Thursday, 30 October 2014

Mambo Ya Kufanya Siku Ya Ijumaa


Ijumaa hii tunaelezea utukufu wa siku hii kwa kujulisha mambo yanayotupasa kuyafanya yenye fadhila  na thawabu nyingi.

Kukoga (Ghuslu) Ni Wajibu

حديث أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ، عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: الْغُسْلُ يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَاجِبٌ عَلَى كُلِّ مُحْتَلِمٍ ( أخرجه البخاري)   
Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy ambaye alisema: Mtume صلى الله عليه وسلم  kasema  Ghuslu ( kukoga kwa kujitia twahara) siku ya Ijumaa ni wajibu kwa kila Muislamu aliyebaleghe.  [Al-Bukhaariy]

Inapendekezwa kwa kila anayekwenda kuswali kujisafisha, kupiga mswaki, kujitia mafuta mazuri (isipokuwa mwanamke) na kuvaa nguo iliyo nzuri kabisa. Muislamu akitimiza adabu ya Swalah ya Ijumaa hufutiwa madhambi yake ya wiki.

عن سلمان رضي الله عنه قال: قال رسول الله  صلى الله عليه  وسلم  لا يغتسل رجل يوم الجمعة، ويتطهر ما إستطاع من طهر، ويدّهن من دهنه، أو يمس من طيب بيته، ثم يخرج فلا يفرق بين إثنين، ثم يصلي ما كتب له، ثم ينصت إذا تكلم الإمام، إلا غفر له ما بينه وبين الجمعة الأخرى) رواه البخاري(

Kutoka kwa Salmaan رضي الله عنه  ambaye alisema:  Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم "Muislamu atakayekoga (Ghuslu)  siku ya Ijumaa, akajisafisha vizuri awezavyo, akatia rangi (nywele zake) (isiyo nyeusi),  au akajipaka mafuta mazuri  aliyonayo nyumbani kwake, kisha akaenda Msikitini bila ya kufarikisha (kuwapangua akipita) watu wawili (ambao wameshakaa kitako msikitini), akaswali aliyofaridhishwa, kisha akasikiliza  (khutbah) kimya, hufutiwa madhambi yake yaliyo baina ya Ijumaa hiyo na Ijumaa ijayo.  [Al-Bukhaariy na Ahmad]

Swalah Ya Ijumaa 

Allaah سبحانه وتعالى Ametuamrisha kwenda kuswali Swalah ya Ijumaa
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِي لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَى ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi mlioamini! Ikiadhiniwa Swalah siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Allaah, na acheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua” [Al-Jumu’ah 62: 9]

Ni wajibu kwa kila mwanamme Muislamu kwenda kuswali Ijumaa, na hatari ya  kutokwenda kuswali bila ya kuwa na sababu iliyoruhusu shari’ah ni kuwa  Allaah سبحانه وتعالى  humpiga muhuri mtu  moyoni  mwake, kama katika Hadiyth sahihi ifuatayo:

 قال رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: من ترك ثلاث جمع تهاونا طبع الله على قلبه (رواه أحمد وأصحاب السنن،)

Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم : Atakayeacha (kuswali Swalah ya) Ijumaa mara tatu bila ya sababu yeyote, Allaah سبحانه وتعالى humpiga muhuri katika moyo wake.” [Ahmad na wapokezi wa Hadiyth wengine wenye vitabu vya ‘Sunnan’]

Kupigwa muhuri huo inamaanisha kwamba Allaah سبحانه وتعالى Ameshampa chapa huyu mtu kuwa ni 'Aasi na amekwishatumbukia katika makemeo ya Allaah سبحانه وتعالى  kwamba   ni katika walioghafilika  kama alivyotutahadharisha Mtume صلى الله عليه وسلم :

حديث ابن عمر وأبي هريرة رضي الله عنهما المخرج في صحيح مسلم من أنهما سمعا رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول على أعواد منبره: لينتهين أقوام عن ودعهم الجمعات أو ليختمن الله على قلوبهم ثم ليكونن من الغافلين

Kutoka kwa Ibn 'Umar na Abu Hurayrah رضي الله عنهما kwamba wamemsikia Mtume صلى الله عليه وسلم akisema: “Wasiohudhuria  Swalah ya Ijumaa  wabadilishe  mtindo wao huo au sivyo Allaah سبحانه وتعالى Atawapiga mihuri katika nyoyo zao  na watakuwa  miongoni wa walioghafilika.” [Muslim]


Kufika Mapema Msikitini   

Kila atakapofika mtu mapema msikitini huwa amepata daraja Fulani na muhimu kabisa ni kufika kabla ya khutba kuanza, akichelewa mtu kufika akakosa khutba atakuwa amekosa Swala ya Ijumaa

حديث أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، أَنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ ثُمَّ رَاحَ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الرَّابِعَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ دَجَاجَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الْخَامِسَةِ فَكَأَنَّما قَرَّبَ بَيْضَةً، فَإِذَا خَرَجَ الإِمَامُ حَضَرَتِ الْمَلاَئِكَةُ يَسْتَمِعُونَ الذِّكْرَ (أخرجه البخاري )

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye alisema:  Mtume صلى الله عليه وسلم kasema: “Atakayekoga (Ghuslu) siku ya Ijumaa kisha akaenda Msikitini, itakuwa kama mfano ametoa (kafara ya) ngamia. Akienda  saa ya pili yake, itakuwa kama katoa (kafara ya) nġ’ombe.  Akienda saa ya tatu yake, itakuwa kama katoa (kafara ya) kondoo mwenye pembe. Akienda saa ya nne yake, itakuwa kama katoa   kuku. Akienda saa ya tano yake itakuwa kama katoa yai. Imaam akifika, Malaika watatoka kuja kusikiliza dhikr” [Al-Bukhaariy]


Surah Za Kusoma Siku Ya Ijumaa

·         Suratul Kahf

عن أبي سعيد الخدري رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه  وسلم  قال: من قرأ سورة الكهف يوم الجمعة أضاء له من النور ما بين الجمعتين ( رواه الترمذي)
Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy رضي الله عنه ambae alisema: Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم : “Atakayesoma Suratul-Kahf siku ya Ijumaa atakuwa katika mwangaza baina ya Ijumaa mbili.”  [At-Tirmidhiy]

Pamoja na kusemwa kuwa Hadiyth hiyo imetoka kwa Mtume صلى الله عليه وسلم, lakini Wanachuoni wa Hadiyth wengi wamesema ni Hadiyth 'Mawquuf' ambayo haijaelezwa na Mtume bali ni kutoka kwa Maswahaba, na kwa nyongeza ya neno 'atakayeisoma Ijumaa' haikuthibiti kwa Mtume, na maelezo hayo hapo juu ni ya kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy na yeye ndiye aliyekuwa akiisoma Surah hiyo katika siku ya Ijumaa, na Wanachuoni wanasema kuwa maadam Maswahaba walikuwa wakiisoma Surah hiyo siku ya Ijumaa, basi hakuna neno kuisoma Ijumaa, japo kuisoma siku yoyote ni sawa na mtu atapata fadhila zilizotajwa kwenye Hadiyth hiyo. Ama kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وسلم, Wanachuoni wamesema haikuja na lafdhi ya 'kuisoma Ijumaa', bali imekuja kwa ujumla wake wa kuisoma Surah hiyo siku yoyote ile kama ilivyokuja hapa chini:

((وقال صلى الله عليه وسلم : من قرأ سورة الكهف كما أنزلت كانت له نورا يوم القيامة ، من مقامه إلى مكة ، و من قرأ عشر آيات من آخرها ثم خرج الدجال لم يضره ....))  صححه الألباني في سلسلة الأحاديث الصحيح 
((Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم atakayesoma Suratul-Kahf kama ilivyoteremshwa, atakuwa na mwangaza siku ya Qiyaamah pale alipo mpaka Makkah, na atakayesoma Aya kumi za mwisho kisha akitokea Dajjaal hatomdhuru)) [Swahiyh kama alivyoeleza Shaykh Al-Albaaniy katika Silsilatul-Ahaadiyth As-Swahiyhah]

·         Swalah ya Alfajiri

حديث أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، قَالَ: كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ، فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ، آلَم تَنْزيلُ، السَّجْدَةَ، وَ هَلْ أَتَى عَلَى الإِنْسَانِ ( أخرجه البخاري)

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye alisema:  Alikuwa Mtume صلى الله عليه وسلم  akisoma surah ya Alif-Laam-Tanziylu (Suratus Sajdah) na Hal-Ataa 'Alal-Insaan (Suratul Insaan)”  [Al-Bukhaariy]

·         Kumswalia Mtume صلى الله عليه وسلم

عن أوس بن أوس رضي الله عنه قال: قال رسول الله  صلى الله عليه  وسلم  إن من أفضل أيامكم يوم الجمعة، فأكثروا علي من الصلاة فيه، فإن صلاتكم معروضة علي  ) رواه أبو داود)
Kutoka kwa Aws Ibn Aws رضي الله عنه ambaye alisema:  Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم : “Siku bora kabisa kwenu ni siku ya Ijumaa, kwa hiyo zidisheni kuniswalia,  kwani Swalah (kuniombea) zenu zinaonyeshwa (zinaletwa mbele yangu) kwangu.” [Abu Daawuud]
 

Usimuombe Muhammad, Bali Muombe Allaah

 
Waislamu sote tunakiri na kutamka kwa ndimi zetu kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mtume wa mwisho, naye ni mbora wa viumbe, mwenye tabia bora za kupigiwa mfano na sisi tunawajibika kuzifanyia kazi.
 
Hata hivyo, juu ya hikmah zake, cheo na daraja alichonacho, hatustahiki hata kidogo kumuomba Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika lolote tunalohitajia kuliomba. Wala hatuwajibiki kuamini kwamba du’aa isiyopita transit kwake, haikubaliwi. Hilo sio sahihi katu, kwani Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa malaaikah wala jamii isiyokuwa yetu sisi. Ni mwenzetu, mwenye maumbile sawa na sisi, kilichobadilika kutoka kwake ni kupokea wahyi tu.
 
Mola wetu, Anasema kwamba tumuombe Yeye, kwani Ndiye Anayezisikia du’aa zetu na malalamiko yetu:
 
{{Na waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi Nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.)) [Al-Baqarah:186]
 
Pia Amesema:
 
{{Na Mola wenu Anasema: Niombeni nitakuitikieni.}} [Suratul-Ghaafir: 60]
 
Kwa upande wake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba tusimtukuze kama walivyomtukuza Manasara kwa Nabii ‘Iysaa hadi kumpa daraja na cheo sawa cha Uungu:
 
((Msinitukuze (kwa kunipandisha cheo kama cha Allaah) kama walivyomtukuza Manasara ‘Iysaa mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja, kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Mjumbe Wake.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
 
Wala hawa Manasara hawakuishia hapo, nao pia wakajitukuza na kujipachika vyeo vya Unabii na Utume, na kujidai kuweza kuombwa na wanaadamu wenzao pamoja na kusamehe madhambi. Hayo kwetu yatabakia ni uzushi mkubwa na ni shirki iliyo wazi.
 
Kwa hapa, tunaomba tuzingatie kwamba du’aa yoyote inatakiwa kuelekezwa moja kwa moja, kiroho na kimatamshi kwake Muumba wala sio kwa Mtume. Tunaona ndani ya jamii zetu za Kiswahili, mtu anapojitoka, anapotokewa na tatizo la ghafla au mfano wa hayo; basi kauli ya mwanzo linalomjia mdomoni ni la kishirikina: Mtume! na mfano wa hayo.
 
Ewe ndugu yangu Muislamu, umesahau ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti. Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti, asiyeweza hata kusikia maombi yetu, seuze kuweza kutuombea kwa Mola. Sasa iweje leo neno lako la mwanzo unapotokezewa na shida liwe Mtume!?
 
Na wengine wapo waliochupa mipaka, wakawapatia vyeo wanaowaita masharifu, mashekhe, mamufti, maqadhi, mawalii na kadhalika, wakawatumia kuzipitisha du’aa zao kwao. Ni ushirikina na uzushi ulioje. Utakuta kwenye du’aa zao wakisema: Kwa kuhudhuria Sayyiduna Muhammad, mawlaana, sharful-anbiyaa, wa shuyukhina, al-faatihah! Ujahili ulioje huu, Mola wetu yupo karibu kuliko mapigo ya mioyo yetu, ya nini kupata taabu kuzipitisha du’aa kupitia kwa viumbe vinavyotegemea rahmah zake?
 
Tunamalizia kwa kuzinasihi nyoyo zetu na za Waislamu wote, kuachana na aina hii ya shirki, kwani tutakuwa tunamuomba kiumbe badala ya kumuomba Muumba.
 

Kutafuta Elimu Ni Wajibu

Jibriyl (‘Alayhis Salaam) aliposhuka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtikisha na kumbana barabara akimuamuru kusoma kwa jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Mola Ambaye Amemuumba mwanadamu kwa tone la damu na kumfunza kwa kutumia kalamu.
 
Iwapo kipenzi cha Mola Mlezi asiyejua kusoma wala kuandika ametikishwa namna hiyo, je sisi tutarajie nini katika kutafuta elimu? Wengi wa Waislamu ni wenye kwenda na kurudi bila ya kutilia mkazo elimu ya Kiislamu. Na kama Waislamu watasimama kihaki liLlaahi kuitafuta elimu, basi ndio itakuwa sababu ya kuondoka udhalilifu walionao Waislamu hivi sasa.
 
Katika baadhi ya miji ya Waislamu, utakuta kuna Misikiti chungu nzima lakini Madrasah zikiwa kidogo kweli kweli. Sasa hiyo Misikiti ikaswalishwe na kusomeshwa darsa na nani? Ingawa hizo Madrasah pia zipo na zimejaa taa na mazulia mazuri mazuri, lakini wanafunzi wake ni wachache kabisa. Kwanza Waislamu watilie mkazo kusoma na kusomesha, badaye ndio wasambazwe hao waliosoma ndani ya Misikiti. Na kwa bahati mbaya, hivi sasa Misikiti na Madrasah ni vitu viwili tofauti. Misikiti mingi inajengwa kwa ajili ya kuswalia tu, na Madrasah kwa ajili ya kusoma tu. Tumesahau ya kwamba Mtume aliujenga Msikiti ambao ndio kiini cha elimu ya Kiislamu na hivi sasa unatoa shahada za juu kabisa kwa wanafunzi.
 
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa utume kwa kauli ya "Iqraa" iliyomo ndani ya Suratul-'Alaq na akaamrishwa kulingania kupitia aya za mwanzo za Suratul-Muddathir. Tunachojifunza hapa ni kwamba amri ya kusoma imekuja mwanzo kabla ya kulingania. Na bila ya shaka Mola Amemuamuru mwanaadamu kutafuta elimu kabla ya kumuamuru kumuelewa Mola Mwenyezi (elimu ya tawhiyd). Kwani kupitia elimu ndio atapata wepesi wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema ndani ya Qur-aan:
 
{{Jua ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Mwenyezi Mungu.}} [Suratu-Muhammad: 19]
 
Amri ya Mola inayosema "jua" ina maana sawa na "soma". Kilichopo hapo ni kwamba kwanza tusome na ndani ya hiyo elimu tutaelewa kuwa hakuna aabudiwaye kwa haki ila Mwenyezi Mungu. Hii inatutambulisha kwamba amri ya kumtambua Mola ipo chini kulinganisha na amri ya kutafuta elimu.
 
Tuzingatie na tuelewe ule msemo wa Waarabu unaosema: "العلم من المعهد إلى العهد"
wenye maana kwamba elimu ni ya kutafutwa milele kuanzia chuoni hadi mwisho wa maisha yake mtu. Tusikate tamaa katika kutafuta elimu. Kwani elimu ni ngumu kuipata na ndio silaha yako hapa duniani na kesho Akhera iwapo utaitumia vyema. Hata unapofariki, warithi wako hawataipata kwani unaondoka nayo kama vile unavyoondoka na ‘amali zako. Watabaki kurithi hizo pumbao za dunia. Na kama umeisoma kisha ukaisomesha na kuwapatia manufaa watu, basi thawabu zake utaendelea kuzichuma hadi kaburini insha Allaah.
 
Tunamuomba Mola Atupatie fahamu ya Manabii na nyoyo zenye kuelewa mambo kwa wepesi kabisa. Atufunulie akili zetu kwa mambo yenye manufaa na kuzifunga akili zetu zisifahamu wala kuelewa hata kidogo yale yasiyo na manufaa. Aamiyn!

Ibilisi Hakati Tamaa

 
Imesimuliwa ya kwamba kulikuwa na mcha Mungu aliyependwa sana na watu wa wakati wake akiitwa Wadd. Alipofariki, swahiba zake walilizunguka kaburi lake huko Babylon kwa masikitiko makubwa. Ibilisi alipoona hilo, aliwashauri kumtengenezea sanamu ili wapate kumkumbuka.
 
Walikubaliana na hilo, hivyo likatengenezwa na kuwekwa mbele ya umma wa watu. Kizazi kilipokuja kuona namna sanamu la Wadd linavyotukuzwa, wakaamua kuweka sanamu hilo ndani ya kila nyumba. Baada ya kupita muda mrefu na pia kuondoka elimu ya Dini, watoto wa hao watu walikuja kuabudia masanamu hayo.
 
Kisa cha Wadd kinatudhihirishia ya kwamba hawakuanza kuabudia masanamu kwa ghafla moja tu. Walianza kidogo kidogo hadi kuingia kwenye shirki moja kwa moja. Na kisa hichi kinadhihirisha Qawl ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwamba Ibilisi ni adui aliye wazi kabisa:
 
{{Hakika Shaytwaan kwa mwanadamu ni adui aliye dhahiri}} [17:53]
 
Ibilisi hana haraka ya kuwavuta viumbe na wala hakati tamaa, huanza kidogo kidogo na hatimaye kuwatumbukiza ndani ya dimbwi la maasi bila ya kujijua. Mfano mwengine ni wa Muislamu mwenye kusimamisha Swalah tano. Ibilisi huanza kumuondoshea hamu ya kufika Masjid mapema, baadaye humshughulisha ili asipate kuswali, huendelea kwa kuswali nyumbani na hatimaye huacha kabisa.
 
Maandishi ya SW kusimama kwa Subhaanahu Wa Ta’ala na SAW kuelezea Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam ni mambo mengine ambayo hapana budi kuyafikiria vizuri. Kwa hali hii, haitokuwa ajabu kuona kizazi kinachofuata kikitamka: Allaah Ess Dabal Yuu (SW) au Mtume Ess Eee Dabal Yuu (SAW).
 
Halikadhalika, mambo ya kusherehekea birthday hayana mnasaba ndani ya Diyn hii tukufu. Wanaswara wanayo birthday ya Yesu (Krismasi), Waislamu nao wakaweka birthday ya Mtume! Laa hawla! Jina la birthday likabadilishwa ili lipate lafdhi zile za Kiarabu na kuitwa Mawlid. Kwa mtindo huu, ndio tunaona sasa hata Waislamu hawaelewi kufunga Jumatatu wala Alkhamisi, Sunnah za Swalah ya dhuhaa na witri zote kaachiwa mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wanasubiri Mfunguo sita waende kusoma hayo Mawlidi wakielewa kuwa ndio kumtukuza kipenzi chetu.
 
Yeye Ibilisi hamuachi mtu hadi mauti yamfike. Hivyo, haifai kusema kwamba ‘nitatubu baadaye’ au ‘nitaanza kuvaa hijabu nikifika umri kadhaa’. Kwani tunashuhudia ndani ya jamii zetu kizee cha kupindukia miaka 85 kikiwa kinaimba kwa matusi ya juu na kunywa pombe mithili ya kijana wa miaka 20!
 
 
Vipi tutaepukana naye?
 
Kuna njia mbili kuu za kuepukana na Ibilisi ambazo ni:
 
Kwanza ni kufuata amri za Allaah. Hii ni pamoja na kukumbuka wasia wa Mola Mlezi wa kutomfuata Ibilisi na badala yake kumuabudia Yeye pekee kwani hii ndiyo njia iliyonyoka:
 
{{Je, Sikukuagizeni (Sikukuusieni) enyi wanaadamu kuwa msimuabudu Shaytwaan? Hakika yeye ni adui aliye dhahiri kwenu. Na ya kwamba niabuduni Mimi. Hii ndiyo njia iliyonyoka.}} [36:60-61]
 
Pili ni kushikamana kwa hali zote katika mwendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Makhalifa wake waadilifu:
 
"... Basi shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa wangu waongofu, kamataneni nazo kwa magego (shikamaneni nazo kwa nguvu zote)" [Abu Daawuud 4607, At-Tirmidhy 2676 Nayo ni Hadiyth Nzuri Sahihi]
 
Huyo ndie Ibilisi ambaye Radhi za Allaah zipo mbali na yeye. Athari ya kumfuata Ibilisi ni mbaya mno, kwani hutuwekea kizuizi baina yetu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na kila mwenye kumfuata yeye ataelekea kwenye njia potofu.
 

Akili Zinapotawaliwa...Daima Hazitofanikiwa


Uislamu ni dini ambayo imekamilika kwa namna ambayo yeyote aweza kuifuata na kuisimamisha. Sio dini ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) pekee. Bali ni dini ya Ulimwengu mzima. Historia yaonesha kwamba Uislamu ulikuwa na nguvu kubwa enzi za nyuma kuliko hali tuliyokuwa nayo sasa. Hivyo, kama misingi hii inaweza kufuatwa na wasiokuwa Waislamu, kwanini Waislamu wenyewe washindwe kuzifuata?

Yaonesha dhaahir kwamba hila zinabuniwa, kutekelezwa na kufanikiwa katika kuangusha mila na desturi za Kiislamu kwani hakuna taifa wala Kiongozi mmoja wa kuwaunganisha Waislamu. Uislamu ni dini yenye Shahadah moja, Qiblah kimoja, Mfungo wa Swawm mmoja na Hijjah moja tu. Hivyo yaonesha wazi wazi kuwa ni dini ya mshikamano, lakini bado haitendewi haki namna inavyotakiwa. Kilio kikubwa ni kwamba, juu ya kuwepo nguzo hizi za kutuunganisha lakini hatuna kauli moja wala vitendo vyenye muelekeo mmoja katika mila na desturi zetu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba Waumini ni wamoja na wanafanana na jengo:
((Hakika Muumini Kwa Muumini ni kama jengo, wanashikamana pamoja)) Akafungamisha Vidole vyake pamoja [Al-Bukhaariy na Muslim]
Badala yake, tunaiendea kinyume Hadiyth hiyo na kuwa pamoja na hila za Magharibi katika kuupiga vita Uislamu.

Tunashuhudia kuwepo mlolongo mkubwa wa shughuli za kuwadumaza Waislamu ili wasiwe ni wenye kuona mbali na kuweza kutoa mawazo ambayo yatakwenda kinyume na misingi ya kibepari. Misingi hii ya kibepari ni ile ambayo inamtoa thamani mwanamke, kuwadhalilisha viumbe kwa neno la demokrasia na uhuru. Imekuwa hii dunia ni uwanja wa fujo tu, mpate mpatae, mshike mshike. Hajulikani nani muadilifu wala mtenda madhambi.

Waislamu tumefanana na mbu kukosa kumbukumbu. Kwani hatukumbuki namna walivyopigwa vita, kubakwa, kuuawa na kuteswa Waislamu waliopo Afghanistan kwa neno la ‘ugaidi’, Iraaq kwa neno la ‘dikteta’ na Chechnya kwa neno la ‘usalama’. Yote haya yanafanywa kwa nani na kwa ajili ya kupata nini? Hakuna chengine kinachogombaniwa hapa ila kuhodhi mamlaka chini ya mkono mmoja wenye nguvu za kushika na kuachia.

Utawala huu wa kimabavu duniani bado unaendelea, na unalenga zaidi kunufaisha nchi za Magharibi. Mfano mzuri tu ni namna Waislamu wanavyoshughulishwa mno na mambo ya anasa na kupoteza muda.

Mechi za mpira ni moja kati ya zana kuu zinazotumiwa kuupiga vita Uislamu. Kama hatutakuwa makini, daima tutakuwa wapofu kwa kuhifadhi majina ya wachezaji pamoja na historia ya klabu za mpira. Huku tukiacha nyuma Siyrah tukufu ya Uislamu pamoja na matendo sahihi ya Uislamu. Hatukai kufikiria namna mzunguko wa mechi hizi zinavyopokezana, mechi zisizokuwa na mwisho kana kwamba wanaoshuhudia pia ni wenye kufanya mazoezi ya mpira.

Kuna mechi za ligi kuu ndani ya mikoa, nchi nzima, nchi jirani pamoja na Afrika nzima. Ukipiga hesabu utapata takriban sio chini ya mechi 100 kwa mwaka mzima. Tukitoka Afrika, tunakwenda chimbuko la ukoloni duniani na kupata mashindano ya kombe la Uingereza, carling cup na FA yanayoshindaniwa kila mwaka. Kabla yake kuna mechi za Uingereza, Spain na Ujerumani. Kama hizo hazitoshi, kuna kombe la dunia la kila baada ya miaka minne. Huku mechi zikichuja hatua kwa hatua kupata mataifa yatakayoshiriki kombe la dunia.

Huko ndiko akili zilipoelekezwa. Ni kutokana na mechi hizi, Waislamu wanaswali kwa kudonoa donoa namna kuku anavyodonoa mtama. Akili hazijajikomboa kuona namna Uislamu unavyoangushwa na kutengenezewa hila mpya kila siku. Iblisi na kundi lake la Magharibi hawalali wakitafakari njia mbadala za kuwapotosha Waislamu bila ya kuwabatiza.

Mechi hizi ndizo zinazowafanya Waislamu kushindwa kusoma fiqhi na kuelewa taratibu za ndoa, mirathi na kadhalika. Mtandao wa Alhidaaya   umejaa masuala kede kede yenye kuonesha dhaahir mmommonyoko wa maadili. Inafikia hatua Muislamu anauliza kama uzinifu (kuwa na girlfriend au boyfriend) ni halali au haramu? Yote hayo yanatokana na kukosa elimu kwa kufuata mdundiko wa pumbazo kama hizi.

Jee hatujafikia hatua ya kuamini namna hizi akili zilivyotekwa nyara? Bila ya shaka yoyote hazitakuwa ni akili zenye kuona mbali isipokuwa kuweka mbele mazungumzo ya mpira badala ya kupanga mikakati ya kukuza Uislamu, kuchangia miradi ya Uislamu pamoja na kuhisabu Waislamu wanaouawa kila leo na kudhulumiwa kila sekunde. Mechi hizi ndizo zinazotengeneza njia ya kuendeleza biashara za ulevi kwa matangazo ya pombe kwenye viwanja na fulana za wachezaji, kukuza uchumi wa Magharibi na kuwadumaza Waislamu.

Tuanze leo, tusisubiri zaidi kubadilika na kuishi Kiislamu katika kila hatua. Kama kweli tunahitaji mpira, tusiwe ni wenye kufuata tu kila kitu. Tutumie muda muafaka kufanya mazoezi ya kweli kweli kusakata kandakanda huku tukitumia muda mwingi zaidi kutafakari juu ya Uislamu wetu. Kuwa bwana wa nafsi yako na wala usiwe mtumwa kwa nafsi yako kufuata kila kipendacho nafsi.

Je, Wewe Ni Miongoni Mwa Waumini?


Je, wewe ni miongoni mwa Waumin? Kama humo basi usikate tamaa, utakuwemo in shaa Allaah kwa kufanya bidii ili nawe uwe miongoni mwa hao waitwao Waumin kwa tawfiq ya Allaah na Rehma Zake.

Kwa kawaida kila mwanaadamu hupenda kufikiwa na mambo mazuri na habari nzuri bila ya kutafakari ya kwamba, je ametimiza sifa za kufikiwa na habari hiyo nzuri au sifa hizo au malipo yanayostahiki na huo uzuri au laa?

Waislamu wote hupenda kuwa na sifa ya kuwa Waumin. Hata hivyo, suali linabaki kuwa: Je, kila Muislamu anaingia kwenye sifa ya kuwa Muumin? Kwani ukiwa miongoni mwa Waumin basi utakuwa ni miongoni mwa watakaoingizwa kwenye pepo ya Firdausi.

Muumin wa kweli ni yule mwenye sifa zitakazotajwa hapa chini. Hivyo, tujiangalieni tumetimiza sifa hizo ili kuwa miongoni mwa hao Waumin wa kweli? Kama bado, basi tujitahidini insha Allaah Mwenyezi Mungu Atujaalie tuwe miongoni mwa hao wanaoitwa Waumin wa kweli na Mwenyezi Mungu mwenyewe.
Zifuatazo Ni Sifa Za Muumin Wa Kweli:

1)    Anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu, iwapo hujai hofu basi umekosa sifa ya kwanza ya kuwa Muumin.
2)    Inaposomwa Qur-aan imani zao huzidi, iwapo imani yako haizidi basi umekosa sifa ya pili ya Waumin.
3)    Waumin haswa humtegemea Mola wao, iwapo humtegemei Mola wako basi umekosa sifa ya tatu ya kuwa Muumin.
4)    Ambao wanashika Swalah na wanatoa katika yale wanayoruzukiwa, iwapo husimamishi Swalah na hutoi ulivyoruzukiwa basi si katika Waumin.

Hao ndio Waumin wa haki (kweli).

Ni nani atakaekupima ya kwamba umefikia sifa za kuwa wewe au mimi ni miongoni mwa Waumin?

Jibu: Kila mwanadaam huweza kujifahamu au kujipima yeye mwenyewe, kama Alivyosema Allaah ndani ya Qur-aan ya kwamba:

{{Bali mtu juu ya nafsi yake ni mwenye kuiona (kuifahamu). Na ingawa atatoa chungu ya udhuru.}} [Al-Qiyaamah 75: 14-15]
 
Zifuatazo ni sifa za Muumin kama Allaah Alivyomsifu huyo Muumin ndani ya Qur-aan, sifa ambazo zipo hapo juu tulizozitaja:

{{Hakika Waumin ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu, nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aayah Zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao. Hao ambao wanashika Swalah na wanatoa katika yale tunayowaruzuku. Hao kweli ndio Waumin. Wao wana vyeo na maghfira na rizki bora kwa Mola wao.}} [An-Anfaal 8: 2-4]

Ikiwa umetimiza sifa hiyo hapo juu ya kuwa Muumin basi unaingia kwenye hatua ya pili, kama ambavyo Allaah Alivyomuamrisha Mtume Wake kwa kumwambia:

{{Sema: Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.}} [Az-Zumar 38: 53]


Zifuatazo Ni Sifa Za Muumin Atakaefuzu

Zifuatazo ni sifa za Muumin aliyefuzu baada ya kutimiza sifa za kuwa Muumin. Basi jiangalie, je utakuwa miongoni mwa Muumin aliyefuzu?

1)    Muumni ambaye ananyenyekea kwenye Swalah yake, iwapo mtu hunyenyekei basi hujafuzu.
2)    Ambae anajiepusha na mambo ya upuuzi, iwapo hujiepushi na mambo ya kipuuzi basi utakuwa hujafuzu. Labda mtu atajiuliza suali - mambo ya kipuuzi ni yepi? Tukipata wasaa in shaa Allaah tutakuja kuyaeleza mambo ya kipuuzi ni yepi kutokana na mtizamo wa Kiislamu.
3)    Ambaye anatoa Zakaah, iwapo upo kwenye kundi la wenye kuwajibika kutoa Zakaah na ukawa huitoi, basi utakuwa hujafuzu.
4)    Ambaye analinda tupu yake isipokuwa tu kwa wake zake, iwapo huilindi tupu yako basi utakuwa hujafuzu, na ndie yule anaeitwa mzinifu. Allaah Atuepushe na uzinifu.
5)    Ambaye hutimiza amana na ahadi, iwapo ukiwa unaifanyia khiyana amana na huna ahadi, basi hujafuzu.
6)    Ambaye Swalah zake anazihifadhi, iwapo huhifadhi Swalah zako basi hujafuzu (hujafanikiwa).

Ikiwa basi unatimiza sifa hizi, basi utakuwa umefuzu (umefanikiwa), na ndio utarithi Pepo iitwayo Firdaws kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Mnapomuomba Mwenyezi Mungu pepo, Muombeni (Pepo) ya Firdaws kwani (pepo hiyo) ni ya kati na kati na ndani yake inatiririka mito, juu yake kuna Arshi ya Ar-Rahmaan.” (Al-Bukhaariy na Muslim)

Habari hii Allaah Ameizungumza kwenye Suratul-Muuminuun Aayah 1-11.

{{Hakika wamefanikiwa Waumin. Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi. Na ambao wanatoa Zakaah. Na ambao wanazilinda tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao. Na ambao Swalah zao wanazihifadhi. Hao ndio warithi. Ambao watairithi Pepo ya Firdaws, wadumu humo.}}


Hitimisho

La muhimu ni kuwa, maadam tuko hai tusikate tamaa, tujitahidi. Yule ambae anahisi yuko miongoni mwa Waumin aongeze bidii, asije akatoka humo na yule aliyekuwa bado hajatimiza sifa za Muumin. Basi na azidishe bidii ili aingie humo Firdaws na akabidhi roho yake huku akiwa Muumin wa kweli.

Wasiya Kumi Wa Allaah - Wasiya Wa 2 Kuwafanyia Wema Wazazi



Wasia wa pili wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama tulivyosoma katika Aayah zilizotangulia ni, kuwafanyia wema wazazi wawili:
 ((...وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا...)) 
((…Na wazazi wenu wafanyieni wema…))
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesisitiza sana kuwafanyia wazazi ihsaan (wema). Wema huo unaweza kuwafanyia wangali bado wahai au hata baada ya kufariki kwao. Tunaona kwamba Swahaba alipoumuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kitendo bora kabisa, akajulishwa kuwa mojawapo ni kuwafanyia wazazi wema:
  ((عَنْ اِبْن مَسْعُود رَضِيَ اللَّه عَنْهُ أَنَّهُ قَالَ : سَأَلْت رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَيّ الْعَمَل أَفْضَل ؟ قَالَ الصَّلَاة عَلَى وَقْتهَا قُلْت ثُمَّ أَيّ ؟ قُلْ بِرّ الْوَالِدَيْنِ قُلْت ثُمَّ أَيّ ؟ قَالَ الْجِهَاد فِي سَبِيل اللَّه)) البخاري و مسلم
Kutoka kwa Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nilimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Kitendo gani bora kabisa? Akasema: ((Swalah kwa wakati wake)) Kisha nikasema: Kisha kipi? Akasema: ((Kuwafanyia wema wazazi wawili)): Kisha nikasema: Kisha kipi? Akasema: ((Jihaadi katika njia ya Allaah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwa umuhimu wake kitendo hiki hata ikiwa ni wazazi makafiri basi tunapaswa kuwatendea wema, ila tu watakapomuamrisha Muislamu kumshirikisha Allaah au maovu mengineyo hapo hawapaswi kutiiwa:
((وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ))
((Na Tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyokuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na Nitakwambieni mliyokuwa mkiyatenda)) Al-‘Ankabuut: 8]
Utakuta Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) mara Anapotaja kumuabudu Yeye, Hutaja na kuwafanyia wema wazazi wawili. Hii ni dhahiri jinsi gani jambo hili lilivyokuwa zito mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَ بَنِي إِسْرَائِيلَ لاَ تَعْبُدُونَ إِلاَّ اللّهَ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَاناً))
((Na Tulipofunga agano na Wana wa Israaiyl Hamtamuabudu yeyote ila Allaah na muwafanyie wema wazazi)) [Al-Baqarah: 83]
Maelezo zaidi kwa upana kuhusa mas-ala haya tumeshayatoa katika Nasiha za Ijumaa wiki zilizopita na yote yanapatikana katika viungo vifuatavyo:


Itaendelea InshaAllaah…