Uislamu
ni dini ambayo imekamilika kwa namna ambayo yeyote aweza kuifuata na
kuisimamisha. Sio dini ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) wala Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) pekee. Bali ni dini ya
Ulimwengu mzima. Historia yaonesha kwamba Uislamu ulikuwa na nguvu kubwa
enzi za nyuma kuliko hali tuliyokuwa nayo sasa. Hivyo, kama misingi hii
inaweza kufuatwa na wasiokuwa Waislamu, kwanini Waislamu wenyewe
washindwe kuzifuata?
Yaonesha
dhaahir kwamba hila zinabuniwa, kutekelezwa na kufanikiwa katika
kuangusha mila na desturi za Kiislamu kwani hakuna taifa wala Kiongozi
mmoja wa kuwaunganisha Waislamu. Uislamu ni dini yenye Shahadah moja,
Qiblah kimoja, Mfungo wa Swawm mmoja na Hijjah moja tu. Hivyo yaonesha
wazi wazi kuwa ni dini ya mshikamano, lakini bado haitendewi haki namna
inavyotakiwa. Kilio kikubwa ni kwamba, juu ya kuwepo nguzo hizi za
kutuunganisha lakini hatuna kauli moja wala vitendo vyenye muelekeo
mmoja katika mila na desturi zetu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema kwamba Waumini ni wamoja na wanafanana na
jengo:
((Hakika Muumini Kwa Muumini ni kama jengo, wanashikamana pamoja)) Akafungamisha Vidole vyake pamoja [Al-Bukhaariy na Muslim]
Badala yake, tunaiendea kinyume Hadiyth hiyo na kuwa pamoja na hila za Magharibi katika kuupiga vita Uislamu.
Tunashuhudia
kuwepo mlolongo mkubwa wa shughuli za kuwadumaza Waislamu ili wasiwe ni
wenye kuona mbali na kuweza kutoa mawazo ambayo yatakwenda kinyume na
misingi ya kibepari. Misingi hii ya kibepari ni ile ambayo inamtoa
thamani mwanamke, kuwadhalilisha viumbe kwa neno la demokrasia na uhuru.
Imekuwa hii dunia ni uwanja wa fujo tu, mpate mpatae, mshike mshike. Hajulikani nani muadilifu wala mtenda madhambi.
Waislamu
tumefanana na mbu kukosa kumbukumbu. Kwani hatukumbuki namna
walivyopigwa vita, kubakwa, kuuawa na kuteswa Waislamu waliopo
Afghanistan kwa neno la ‘ugaidi’, Iraaq kwa neno la ‘dikteta’ na
Chechnya kwa neno la ‘usalama’. Yote haya yanafanywa kwa nani na kwa
ajili ya kupata nini? Hakuna chengine kinachogombaniwa hapa ila kuhodhi
mamlaka chini ya mkono mmoja wenye nguvu za kushika na kuachia.
Utawala
huu wa kimabavu duniani bado unaendelea, na unalenga zaidi kunufaisha
nchi za Magharibi. Mfano mzuri tu ni namna Waislamu wanavyoshughulishwa
mno na mambo ya anasa na kupoteza muda.
Mechi za mpira ni moja kati ya zana kuu zinazotumiwa kuupiga vita Uislamu. Kama
hatutakuwa makini, daima tutakuwa wapofu kwa kuhifadhi majina ya
wachezaji pamoja na historia ya klabu za mpira. Huku tukiacha nyuma Siyrah
tukufu ya Uislamu pamoja na matendo sahihi ya Uislamu. Hatukai
kufikiria namna mzunguko wa mechi hizi zinavyopokezana, mechi zisizokuwa
na mwisho kana kwamba wanaoshuhudia pia ni wenye kufanya mazoezi ya
mpira.
Kuna
mechi za ligi kuu ndani ya mikoa, nchi nzima, nchi jirani pamoja na
Afrika nzima. Ukipiga hesabu utapata takriban sio chini ya mechi 100 kwa
mwaka mzima. Tukitoka Afrika, tunakwenda chimbuko la ukoloni duniani na
kupata mashindano ya kombe la Uingereza, carling cup na FA
yanayoshindaniwa kila mwaka. Kabla yake kuna mechi za Uingereza, Spain na Ujerumani. Kama
hizo hazitoshi, kuna kombe la dunia la kila baada ya miaka minne. Huku
mechi zikichuja hatua kwa hatua kupata mataifa yatakayoshiriki kombe la
dunia.
Huko
ndiko akili zilipoelekezwa. Ni kutokana na mechi hizi, Waislamu
wanaswali kwa kudonoa donoa namna kuku anavyodonoa mtama. Akili
hazijajikomboa kuona namna Uislamu unavyoangushwa na kutengenezewa hila
mpya kila siku. Iblisi na kundi lake la Magharibi hawalali wakitafakari
njia mbadala za kuwapotosha Waislamu bila ya kuwabatiza.
Mechi hizi ndizo zinazowafanya Waislamu kushindwa kusoma fiqhi na kuelewa taratibu za ndoa, mirathi na kadhalika. Mtandao wa Alhidaaya umejaa masuala kede kede yenye kuonesha dhaahir mmommonyoko wa maadili. Inafikia hatua Muislamu anauliza kama uzinifu (kuwa na girlfriend au boyfriend) ni halali au haramu? Yote hayo yanatokana na kukosa elimu kwa kufuata mdundiko wa pumbazo kama hizi.
Jee
hatujafikia hatua ya kuamini namna hizi akili zilivyotekwa nyara? Bila
ya shaka yoyote hazitakuwa ni akili zenye kuona mbali isipokuwa kuweka
mbele mazungumzo ya mpira badala ya kupanga mikakati ya kukuza Uislamu,
kuchangia miradi ya Uislamu pamoja na kuhisabu Waislamu wanaouawa kila
leo na kudhulumiwa kila sekunde. Mechi hizi ndizo zinazotengeneza njia
ya kuendeleza biashara za ulevi kwa matangazo ya pombe kwenye viwanja na
fulana za wachezaji, kukuza uchumi wa Magharibi na kuwadumaza Waislamu.
Tuanze leo, tusisubiri zaidi kubadilika na kuishi Kiislamu katika kila hatua. Kama
kweli tunahitaji mpira, tusiwe ni wenye kufuata tu kila kitu. Tutumie
muda muafaka kufanya mazoezi ya kweli kweli kusakata kandakanda huku
tukitumia muda mwingi zaidi kutafakari juu ya Uislamu wetu. Kuwa bwana
wa nafsi yako na wala usiwe mtumwa kwa nafsi yako kufuata kila
kipendacho nafsi.
No comments:
Post a Comment