtazamo huo wa Kaniki mzalendo kama Abdulwahid
Sykes hakuwa mwanasiasa, ila Nyerere ndiye mwanasiasa. Iliffe (1968)310
alidokeza kuwa historia ya TANU iliyokuwa imeandikwa hadi wakati ule ilikuwa
haijakamilika na katika uchambuzi wake alisema kuwa African Association
kutokana na mwelekeo na wanachama wake ilikuwa ni chama cha siasa. Kandoro
na Japhet, 311 waasisi wa TANU walipata umaarufu wakati Abdulwahid
akiwa rais wa TAA mwaka 1952. Hawa walikuwa ndiyo waasisi pekee ambao walifanya
kazi na Abdulwahid wakati wa Mgogoro wa Ardhi ya Wameru. Safari ya Kirilo
kuja Dar es Salaam na kule kumweka Seaton kama mwanasheria kushughulikia
mgogoro ule, kazi yote hiyo ilifanywa na Abdulwahid na uongozi a TAA wa
wakati ule. Ilikuwa Abdulwahid ndiye aliyemhangaikia Kirilo kupata pasi
ya kusafiria baada ya kunyimwa pasi kule Arusha. Kirilo na Seaton na halikadhalika
Kandoro wamenadika kumbukumbu zao kuhusu ukoloni, lakini cha ajabu na kusikitisha
ni kuwa hakuna hata sehemu moja waandishi hawa wametaja mchango wa Abdulwahid
hata kwa kuparazia tu. Waandishi hawa wamejaribu kumtumbukiza Nyerere kama
kiongozi aliyehusika katika Mgogoro wa Ardhi ya Wameru, wakati yeye hata
kuwapo nchini wakati ule hakuwapo. Ukweli ni kuwa wakati mgogoro wa ule
ulipofikishwa mbele ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, New York,
Nyerere alikuwa masomoni Chuo Kikuu cha Edinburgh Uskochi akisomea shahada
ya pili. Mwandishi aliyejipambanua na hawa wote kwa kutomtaja Abdulwahid
ni mama wa Kiingereza Judith Listowel (1965) 312 ambae ingawa
amemtaja kijuujuu, ameandika kwenye kitabu chake kuwa Abdulwahid alikuwa
mmoja wa waasisi wa TANU.
Katika miaka hii ya karibuni kumejitokeza hamu
ya kutaka kuielewa historia ya siasa katika Tanzania na jina la Abdulwahid
limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika majarida, 313 magazeti,
314 magazeti ya kimataifa, 315 na katika vitabu.
316 Maandiko yote haya yanamtazama Abdulwahid kwa sura tofauti.
Yapo yanasema kuwa yeye ndiye alikuwa kinara katika kuunda TANU na kumtia
Nyerere katika siasa. Katika maandiko haya Abdulwahid anaelezwa kama mzalendo
na mwanamapinduzi. Tandon anamweleza Abdulwahid na wazalendo wengine katika
Afrika ya Mashariki kama Chege Kibachia, Makham Singh, Fred Kubai, James
Kivu, I.K. Musazi, Erika Fiah na Gama Pinto kama 'viongozi maveterani wa
watu wa Afrika ya Mashariki ambao wanahistoria wetu wa sasa wamewasahau'.
317 Wapo waandishi wanaomuona Abdulwahid kama 'kabaila uchwara'
kutokana na kuwa alikuwa mtoto wa mfanyabiashara Mwafrika tajiri, Kleist
Sykes.
Profesa Shivji anamtuhumu Abdulwahid kwa kushirikiana
na wakoloni na anamchukulia kama kabaila uchwara ambae yeye mwenyewe hatoki
katika tabaka la wafanyakazi. Akitafakari nafasi ya Abdulwahid kama kiongozi
wa makuli katika bandari ya Dar es Salaam wakati wa ukoloni Shivji ansema:
serikali ilipenyeza uongozi wa makabaila uchwara
katika chama. Mwezi February 1948 Abdul Sykes, mtoto wa mfanya biashara
Mwafrika maarufu, aliombwa na serikali awe katibu wa chama cha makuli.
Abdul Sykes hakuwa akifanyakazi bandarini wala hakuwa anatoka katika tabaka
la wafanyakazi.318
Hapa Shivji alikuwa anaeleza jinsi Abdulwahid
alivyochaguliwa kuwa katibu mkuu wa kwanza katika historia ya vyama vya
wafanyakazi Tanganyika. Kwa kutoijua vyema historia ya maisha ya Abdulwahid
na vilevile kwa hamaki za misimamo ya mrengo wa kushoto ya Ki-Marx, Shivji
ametumia vipimo visivyo sawa katika kumchambua Abdulwahid. Engels anasema
bepari uchwara ni 'tabaka la makabaila wa kisasa ambao wanahodhi njia zote
za uzalishaji mali za jamii na vilevile wanawaajiri na kuwalipa'.319
Hata hivyo Sklar anasema kuwa dhana hiyo sasa imebadilika kwa hiyo hata
ile maana yake ya awali imebadilika:
Hivi sasa neno hilo linatumiwa na wafuasi wa Marx
kuieleza tabaka lililo juu katika jamii ambazo linafuata soko huria na
kuachia kuhodhiwa kwa mali kama matokeo ya mali binafsi katika uzalishaji
wake.320
Kama Shivji angeliyajua maisha ya Abdulwahid ni
wazi kuwa angetumia kipimo kingine kabisa katika kumweleza. Lakini kwa
kuwa kilichotumika ni kipimo kisicho sawa, matokeo yake hayakuweza kuwa
barabara. Hakuna biashara ya Mwafrika wakati wa ukoloni inaweza kuitwa
biashara ya bepari na katika mkumbo wa kujumuishwa katika dhana ya ubepari,
kama ubepari ulivyokuwa ukifahamika huko Ulaya. Haya ndiyo matatizo yanayoikumba
historia ya Abdulwahid na kwa kweli historia nzima ya taifa la Tanganyika.
Katika wale walioasisi TANU, ni wale tu aliokuwa
makao makuu ya TAA ndiyo wanaoweza kueleza historia ya kweli ya chama hiki.
Hawa ni John Rupia, Dossa Aziz, Tewa Said Tewa, Julius Nyerere, Dome Budohi,
Abdulwahid na Ally Sykes. Hawa ndugu wawili, Abdulwahid na Ally, wao ni
baba yao ndiye aliyekuwa muasisi wa African Association akiwa kama katibu
wake wa kwanza hapo mwaka wa 1929. Majalada ya akina Sykes kuhusu African
Association na TANU yana habari muhimu sana kwa mtafiti kuhusu historia
ya ukoloni na juhudi walizofanya waasisi wa taifa la Tanganyika katika
kujikomboa. Majalada haya yana habari muhimu na za kutosha kuhusu Nyerere
na jinsi alivyopokelewa Dar es Salaam na akina Sykes na jinsi alivyoingizwa
katika siasa. Inastaajabisha kuwa kumbukumbu hizi zenye habari muhimu sana
kuhusu Nyerere na TANU hazikuguswa kabisa wakati watafiti wa historia ya
TANU walipokuwa wakifanya utafiti wao. Inastaajabisha vilevile kuwa, si
Ally wala mdogo wake, Abbas ndugu wawili walio hai baada ya kifo cha kaka
yaoAbdulwahid, walifanyiwa mahojiano yoyote na watafiti wale.
Katika miaka ya mwishoni ya 1960, John Iliffe
akiwa Idara ya Historia ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, alipoanza utafiti
wake wa historia ya Tanzania, aliweza kukusanya habari nyingi sana na muhimu
kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wake, Aisha Daisy Sykes, binti wa Abdulwahid.
Ingawa Daisy alimfahamisha Iliffe kuwa habari zile alizokuwa akiandika
katika semina kuhusu historia ya Tanganyika alikuwa akizipata kutoka kwa
baba yake, inastaajabisha kuwa, Iliffe japo kuwa alikua muhihataji sana
wa kutaka kujua historia ya Tanganyika, hakuchukua tabu ya kuonana na Abdulwahid
ili apate habari zile moja kwa moja kutoka kinywani kwake.
Iliffe hata hivyo kwa kujua hazina ya historia
iliyokuwa katika kumbukumbu za akina Sykes, alimtia hima Daisy aandike
historia ya maisha ya babu yake, Kleist Sykes. Utafiti huu Daisy aliufanya
kwa ufanisi mkubwa. 321
Baba yake alipofariki dunia mwaka wa 1968, Daisy
kutokana na mafanikio ya kuandika habari za babu yake sasa akataka kufanya
utafiti na kuandika maisha ya marehemu baba yake. Daisy aliamua kufanya
hivyo kwa uchungu alipokuja kugundua kuwa historia ilikuwa haimtendei haki
baba yake. Daisy alihisi ilikuwa ni wajibu wake kuueleza ulimwengu baba
yake alikuwa nani na nini mchango wake katika kuikomboa Tanganyika kutoka
ukoloni wa Waingereza. Hiki alikiona kitu muhimu ili kuiweka sawa historia
ambayo kwa makusudi ilikuwa inapotoshwa. Daisy alikuwa na majalada na shajara
zote za baba yake. Iliffe kwa sababu ambazo kwa wakati ule Daisy hakuweza
kuzitambua, alimkataza asifanye hivyo kwa kuwa wakati wa kuandika historia
ya baba yake ulikuwa bado. Iliffe alimwambia Daisy afanye subira hadi hapo
baadae. Ni wazi kuwa Iliffe alikuwa akijua kuwa Abdulwahid alikuwa mtu
muhimu na wa kuaminika katika historia ya TANU; na kuwa utafiti wowote
katika maisha yake kungesaidia sana kuielewa historia ya Tanzania. Kutokana
na msimamo huu wa Iliffe Daisy hakujaaliwa tena kuandika maisha ya baba
yake.
Historia ya TANU siku zote imekuwa ikitawaliwa
na mambo kama haya. Mwaka wa 1962 Ally Sykes alijaribu kuandika historia
ya TANU katika gazeti la Mambo Leo. Mhariri wa gazeti lile M.J.
Sichwale alimuandikia Ally Sykes kumfahamisha kuwa hawezi kuchapisha makala
yake kwa kuwa mwandishi hana utaalamu na somo aliloliandikia.322
TAA ilipogeuzwa kuwa TANU, wanaharakati wa TAA,
labda kwa kuanza kuhisi kuwa historia yao ilikuwa inataka kupotoshwa na
wale waliokuja katika siasa na TANU, walikuwa na fikra za kuandika historia
ya TANU. Mwalimu Kihere, mmoja wa viongozi wa TAA Tanga, alipata wakati
fulani kumwambia Abdulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz na John Rupia kuwa
ingekuwa vyema historia ya siasa katika Tanganyika ikaandikwa na kuhifadhiwa
wakati wao wangali hai kuepusha kuingizwa uongo ndani yake na kupindisha
ukweli na hao watakaokuja hapo baadae baada ya wao kutoweka. Bahati mbaya
wazo hili halikupewa uzito iliostahili na hadi Mwalimu Kihere, Abdulwahid
na John Rupia, Stephen Mhando na Hassan Suleiman wanafariki dunia, hakuna
hata mmoja katika wale wakongwe wa siasa alikuwa wameandika kitu chochote.
Hassan Suleiman anawalaumu wanahistoria kwa kukosekana
kuandikwa historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika kwa kuwapuuza wazalendo
wengine na badala yake kuandika historia ya Tanganyika kwa kuegemeza historia
hiyo kwa Nyerere. Kabla hajafariki, Hassan Suleiman alichukua nyaraka zake
zote binafsi za African Association wakati alipokuwa kiongozi na kuzikabidhi
kwa Katibu Mkuu wa CCM wakati ule Rashid Kawawa katika sherehe mahsusi
iliyofanyika Makao Makuu ya CCM, Dodoma.
Kwa mara ya kwanza historia ya TANU ilitaka kuandikwa
na Abdulwahid mwenyewe. Baada ya kupatikana kwa uhuru mwaka 1961 na TANU
ilipokuwa sasa inataka kujiimarisha kama chama cha umma, inasemekana Nyerere
wakati ule Waziri Mkuu alimuomba Abdulwahid aandike historia ya harakati
ya Waafrika wa Tanganyika dhidi ya ukoloni wa Waingereza. Hii kwa hakika
ndiyo historia ya TANU. Dr Wilbert Kleruu ambae ndiyo kwanza alikuwa ametoka
masomoni Marekani alichaguliwa na TANU asaidiane na Abdulwahid katika utafiti
na uandishi wa historia ile.
Abdulwahid alirudi kwenye ofisi za TANU makao
makuu; kwenye ofisi yake ya zamani aliyokuwa akiitumia kama rais wa TAA.
Nyaraka zake binafsi, za baba yake nyingine kuanzia mwaka wa 1929 wakati
wa enzi za African Association zililetwa pale kwa utafiti kama ushahidi
wa yale yaliyopitika zama hizo. Maelezo ya Abdulwahid katika kuanzishwa
kwa Africa Association inasemekana hayakumpendeza Nyerere, kwa kuwa mwanzo
wa harakati dhidi ya ukoloni jina la baba yake Abdulwahid Kleist
Sykes, lilikuwa likitawala. Halikadhalika ilipofika kueleza namna TAA ilivyokujabadilishwa
kuwa TANU watoto wake wote watatu Abdulwahid, Ally na Abbas wakiongozwa
na kaka yao mkubwa Abdulwahid halikadhalika likawa linatawala harakati
zile. Historia hii inasemekana haikumpendeza Nyerere na baadhi ya viongozi
wa TANU. Haukupita muda Abdulwahid akatambua kuwa viongozi wapya walioshika
nafasi katika TANU kwa kweli hawakuwa na nia hasa ya kutafiti na kuandika
historia ya Tanganyika bali nia na azma yao ilikuwa na kumjenga Nyerere
na kumkuza kwa sifa ambazo hazikumstahili. Abdulwahid alipong'amua hili
haraka akajitoa katika kazi ile. Hata hivyo Dr Kleruu aliendelea na utafiti
na akaandika historia ya TANU. Historia hii iansemekana ilifuta mchango
mzima wa akina Sykes katika kuunda TAA na baadae TANU. Hata hivyo baada
ya kazi hii kukamilika haikuchapishwa na ikabaki katika maktaba ya TANU,
Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam. Lakini baadae kazi ile ilitoweka na ikachapishwa
baada ya 'mwandishi' kufanya mabadiko kadhaa katika mswada ule ili usitambulike
chanzo chake. Hata hivyo TANU iligundua kuwa ile ilikuwa historia yao iliyoandikwa
na Dr. Kleruu na wakafanya bidii kuzuia isichapishwe. Kimya kimya TANU
ikafanya juhudi ya kuzuia kitabu hicho kisitoke toleo la pili. Lakini hili
halikuwezekana na kitabu hicho kimechapishwa sasa mara kadhaa. Uandishi
wa kitabu kile haukutofautiana sana na kitabu cha TANU kilichotoka mwaka
1981 kilichoandikwa na Chuo cha TANU cha Kivukoni.
Hata hivyo kuna kasoro katika kitabu hicho ambacho
'mwandishi' alishindwa kugundua na kuweza kujikinga asijulikane kama kile
kitabu hakikuandikwa na kalamu yake. 'Mwandishi' kama tunavyoweza kumwita,
akiandika katika nafsi ya kwanza, anaeleza kuwa amekiandika kitabi kile
mwaka wa 1964. Katika maelezo hayo 'mwandishi' anatoa habari ambazo msomaji
makini anahisi kuwa 'mwandishi' alikuwa marika sawa na anawafahamu vyema
wale wazalendo anaoandika habari zao. Lakini mwandishi anasahau kuwa mwaka
1964 wakati yeye anadai alikuwa akiandika habari hizo yeye alikuwa mvulana
mdogo na asingeweza kuwajua vile wale wazalendo na habari zilizotokea miaka
ya 1950 wala asingeweza kuwa na ubongo wa kutafakari mambo kama yale. Sasa
swali linakuja. Huyu aliyeandika habari zile ni nani hasa? Kutokana na
maelezo ambayo kitabu hiki kimeeleza ni wazi aliyeandika habari zile hawezi
kuwa Dr Kleruu kwa sababu Kleruu katika kipindi kile, hakuwapo katika harakati
zile za kuunda TANU. Ni mtu mmoja tu ndiye anaeweza kuwa na habari zile
na kuwa na ufahamu wa mambo yalivyokuwa miaka ile. Huyu atakuwa ni marehemu
Abdulwahid akiandika mwaka 1964. 'Mwandishi' kwa ujinga amenakili kutoka
kwenye maandishi ya Abdulwahid ambayo yalikuwa yamehifadhiwa katika Maktaba
ya TANU, Dar es Salaam. Na huyu 'mwandishi' wala hakunakili maandishi yale
mwaka 1964, bali miaka mingi baada ya kifo cha Abdulwahid kutokea.
Abdulwahid alipobaini kuwa historia ya Tanganyika
inaweza kuwa chanzo cha husda na hasama kati yake na Nyerere na viongozi
wengine wa TANU, akaamua kutosema chochote kuhusu hilo ingawa kabla hajafa
alikubali mwaliko wa Chama Cha Historia Cha Tanzania (Historical Association
of Tanzania) (HAT). Imeshindikana kujua Abdulwahid alizungumza kuhusu nini
katika mwaliko ule, lakini inasemekana moja ya maswali aliyoulizwa ilikuwa
kuwa kama si kweli Nyerere ndiye aliyekipa chama uhai kuanzia mwaka wa
1954. Katika kujibu swali hili Abdulwahid alilirudisha swali lile kwa wasikilizajiwake
kwa kutoa mfano wa John Glenn, Mmarekani wa kwanza kwenda angani kuzunguka
dunia. Abdulwahid aliwauliza wasikilizaji wake, 'Nani apewe sifa, wanasayansi
wa Kimarekani waliotengeneza roketi ile au John Glenn aliyekuwa rubani
wa chombo?'
Mwaka 1962 Judith Listowel alipokuja Tanganyika
kufanya utafiti kabla hajaandika kitabu chake The Making of Tanganyika,
alitaka sana kufanya mahojiano na Abdulwahid. Kwa kujua matatizo yaliyokuwa
yanakabili historia ya Tanganyika mara ya kwanza ilipojaribiwa kuandikwa,
Abdulwahid alijaribu sana kumkwepa Listowel. Listowel alipokuja kumkamata
Abdulwahid nyumbani kwake Magomeni Mikumi, yeye hakupenda kueleza mchango
wake wala wa baba yake katika kuaisisi African Association na TANU. Kwa
kweli katika mahojiano yake Listowel hakupata chochote cha maana sana.
Hata hivyo Listowel aliweza kuelezwa na Abdulwahid jinsi TANU ilivyokuja
kuasisiwa. Listowel alikuja kuandika katika kitabu chake kuwa: 'Abdul Sykes,
kaka yake Ally, alisema kuwa ilibidi waamshe fikra za siasa za wananchi
ili kiundwe chama cha siasa'.323 Kutokana na mazungumzo haya
na Abdulwahid, Listowel alimwandikia Ally Sykes: 'Nimependezwa sana na
kaka yako na ningefurahi kama ningepata wasaa wa kuwa na mazungumzo na
yeye zaidi'.324 Akiwa London Listowel alimuandikia Ally Sykes
mara kadhaa akitaka ufafanuzi kuhusu mambo mengi muhimu katika historia
ya Tanganyika.
Abdulwahid alipofariki Wizara ya Habari ilitoa
taarifa ikieleza kuwa Rais Nyerere amehudhuria maziko ya Abdulwahid Sykes.325
Kingine kinachostaajabisha ni kuwa taarifa ile ilitoa maelezo machache
ya uajiriwa wake katika serikali na kuacha maelezo muhimu ya Abdulwahid
katika siasa. Ilikuwa Mwingereza, Brendon Grimshaw, mhariri wa Tanganyika
Standard, ndiye aliyempa Abdulwahid heshima na hadhi anayostahili baada
ya kifo chake kwa kuchapisha taa'zia ambayo ilimweleza Abdulwahid kama:
'mmoja wa wapangaji wa vuguvugu la kudai uhuru na mmoja wa watu waliomsaidi
Nyerere kuingia katika siasa '
Taa'zia ile ilitoa sifa kemkem kwa ukoo wa Sykes
katika kuleta maendeleo ya siasa Tanganyika kwa kusema kuwa, 'msukumo mkubwa
wa Waafrika wa Tanganyika kupata chama cha siasa chenye nguvu ulitokana
na juhudi za ukoo wa Sykes'.326 Inasemekana taa'zia hii iliyompa
marehemu Abdulwahid heshima na sifa za uzalendo wa hali ya juu iliwaudhi
baadhi ya viongozi katika TANU. Viongozi hao wakawa wakisikika wakisema
kuwa Ally na Abbas Sykes walikuwa wanajaribu kumtukuza kaka yao. Hali hii
ilijitokeza tena wakati CCM ilipokuwa ikitafiti historia yake. Hassan Upeka,327
mmoja katika wasaidizi wa utafiti ule alipeleka katika jopo lile la utafiti
na uandishi wa historia ya TANU, mahojiano aliyofanya na Abdulwahid miaka
mingi iliyopita kuhusu historia ya TANU. Hassan Upeka alifahamishwa kuwa
historia inayoandikwa haimhusu Abdulwahid Sykes. Wakati Abdulwahid anafariki
dunia, Abbas alikuwa Councellor katika Ubalozi wa Tanzania Canada na Ally
Sykes alikuwa amejiuzulu kazi na kushughulika na biashara. Ally Sykes alikuwa
amelazimika kujiuzulu kazi kwa shinikizo kutoka serikalini kwa kuwa alikuwa
ameshindwa kufuata masharti ya uongozi yaliyomtaka kiongozi asiwe na mali
wala asifanye biashara.
Mwaka wa 1974 Rais Julius Nyerere aliwatwisha
Chuo Cha Kivukoni jukumu la kuandika historia ya TANU. Chuo hiki kilianzishwa
kama shule ya kuwasomesha makada wa TANU katika mambo ya itikadi, propaganda
na uhamasishaji umma wakiiga mfano wa Ruskin College ya Uingereza. Chuo
Cha Kivukoni kwa ajili hii kisingeweza kufanya utafiti huru wala kuandika
historia sahihi ya TANU. Mwaka 1976, katika mkutano wa kumi na sita wa
TANU Nyerere alisisitiza tena kuandikwa kwa historia rasmi ya TANU. Lakini
historia rasmi ziku zote zimekuwa za kupotosha kama anavyoeleza Maslov:
Kuwafuta watu waliopita ni kasoro nyingine katika
maandishi yanayohusu historia ya Chama Cha Kikomunisti cha Urusi. Katika
vitabu na makala za utafiti, kama vile ni sheria, watu walio muhimu katika
historia huwa wanaorodheshwa katika katika 'orodha' na baadhi yao hawatajwi
kabisa.328
Historia ya Chama Cha Kikomunisti cha Urusi haina
tofauti na historia ya TANU. Mwaka 1985, Rais Nyerere alipokuwa anamtunukia
digrii ya heshima Basil Davidson, alitoa changamoto kwa Chuo Kikuu Cha
Dar es Salaam kuandika historia ya kweli ya Tanzania. Mwaka 1988, katika
sherehe ya kuadhimisha miaka thelathini ya Azimio la Tabora, Nyerere aliwasifu
wanachama wa mwanzo wa TANU ambao walijiunga na chama kati ya mwaka 1954
na mwaka 1958. Nyerere alisema: 'Hicho kilikuwa kipindi kigumu sana katika
historia ya Chama chetu na ni watu wachache sana walikuwa na ujasiri wa
kujiunga na chama na kukifanyika kazi'. 329 Jambo la kustaajabisha
katika kauli ya Nyerere ni kuwa wakati yeye anawasifu watu waliojiunga
na TANU katika ya mwaka wa 1954 na 1958 yeye binafsi hajawaenzi wale ambao
siyo tu walijiunga na TANU bali ndiyo waasisi wa TANU yenyewe. Kwa hali
hii inakuwa vigumu kuamini kama kauli yake ilikuwa inatoka kwenye dhati
ya nafsi yake.
Katika kuunga mkono kauli ya Nyerere kuhusu kuwakumbuka
mashujaa wa uhuru wa Tanganyika, na kwa kutaka kuitikia ile changamoto
yake ya kutaka historia ya kweli ya TANU iandikwe kama alivyosema mwaka
wa 1974 na 1985, mwandishi wa kitabi hiki alichapisha makala katika Africa
Events 330 ambayo Abdulwahid na wazalendo wengine wa TANU
zilielezwa habari zao. Katika makala yale mwandishi alifanya jambo ambalo
kabla yake lilikuwa halijafanywa na mwandishi yeyote. Mwandishi alisema
kuwa Waislamu ndiyo walikuwa mstari wa mbale katika kupigania uhuru. Wakati
ule ilikuwa mwiko kabisa kunasibisha Uislam au Waislamu na harakati za
kudai uhuru. Mwandishi alipewa kemeo kali kutoka kwa mwanahistoria wa CCM,
Dr Mayanja Kiwanuka,331 kiongozi wa jopo lililoandika Historia
ya Chama Cha TANU 1954-1977, kitabu kinachoeleza historia rasmi ya
Chama. Mwanahistoria wa Chama Cha Mapinduzi alikuwa na haya ya kusema dhidi
ya mwandishi:
"Makala inadai kuwa ingawa Waislam Tanzania walitoa
mchango muhimu katika harakati za kudai uhuru, zipo juhudi za makusudi
za kufifilisha mchango wao. Kutokana na hayo, makala nzima ina ngano ili
kuipa nguvu fikra zake, zaidi kwa kutaja majina ya wazalendo wa TANU ambao
imetokea kuwa ni Waislam Ukuu wa TANU, na hasa ukuu wa kiongozi-muasisi
wake, Mwalimu Nyerere, ni kuwa, baada ya muda mfupi tu toka kuasisiwa (TANU),
ikaweza kuwaunganisha watu katika vuguvugu la utaifa lenye nguvu, lau kama
watu hao walikuwa tofauti kwa kabila, utamaduni na dini zao Nia ya Said
ni kupandiza chuki, kwa bei yoyote ile, ukweli kwake yeye si kitu muhimu.332
Hizi ndizo fikra za Kiwanuka, ambae aliaminiwa
na CCM kusimamia utafiti na uandishi wa historia mahsusi ya TANU. Kilichomkera
ni kusema kuwa Waislamu ndiyo waliokuwa mstari wa mbele katika kudai uhuru
wa Tanganyika. Kwa ajili ya kuwataja Waislam, makala ya utafiti ikawa sawasawa
na ngano, yaani hadithi. Mwandishi akatuhumiwa kusema uongo. Kiwanuka hakuweza
kuuepuka msimamo wa Chama wa kutia mkazo katika kumsifu mtu mmoja, Nyerere
peke yake katika kuasisi TANU - 'Ukuu wa TANU, na hasa ukuu wa kiongozi-muasisi
wake, Mwalimu Nyerere ' Wakati akiandika maneno haya Kiwanuka alikuwa Katibu
Msaidizi katika Idara ya Propaganda na Uhamasishaji Umma katika Chama Cha
Mapinduzi. Mwandishi alijibu mashambulizi ya Kiwanuka kwa kueleza kuwa
yote aliyoyaandika ni matokeo ya utafiti.333 Kufuatia majibu
haya Kiwanuka aliandika fedhuli kwa kumuita mwandishi 'mwanahistoria asiye
kuwa na kimo' na akamtisha mwandishi kwa kuapa kuwa endapo atajaribu kuibadisha
historia ya Tanzania atamwandama yeye na ndugu zake.334 Baada
ya mjadala huu baina ya mwandishi na Kiwanuka, watu wengi walijitokeza
kumuunga mkono mwandishi na huo ndiyo ukuwa mwisho wa ubishi. Kingine cha
kustaajabisha ni kuwa anaeiweka historia kwa kufanya utafiti na kuiandika
sawa, ndiyo anayetishwa na wale waliopotosha historia wanaachiwa waendelee
kuipotosha historia na kuifanyia fisadi kadri watakavyo. Kiwanuka akiwa
mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, aliandika tasnifu kuhusu uhusiano
wa Waislam na Wakristo Tanzania. Tasnifu hii ni muhimu kwa kila mwanafunzi
wa historia ya uhuru wa Tanzania, hasa miaka kumi ya mwanzo baada ya uhuru.
335
Kutokana na makala za mwandishi zilizokuwa zinaitafsiri
upya historia ya Tanzania kwa kuuweka mbele Uislam kama itikadi ya kupinga
dhulma ya aina yoyote pamoja ukoloni, Fr. Peter Smith, mtaalamu wa uhusiano
kati ya Waislam na Wakristo katika Kanisa Katoliki, katika juhudi za kupinga
ukweli huo, alijibu kwa makala mbili.336 Katika makala moja
alisema:
Kuna historia mpya zinazoandikwa hivi sasa zinazojaribu
kuonyesha kuwa vuguvugu la mwanzo kuiunga mkono TANU lilikuwa vuguvugu
la Kiislam. Ukweli ni kuwa Waislam walihusika, halikadhalika Wakristo
vuguvugu lilikuwa la utaifa, ingawa halikuwa la kupinga dini, lilikuwa
ni vuguvugu la kisekula.337 (tafsiri yangu).
Father Smith wa Kanisa Katoliki na CCM inaelekea
wote wana mawazo sawa katika utata huu wa historia ya Waislam na uhuru
wa Tanganyika.338 Wote wawili, Kiwanuka, mwanahistoria wa CCM
na Padri Smith, mtaalamu wa Uislam katika Kanisa Katoliki wanatoa mawazo
yao binafsi. Hawaangalii historia unadhihirisha ukweli gani. Hakuna anaekataa
kuwa Wakristo walikuwepo. Ukweli ni kuwa majina ya Kikristo yapo katika
historia ya uhuru wa Tanganyika. Lakini walikuwa ni wachezaji wa pembeni
si katikati ya jukwaa. Kitabu hiki kimeonyesha nafasi ya Waislam na Uislam
katika kupambana na ukoloni, mchango wao katika kuunda TANU, kukipa chama
wanachama na katika kuutumia Uislam wenyewe kama itikadi ya mapambano.
Baraza la Wazee wa TANU Jimbo la Dar es Salaam chini ya mwenyekiti wake
wa kwanza Sheikh Suleiman Takadir lilikuwa na wajumbe mia mmoja na sabini
na tatu, wote Waislam.339
Kutokana na Kiwanuka, mwandishi katika kumbukumbu
ya miaka ishirini toka Abdulwahid afariki dunia, aliamua kuandika historia
fupi ya maisha yake.340 Abdulwahid ili kukomesha upinzani wote
kwa wakati ule na hapo baadae kuhusu nafasi ya Abdulwahid katika kuasisi
TANU na kudai uhuru wa Tanganyika. Makala hii ilifuatiwa na kumbukumbu
iliyotolewa na watoto wake katika gazeti la CCM - Uhuru, na gazeti
la serikali Daily News. 341 Wahariri wa magazeti
ya Chama na serikali waliposoma wasifu wa Abdulwahid tayari wakawa wameshatatizwa
na habari zilizokuwa katika kumbukumbu ile. Tatizo kubwa lilikuwa habari
zilizoandikwa katika kumbukumbu ile zilizokuwa zinahusisha jina la Abdulwahid
na matukio muhimu katika historia ya Tanganyika. Mhariri wa Daily News,
Reginald Mhango, alimpigia simu mtoto wa Abdulwahid, Kleist na kumweleza
kuwa hatoweza kuchapisha kumbukumbu ile hadi amepata idhini kutoka Dodoma,
Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi. Hakijulikani kilichofanyika lakini
kwa bahati nzuri kumbukumbu zote mbili zilichapishwa na kutokea katika
magazeti yote, ya chama na serikali siku ya pili yake.
Mwaka a 1986, miaka miwili kabla, baada ya takriban
miaka ishirini na tano ya ukimya, Ally Sykes alikubali kufanya majadiliano
na mwandishi wa Kiingereza Paula Park. Park akachapisha majadiliano aliyofanya
na Ally Sykes kuhusu ukoo wa Sykes na mchango wao katika historia ya uhuru
wa Tanganyika.342 Makala ile iliposomwa Ally Sykes akawa anapata
simu kutoka kwa marafiki zake na kwa wafanyabiashara wenzake wakitaka uhakika
kama yale yaliyoandikwa katika gazeti lile kweli yeye ameyasema. Haukupita
muda mrefu, maofisa wa Idara ya Uhamiaji walimtembelea Park na kumuomba
aondoke nchini.
Hivi ndivyo mambo yalivyo na mwandishi amekuwa
akiulizwa maswali mengi na watu mbalimbali kuhusu ukweli ya yale aliyokuwa
akiyaandika katika mchango wa Abdulwahid katika uhuru wa Tanganyika. Wasiwasi
huu umekuwapo lau kama mwandishi amefanya rejea nyingi na za kutosha kutoka
magazeti ya zamani, vitabu,majarida na kumbukumbu zingine za wakati wa
ukoloni. Juu ya wasiwasi wote uliokuwapo hakuthubutu kujitokeza yeyote
kupinga yake mwandishi aliyoandika kuhusu historia ya Abdulwahid katika
TANU na uhuru wa Tanganyika. Hata mwanahistoria wa CCM hakunyanyua kalamu
yake. Hali hii ya CCM kuikataa historia yake na wakati huo huo ikidai kuwa
haijaweza kuihifadhi historia yake inatoa mvuto fulani kwa watafiti kutaka
kujua kulikoni. Ukweli wa kuwa CCM imeandika historia yake lakini hapo
hapo imeonekana upo upungufu mkubwa unaweka wazi suala la utafiti ufanywe
na watafiti huru ili ukweli upate kujitokeza. Somo la historia ya uhuru
wa Tanganyika bado lipo wazi kwa utafiti zaidi.
Ni kitu gani kimesababisha haya yote. Huu ukweli
unafichwa ni mpango maalum wa viongozi walioingia TANU katika siku zamwisho
za mapambano kuanzia mwaka 1958 baada ya Mkutano wa Tabora ? Kwa nini jina
la Abdulwahid na majina ya wazalendo wengine yamefutwa katika historia?
Hao wanaofanya hivi wanataka wapate nini na kwa manufaa ya nani? Unapoingia
mlango mkuu wa Makao Makuu ya CCM Dodoma huwezi kukosa kuiona picha kubwa
sana iliyotundikwa juu ya ukuta ikitazama mlango. Picha hii ni ile picha
ya waaasisi wa TANU iliyopigwa tarehe 7 Julai, 1954 na mpiga picha maarufu
wa wakati ule Gomez. Abdulwahid anaonekana akiwa amevaa miwani ya jua akiwa
amesimama kushoto kwa Dossa Aziz; wote wamevaa suti na tai. Abdulwahid
anaiangalia kamera. Rais mstaafu Julius Kambarage Nyerere amevaa kaptura
na soksi ndefu hadi magotini amekalia benchi mkono wa kushoto wa John Rupia.
Aliyesimama nyuma ya Nyerere, Saadani Abdu Kandoro. Picha hii ndiyo kumbukumbu
ya Abdulwahid iliyobaki katika Chama. Jina lake litaandikwa katika orodha
ya jumla pale inapobidi kuorodheshwa majina ya wale waasisi kumi na saba
wa TANU.
Haiwezekani kabisa mtafiti akafanya utafiti kuhusu
TANU na asimtaje Abduwahid. Haiwezekani kabisa akatajwa Abdulwahid na ikaachwa
kutajwa Al Jamiatul Islamiyya. Haiwezekani kabisa ikatajwa Al Jamiatul
Islamiyya na ikaachwa kutajwa TANU na kinyume chake ni hivyo hivyo. Haiwezekani
akasifiwa Abdulwahid kwa yale yote aliyoifanyia nchi yake na baba yake
asitajwe pamojanae. Hakuna mtafiti yeyote atakaeweza kuandika maisha ya
Nyerere na akaacha kumtaja Abdulwahid na wale waliokuwanao wakati ule na
jinsi walivyomsaidia kufika pale alipofika. Wengi wanahofu kuwa katika
kufanya hivyo ni sawa na kutonesha kidonda kutoka kwa jamii ya Waislam.
Ingawa Waislam ndiyo walioleta uhuru wa Tanganyika, manufaa ya uhuru ni
madogo sana kwao. Ni vyema kama simanzi katika kumbukizi hizi zikabaki
zimesahaulika. Njia iliyobaki kuziacha ziwe zimesahaulika ni kujaribu kufuta
historia ya uhuru wa Tanganyika.
No comments:
Post a Comment