Enyi watu, Mcheni Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na mjuwe ya
kuwa hakika Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) huumba atakavyo na
huchagua atakavyo. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى: (وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَيَخْتَارُ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ(
{{Na Mola wako huumba atakavyo na huchagua atakavyo, hawana viumbe
hiari}}.. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ndie anaye jua hekima
kwa kila kitu anacho kichagua miongoni mwa viumbe vyake. Mwenyezi Mungu
(Subhaanahu wa Taala) huchagua Mitume miongoni mwa Malaika na watu. Na
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ameufadhilsha Mji wa Makka kushinda
sehemu nyingine. Na akauchagua Mji wa Madina kuwa ni mji aliohamia
Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na Masahaba. Kisha akauchagua
Baytul Maqdis akajalia ni sehemu ya Mitume wengi ambayo Mwenyezi Mungu
(Subhaanahu wa Taala) ametuelezea habari zao katika Qur’an Tukufu. Na
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) amefadhilisha baadhi ya Miezi
kuliko mingine na Usiku na Mchana. Akachagua Miezi mine Mitukufu
(Dhul-qa’ada, Dhul-hijja, Muharam na Rajab). Na bora wa masiku ni siku
ya Ijumaa. Kwa hivyo, mtukuzeni Allah (Subhaanahu wa Taala) na kumsifu
na kumsalia Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).
Hukumu ya Swala ya Ijumaa
Swala ya Ijumaa ni miongoni mwa swala muhimu za faradhi. Na sharia
imetia mkazo zaidi na kusisitiza kutekelezwa swala ya ijumaa kwa jamaa.
Na malipo yake ni makubwa zaidi.
Fadhila za siku ya Ijumaa:
Kupata Thawabu na Malipo kwa kila hatua ya kwenda Msikitini sawa na
Mtu aliyesimama kuswali na kufunga Mwaka mzima. Amesema Mtume (Swalla
Llahu ‘alayhi wasallam) : [ Mwenye kuoga na kujisafisha, kisha akaenda
Msikitini na mapema na akamkurubia Khatibu na akasikiliza kwa utulivu.
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) atamlipa kwa kila hatua malipo sawa
na Mtu aliyesimama kuswali na kufunga Mwaka mzima] (Imepokewa na
Ahmed).
Kusamehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu za ziada.
Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [ Mwenye kutawadha
vizuri, kisha akaja Msikitini na akamsikiliza Khatibu na kunyamaza.
Anasemehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu]. Imepokewa
na Muslim.
Kukubaliwa dua katika siku hii tukufu. Amesema Mtume (Swalla Llahu
‘alayhi wasallam) : [Hakika katika Siku ya Ijumaa kuna wakati, haafikiwi
Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah, ila Mwenyezi Mungi
humkubalia Dua yake].
Adabu na Sunna za Siku ya Ijumaa:
Kuoga na kujisafisha na kupaka manukato mazuri pamoja na kuondosha
harufu mbaya mwilini.. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) :
[Mwenye kuoga siku ya Ijumaa, kisha akaenda Msikitini na mapema. Mfano
wake ni kama mtu aliyetowa sadaka ya Ngamia].
Kwenda Msikitini mapema na kumkurubia khatibu. Amesema Mtume (Swalla
Llahu ‘alayhi wasallam) : [Nedeni mkasali sala ya Ijumaa, na mkae karibu
na khatibu].
Kujishughulisha kwa Kumtaja Allah, kusoma Qur’an, kuomba msamaha,
kuomba dua kwa wingi na kumsalia Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam).
Kumsilikiza Khatibu kwa utulivu, bila ya kujishughulisha na mambo
mengine. Asema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Mwenye kutawadha
vizuri, kisha akaja Msikitini na akamsikiliza Khatibu na kunyamaza.
Anasemehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu]. Imepokewa
na Muslim.
Mambo yalio katazwa katika swala ya Ijumaa:
Kuja Msikitini kuchelewa na kukata safu kwa kuruka watu, kwa lengo la
kutaka kukaa safu ya mbele. Siku moja Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam) alimuona mtu akikata safu na kuruka watu; Akamuambia kaa
chini kwa hakika umewaudhi watu na umefanya maasi makubwa.
Kuwashawishi waja wa Mwenyezi Mungu, kwa kusoma Qur’an kwa sauti
kubwa, au kufanya Dhikri kwa sauti ya juu. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam) aliwakataza Masahaba kusoma kwa sauti ya juu, na akawambia;
Asisome mmoja wenu Qura’n kwa sauti ya juu kuliko mwingine.
Kuzungumza wakati wa Khatibu anatoa khutbah ya Ijumaa. Amesema Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Ukimuambia mwenzako nyamaza na
Khatibu akiwa anazungumza, kwa hakika umeharibu swala ya Ijumaa].
Khatari ya kuacha kuswali swala ya Ijumaa
Mtume Muhammad amesisitiza na kutilia mkazo juu la suala la
kutekeleza swala ya Ijumaa. Na akawatahadharisha Waislamu wanaoacha
kutekeleza swala hii. Adhabu kubwa watakayo pata watu hao hapa duniani
ni nyoyo zao kuwa ngumu na kupigwa muhuri wa kughafilika. Amesema Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Hawataendelea watu kuacha swala ya
Ijumaa, mpaka Mwenyezi Mungu apige muhuri nyoyo zao, kisha watakuwa
niwenye kuishi katika mughafala].
Ndugu Waislamu, tujihadhari sana na kuacha swala ya Ijumaa,
kwasababu adhabu yake ni nzito sana. Moyo ukiwa mgumu, basi mwanadamu
anakuwa sawa na myama, hajali lolote wala chochote. Utamuona hamuogopi
Mwenyezi Mungu, kwa kufanya maasi usiku na mchana.
Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Taala) athibitishe nyoyo zetu juu ya twaa yake, na atulinde na machafu yote.
Ndugu Waislamu, katika Mafundisho ya Mtume Muhammad (Swalla Llahu
‘alayhi wasallam) ni kuitukuza siku hii ya Ijumaa, kwani hii ni siku
tukufu ilio chaguliwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na
kupatiwa Umma huu wa mwisho.
Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikhusisha baadhi ya vitendo katika siku ya Ijumaa:
Kusoma Surat Sijdah na Surat Insaan katika swala ya Al-Fajiri.
Imepokewa na Abu Hureirah – Radhi za Allah ziwe juu yake- {Alikuwa Mtume
akisoma katika swala ya Al-Fajri siku ya Ijumaa (Surat Sijdah) katika
rakaa ya kwanza. Na katika rakaa ya pili (Surat Insaan)} Muslim.
Kusoma Surat Al-Kahfi. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam):
{Mwenye kusoma Surat Al-Kahfi siku ya Ijumaa, Mwenyezi Mungu anampa
mwangaza baina ya Ijumaa mpaka Ijumaa nyingine}. Al-Bayhaqi na Haakim.
Kuzidisha kwa wingi kumsalia Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam). Amesema Ibnu-Qayyim: “Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Bwana wa
viumbe vyote, na siku ya Ijumaa ni bwana wa siku zote. Kumswalia Mtume
siku hii ina malipo mengi kushinda siku nyingine”.
Kuzidisha kumuomba Allah (Subhaanahu wa Taala) katika siku hii.
Kwasababu kuna wakati wa kukubaliwa dua ya Muislamu. Amesema Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Hakika katika Siku ya Ijumaa kuna
wakati, haafikiwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah, ila
Mwenyezi Mungu humkubalia Dua yake].
Mwisho
Ndugu katika Imani, kama tulivyo sikia umuhimu wa siku ya Ijumaa, na
namna sheria ilivyo tilia mkazo siku hii. Na vilivile malipo na
thawaabu nyingi kwa Yule atakae tekeleza ibada kwa masharti yake na
nguzo zake. Ni jukumu letu kufanya bidii kwa kufanya ibada mbali mabali
kama alivyo tufundisha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), ili tuweze
kupata malipo na thawabu nyingi kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Taala).
Enyi Waislamu, Tushindaneni kufuata Sunna na Mafundisho ya Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika siku hii kuu.
Mwenyezi Mungu atujaalie miongoni mwa waja wake wema na atupe uwezo
wa kufuata Sunna za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Tunamuomba
Allah atukubalie ibada zetu na atupe mwisho mwema tukiondoka duniani.
No comments:
Post a Comment