Wednesday, 29 July 2015

Yajue Mambo Anayopaswa Kufanyiwa Mtu Akifariki


Yampasa Muislam ajiandae kufikiwa na mauti kwa kukithirisha (kufanya sana) matendo mema na kujiepusha na makatazo (vilivyoharamishwa). Vilevile mauti yawe akilini mwake, kwa maneno ya Mtume صلي الله عليه وآله وسلم:
“Zidisheni kukumbuka kiondoshacho ladha (yaani mauti)”. Hadiyth hii imepokewa na Imaam at-Tirmidhiy na akaithibitisha usahihi wake Imaam al-Albaaniy katika kitabu chake Irwaaul-Ghaliyl uk. 682.

Anapofariki Muislam yampasa yule au wale waliopo pale karibu na maiti kumfanyia mambo yafuatayo:
1.     Kuyafumba macho ya maiti huyo kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliyafumba macho ya Abu Salamah alipofariki kisha akasema: “Hakika macho yanafuata roho inapotolewa”. Imesimuliwa na Imaam Muslim.

2.     Avilainishe viungo vya maiti ili visikakamae.

3.     Aifunike maiti hiyo kwa nguo ambayo itasitiri mwili mzima kwa kauli ya mama wa waumini ‘Aaishah:“Hakika alipofariki Mtume صلي الله عليه وآله وسلم alifunikwa kwa nguo iliyomsitiri kote.” Imesimuliwa na Imaam al-Bukhaariy na Imaam Muslim.

4.     Waharakishe kuiandaa maiti, kuiosha, kuikafini, kuiswalia na kuizika. Kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم amesema: “Liharakisheni jeneza…” Imesimuliwa na Imaam al-Bukhaariy na Imaam Muslim.

5.     Waizike katika mji au eneo alilofia kwa vile katika vita vya Uhud “Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliamrisha mashahidi wa vita wazikwe pahala pale walipofia wala wasihamishwe”. Imepokewa na Ahlus Sunan (Ma-Imaam Abu Daawuud, an-Nasaaiy, at-Tirmidhiy, Ibnu Maajah) na ameithibitisha usahihi wa Hadiyth hiyo Imaam al-Albaaniy katika kitabu chake cha Ahkaamul Janaaiz uk. 14.
 

No comments: