Wednesday, 17 June 2015

Tafsiyr Ya Imaam As-Sa'dy: Enyi Mlioamini! Mmeandikiwa Swawm Kama Ilivyoandikwa Kwa Wale Ambao Wa Kabla Yenu Mpate Kuwa Na Taqwa

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾
Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm kama ilivyoandikwa kwa wale ambao wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa (Al-Baqarah: 183)

Allaah Anajulisha katika Aliyoyafadhilisha kwa waja Wake kwamba Amewajibisha Swawm kama Alivyowajibisha ummah zilizopita kwa sababu ni shariy’ah (hukmu) na amri zinazomnufaisha binaadamu katika kila zama.
Nayo ni changamoto ya kumhuisha mtu nafsi yake kwani inapasa kushindana na wengine katika mambo ya kheri ili mkamilishe amali zenu na mkimbilie (kuchuma) sifa njema na hakika hayo si katika mambo mazito mliyohusishwa nayo.

Kisha Allaah Anataja hikma Yake kuhusu Shariy’ah ya Swawm ndipo Anasema:

لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
mpate kuwa na taqwa

kwamba Swawm ni sababu kuu ya taqwa (kumcha Allaah) kwa kuwa ni kutekeleza amri za Allaah na kujiepusha na yaliyokatazwa.

Kwa hiyo katika Swawm yanapatikana:

1.   Taqwa ya asw-swaaim (anayefunga swawm) huacha yote Aliyoyakataza Allaah; kula, kunywa, kujimai na kama hayo, na yote yanayoelemea nafsi yake kuyatamani; hapo basi hujikurubisha kwa Allaah kwayo akitaraji thawabu kwa kujiepusha nayo. Haya yote ni kutokana na taqwa. 

2.   Na Swawm pia inamfunza mtu kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) basi hujiepusha na hawaa ya nafsi yake, kwa (kutegemea) Uwezo Wake (Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kuwa anatambua kwamba Allaah Anamuona (ayatendayo yote).

3.   Swawm pia inamzuia mtu na shaytwaan kwani hakika shaytwaan anatembea katika mishipa ya damu ya mwanaadamu. Kwa hiyo Swawm inamvunja nguvu shaytwaan (na uchochezi wake), hivyo madhambi hupunguka. 

4.   Swawm pia humfanya mtu azidishe utiifu na utiifu ni katika sifa za taqwa.

5.   Swawm pia inamfanya tajiri anaposhikwa na njaa inayombidi imshike (kwa kuwa ni fardhi kwake, huwafikiria na) huwahurumia  masikini na mafuqara na hii ni miongoni mwa sifa za taqwa.  

TAQABBALA ALLAAHU MINNAA WA MINKUM - FAIDA MBALIMBALI ZA RAMADHWAAN


Assalaamu 'alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh,
ALHIDAAYA inawaombea Ramadhwaan ya kheri na Baraka nyingi, mchume thawabu tele, Swawm zikubaliwe, dhambi zighufuriwe, na Allaah Atutakabalie 'amali zetu.  
Tusiache kuwaombea du’aa ndugu zetu Waislam popote walipo ulimwenguni walio katika dhiki za ukandamizwaji, vita, njaa na machafuko. Na pia tukumbukane kwa du’aa kwani Mtume Swalla-Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam amesema katika Hadiyth kutoka kwa Ummu Dardaa Radhwiya-Allaahu ‘anhaa: ((Atakayemuombea ndugu yake kwa siri Malaika aliyewakilishwa kwake husema: “Aamiyn nawe pia upate mfano wake)) (wa kama unayomuombea) [Muslim] 
Kwa Munaasabah wa mwezi mtukufu wa Ramadhwaan, Alhidaaya imewaekea tayari mafundisho mbalimbali yenye manufaa katika kuongeza elimu na kuimarisha 'ibaadah zenu ili muweze kuchuma mema mengi na muweze kufikia kuipata taqwaa ambayo ndio lengo kuu la Swawm.