Fadhila za swahumu

Adabu Za Kufunga




Imetayarishwa na Sayyid Saabiq kutoka kitabu cha FIQHUS-SUNNAH
Na kutafsiriwa na Ummu Ummu Ayman
  

Kula Daku (chakula kabla ya Alfajiri)

Imependekezwa kula daku  na hakuna madhambi kwa yule ambae hakufanya hivyo. Anas (radhiya Allahu 'anhu) , ameripoti kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam), amesema: “Kuleni daku, kwani ndani yake kuna baraka” [Al-Bukhaariy na Muslim].
Sababu ni kuwa kula daku kunampa nguvu mfungaji, kunamfanya awe mkakamavu, na kuifanya saumu kuwa ni nyepesi kwake.
Ni Nini kinachotimiza Sunnah ya kula daku:
Sunnah hii itatimizwa kwa kula kiasi kidogo au kikubwa cha chakula, au hata japo kwa kunywa funda la maji. Abu Sa’iyd Al-Khudriy (radhiya Allahu 'anhu)  ameripoti kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Daku ni mlo uliobarikiwa, hivyo usiupuuze japo kwa fundo la maji, Kwani Allaah na Malaika wanamswalia yule mwenye kula daku” [Ahmad]
Wakati wa kula daku:
Wakati wa kula daku ni baina ya usiku wa manane na alfajiri. Inakuwa ni vizuri zaidi kuichelewesha (yaani, karibu zaidi ya alfajiri kwa kadri inavyowezekana). Zayd Ibn Thabit (radhiya Allahu 'anhu), ameripoti:
 “Tulikula daku pamoja na Mjumbe wa Allaah na kisha tukanyanyuka kuswali. Akaulizwa: ‘Ni kiwango gani  (baina ya viwili hivyo) daku na Swalah?’ Akajibu: ‘[Ni kiasi cha kusoma] ayah khamsini’  ” [Al-Bukhaariy na Muslim]


Shaka katika kuingia wakati wa Alfajiri:
Iwapo mtu atakuwa na shaka kama wakati wa Alfajiri umeshaingia au la, anaweza kuendelea kula na kunywa mpaka atapopata uhakika kuwa Alfajiri imeingia. Asitegemeze kitendo chake kwenye shaka au dhana. Allaah Amezifanya dalili za kuingia alfajiri kuwa ziko wazi kabisa na wala hazina utata. Allaah Amesema  “Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.” [Qur-aan, 2:187]
Mtu mmoja alimwambia Ibn 'Abbaas (radhiya Allahu 'anhu)  “ Ninakula mpaka ninapodhani kuwa wakati wake (yaani Daku) umemalizika na ninaacha. Ibn ‘Abbaas (radhiya Allahu 'anhu) akabainisha: “Endelea kula mpaka uwe na uhakika na wakati wake” Abu Daawuud aliripoti kuwa Ahmad Ibn Hanbal (radhiya Allahu 'anhu) amesema: “Iwapo huna uhakika kama  wakati wa alfajiri umeingia au la, basi kula mpaka uwe na uhakika kuwa umeshaingia”.
Kufanya haraka kufutari:
Imependekezwa mtu kukimbilia kufutari wakati wa kuchwa kwa jua. Sahl Ibn Sa’ad (radhiya Allahu 'anhu) , ameripoti kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Watu wataendelea kuwa katika kheri madhali watakuwa wanaharakisha kufutari” {Al-Bukhaariy na Muslim}
Imependekezwa kufutari kwa tende zenye idadi ya witri (isiyogawika kwa mbili) au, kama hapana, basi kwa kunywa maji. Anas (radhiya Allahu 'anhu) ameripoti: “Mjumbe wa Allaah alikuwa akifungua kwa tende mbivu (laini), na anapokosa basi huwa anafungua kwa tende kavu, na anapokosa huwa anafungua kwa maji” Abu Daawuud, Al-Haakim na At-Tirmidhiy}
Sulaymaan ibn ‘Amr (radhiya Allahu 'anhu), ameripoti kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Anapofunga mmoja wenu, basi afungue kwa tende. Akikosa tende, basi afungue kwa maji, kwani maji ni tohara” [Ahmad na At-Tirmidhy]
Dua wakati wa kufutari na wakati wa saumu:
Imehakikishwa kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam), alikuwa akisema wakati wa kufutari: “Kiu kimeondoka, na mishipa imelainika, na kumethibiti malipo kwa uwezo wa Allaah”. [Abu Daawuud na An-Nasaaiy]
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Watu watatu du’a zao hazitokataliwa; Aliyefunga hadi atakapofungua, Imaam muadilifu, na mwenye kudhulumiwa” [At-Tirmidhiy]
Kujiepusha na kufanya tendo lolote ambalo si muwafaka kwa saumu:
Kufunga ni tendo la ibada linalomkaribisha mtu kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala). Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala)  Ameifaradhisha ili Kuisafisha nafsi na Kuizowesha katika matendo mema. Mtu aliefunga ni lazima ajilinde dhidi ya tendo lolote linaloweza kusababisha kupoteza faida za saumu yake. Kwa kufanya hivyo, saumu yake itamuongezea kumjua Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala), na Allaah Anasema katika Qur-aan: Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Saumu, kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu. [Qur-aan, 2:183]  


Kufunga sio kujizuilia kula na kunywa tu, bali pia kujizuilia na jambo jengine lolote ambalo Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala)  Amelikataza. Abu Hurayrah (radhiya Allahu 'anhu), ameripoti kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Funga si kujizuia na kula na kunywa tu, bali pia (kujizuia) na maneno ya kipuuzi na mazungumzo machafu. Anapotukanwa mmoja wenu au kuudhiwa, anatakiwa aseme: “Mimi nimefunga, mimi nimefunga.” [Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaan na Al-Haakim]
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam), pia amesema: “Mwenyeezi Mungu hana haja na saumu ya yule asiyejizuia na maneno ya uongo na matendo yake” [Al Bukhaariy]

Abu Hurayrah, (radhiya Allahu 'anhu) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Huenda mwenye kufunga asipate ujira wowote wa kukaa kwake na njaa, na huenda yule mwenye kusimama kisimamo cha usiku (kusali) asipate chochote kwa kusimama kwake ila kuacha kulala” [An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Al-Haakim]

Kupiga mswaki:
Imependekezwa kwa mtu aliyefunga kupiga mswaki. Hakuna tafauti iwapo atapiga mswaki mwanzo au mwisho wa siku. Imehakikishwa kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) alipiga mswaki huku akiwa amefunga.

No comments: