A / Alaikum brother Muslim men and women either after greetings are you ignorant of blogs this is Islam referencing everything apply Islam and Muslims problems all questions feedback analysis of various topics and highlights from our religion of Islam but God is the one most skillful Insha'llah to comment questions do not hesitate to write abdulmohamedy23@gmail.com or +255762084268 inshallah
Monday, 16 November 2015
Historia Ya Waja Wema Kwa Kifupi - Karne Ya kwanza
KARNE YA KWANZA (1H - 99H)
Imefasiriwa Na:
Abu Sumayyah
‘Abdullaah Abu Jaabir (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Abdullaah
Abu Jaabir bin ‘Amr bin Hazzam bin Tha’labah al-Answaariy al-Khazrajiy
as-Sulamiy, ni miongoni mwa waliotoa ahadi ya ‘Uqbah. Alihudhuria vita
vya Badr na alikufa shahidi katika vita vya Uhud.
‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Abdullaah
bin ‘Abbaas bin ‘Abdul-Muttwalib bin Haashim bin ‘Abd Manaaf
al-Qurashiy al-Haashimiy, alikuwa ni binamu yake Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mfasiri wa Qur-aan. Alizaliwa
miaka mitatu baada ya Hijrah na alikuwa anaitwa ‘Bahari ya Elimu.’
Alishiriki katika Jihaad kule Kaskazini mwa Afrika kwenye mwaka 27H na
alikufa mwaka 68H.
‘Abdullaah bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Abdullaah
bin ‘Amr bin al-’Aasw bin Waail bin Haashim bin Su’ayd bin Sa’d bin
Sahm as-Sahmi. Yeye na baba yake walikuwa ni Maswahaba. Alikuwa anajua
kusoma na kuandika na alipata ruhusa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuandika yote yale aliyokuwa
akiyazungumza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Alikufa katika mwaka 65H.
‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Alikuwa
Swahaba mkubwa wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),
‘Abdullaah bin Mas’uwd bin Ghaafil bin Habiyb (Radhiya Allaahu ‘Anhu),
alikufa katika mwaka 32H huko Madiynah. Az-Zubayr aliongoza Swalah ya
Janaazah lake na kuzikwa Baqiy’.
Alikuwa
ni mtu wa sita kusilimu hata kabla ya ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya
Allaahu ‘Anhu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alimbashiria makazi yake Peponi. ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alitaja
jambo hii kusema ya kwamba Mtume alimuamuru Ibn Mas’uwd kupanda mti
kuchuma kitu fulani na kuleta chini. Maswahaba walikuwa wakiangalia
miundi ya Ibn Mas’uwd wakati akipanda mti na waliaanza kumcheka kutokana
na uwembamba wa miundi yake. Mjumbe wa Allaah alisema: “Ni kitu gani
kinachowachekesha? Miguu ya Ibn Mas’uwd ni mizito kwenye mizani siku ya
Qiyaamah kuliko Mlima Uhud.”
[Imesimuliwa na Imaam Ahmad katika Musnad yake na kuthibitishwa na Shaykh Ahmad Shaakir (920)].
‘Abdullaah
bin Mas’uwd alikuwa msomaji mkubwa wa Qur-aan. Inasemekana alikuwa ni
mmoja wa watu wenye kufuata kwa karibu sana muongozo wa Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Imekusanywa kutoka kwenye kitabu cha Siyaar A‘laam an-Nubalaa - cha Adh-Dhahabiy na Tahdhiyb At-Tahdhiyb cha Ibn Hajr.
Abu ad-Dardaa (Radhiya Allaahu ‘Ahnu)
Abu
ad-Dardaa Uwaymir bin Maalik bin Zayd bin Qays al-Khazrajiy
al-Answaariy. Kuna maoni tofauti kuhusu jina lake. Alisilimu wakati wa
vita vya Badr na alishuhudia vita vya Uhud. Alikuwa ni Mwanachuoni wa
Shari’ah. Mchaji Allaah miongoni mwa Swahaba. Alikufa katika mwaka 32H.
Abu Dharr al-Ghifaariy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu
Dharr al-Ghifaariy Jundub bin Junaadah bin Sakn alikuwa ni miongoni
waliosimu mwanzoni lakini alichelewa kufanya Hijrah hivyo hakushiriki
vita vya Badr. Fadhila zake ni nyingi na alikufa mwaka 32H.
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu
Hurayrah, ‘Abdur-Rahmaan bin Swakhr ad-Dawsiy alikwenda kwa Mtume kama
Muhaajir wakati wa vita vya Khaybar. Alihifadhi idadi kubwa ya Hadiyth.
Zaidi ya Hadiyth elfu nane zilisimuliwa kutoka kwake. Alikufa katika
mwaka 58H.
Mtume
Alimuombea du’aa yeye na mama yake kwa kusema: “Ee Allaah! Wajaalie hawa
waja wako (wawili) ni wenye kupendwa na Waumini na wafanye Waumini ni
wenye kuwapenda.” [Imesimuliwa na Muslim].
Abu Muwsaa al-Asha’riy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu
Muwsaa al-Ash’ariy ‘Abdullah bin Qays bin Saalim alikuwa ni mwenye sauti
nzuri wakati wa kusoma Qur-aan na ni mmoja wa Wanachuoni miongoni mwa
Maswahaba. Inasemekana alikufa mwaka wa 42H au 44H.
Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu
Sa’iyd al-Khudriy Sa’ad bin Maalik bin Sinaan bin ‘Ubayd al-Answaariy
al-Khazrajiy. Yeye na baba yake wote walikuwa ni Maswahaba na
alishuhudia vita vyote vilivyofuata baada ya vita vya Uhud. Alikuwa ni
mmojawapo wa Wanachuoni miongoni mwa Maswahaba na alisimulia Hadiyth
nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa
katika mwaka 74H.
‘Adiy Bin Haatim (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Adiy
bin Haatim bin ‘Abdillaah bin Saa’d bin al-Hashraj bin ‘Aamr al-Qays
at-Twaaiy, Abu Tarif. Alikuwa Mkristo aliyesilimu na kuhudhuria vita vya
Jamal, Swiffiyn na an-Nahrawaan pamoja na ‘Aliy. Alikufa katika mwaka
68H.
Al-Bara’a bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Al-Bara’a
bin Maalik bin an-Nadr al-Answaariy.Alihudhuria vita vya Uhud na alitoa
ahadi ya utii chini ya mti. Alikufa shahidi katika mwaka wa 20H kwenye
siku Tustar.
Al-Mughiyrah Bin Shu’bah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Al-Mughiyrah
bin Shu’bah bin Abi ‘Aamir bin Mas’uwd ath-Thaqafiy, Abu ‘Abdillaah.
Alihudhuria vita vya Hudaybiyyah, Al-Yamaamah na alipata ushindi kule
Syria na Iraq. Alikufa katika mwaka 50H.
‘Amr Bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Amr
bin al-’Aasw bin Wa’il al-Qurashiy as-Sahmiy Alisilimu katika mwaka wa
Sulhu Hudaybiyyah na alikuwa ni mmoja wapo kati ya wale walioshinda
kule Misr. Alifariki katika mwaka 43H.
Anas Bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Anas
bin Maalik bin an-Nadr, Abu Hamzah, al-Answaariy, an-Najjaariy. Alikuwa
mfanyakazi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). ambaye
alikaa nae karibu kwa takriban miaka kumi tangu alipohama mpaka kifo
cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa ni
miongoni mwa Maswahaba wa mwisho kufariki. Alifariki akiwa na miaka 93H
kule Baswrah akiwa na miaka 103.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alimuombea du’aa kwa kusema: “Ee Allaah Mjalie utajiri na watoto na Vibariki vile ulivyomruzuku.” [Muslim].
Na katika mapokezi mengine Anas Aliongezea kwa kusema: “Na
(kutoka kwa) Allaah fungu langu imekuwa kubwa watoto wangu na wajukuu
wameongezeka kiasi cha kufikia mia moja kwa kuwahesabu.” [Muslim].
‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha)
‘Aaishah
bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhuma). Mke wa Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baada ya Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘Anha)
kufariki, Malaika Jibriyl alimuonyesha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) kwenye ndoto kabla ya kumuoa na alikuwa na miaka kumi
na nane wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alipofariki.
Alifariki katika mwaka 59H kwenye tarehe kumi na saba ya mwezi wa Ramadhwaan. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alimzika.
Alikuwa
Mama wa Waumini Asw-Swiddiyqah (Radhiya Allaahu ‘Anha). ‘Umar
alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni nani
unayempenda zaidi miongoni mwa watu? Akajibu: ‘Aaishah’. Kisha,
akamuuliza miongoni mwa wanaume (ni nani unayempenda zaidi)? Akajibu:
Baba yake.”
Ash-Sha’abiy
alisema: Wakati Masruwuq anatusimulia kuhusu ‘Aaishah, alisema:
‘Niliambiwa na mkweli, bint wa mkweli, mpendwa miongoni mwa vipenzi vya
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Asiye na hatia
ambaye ndoa yake ilianzishwa kutoka mbingu ya saba.
Az-Zuhriy
alisema: “Iwapo elimu ya Mama ‘Aaishah itakusanywa na kulinganishwa na
elimu ya wakeze wengine Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) na wanawake wengine wote basi elimu ya Mama ‘Aaishah ingelibakia
kuwa isiyo na kifani.”
‘Imran Bin Huswayn (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Imran
bin Huswayn al-Khuza’iy al-Ka’biy, Abu Nujayd. Alisilimu mwaka wa vita
vya Khaybar na aliripoti baadhi ya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa katika mwaka 52H.
Jaabir Bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Jaabir
bin ‘Abdillaah bin ‘Amr bin Harram al-Answaariy as-Sulamiy. Alishuhudia
‘Uqbah wakati wa pili huku akiwa mtoto. Inasemekana alihudhuria vita
vya Badr na Uhud na kuripoti Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alifariki katika Mwaka wa 74H.
Tuesday, 25 August 2015
Mola
wetu Mtukufu Amemuumba mwanaadamu katika umbo bora lisilomithilika na
kiumbe chochote. Naye ameumbwa kwa kutumia udongo uliopulizwa roho
itokayo kwa Mola Mlezi.
Akamjaalia
mwanaadamu ni mwenye kupata shida, mitihani, mtenda dhambi na mwenye
kupata maradhi. Hakusita hapo Mola wetu Mtukufu, bali Akajaalia mlango
wa pili wa kutokea kwenye mashaka ya dunia; Akajaalia kuwepo starehe,
utulivu, toba na afya. Basi ni kwa neema zipi mwanaadamu anaweza kumlipa
Mola wake!?
Tutambue
kwamba hii roho tuliyokuwa nayo yatosha kuwa ni sababu ya kushukuru
neema za Mola Mlezi kwa vitendo na kauli. Tusisahau wapi tulipotoka na
wapi tunaelekea, hatukuwa chochote miaka 100 iliyopita. Basi ni nani
kati yetu alikuwa na uhakika kwamba atadhihiri duniani kwa jina na umbo
lake kabla ya kuzaliwa? Kuwa na adabu kwa kumcha Mola wako!
Muislamu
yupo juu ya mgongo wa ardhi akiruzukiwa kila chenye manufaa na yeye, ni
mwenye kula akapata njia ya kutolea uchafu, na siku uchafu unaposhindwa
kutoka ndani ya tumbo ndio unaelewa umuhimu wa neema ya kuyeyusha
chakula kwenye mwili. Ameumba kila kitu kwenye kiwango maalumu, kwani
tumbo likiyeyusha kupita kiwango, mwanaadamu ataugua maradhi ya tumbo la
kumuendesha. Hivyo, kumbuka na yazingatie maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{Na mkihesabu neema za Allaah hamtaweza kupata idadi yake. Hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.}} [An-Nahl: 18]
Basi
elewa ndugu yangu, kwamba sisi si chochote si lolote zaidi ya tone la
manii lililoengwa engwa hadi likafikia miezi tisa likaweza kutoka kwa
sura ya mwanaadamu. Ndani ya tumbo, Mola wetu Mlezi Alitulinda na wala
hatukuhitaji askari, jeshi, polisi, ultimate security au mwengineye.
Ukatoka kwa ukenya wa kilio cha juu ukiomba msaada kwa mama yako.
Ukafikia baleghe ukaweza kuoa/kuolewa na sasa kwa Qadar ya Mola unaweza
nawe kupata mtoto. Aliyekuwa mbabe kati yetu azihesabu neema ngapi
zimepita baina ya kuzaliwa kwake hadi hivi sasa, kisha aangalie ni kwa
kiwango gani ataweza kuzishukuru neema hizo. SubhaanaLlaah! Yuko umbali
gani mwanaadamu kwa kuzitilia maanani neema za Mola wake?
Ugeuze
uso wako, uangalie mbingu ilivyotanda na ardhi ilivyotandikwa, kisha
useme kwamba Mola wako amekutupa. Rizki zako Akazimimina kutoka mbinguni
na Akazichimbua kutoka ardhini. Ni kipi basi katika chakula chako
kitokacho nje ya mfumo huu? Basi kwa Kiburi Chake Mola Mlezi Anastahiki
kuyaambia makundi ya wanaadamu na majini:
{{Enyi
jamii ya majini na watu! Kama mtaweza kupenya katika mbingu na ardhi
(ili mkimbie Nisikupateni), basi penyeni (Nikuoneni)! Hamtapenya ila kwa
nguvu (Zangu. Nikikupeni nguvu hizo mtaweza).}} [Ar-Rahmaan: 33]
Tumcheni
Mola wetu kwa kila kitu, kwa dogo na kubwa, kwa tunayoyajua na
tusiyoyajua. Tutende mema kabla ya kutufika yale yasiyoweza kuhimili
miili yetu. Wahenga wanatuambia: "Kijua ndi hichi usipouanika utaula
mbichi."
Uchungaji
wa viungo vya Muislamu katika maisha haya umekuwa ni wa chini usio na
maana yoyote. Mkono unaiba, mguu unampeleka baa au kuzini, na ulimi
unadiriki kutoa kiapo cha uongo.
Ulimi
ni kiungo kimoja ambacho chatumiwa vibaya mno takriban na wanaadamu
wote, na ndani yake kuna kundi kubwa la Waislamu ambao hawajali yale
yanayotoka ndani ya vinywa vyao.
Tutambue
kwamba, kiapo juu ya viumbe ni haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
kuviapia. Ni kwa mfano pale Anaposema: Ninaapa kwa Siku ya Qiyaamah,
Ninaapa kwa Jua na kadhalika. Mwanaadamu yeyote hana ruhusa ya kutoa
kiapo kama hicho.
Kwa
mujibu wa mafundisho ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) kiapo cha Muislamu kinaelekezwa kwa Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala). Na nini maana ya kiapo? Kiapo ni kuweka dhamana ya lile
unalosema kwa Yule Unayemwapia. Kwamba hayo unayoyaapia ni ya kweli
unahitaji kusadikiwa na wanaadamu wenzio. Basi ole wake yule ambaye
anaweka kwa Muumba wake kiapo cha uongo.
Hivyo,
kiapo ni chenye kuchungwa mno na wala sio kukifanya kuwa ni dhikri ya
ulimi ukataka kila kitu kukifanyia kiapo hadi kuwa ni sababu ya
kutumbukia kwenye dimbwi la moto. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Anatuambia tusimtii yule mwenye kuapa kila wakati:
{{Wala usimtii kila muapaji sana, aliye dhalili.}} [Suratul-Qalam: 10]
Kitu
ambacho kimejaa ndani ya maisha yetu Waislamu ni viapo visivyokuwa na
kichwa wala mguu. Na kila wanapokumbushwa wao wanaufanyia kazi ule
msemo: "Kelele za mlango hazimughasi mwenye nyumba". Wanakuwa hawajali
wala hawakubali maneno ya Qur-aan au Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtume
wetu amekataza mno Muislamu kula kiapo ovyo ovyo. Kinyume chake
Muislamu anakula kiapo cha uongo katika biashara ingawa Mtume wetu
amesema kwamba Allaah Hatamuangalia (kwa jicho la huruma) mtu namna hiyo
Siku ya Qiyaamah. [Imesimuliwa na Abu Dharr na kupokelewa na Muslim].
Lililo
kubwa ndani ya jamii zetu ni kufikishana mbele ya vyombo vya sheria kwa
namna za udanganyifu, utapeli na uongo mtupu. Muislamu anadiriki kuweka
kiapo cha uongo kwa Mola wake ili apate mali ya mwengine bila ya
halali. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesimuliwa
akisema kama ilivyopokewa na Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘Anha):
((Mimi ni binaadamu tu na nyinyi mnaleta migogoro yenu kwangu mimi, mukiwa wenye fasaha katika viapo vyenu kuliko wengine, ili ya kwamba nitoe hukumu kwa niaba yenu kwa mujibu wa ninayoyasikia kutoka kwenu. Hivyo, vyovyote nitakavyoamua kwa yeyote, ambapo kwa haki ni ya ndugu yake, asichukue kwani simpatii chochote ila kipande cha moto.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy].
Tunawanasihi
wale waliochukua viapo vya uongo wakamilikishwa mali kwa njia za haramu
wazirejeshe amana hizo haraka iwezekanavyo. Ya Ar-Rahmaan! Na wapo
miongoni mwa viumbe Vyako waliokula kiapo kwa kudhulumu mayatima na
wakala kiapo kwa lengo la kuzini na wake za watu. Umetakasika! Shingo
zao zipo mikononi Mwako!
Ya
Allaah! Tunategemea kwako, na tunageuka kuja Kwako, na Kwako tu ndiko
marejeo yetu. Basi tunakuomba Mola wetu! Tutimizie nuru yetu, na
Utughufirie, hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Toa Swadaqah Kwa Ajili Ya Allaah
Naaswir Haamid
Ihsaan
ni kinyume cha ufisadi, na miongoni mwa Ihsaan ni kufanya wema bila ya
kujali mipaka ya Kaskazi wala Kusi, na kutoa kwa ajili ya Allaah ni wema
na Ihsaan kwa mwanaadamu.
Hakuna
shaka yoyote kwamba Swadaqah ni katika tabia njema, na iwapo tutafungua
kurasa za Siyrah za wema waliotangulia, tutaona kwamba walikuwa
wakikithiri mno kwenye kutoa Swadaqah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Anasema:
{{Chukua Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao).}} [At-Tawbah: 103]
Kupitia
Tamko hilo hapo juu, tunafahamu kwamba kumbe kuisafisha nafsi kutokana
na takataka za upungufu na kuiinua jamii mpaka kuifikisha kwenye daraja
tukufu kabisa, ndio hekima ya juu. Ni kwa ajili hii ndio Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanua wigo katika kuelezea maana
ya neno “Swadaqah” ambayo Muislamu anatakiwa kuitoa, akasema:
((Tabasamu
lako usoni kwa nduguyo (Muislamu mwenzio) ni Swadaqah, kuamrisha kwako
mema na kukataza kwako maovu ni Swadaqah. Na kumuongoza kwako njia mtu
katika ardhi (nchi) ya upotevu, hilo kwako ni Swadaqah. Na kuondosha
kwako njiani udhia, mwiba na mfupa, hilo kwako (nalo) ni Swadaqah. Na
kumtekea kwako maji nduguyo, kwako ni Swadaqah na kumsaidia kwako mtu
dhaifu wa uoni kuongoza njia, (hilo nalo) kwako ni Swadaqah)). [Al-Bukhaariy]
Swadaqah
huanza kwa kuuzoesha mkono kutoa kila mara bila ya kinyongo wala
manuuniko. Mkono una dhima kuu ya kukulingania kutoa Swadaqah katika
vile ulivyoruzukiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama Alivyosema:
{{Yule
anayetoa (Zakaah, Swadaqah na vinginevyo) na kumcha Allaah. Na kusadiki
jambo jema (akalifuata). Tutamsahilishia njia ya kwenda Peponi.}} [Al-Layl: 5-7]
Hiyo
ndio faida na jazaa ya aliyeutumia vyema mkono wake katika kutoa
Swadaqah. Akautumia mkono wake katika kutoa vile Alivyoruzukiwa na
Allaah Ar-Razzaaq, katika kuisadia jamii na kuupeleka mbele Uislamu.
Ni vyema ukakumbuka kwamba kutoa katika mambo ya khayr ni katika kuishukuru neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ambako hakumaanishi ila kuzidishiwa neema, tusome kwa mazingatio:
{{Na
(kumbukeni) Alipotangaza Mola wenu (kuwa): "Kama mkishukuru,
Nitakuzidishieni; na kama mkikufuru, (jueni) kuwa adhabu Yangu ni kali
sana.}} [Ibraahiym: 7]
"Mtenda wema hutendea nafsi yake na mtenda ovu humrejea mwenyewe". Hivyo
elewa kamba kuishukuru neema kikweli kweli na kuitumia vile
inavyostahiki sio tu kusema au kuandika kwenye milango kwa mbwembwe: ‘AlhamduliLlaah’ au ‘Hadha Min Fadhli Rabiy’! Na ni ubaya ulioje kuzitumia neema hizi kinyume na vile Alivyoamrisha Ar-Razzaaq.
Dunia
ni tamu na kawaida ya mwanaadamu kupenda mazuri mno. Hujitahidi kadiri
ya juhudi zake kukusanya yale ayaonayo kuwa ni yenye kufurahisha nafsi
yake. Hutafuta yale yenye laghai na anasa - 'material world'.
Hilo
halina shaka na hata Qur-aan na Sunnah yatuthibitishia kwamba dunia
imeumbwa kuunganishwa na matamanio ya mwanaadamu. Lakini sio yote ambayo
Muislamu anatakiwa kuyatilia mkazo kwa kuyavamia. Ndio lengo la kuwepo
halali na haramu ndani ya Uislamu ili kumtofautisha mwanaadamu na
Muislamu.
Waislamu
walio wengi kabisa wanatamka shahaadah ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) ni Mmoja na Ndiye Apaswaye kuabudiwa pamoja na kutiiwa Mtume
Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kikomo cha wengi
kinamalizia hapa kwenye kauli tu. Matendo yao
yanakuwa kinyume na kauli hii. Hivyo, hufanya ibada kwa kudanganya
macho ya waumini, kwani wanatenda mbele ya kadamnasi, wanapokuwa peke yao huingia kwenye hiyo 'material world' kwa mapana na marefu. Hiyo sio iymaan inayopigiwa mfano na Mola Mlezi:
{{Ambao wanamuogopa Mola wao (hata) wanapokuwa faraghani, na pia hukiogopa Qiyaamah.}} [21:49]
Taariykh
yatufunza kwamba Waislamu hapo kale walilelewa kwenye Tawhiyd ya
kumuamini Allaah pamoja na Malaika, Mitume, Vitabu, Siku ya Mwisho,
Qadar kheri na shari. Kwa wakati wa sasa ni Kitabu cha Qur-aan pekee
ndicho kilicho mbele ya macho yetu. Vilivyobaki vyote vinabaki kuwa
nyuma ya pazia 'ghayb'.
Imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu): amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba:
"Iymaan
ni kumuamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Kukutana
Kwake (Siku ya Qiyaamah), na Mitume Wake na kuamini ufufuo wa Siku ya
Mwisho." (Imepokewa na Shaykhaan)
Kukosa
kuamini moja ya nguzo za iymaan, kunapelekea kutoamini ghayb. Hivyo,
kuanguka kwa iymaan ya ghayb kutasababisha kuondoka iymaan ya kwamba
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Yupo.
Ni
ghayb hii inayomfanya mwanaadamu na hata Muislamu kutotilia mkazo
kuutafuta ukweli halisi wa Uislamu, ghayb ndiko kunakomfanya Muislamu
kutotenda mema kwa lengo la kupata ridhaa ya Allaah. Thawabu wala dhambi
hazioni mtu, Malaika wanaoandika mema na maovu nani anayewaona? Haya
yote yapo kwenye ghayb. Muislamu anatakiwa kuamini hii ghayb bila ya
mjadala. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuambia:
{{Tendeni
mambo (mazuri). Allaah Atayaona mambo yenu hayo na Mtume Wake na
Waislamu. Na mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri; Naye Atakwambieni
(yote) mliyokuwa mkiyatenda.}} [9:105]
Apambanue
Muislamu juu ya kukosa kwake iymaan ya ghayb na kuirudisha nyuma akili
kabla ya kuwepo kwake; yeye alikuwa ni nani? Nani aliyemhifadhi ndani ya
tumbo la mama kwa miezi tisa? Hivyo, ghayb ni wajibu kuiamini na kwamba
yapo mambo nyuma ya macho yetu yanatokea au yapo tayari kutokea.
Kukosekana
kwa iymaan ya ghayb ndani ya nafsi ya Muislamu ndio kwamfanya awache
himma ya kutenda mema. Ni sababu hii inayowafanya vijana walio wengi
kujishughulisha mno na ratiba za mipira inayokula muda wa Waislamu. Nao
kina dada kutilia mkazo urembo, mikusanyiko ya haramu na kutembea kwao
utupu kunatokana na kukosa kwao kuamini ghayb.
Basi
na aangalie Muislamu alivyoumbwa, chakula chake kinavyoyayushwa na
kugaiwa sehemu mbali mbali. Vitamini, damu, madini, sukari, chumvi,
mafuta na vyengineo; vyote vinapelekwa na kuhifadhiwa sehemu zake
maalum. Atupe jicho lake kwa kuangalia linapotoka na kuzama jua, tofauti ya usiku na mchana, hali ya uzima na ugonjwa, maisha na mauti na mengineyo:
{{Naye
ndiye Aliyeziumba mbingu na ardhi kwa haki. Na wakati Anaposema
(kuliambia jambo): "Kuwa," basi huwa… Mjuzi wa ya siri na dhahiri…}} [6:73]
Basi ni mengi yaliyopo Mkononi Mwako yaa Allaah! Namna tutakavyojifunza katu hatutafikia chembe ya 'ilmu Yako. Hivyo, tunatamka kama ambavyo Umetufunza:
Wasiya Wa Pili Wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – Swalaah Ya Adhw-Dhwuhaa.
وعَنْ
أَبِي الدَّرْدَاءِ رضي الله عنه قَالَ : "أَوْصَانِي حَبِيبِي صَلَّى
اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِثَلَاثٍ لَنْ أَدَعَهُنَّ مَا عِشْتُ :
بِصِيَامِ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ، وَصَلَاةِ الضُّحَى
وَبِأَنْ لَا أَنَامَ حَتَّى أُوتِرَ" رواه مسلم
Imepokelewa
kutoka kwa Abu Ad-Dardaai (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: “Ameniusia
mpenzi wangu Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam [mambo] matatu nisiyaache
maishani mwangu; Swiyaam (kufunga) siku tatu kila mwezi na Swalaah ya
Adhw-Dhwuhaa na nisilale mpaka niswali Witr” [Muslim]
Swalaah ya Adhw-Dhwuhaa – Fadhila zake, idadi ya raka’ah zake na wakati wake:
Ukumbusho Wa Swiyaam (Funga) za Ayyaamul-biydhw (Masiku meupe) Dhul-Qa'dah 1436H
Tunapenda
kuwakumbusha Swiyaam (funga) za Ayyaamul-biydhw (masiku meupe) ambayo
ni tarehe 13, 14, 15 katika kila mwezi wa Kiislaam (Hijriyyah). Masiku
hayo mwezi huu wa Dhul-Qa’dah 1436H, yataangukia tarehe 28, 29, 30
August (Ijumaa, Jumamosi, Jumapili). Bonyeza 'Endelea' upate fadhila
kadhaa za Ayyaamul-biydhw na fadhila za Swiyaam siku tatu kila mwezi,
pamoja na fadhila za Swiyaam kwa ujumla. Soma na utekeleze ili
ufaidike na ujichumie thawabu tele In Shaa Allaah. Na hakuna tawfiyq
isipokuwa ya Allaah ‘Azza wa Jalla, Kwake tunatawakali na Kwake
tunarudia kutubia.
Nasiha Za Minasaba Mbali Mbali
Tumeingia Katika Miezi Mitukufu Inatupasa Kuitakasa Kwa Kuacha Maovu Na Kuzidisha Mema
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُم))
((Hakika
idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya
Allaah, tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne
mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu
humo)) [At-Tawbah: 36].
Miezi minne hiyo imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ
أَبَى بَكْرَة أَنَّ رَسُول اللَّه - صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ -
قَالَ فِي حَجَّة الْوَدَاع : ((إِنَّ الزَّمَان قَدْ اِسْتَدَارَ
كَهَيْئَتِهِ يَوْم خَلَقَ اللَّه السَّمَوَات وَالْأَرْض السَّنَة اِثْنَا
عَشَر شَهْرًا مِنْهَا أَرْبَعَة حُرُم : ثَلَاث مُتَوَالِيَات ذُو
الْقَعْدَة وَذُو الْحِجَّة وَالْمُحَرَّم وَرَجَب مُضَر الَّذِي بَيْن
جُمَادَى وَشَعْبَان)) صَحِيح الْبُخَارِيّ
Friday, 31 July 2015
Wednesday, 29 July 2015
Rudi Tena Ukaswali, Kwani Hukuswali
Imefasiriwa na Ilyaasa Mawlaana
Kwa jina la Allaah, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu.
Sehemu Ya Kwanza
Katika usiku wa giza, Abu Lu’lu’ Al-Majuusi (kipenzi cha Mashia) alijificha katika vivuli akijiandaa kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri, wakati ambapo ataendesha mipango yake ya kishetani kumuua Amiyr wa waumini – ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allahu ‘anhu).
‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) alikuwa (na kawaida) ya kuongoza Swalah ya Alfajiri huku akisoma surah ndefu, akiwapa wafuasi wa jamii, muda wa kuhudhuria mkusanyiko (wa Swalaah). Katika siku hii, wakati (‘Umar) akisoma (Qur-aan), Abuu Lu’Lu’ akachukua hatua kutoka kwenye nguzo inayofifia, hali ya kuwa ana kisu cha sumu katika mkono wa vazi lake. Akaruka mbele ya ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) na akamkata tumbo wazi kwa (kile) kisu. Baada ya hapo, akajaribu kuukimbia mkusanyiko. Akiwa ana chana chana mbele na nyuma, akiwauwa watu wengi zaidi ambao walikuwepo katika njia yake. Swahaabah mmoja akamtupia nguo juu yake na alipo tahayari kwamba keshakamatwa Abu Lu’lu’ akajiua.
‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allahu ‘anhu) akaikamilisha Swalaah ya Alfajiri ambayo aliianza ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu). ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) alikamilisha Swalaah yake hali ya kuwa ni miongoni mwa watu (maamuma) katika Jama’ah na akafariki dunia baadaye katika kitanda chake, (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Umuhimu wa Swalaah katika Uislamu hauwezi kudharauliwa. Ni nguzo ya kwanza ya Uislamu iliyotajwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya tamko la Imani (shahaadah), ambayo kutokana nayo mtu huwa Muislamu.
Swalaah imefaradhishwa kwa Manabii na watu wote. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alitangaza hadhi yake ya kuwa ni faradhi katika tukio Tukufu. Kwa mfano, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipozungumza na Muusa (‘Alayhis Salaam), Amesema:
{{Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayofunuliwa. Hakika Mimi ndiye Allaah. Hapana muabudiwa wa haki ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Swalah kwa ajili ya kunikumbuka Mimi}} [Twaaha: 13-14]
Hivyo hivyo, Swalaah imefaradhishwa kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipopelekwa mbinguni. Zaidi, wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anawasifu waumini kama katika Suratul-Al-Mu-uminuun, moja katika sifa ambazo Anazitaja kuhusiana nao ni kule kushikana kwao na Swalaah:
{{Hakika wamefanikiwa Waumini. Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao}} [Al-Mu’minuun: 1-2]
Umuhimu wa Swalaah unaendelea kuonyeshwa katika kauli nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mfano, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Jambo la kwanza ambalo mja atahukumiwa katika Siku ya Hisabu ni Swalaah. Kama ikiwa ni nzuri basi amali zake zilizobakia zitakuwa nzuri. Na ikiwa ni mbaya, basi amali zake zilizobakia zitakuwa mbaya.” [At-Twabaraaniy].
Kwa kweli, ikiwa Swalaah imeswaliwa vizuri ikiambatana na ukumbusho wa kweli wa kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na kumgeukia Yeye kutaka msamaha, itakuwa na athari kubwa juu ya mtu kwa kipindi kirefu. Mtu anapokamilisha Swalaah yake, moyo wake utajaa ukumbusho wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Atakuwa ana hofu na pia vilevile matarajio juu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Baada ya tukio hilo, hatotaka tena kuondoka kutoka katika sehemu hiyo ya fakhari kuelekea kwa ile ambayo ndani yake atamuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anaitaja hali hii ya Swalaah katika Qur-aan:
{{Hakika Swalah inazuilia mambo machafu na maovu}} [Al-‘Ankabuut: 45].
Lakini katika wale ambao wanaoswali, utakuta kuna vitendo vya kivivu ambavyo vinahitaji kumulikwa. Kwa mfano:
· Wengine hawazingatii kile ambacho wanakisema.
· Wengine wanafanya haraka katika Swalah zao
· Wengine wanaachilia nadhari yao ya macho izurure wakati wa Swalah
· Wengine mara kwa mara husahau nambari ya rakaa zilizotimizwa.
· Dunia inakumbatia mioyo ya baadhi ya watu wakati wa Swalah na inafunika akili zao.
· Na watu wengine katika Jamaa’ah wanaanza kusujudu kabla hata ya Imaam kusema “Allaahu Akbar”
Linganisha hii (hali yetu katika Swalaah) na Swalaah za watu ambao walikuja kabla yetu. Watu walikuwa wanafikiria ya kwamba Ar-Rabiy’ bin Khaytham alikuwa ni kipofu kwa sababu ya kuinamisha macho yake mara kwa mara. Alikuwa akiishi nyumbani kwa Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allahu ‘anhu) kwa miaka ishirini na mtumwa wake wa kike akimuona alikuwa akisema: “Rafiki yako kipofu anakuja” na Abdullaah alikuwa akimcheka kwa kauli yake.
Ndani ya Al-Bukhaariy na Muslim, Abuu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) anatueleza ya kwamba, kuna mtu aliingia msikitini, ambao Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa. Akaswali rakaa mbili na kisha akaja kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu salamu yake na halafu akasema, “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.” Hivyo, yule mtu akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara ya kwanza, akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu salamu na akasema “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.” Hivyo, yule mtu akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara ya kwanza akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu salamu kwa mara nyingine tena na kwa mara nyingine tena akasema: “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali”. Hadi kufikia mara hii ya tatu, mtu huyo alisema: “Naapa kwa Yule ambaye alikutuma wewe na ukweli, Ewe Mtume wa Allaah, sijui vyovyote isipokuwa hivi, Nifundishe.” Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
“Ikiwa unasimama kwa ajili ya Swalaah sema “Allaahu Akbar”. Halafu soma ambacho kitakujia kwa wepesi katika Qur-aan. Kisha rukuu mpaka utakapohisi kwamba umetulia katika rukuu yako. Kisha, simama mpaka uwe umesimama wima kisawa sawa. Kisha, sujudu mpaka uwe umetulia katika sujudu yako. Kisha keti mpaka uwe umetulia katika juluus yako. Kisha sujudu mpaka uwe umetulia katika sujudu yako. Na uwe unafanya hivi ndani ya Swalaah yako yote”.
(Kwahiyo turudi tukarudie Swalah zetu)
Kwanini tunakuja msikitini; nini sababu yetu ya kutekeleza Swalah? Tunafanya hivyo kwa kufuata amri ya Muumba wetu (Subhaanahu wa Ta’ala). Kwanini hasa tupoteze baraka na thawabu kwa sababu ya moyo usiotulia na mkono unaowasha. Khushuu ni kiini cha Swalaah zetu. Khushuu ni matunda ya imani yetu. Lakini, hata baada ya kujua haya, watu hawafanyi juhudi kukamilisha Swalah zao na kwa hiyo huandikiwa sehemu ndogo tu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;
“Kwa hakika, mtu ataondoka (katika Swalaah yake) na ataandikiwa (thawabu) kumi za Swalaah yake; tisa, nane, saba, sita, tano, nne, tatu, nusu.” [Abu Daawuud na at-Tirmidhiy]
‘Uthmaan bin Abii Dahshah (Radhiya Allahu ‘anhu) alisema: “Sijawahi kuswali Swalah ambayo baada yake nilikosa kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anisamehe kwa upungufu wangu katika Swalah ile.”
Mtu ambaye anaharakisha Swalah yake ni mwizi. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema katika Hadiyth sahihi, “Mwizi muovu kuliko wote ni yule ambaye anaiba katika Swalaah yake”. Swahaaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakauliza: “Ewe Mjumbe wa Allaah, anaibaje katika Swalah yake?” Naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakamilishi rukuu na sujudu zake”
Kwa sababu ya kasi ya jinsi ya watu wanavyoswali, wanaonekana kama ndege, wanaodonoa juu na chini. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza mtu kudonoa (katika Swalah) kama kunguru.
‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) wakati mmoja alisimama katika Minbari akiuhutubia umati wa watu kwa sauti ya nguvu akisema, “Mtu anaweza akakulia mpaka utu uzima katika Uislamu na asiweze kamwe kukamilisha kwa ajili ya Allaah hata Swalah moja!” (Watu) wakasema, “Vipi hali hii?” (‘Umar) (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema: “Hakamilishi khushuu yake, hata unyenyekevu wake, hata nadhari yake juu ya Allaah ‘Azza wa Jalla.”
Wakati mmoja, Ma’aruuf Al-Karkhiy (Rahimahu Allaah) aliposimama miongoni mwa wanafunzi wake, mmoja wao akamwambia mwenziwe, “Tafadhali swalisha Swalaah ya ‘Ishaa”. Mwanafunzi wa kwanza akakubali lakini akasema “Nitaswalisha Swalaah ya ‘Ishaa kwa sharti ya kwamba wewe utaswalisha Swalaah ya Alfajiri sio mie” Ma’aruuf Al-Karkhiy alishtushwa na kauli aliyoisema na akasema, “Naapa kwa Allaah, ikiwa unafikiria ya kwamba utakuwa hai wakati wa Alfajiri, basi naapa kwa Allaah, hujakamilisha Swalah yako”.
Sehemu Ya Pili
Jinsi ya kuwa na Khushuu ndani ya Swalah
Al-Qaasim bin Muhammad (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilikwenda nje siku moja, na kila nilipotoka ni lazima nipite kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha) na kumsalimia. Siku hiyo nilitoka na nilipomkuta mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha) akiswali Swalah ya Dhwuhaa, akisoma tena na tena Aayah ya Allaah:
{{Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa (adhabu ya Allaah). Basi Allaah Akatufanyia hisani na Akatulinda na adhabu ya Moto.}} [Atw-Twuur: 26-27]
Alikuwa analia na akimwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na huku akirudia Aayah hiyo. Nilisimama pale mpaka nikachoka, hali ya kuwa yeye amebaki kama nilivyomkuta. Nilipoona haya nilijiambia, “Hebu niende sokoni, nifanye ninachotakiwa kufanya, halafu nije tena”. Kwa hiyo, baada ya kumaliza kufanya nilichotaka kufanya sokoni, nilirudi kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha). Alikuwa kama nilivyomuacha, akirudia Ayaah, akimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na akilia”.
Vipi tuwe na khushuu katika Swalaah?
Katika Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)tunafundishwa yafuatayo:
1. Njoo mapema kwa ajili ya Swalaah na jitayarishe kuwa na khushuu.
Fuatiliza adhana pamoja na Mu’adhin na baada ya adhana, sema dua iliyoamriwa. Omba dua baina ya Adhaana na Iqaamah. Tia wudhuu vizuri, hali ukisukutuwa mdomo wako, na vaa nguo zako nzuri kabisa.
2. Nuia kupata dhawabu zote za Swalaah yako.
Abu Bakr bin ‘Iyaash alisema, “Nilimuona Habiyb bin Thaabit katika sujudu. Ukimuona utadhania kwamba kashakufa (kwa urefu wa sujudu zake).”
3. Zingatia Aayah na adhkaar ambayo inasomwa ndani ya Swalaah.
Fikiria kuhusu maana za Aayah ambazo unazisoma. Je haivunji moyo ya kwamba mtu anaweza kuswali miaka kumi baada ya kumi, siku baada ya siku na pia bado hajui anasema nini? Qur-aan iliteremshwa ili itafakariwe! Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kateremsha (katika Qur-aan Ayaah inayosema):
{{Na hiki Kitabu, Tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.}} [Swaad: 29].
4. Swali Jama’ah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaamrisha:
{{Na simamisheni Swalah, na toeni Zakaah, na rukuuni pamoja na wenye kurukuu.}} [Al-Baqarah: 43].
5. Usikose kamwe kuswali Swalah zako za nawaafil (Sunnah zilizotiliwa mkazo), hasa zile ambazo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali siku zote, kama vile Witri na Sunnah ya Alfajiri.
6. Usiharakishe Swalah yako.
Chukua muda wako na usikubali kuifanya Swalah yako kuwa kitendo kilichokuwa hakina thamani katika siku yako. Ibn Wahb (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilimuona Ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) kwenye Kaa’bah. Baada ya Swalah ya Magharibi, alinyanyuka kuswali na kisha akasujudu. Hakunyanyuka katika ile sujudu mpaka adhana ya ‘Ishaa ilipoadhiniwa.”
7. Jua ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajibu Swalah yako. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyetukuka alisema: “Nimeigawa Swalah kati Yangu na mja Wangu katika nusu mbili, na mja Wangu atapata alichokiomba” [Kutoka katika Surat ul- Faatiha ] Wakati mja anaposema, “Sifa njema zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), Mola wa viumbe vyote,” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Mja Wangu Amenihimidi” . Wakati mja anaposema “Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Mja wangu Amenisifu.” Wakati mja anaposema, “Mwenye Kumiliki Siku ya Malipo”, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema mja Wangu Amenitukuza”. Wakati mja anaposema, “Wewe tu tunakuabudu na wewe tu tunakuomba msaada.” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema, Hii ni kati Yangu Mimi na mja Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba”. Wakati mja anaposema “Tuongoze katika njia iliyonyooka, njia ya uliowaneemesha, sio ya wale uliowakasirikia, wala ya wale waliopotea,” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Hivi vyote ni kwa ajili ya mja Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba” [Muslim]
8. Swali pamoja na kizuizi (weka sutrah) mbele yako na swali karibu yake.
Kitu chengine ambacho kitakusaidia kuwa na khushuu’ [utulivu] ni kushughulika (au kuwa makini) katika suala la kuwa na kizuizi (sutrah) na kuswali karibu yake. Kuwa na sutrah kutazuia uoni wako, kutakulinda juu ya Shaytwaan, na kutazuia watu kupita mbele yako, kitu ambacho husababisha wasiwasi na hupunguza thawabu za Swalah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Ikiwa mmoja wenu ataswali basi na aswali akielekea kwenye sutrah, na awe karibu nayo” [Abuu Daawuud].
9. Tafuta ulinzi] kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na Shaytwaan.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha vipi tupambane na wasi wasi wa Shaytwaan. Abul- ‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu) kasimulia ya kwamba alisema, “Ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Shaytwaan ananisumbua wakati ninaswali, na hupata wasiwasi katika kisomo changu.” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Huyo ni Shaytwaan ambaye jina lake ni Khanzab. Ikiwa utahisi kwamba yupo, jilinde kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana naye, na tema mate (makavu) katika upande wako wa kushoto mara tatu”. Abu’l –‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu) alisema: “nilifanya hivyo na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akaniondoshea.” [Muslim].
10. Swali kama kwamba umeambiwa kuwa baada kumaliza Swalah utarudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Abu Bakr Al-Muzaniy (Rahimahu Allaah) alisema, “Kama unataka Swalah yako ikufae, basi sema: “Nitakufa baada tu ya Swalah hii!”
Kumuoa Mkristo Atakayesilimu Siku Ya Ndoa
SWALI:
Je inakubalika kumuoa Mkiristo atakaesilimu siku ya ndoa?
JIBU:
Sifa
zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah
na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na
watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakuna
tatizo lolote endapo atasilimu kidhati, Imepokewa kutoka kwa Anas
amesema: Abu Twalha alipomuoa Ummu Sulaym, mahari yao ilikuwa ni
kusilimu, Ummu Sulaym alisilimu mwanzo kabla ya Abu Twalha,
alipomchumbia, akasema kwa hakika mimi nimeshasilimu, ikiwa utasilimu
utanioa, akasilimu na ikawa kusilimu ndiyo mahari yao" (An-Nasaaiy
6/114).
Lakini
Muislamu mwanamume awe makini na mwanamke mwenye kutaka kusilimu siku
ya ndoa, isijekuwa ni mwenye kumdanganya akawa anasubiri siku hiyo
wakati ameshatayrisha mambo ya harusi kisha amgeukie. Ikiwa hili ndilo
sharti aliloliweka huyo mwanamke basi nasiha yetu ni kuwa uwe makini na
ujaribu kuchunguza kwanza dhamira yake.
Na Allaah Anajua zaidi
Yajue Mambo Anayopaswa Kufanyiwa Mtu Akifariki
Yampasa Muislam ajiandae kufikiwa na mauti kwa kukithirisha (kufanya sana) matendo mema na kujiepusha na makatazo (vilivyoharamishwa). Vilevile mauti yawe akilini mwake, kwa maneno ya Mtume صلي الله عليه وآله وسلم:
“Zidisheni kukumbuka kiondoshacho ladha (yaani mauti)”. Hadiyth hii imepokewa na Imaam at-Tirmidhiy na akaithibitisha usahihi wake Imaam al-Albaaniy katika kitabu chake Irwaaul-Ghaliyl uk. 682.
Anapofariki Muislam yampasa yule au wale waliopo pale karibu na maiti kumfanyia mambo yafuatayo:
1. Kuyafumba macho ya maiti huyo kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliyafumba macho ya Abu Salamah alipofariki kisha akasema: “Hakika macho yanafuata roho inapotolewa”. Imesimuliwa na Imaam Muslim.
2. Avilainishe viungo vya maiti ili visikakamae.
3. Aifunike maiti hiyo kwa nguo ambayo itasitiri mwili mzima kwa kauli ya mama wa waumini ‘Aaishah:“Hakika alipofariki Mtume صلي الله عليه وآله وسلم alifunikwa kwa nguo iliyomsitiri kote.” Imesimuliwa na Imaam al-Bukhaariy na Imaam Muslim.
4. Waharakishe kuiandaa maiti, kuiosha, kuikafini, kuiswalia na kuizika. Kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم amesema: “Liharakisheni jeneza…” Imesimuliwa na Imaam al-Bukhaariy na Imaam Muslim.
5. Waizike katika mji au eneo alilofia kwa vile katika vita vya Uhud “Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliamrisha mashahidi wa vita wazikwe pahala pale walipofia wala wasihamishwe”.
Imepokewa na Ahlus Sunan (Ma-Imaam Abu Daawuud, an-Nasaaiy,
at-Tirmidhiy, Ibnu Maajah) na ameithibitisha usahihi wa Hadiyth hiyo
Imaam al-Albaaniy katika kitabu chake cha Ahkaamul Janaaiz uk. 14.
[Utangulizi] [Kumuosha maiti] [Kumkafini maiti] [Swala ya jenaza] [Kubeba jenaza na kuzika] [Kuomboleza na taazia]
Subscribe to:
Posts (Atom)