Jibriyl
(‘Alayhis Salaam) aliposhuka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) alimtikisha na kumbana barabara akimuamuru kusoma kwa
jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Mola Ambaye Amemuumba mwanadamu
kwa tone la damu na kumfunza kwa kutumia kalamu.
Iwapo
kipenzi cha Mola Mlezi asiyejua kusoma wala kuandika ametikishwa namna
hiyo, je sisi tutarajie nini katika kutafuta elimu? Wengi wa Waislamu ni
wenye kwenda na kurudi bila ya kutilia mkazo elimu ya Kiislamu. Na kama
Waislamu watasimama kihaki liLlaahi kuitafuta elimu, basi ndio itakuwa
sababu ya kuondoka udhalilifu walionao Waislamu hivi sasa.
Katika
baadhi ya miji ya Waislamu, utakuta kuna Misikiti chungu nzima lakini
Madrasah zikiwa kidogo kweli kweli. Sasa hiyo Misikiti ikaswalishwe na
kusomeshwa darsa na nani? Ingawa hizo Madrasah pia zipo na zimejaa taa
na mazulia mazuri mazuri, lakini wanafunzi wake ni wachache kabisa.
Kwanza Waislamu watilie mkazo kusoma na kusomesha, badaye ndio
wasambazwe hao waliosoma ndani ya Misikiti. Na kwa bahati mbaya, hivi
sasa Misikiti na Madrasah ni vitu viwili tofauti. Misikiti mingi
inajengwa kwa ajili ya kuswalia tu, na Madrasah kwa ajili ya kusoma tu.
Tumesahau ya kwamba Mtume aliujenga Msikiti ambao ndio kiini cha elimu
ya Kiislamu na hivi sasa unatoa shahada za juu kabisa kwa wanafunzi.
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa utume kwa kauli ya
"Iqraa" iliyomo ndani ya Suratul-'Alaq na akaamrishwa kulingania
kupitia aya za mwanzo za Suratul-Muddathir. Tunachojifunza hapa ni
kwamba amri ya kusoma imekuja mwanzo kabla ya kulingania. Na bila ya
shaka Mola Amemuamuru mwanaadamu kutafuta elimu kabla ya kumuamuru
kumuelewa Mola Mwenyezi (elimu ya tawhiyd). Kwani kupitia elimu ndio
atapata wepesi wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) Anasema ndani ya Qur-aan:
{{Jua ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Mwenyezi Mungu.}} [Suratu-Muhammad: 19]
Amri
ya Mola inayosema "jua" ina maana sawa na "soma". Kilichopo hapo ni
kwamba kwanza tusome na ndani ya hiyo elimu tutaelewa kuwa hakuna
aabudiwaye kwa haki ila Mwenyezi Mungu. Hii inatutambulisha kwamba amri
ya kumtambua Mola ipo chini kulinganisha na amri ya kutafuta elimu.
Tuzingatie na tuelewe ule msemo wa Waarabu unaosema: "العلم من المعهد إلى العهد"
wenye
maana kwamba elimu ni ya kutafutwa milele kuanzia chuoni hadi mwisho wa
maisha yake mtu. Tusikate tamaa katika kutafuta elimu. Kwani elimu ni
ngumu kuipata na ndio silaha yako hapa duniani na kesho Akhera iwapo
utaitumia vyema. Hata unapofariki, warithi wako hawataipata kwani
unaondoka nayo kama vile unavyoondoka na ‘amali zako. Watabaki kurithi
hizo pumbao za dunia. Na kama umeisoma kisha ukaisomesha na kuwapatia manufaa watu, basi thawabu zake utaendelea kuzichuma hadi kaburini insha Allaah.
Tunamuomba
Mola Atupatie fahamu ya Manabii na nyoyo zenye kuelewa mambo kwa wepesi
kabisa. Atufunulie akili zetu kwa mambo yenye manufaa na kuzifunga
akili zetu zisifahamu wala kuelewa hata kidogo yale yasiyo na manufaa.
Aamiyn!
No comments:
Post a Comment