A / Alaikum brother Muslim men and women either after greetings are you ignorant of blogs this is Islam referencing everything apply Islam and Muslims problems all questions feedback analysis of various topics and highlights from our religion of Islam but God is the one most skillful Insha'llah to comment questions do not hesitate to write abdulmohamedy23@gmail.com or +255762084268 inshallah
Thursday, 30 December 2021
HAYA NDIO MAISHA YA MUISLAMU WA KWELI.
1. TUZUNGUMZE KIISLAM
Muislam wa kweli ni lazima awe ni mkweli, hatakiwi kuzua uongo, kufitinisha, kusengenya wala kuzungumza kwa sauti ya juu. Haya tunayapata ndani ya Qur-aan:
{{Na uteremshe sauti yako; bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote (kwa makelele yake ya bure).}}
[Surat Luqmaan: 19]
Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kushikamana katika kusema ukweli:
“Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli unapeleka katika wema, na wema unapeleka Peponi.”
[Muslim]
*2. TULE KIISLAM*
Muislam anatakiwa ale kilicho mbele yake kwa kutumia mkono wa kulia na asiwe na papara ya kusukuma tonge namna ya kima anavyokula. Aanze kula kwa kusema “BismiLlaah” na amalize kwa kusema “AlhamduliLlaahilladhi atwa'amani haadha ttwa'am warazaqanihi min ghairi hauli minni walaquwwa”.
Chakula cha Muislam ni lazima kiwe ni cha halali, hatakiwi kula ovyo ovyo kama wanavyofanya wasiokuwa Waislam. Anapokula aligawe tumbo lake kwenye thuluthi tatu. Thuluthi moja ni ya chakula, nyengine ni ya maji na mwisho ni hewa. Hii ni kwa mujibu wa dalili ya Hadityh:
"Kama ukilazimika kula hakikisha theluthi moja ya tumbo lako unaijaza chakula, theluthi moja maji na acha theluthi moja kwa ajili ya hewa (yaani iache tupu)” (At-Tirmidhiy).
*3. TUSIKILIZE KIISLAMU*
Muziki ni haramu na haifai kwa Muislam kuutengeneza, kutengenezewa, kuimba, kuimbiwa, kuutangaza, kuupeleka muziki, kuuza, kula thamani yake, kununua na kuuza.
Muziki umekuwa ni tatizo kubwa kwa Waislam kwani wengine hata usingizi hawapati bila ya kusikiliza muziki. Nyumba za Kiislam sasa zimekuwa sawa na magofu kwa kutopatikana maadili ya Kiislam. Kwani wengi wanaishi tofauti na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni muhimu kwa Waislam wakawa wanasoma Qur-aan kila siku kwa sauti na kwa kusikilizana kwa mtindo wa dawaar (mmoja baada ya mwengine). Tuzibadilishe nyumba zetu kwa kusikiliza idhaa za Kiislam zisizokuwa na mambo ya uchafu na uzushi.
{{Na soma Qur-aan kwa utaratibu na utungo.}}
[Al-Muzammil 73: 4]
Muislam anayesoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam). Hata yule asiyejua kusoma Qur-aan ni vyema akawa na jitihada ya kujifundisha ilhali anakosea au hata kuchekwa. Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Yule ambaye kwamba anasoma Qur-aan naye ni mjuzi (hana shida aina yoyote) atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam) na watiifu. Na yule ambaye kwamba anarudia pamoja na kuwa na shida katika kusoma basi atakuwa na ujira mara mbili )) [al-Bukhaariy, Muslim, Tirmidhy na Ibn Maajah kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha)]
*4. TUVAE NA TUTEMBEE KIISLAM*
Maringo ya kutembea bila ya shaka yanatokana na mtu kuvaa nguo za kifakhari ambazo hazitakiwi kuvaliwa kwa Muislam. Muislam wa kiume anatakiwa avae nguo zisizoburura. Mwanamke hatakiwi kuonekana zaidi ya viganja vya mikono na kipaji cha sura yake. Mapambo yote ni halali kwa mumewe na walio Maharimu wake. Haitakikani Muislam kutembea kwa kujivuna, kujifakharisha na maringo. Hivi sivyo Uislam unavyotufundisha kuishi. Qur-aan inasema:
{{Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala huwezi kufikia urefu wa milima}}
[Surat Israa: 37]
Usiwaangalie watu kwa jeuri au kwa upande mmoja wa uso. Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
{{Wala usiwatazame (usiwafanyie watu jeuri), kwa upande mmoja wa uso, wala usende katika ardhi kwa maringo, hakika Allaah hampendi kila ajivunaye, ajifaharishaye.}}
[Surat Luqmaan:18]
*5. TUJENGE URAFIKI WA KIISLAM*
Miongoni mwa matatizo makubwa ya vijana wetu pamoja na Waislam kukosa maadili ya Kiislam ni kuwa na marafiki wasiokuwa na maadili mema. Ni vyema Muislam akawa hana rafiki hata mmoja kuliko kuwa na marafiki kumi wasioishi Kiislam. Kuishi Kiislam yatakikana juhudi na inaanza kwa kuwa na rafiki mwema atakayekukemea unapofanya kosa na kukupa maneno ya subra wakati wa huzuni.
Lazima tuchague marafiki ambao wako radhi na dini yetu na tuepukane na wale ambao hawako radhi na dini yetu. Na tukiona marafiki zetu matendo yao sio mazuri, ni lazima tuepukane nao kwa sababu tunaweza tukaiga tabia zao ambazo zinakwenda kinyume na diyn yetu.
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Mtu yamkini kufuata dini ya rafiki yake, kwa hivyo muangalie unayemfanya rafiki.” (Abuu Daawuud na At-Tirmidhiy)
*6. TULALE KIISLAM*
Tumalizie kwa kuona namna anavyotakiwa Muislam kuimaliza siku yake kwa kujipumzisha Kiislam. Muislam anatakiwa atie wudhuu kabla ya kulala, wudhuu unaendana na Sunnah ya kupiga mswaki. Ni vizuri ukaswali rakaa tatu za witri (kwa wasioamka usiku).
Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akienda kulala usiku anakusanya viganja vyake kisha akivipuliza na akivisomea Suratul-Ikhlaas, na Suratul-Falaq, na Suratun-Naas, kisha akipangusa kwa hivyo viganja vyake kiasi anachoweza katika mwili wake, akianza kichwani na usoni na mbele (akifanya hivyo mara tatu).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Ukienda kulala soma Ayatul-Kursiy mpaka uimalize kwani Allaah Ataendelea
kukuhifadhi wala hakukaribii shaytwaan mpaka asubuhi”
Unapolala ulaze ubavu kwa upande wa kulia na usome du’aa ifuatayo:
ﺍﻟﻠّﻬُـﻢَّ ﺃَﺳْـﻠَﻤْﺖُ ﻧَﻔْـﺴﻲ ﺇِﻟَـﻴْﻚَ، ﻭَﻓَﻮَّﺿْـﺖُ ﺃَﻣْـﺮﻱ ﺇِﻟَـﻴْﻚَ، ﻭَﻭَﺟَّـﻬْﺖُ ﻭﺍ ﺟْـﻬﻲ ﺇِﻟَـﻴْﻚَ، ﻭَﺃَﻟْـﺠَـﺎْﺕُ ﻇَﻬـﺮﻱ ﺇِﻟَـﻴْﻚَ، ﺭَﻏْﺒَـﺔً ﻭَﺭَﻫْـﺒَﺔً ﺇِﻟَـﻴْﻚَ، ﻻ ﻣَﻠْﺠَـﺄَ ﻭَﻻ ﻣَﻨْـﺠـﺎ ﻣِﻨْـﻚَ ﺇِﻻّ ﺇِﻟَـﻴْﻚَ، ﺁﻣَﻨْـﺖُ ﺑِﻜِﺘـﺎﺑِﻚَ ﺍﻟّـﺬﻱ ﺃَﻧْﺰَﻟْـﺖَ ﻭَﺑِﻨَﺒِـﻴِّـﻚَ ﺍﻟّـﺬﻱ ﺃَﺭْﺳَﻠْـﺖ
“Ewe Allaah nimeisalimisha nafsi yangu kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu kwako na nimeutegemeza mgongo wangu kwako, kwa matarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila kwako, nimekiamini kitabu chako ulichokiteremsha na Mtume wako uliyemtuma”.
Na hizi hapa ni Nyiradi za kulala.
Bila ya shaka tutakapoishi Kiislam tutakuwa mbali na wasiokuwa Waislam. Hivyo maisha yetu yatakuwa hakika ni ya Kiislam. Kila kitu yatakikana juhudi na inaanza kwa nafsi kujifunga kukubali mafundisho ya Kiislam.
Inawezekana kubadilika kwa kuishi Kiislam. Anza sasa, katu usichelewe.
**** Jiunge nasi katika Ukurasa wetu wa Uislamu Dini Yangu kwa Kubonyeza kitufe cha "Like" uwe mmoja wa ndugu walio katika ukurasa huu...
Subscribe to:
Posts (Atom)