Mola
wetu Mtukufu Amemuumba mwanaadamu katika umbo bora lisilomithilika na
kiumbe chochote. Naye ameumbwa kwa kutumia udongo uliopulizwa roho
itokayo kwa Mola Mlezi.
Akamjaalia
mwanaadamu ni mwenye kupata shida, mitihani, mtenda dhambi na mwenye
kupata maradhi. Hakusita hapo Mola wetu Mtukufu, bali Akajaalia mlango
wa pili wa kutokea kwenye mashaka ya dunia; Akajaalia kuwepo starehe,
utulivu, toba na afya. Basi ni kwa neema zipi mwanaadamu anaweza kumlipa
Mola wake!?
Tutambue
kwamba hii roho tuliyokuwa nayo yatosha kuwa ni sababu ya kushukuru
neema za Mola Mlezi kwa vitendo na kauli. Tusisahau wapi tulipotoka na
wapi tunaelekea, hatukuwa chochote miaka 100 iliyopita. Basi ni nani
kati yetu alikuwa na uhakika kwamba atadhihiri duniani kwa jina na umbo
lake kabla ya kuzaliwa? Kuwa na adabu kwa kumcha Mola wako!
Muislamu
yupo juu ya mgongo wa ardhi akiruzukiwa kila chenye manufaa na yeye, ni
mwenye kula akapata njia ya kutolea uchafu, na siku uchafu unaposhindwa
kutoka ndani ya tumbo ndio unaelewa umuhimu wa neema ya kuyeyusha
chakula kwenye mwili. Ameumba kila kitu kwenye kiwango maalumu, kwani
tumbo likiyeyusha kupita kiwango, mwanaadamu ataugua maradhi ya tumbo la
kumuendesha. Hivyo, kumbuka na yazingatie maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{Na mkihesabu neema za Allaah hamtaweza kupata idadi yake. Hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.}} [An-Nahl: 18]
Basi
elewa ndugu yangu, kwamba sisi si chochote si lolote zaidi ya tone la
manii lililoengwa engwa hadi likafikia miezi tisa likaweza kutoka kwa
sura ya mwanaadamu. Ndani ya tumbo, Mola wetu Mlezi Alitulinda na wala
hatukuhitaji askari, jeshi, polisi, ultimate security au mwengineye.
Ukatoka kwa ukenya wa kilio cha juu ukiomba msaada kwa mama yako.
Ukafikia baleghe ukaweza kuoa/kuolewa na sasa kwa Qadar ya Mola unaweza
nawe kupata mtoto. Aliyekuwa mbabe kati yetu azihesabu neema ngapi
zimepita baina ya kuzaliwa kwake hadi hivi sasa, kisha aangalie ni kwa
kiwango gani ataweza kuzishukuru neema hizo. SubhaanaLlaah! Yuko umbali
gani mwanaadamu kwa kuzitilia maanani neema za Mola wake?
Ugeuze
uso wako, uangalie mbingu ilivyotanda na ardhi ilivyotandikwa, kisha
useme kwamba Mola wako amekutupa. Rizki zako Akazimimina kutoka mbinguni
na Akazichimbua kutoka ardhini. Ni kipi basi katika chakula chako
kitokacho nje ya mfumo huu? Basi kwa Kiburi Chake Mola Mlezi Anastahiki
kuyaambia makundi ya wanaadamu na majini:
{{Enyi
jamii ya majini na watu! Kama mtaweza kupenya katika mbingu na ardhi
(ili mkimbie Nisikupateni), basi penyeni (Nikuoneni)! Hamtapenya ila kwa
nguvu (Zangu. Nikikupeni nguvu hizo mtaweza).}} [Ar-Rahmaan: 33]
Tumcheni
Mola wetu kwa kila kitu, kwa dogo na kubwa, kwa tunayoyajua na
tusiyoyajua. Tutende mema kabla ya kutufika yale yasiyoweza kuhimili
miili yetu. Wahenga wanatuambia: "Kijua ndi hichi usipouanika utaula
mbichi."