Je,
wewe ni miongoni mwa Waumin? Kama humo basi usikate tamaa, utakuwemo in
shaa Allaah kwa kufanya bidii ili nawe uwe miongoni mwa hao waitwao
Waumin kwa tawfiq ya Allaah na Rehma Zake.
Kwa kawaida kila mwanaadamu hupenda kufikiwa na mambo mazuri na habari nzuri bila ya kutafakari ya kwamba, je ametimiza sifa za kufikiwa na habari hiyo nzuri au sifa hizo au malipo yanayostahiki na huo uzuri au laa?
Waislamu wote hupenda kuwa na sifa ya kuwa Waumin. Hata hivyo, suali linabaki kuwa: Je, kila Muislamu anaingia kwenye sifa ya kuwa Muumin? Kwani ukiwa miongoni mwa Waumin basi utakuwa ni miongoni mwa watakaoingizwa kwenye pepo ya Firdausi.
Muumin wa kweli ni yule mwenye sifa zitakazotajwa hapa chini. Hivyo, tujiangalieni tumetimiza sifa hizo ili kuwa miongoni mwa hao Waumin wa kweli? Kama bado, basi tujitahidini insha Allaah Mwenyezi Mungu Atujaalie tuwe miongoni mwa hao wanaoitwa Waumin wa kweli na Mwenyezi Mungu mwenyewe.
1) Anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu, iwapo hujai hofu basi umekosa sifa ya kwanza ya kuwa Muumin.
2) Inaposomwa Qur-aan imani zao huzidi, iwapo imani yako haizidi basi umekosa sifa ya pili ya Waumin.
3) Waumin haswa humtegemea Mola wao, iwapo humtegemei Mola wako basi umekosa sifa ya tatu ya kuwa Muumin.
4) Ambao wanashika Swalah na wanatoa katika yale wanayoruzukiwa, iwapo husimamishi Swalah na hutoi ulivyoruzukiwa basi si katika Waumin.
Hao ndio Waumin wa haki (kweli).
Ni nani atakaekupima ya kwamba umefikia sifa za kuwa wewe au mimi ni miongoni mwa Waumin?
Jibu: Kila mwanadaam huweza kujifahamu au kujipima yeye mwenyewe, kama Alivyosema Allaah ndani ya Qur-aan ya kwamba:
{{Bali mtu juu ya nafsi yake ni mwenye kuiona (kuifahamu). Na ingawa atatoa chungu ya udhuru.}} [Al-Qiyaamah 75: 14-15]
Zifuatazo ni sifa za Muumin kama Allaah Alivyomsifu huyo Muumin ndani ya Qur-aan, sifa ambazo zipo hapo juu tulizozitaja:
{{Hakika
Waumin ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu, nyoyo zao hujaa khofu,
na wanaposomewa Aayah Zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao.
Hao ambao wanashika Swalah na wanatoa katika yale tunayowaruzuku. Hao
kweli ndio Waumin. Wao wana vyeo na maghfira na rizki bora kwa Mola
wao.}} [An-Anfaal 8: 2-4]
Ikiwa
umetimiza sifa hiyo hapo juu ya kuwa Muumin basi unaingia kwenye hatua
ya pili, kama ambavyo Allaah Alivyomuamrisha Mtume Wake kwa kumwambia:
{{Sema:
Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye
ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.}} [Az-Zumar 38: 53]
Zifuatazo Ni Sifa Za Muumin Atakaefuzu
Zifuatazo
ni sifa za Muumin aliyefuzu baada ya kutimiza sifa za kuwa Muumin. Basi
jiangalie, je utakuwa miongoni mwa Muumin aliyefuzu?
1) Muumni ambaye ananyenyekea kwenye Swalah yake, iwapo mtu hunyenyekei basi hujafuzu.
2) Ambae
anajiepusha na mambo ya upuuzi, iwapo hujiepushi na mambo ya kipuuzi
basi utakuwa hujafuzu. Labda mtu atajiuliza suali - mambo ya kipuuzi ni
yepi? Tukipata wasaa in shaa Allaah tutakuja kuyaeleza mambo ya kipuuzi
ni yepi kutokana na mtizamo wa Kiislamu.
3) Ambaye anatoa Zakaah, iwapo upo kwenye kundi la wenye kuwajibika kutoa Zakaah na ukawa huitoi, basi utakuwa hujafuzu.
4) Ambaye
analinda tupu yake isipokuwa tu kwa wake zake, iwapo huilindi tupu yako
basi utakuwa hujafuzu, na ndie yule anaeitwa mzinifu. Allaah Atuepushe
na uzinifu.
5) Ambaye hutimiza amana na ahadi, iwapo ukiwa unaifanyia khiyana amana na huna ahadi, basi hujafuzu.
6) Ambaye Swalah zake anazihifadhi, iwapo huhifadhi Swalah zako basi hujafuzu (hujafanikiwa).
Ikiwa
basi unatimiza sifa hizi, basi utakuwa umefuzu (umefanikiwa), na ndio
utarithi Pepo iitwayo Firdaws kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Mnapomuomba
Mwenyezi Mungu pepo, Muombeni (Pepo) ya Firdaws kwani (pepo hiyo) ni ya
kati na kati na ndani yake inatiririka mito, juu yake kuna Arshi ya
Ar-Rahmaan.” (Al-Bukhaariy na Muslim)
Habari hii Allaah Ameizungumza kwenye Suratul-Muuminuun Aayah 1-11.
{{Hakika
wamefanikiwa Waumin. Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao. Na ambao
hujiepusha na mambo ya upuuzi. Na ambao wanatoa Zakaah. Na ambao
wanazilinda tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono
yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anayetaka kinyume
cha haya, basi hao ndio warukao mipaka. Na ambao wanazitimiza amana zao
na ahadi zao. Na ambao Swalah zao wanazihifadhi. Hao ndio warithi. Ambao
watairithi Pepo ya Firdaws, wadumu humo.}}
Hitimisho
La
muhimu ni kuwa, maadam tuko hai tusikate tamaa, tujitahidi. Yule ambae
anahisi yuko miongoni mwa Waumin aongeze bidii, asije akatoka humo na
yule aliyekuwa bado hajatimiza sifa za Muumin. Basi na azidishe bidii
ili aingie humo Firdaws na akabidhi roho yake huku akiwa Muumin wa
kweli.
No comments:
Post a Comment