Uchungaji
wa viungo vya Muislamu katika maisha haya umekuwa ni wa chini usio na
maana yoyote. Mkono unaiba, mguu unampeleka baa au kuzini, na ulimi
unadiriki kutoa kiapo cha uongo.
Ulimi
ni kiungo kimoja ambacho chatumiwa vibaya mno takriban na wanaadamu
wote, na ndani yake kuna kundi kubwa la Waislamu ambao hawajali yale
yanayotoka ndani ya vinywa vyao.
Tutambue
kwamba, kiapo juu ya viumbe ni haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
kuviapia. Ni kwa mfano pale Anaposema: Ninaapa kwa Siku ya Qiyaamah,
Ninaapa kwa Jua na kadhalika. Mwanaadamu yeyote hana ruhusa ya kutoa
kiapo kama hicho.
Kwa
mujibu wa mafundisho ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) kiapo cha Muislamu kinaelekezwa kwa Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala). Na nini maana ya kiapo? Kiapo ni kuweka dhamana ya lile
unalosema kwa Yule Unayemwapia. Kwamba hayo unayoyaapia ni ya kweli
unahitaji kusadikiwa na wanaadamu wenzio. Basi ole wake yule ambaye
anaweka kwa Muumba wake kiapo cha uongo.
Hivyo,
kiapo ni chenye kuchungwa mno na wala sio kukifanya kuwa ni dhikri ya
ulimi ukataka kila kitu kukifanyia kiapo hadi kuwa ni sababu ya
kutumbukia kwenye dimbwi la moto. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Anatuambia tusimtii yule mwenye kuapa kila wakati:
{{Wala usimtii kila muapaji sana, aliye dhalili.}} [Suratul-Qalam: 10]
Kitu
ambacho kimejaa ndani ya maisha yetu Waislamu ni viapo visivyokuwa na
kichwa wala mguu. Na kila wanapokumbushwa wao wanaufanyia kazi ule
msemo: "Kelele za mlango hazimughasi mwenye nyumba". Wanakuwa hawajali
wala hawakubali maneno ya Qur-aan au Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtume
wetu amekataza mno Muislamu kula kiapo ovyo ovyo. Kinyume chake
Muislamu anakula kiapo cha uongo katika biashara ingawa Mtume wetu
amesema kwamba Allaah Hatamuangalia (kwa jicho la huruma) mtu namna hiyo
Siku ya Qiyaamah. [Imesimuliwa na Abu Dharr na kupokelewa na Muslim].
Lililo
kubwa ndani ya jamii zetu ni kufikishana mbele ya vyombo vya sheria kwa
namna za udanganyifu, utapeli na uongo mtupu. Muislamu anadiriki kuweka
kiapo cha uongo kwa Mola wake ili apate mali ya mwengine bila ya
halali. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesimuliwa
akisema kama ilivyopokewa na Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘Anha):
((Mimi ni binaadamu tu na nyinyi mnaleta migogoro yenu kwangu mimi, mukiwa wenye fasaha katika viapo vyenu kuliko wengine, ili ya kwamba nitoe hukumu kwa niaba yenu kwa mujibu wa ninayoyasikia kutoka kwenu. Hivyo, vyovyote nitakavyoamua kwa yeyote, ambapo kwa haki ni ya ndugu yake, asichukue kwani simpatii chochote ila kipande cha moto.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy].
Tunawanasihi
wale waliochukua viapo vya uongo wakamilikishwa mali kwa njia za haramu
wazirejeshe amana hizo haraka iwezekanavyo. Ya Ar-Rahmaan! Na wapo
miongoni mwa viumbe Vyako waliokula kiapo kwa kudhulumu mayatima na
wakala kiapo kwa lengo la kuzini na wake za watu. Umetakasika! Shingo
zao zipo mikononi Mwako!
Ya
Allaah! Tunategemea kwako, na tunageuka kuja Kwako, na Kwako tu ndiko
marejeo yetu. Basi tunakuomba Mola wetu! Tutimizie nuru yetu, na
Utughufirie, hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
No comments:
Post a Comment