Toa Swadaqah Kwa Ajili Ya Allaah
Naaswir Haamid
Ihsaan
ni kinyume cha ufisadi, na miongoni mwa Ihsaan ni kufanya wema bila ya
kujali mipaka ya Kaskazi wala Kusi, na kutoa kwa ajili ya Allaah ni wema
na Ihsaan kwa mwanaadamu.
Hakuna
shaka yoyote kwamba Swadaqah ni katika tabia njema, na iwapo tutafungua
kurasa za Siyrah za wema waliotangulia, tutaona kwamba walikuwa
wakikithiri mno kwenye kutoa Swadaqah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Anasema:
{{Chukua Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao).}} [At-Tawbah: 103]
Kupitia
Tamko hilo hapo juu, tunafahamu kwamba kumbe kuisafisha nafsi kutokana
na takataka za upungufu na kuiinua jamii mpaka kuifikisha kwenye daraja
tukufu kabisa, ndio hekima ya juu. Ni kwa ajili hii ndio Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanua wigo katika kuelezea maana
ya neno “Swadaqah” ambayo Muislamu anatakiwa kuitoa, akasema:
((Tabasamu
lako usoni kwa nduguyo (Muislamu mwenzio) ni Swadaqah, kuamrisha kwako
mema na kukataza kwako maovu ni Swadaqah. Na kumuongoza kwako njia mtu
katika ardhi (nchi) ya upotevu, hilo kwako ni Swadaqah. Na kuondosha
kwako njiani udhia, mwiba na mfupa, hilo kwako (nalo) ni Swadaqah. Na
kumtekea kwako maji nduguyo, kwako ni Swadaqah na kumsaidia kwako mtu
dhaifu wa uoni kuongoza njia, (hilo nalo) kwako ni Swadaqah)). [Al-Bukhaariy]
Swadaqah
huanza kwa kuuzoesha mkono kutoa kila mara bila ya kinyongo wala
manuuniko. Mkono una dhima kuu ya kukulingania kutoa Swadaqah katika
vile ulivyoruzukiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama Alivyosema:
{{Yule
anayetoa (Zakaah, Swadaqah na vinginevyo) na kumcha Allaah. Na kusadiki
jambo jema (akalifuata). Tutamsahilishia njia ya kwenda Peponi.}} [Al-Layl: 5-7]
Hiyo
ndio faida na jazaa ya aliyeutumia vyema mkono wake katika kutoa
Swadaqah. Akautumia mkono wake katika kutoa vile Alivyoruzukiwa na
Allaah Ar-Razzaaq, katika kuisadia jamii na kuupeleka mbele Uislamu.
Ni vyema ukakumbuka kwamba kutoa katika mambo ya khayr ni katika kuishukuru neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ambako hakumaanishi ila kuzidishiwa neema, tusome kwa mazingatio:
{{Na
(kumbukeni) Alipotangaza Mola wenu (kuwa): "Kama mkishukuru,
Nitakuzidishieni; na kama mkikufuru, (jueni) kuwa adhabu Yangu ni kali
sana.}} [Ibraahiym: 7]
"Mtenda wema hutendea nafsi yake na mtenda ovu humrejea mwenyewe". Hivyo
elewa kamba kuishukuru neema kikweli kweli na kuitumia vile
inavyostahiki sio tu kusema au kuandika kwenye milango kwa mbwembwe: ‘AlhamduliLlaah’ au ‘Hadha Min Fadhli Rabiy’! Na ni ubaya ulioje kuzitumia neema hizi kinyume na vile Alivyoamrisha Ar-Razzaaq.
No comments:
Post a Comment