Monday 16 November 2015

Holy Quran - Recitation of Sheikh Ali Abdullah Jabir

Historia Ya Waja Wema Kwa Kifupi - Karne Ya kwanza

KARNE YA KWANZA (1H - 99H)
Imefasiriwa Na:
Abu Sumayyah
‘Abdullaah Abu Jaabir (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Abdullaah Abu Jaabir bin ‘Amr bin Hazzam bin Tha’labah al-Answaariy al-Khazrajiy as-Sulamiy, ni miongoni mwa waliotoa ahadi ya ‘Uqbah. Alihudhuria vita vya Badr na alikufa shahidi katika vita vya Uhud.
‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Abdullaah bin ‘Abbaas bin ‘Abdul-Muttwalib bin Haashim bin ‘Abd Manaaf al-Qurashiy al-Haashimiy, alikuwa ni binamu yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mfasiri wa Qur-aan. Alizaliwa miaka mitatu baada ya Hijrah na alikuwa anaitwa ‘Bahari ya Elimu.’ Alishiriki katika Jihaad kule Kaskazini mwa Afrika kwenye mwaka 27H na alikufa mwaka 68H.
‘Abdullaah bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Abdullaah bin ‘Amr bin al-’Aasw bin Waail bin Haashim bin Su’ayd bin Sa’d bin Sahm as-Sahmi. Yeye na baba yake walikuwa ni Maswahaba. Alikuwa anajua kusoma na kuandika na alipata ruhusa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuandika yote yale aliyokuwa akiyazungumza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa katika mwaka 65H.
‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Alikuwa Swahaba mkubwa wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ‘Abdullaah bin Mas’uwd bin Ghaafil bin Habiyb (Radhiya Allaahu ‘Anhu), alikufa katika mwaka 32H huko Madiynah. Az-Zubayr aliongoza Swalah ya Janaazah lake na kuzikwa Baqiy’.
Alikuwa ni mtu wa sita kusilimu hata kabla ya ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimbashiria makazi yake Peponi. ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alitaja jambo hii kusema ya kwamba Mtume alimuamuru Ibn Mas’uwd kupanda mti kuchuma kitu fulani na kuleta chini. Maswahaba walikuwa wakiangalia miundi ya Ibn Mas’uwd wakati akipanda mti na waliaanza kumcheka kutokana na uwembamba wa miundi yake. Mjumbe wa Allaah alisema: “Ni kitu gani kinachowachekesha? Miguu ya Ibn Mas’uwd ni mizito kwenye mizani siku ya Qiyaamah kuliko Mlima Uhud.”
[Imesimuliwa na Imaam Ahmad katika Musnad yake na kuthibitishwa na Shaykh Ahmad Shaakir (920)].
‘Abdullaah bin Mas’uwd alikuwa msomaji mkubwa wa Qur-aan. Inasemekana alikuwa ni mmoja wa watu wenye kufuata kwa karibu sana muongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Imekusanywa kutoka kwenye kitabu cha Siyaar A‘laam an-Nubalaa - cha Adh-Dhahabiy na Tahdhiyb At-Tahdhiyb cha Ibn Hajr.
Abu ad-Dardaa (Radhiya Allaahu ‘Ahnu)
Abu ad-Dardaa Uwaymir bin Maalik bin Zayd bin Qays al-Khazrajiy al-Answaariy. Kuna maoni tofauti kuhusu jina lake. Alisilimu wakati wa vita vya Badr na alishuhudia vita vya Uhud. Alikuwa ni Mwanachuoni wa Shari’ah. Mchaji Allaah miongoni mwa Swahaba. Alikufa katika mwaka 32H.
Abu Dharr al-Ghifaariy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu Dharr al-Ghifaariy Jundub bin Junaadah bin Sakn alikuwa ni miongoni waliosimu mwanzoni lakini alichelewa kufanya Hijrah hivyo hakushiriki vita vya Badr. Fadhila zake ni nyingi na alikufa mwaka 32H.
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu Hurayrah, ‘Abdur-Rahmaan bin Swakhr ad-Dawsiy alikwenda kwa  Mtume kama Muhaajir wakati wa vita vya Khaybar. Alihifadhi idadi kubwa ya Hadiyth. Zaidi ya Hadiyth elfu nane zilisimuliwa kutoka kwake. Alikufa katika mwaka 58H.
Mtume Alimuombea du’aa yeye na mama yake kwa kusema: “Ee Allaah! Wajaalie hawa waja wako (wawili) ni wenye kupendwa na Waumini na wafanye Waumini ni wenye kuwapenda.” [Imesimuliwa na Muslim].
Abu Muwsaa al-Asha’riy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu Muwsaa al-Ash’ariy ‘Abdullah bin Qays bin Saalim alikuwa ni mwenye sauti nzuri wakati wa kusoma Qur-aan na ni mmoja wa Wanachuoni  miongoni mwa Maswahaba. Inasemekana alikufa mwaka wa 42H au 44H.
Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Abu Sa’iyd al-Khudriy Sa’ad bin Maalik bin Sinaan bin ‘Ubayd al-Answaariy al-Khazrajiy. Yeye na baba yake wote walikuwa ni Maswahaba na alishuhudia vita vyote vilivyofuata baada ya vita vya Uhud. Alikuwa ni mmojawapo wa Wanachuoni miongoni mwa Maswahaba na alisimulia Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa katika mwaka 74H.
‘Adiy Bin Haatim (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Adiy bin Haatim bin ‘Abdillaah bin Saa’d bin al-Hashraj bin ‘Aamr al-Qays at-Twaaiy, Abu Tarif. Alikuwa Mkristo aliyesilimu na kuhudhuria vita vya Jamal, Swiffiyn na an-Nahrawaan pamoja na ‘Aliy. Alikufa katika mwaka 68H.
Al-Bara’a bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Al-Bara’a bin Maalik bin an-Nadr al-Answaariy.Alihudhuria vita vya Uhud na alitoa ahadi ya utii chini ya mti. Alikufa shahidi katika mwaka wa 20H kwenye siku Tustar.
Al-Mughiyrah Bin Shu’bah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Al-Mughiyrah bin Shu’bah bin Abi ‘Aamir bin Mas’uwd ath-Thaqafiy, Abu ‘Abdillaah. Alihudhuria vita vya Hudaybiyyah, Al-Yamaamah na alipata ushindi kule Syria na Iraq. Alikufa katika mwaka 50H.
‘Amr Bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
‘Amr bin al-’Aasw bin Wa’il al-Qurashiy as-Sahmiy Alisilimu katika mwaka wa Sulhu Hudaybiyyah na alikuwa ni mmoja wapo kati ya wale walioshinda  kule Misr. Alifariki katika mwaka 43H.
Anas Bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Anas bin Maalik bin an-Nadr, Abu Hamzah, al-Answaariy, an-Najjaariy. Alikuwa mfanyakazi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). ambaye alikaa nae karibu kwa takriban miaka kumi tangu alipohama mpaka kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa ni miongoni mwa Maswahaba wa mwisho kufariki. Alifariki akiwa na miaka 93H kule Baswrah akiwa na miaka 103.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alimuombea du’aa kwa kusema: “Ee Allaah Mjalie utajiri na watoto na Vibariki vile ulivyomruzuku.” [Muslim].
Na katika mapokezi mengine Anas Aliongezea kwa kusema: “Na (kutoka kwa) Allaah fungu langu imekuwa kubwa watoto wangu na wajukuu wameongezeka kiasi cha kufikia mia moja kwa kuwahesabu.” [Muslim].
‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha)
‘Aaishah bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhuma). Mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baada ya Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘Anha) kufariki, Malaika Jibriyl alimuonyesha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye ndoto kabla ya kumuoa na alikuwa na miaka kumi na nane wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki.
Alifariki katika mwaka 59H kwenye tarehe kumi na saba ya mwezi wa Ramadhwaan. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alimzika.
Alikuwa Mama wa Waumini Asw-Swiddiyqah (Radhiya Allaahu ‘Anha). ‘Umar alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni nani unayempenda zaidi miongoni mwa watu? Akajibu: ‘Aaishah’. Kisha, akamuuliza miongoni mwa wanaume (ni nani unayempenda zaidi)? Akajibu: Baba yake.”
Ash-Sha’abiy alisema: Wakati Masruwuq anatusimulia kuhusu ‘Aaishah, alisema: ‘Niliambiwa na mkweli, bint wa mkweli, mpendwa miongoni mwa vipenzi vya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Asiye na hatia ambaye ndoa yake ilianzishwa kutoka mbingu ya saba.
Az-Zuhriy alisema: “Iwapo elimu ya Mama ‘Aaishah itakusanywa na kulinganishwa na elimu ya wakeze wengine Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wanawake wengine wote basi elimu ya Mama ‘Aaishah ingelibakia kuwa isiyo na kifani.”
‘Imran Bin Huswayn (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Imran bin Huswayn al-Khuza’iy al-Ka’biy, Abu Nujayd. Alisilimu mwaka wa vita vya Khaybar na aliripoti baadhi ya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa katika mwaka 52H.
Jaabir Bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Jaabir bin ‘Abdillaah bin ‘Amr bin Harram al-Answaariy as-Sulamiy. Alishuhudia ‘Uqbah wakati wa pili huku akiwa mtoto. Inasemekana alihudhuria vita vya Badr na Uhud na kuripoti Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alifariki katika Mwaka wa 74H.

Tuesday 25 August 2015

 
Mola wetu Mtukufu Amemuumba mwanaadamu katika umbo bora lisilomithilika na kiumbe chochote. Naye ameumbwa kwa kutumia udongo uliopulizwa roho itokayo kwa Mola Mlezi.
 
Akamjaalia mwanaadamu ni mwenye kupata shida, mitihani, mtenda dhambi na mwenye kupata maradhi. Hakusita hapo Mola wetu Mtukufu, bali Akajaalia mlango wa pili wa kutokea kwenye mashaka ya dunia; Akajaalia kuwepo starehe, utulivu, toba na afya. Basi ni kwa neema zipi mwanaadamu anaweza kumlipa Mola wake!?
 
Tutambue kwamba hii roho tuliyokuwa nayo yatosha kuwa ni sababu ya kushukuru neema za Mola Mlezi kwa vitendo na kauli. Tusisahau wapi tulipotoka na wapi tunaelekea, hatukuwa chochote miaka 100 iliyopita. Basi ni nani kati yetu alikuwa na uhakika kwamba atadhihiri duniani kwa jina na umbo lake kabla ya kuzaliwa? Kuwa na adabu kwa kumcha Mola wako!
 
Muislamu yupo juu ya mgongo wa ardhi akiruzukiwa kila chenye manufaa na yeye, ni mwenye kula akapata njia ya kutolea uchafu, na siku uchafu unaposhindwa kutoka ndani ya tumbo ndio unaelewa umuhimu wa neema ya kuyeyusha chakula kwenye mwili. Ameumba kila kitu kwenye kiwango maalumu, kwani tumbo likiyeyusha kupita kiwango, mwanaadamu ataugua maradhi ya tumbo la kumuendesha. Hivyo, kumbuka na yazingatie maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{Na mkihesabu neema za Allaah hamtaweza kupata idadi yake. Hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.}} [An-Nahl: 18]
 
Basi elewa ndugu yangu, kwamba sisi si chochote si lolote zaidi ya tone la manii lililoengwa engwa hadi likafikia miezi tisa likaweza kutoka kwa sura ya mwanaadamu. Ndani ya tumbo, Mola wetu Mlezi Alitulinda na wala hatukuhitaji askari, jeshi, polisi, ultimate security au mwengineye. Ukatoka kwa ukenya wa kilio cha juu ukiomba msaada kwa mama yako. Ukafikia baleghe ukaweza kuoa/kuolewa na sasa kwa Qadar ya Mola unaweza nawe kupata mtoto. Aliyekuwa mbabe kati yetu azihesabu neema ngapi zimepita baina ya kuzaliwa kwake hadi hivi sasa, kisha aangalie ni kwa kiwango gani ataweza kuzishukuru neema hizo. SubhaanaLlaah! Yuko umbali gani mwanaadamu kwa kuzitilia maanani neema za Mola wake?
 
Ugeuze uso wako, uangalie mbingu ilivyotanda na ardhi ilivyotandikwa, kisha useme kwamba Mola wako amekutupa. Rizki zako Akazimimina kutoka mbinguni na Akazichimbua kutoka ardhini. Ni kipi basi katika chakula chako kitokacho nje ya mfumo huu? Basi kwa Kiburi Chake Mola Mlezi Anastahiki kuyaambia makundi ya wanaadamu na majini:
{{Enyi jamii ya majini na watu! Kama mtaweza kupenya katika mbingu na ardhi (ili mkimbie Nisikupateni), basi penyeni (Nikuoneni)! Hamtapenya ila kwa nguvu (Zangu. Nikikupeni nguvu hizo mtaweza).}} [Ar-Rahmaan: 33]
 
Tumcheni Mola wetu kwa kila kitu, kwa dogo na kubwa, kwa tunayoyajua na tusiyoyajua. Tutende mema kabla ya kutufika yale yasiyoweza kuhimili miili yetu. Wahenga wanatuambia: "Kijua ndi hichi usipouanika utaula mbichi."
 
 
 
Uchungaji wa viungo vya Muislamu katika maisha haya umekuwa ni wa chini usio na maana yoyote. Mkono unaiba, mguu unampeleka baa au kuzini, na ulimi unadiriki kutoa kiapo cha uongo.
 
Ulimi ni kiungo kimoja ambacho chatumiwa vibaya mno takriban na wanaadamu wote, na ndani yake kuna kundi kubwa la Waislamu ambao hawajali yale yanayotoka ndani ya vinywa vyao.
 
Tutambue kwamba, kiapo juu ya viumbe ni haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuviapia. Ni kwa mfano pale Anaposema: Ninaapa kwa Siku ya Qiyaamah, Ninaapa kwa Jua na kadhalika. Mwanaadamu yeyote hana ruhusa ya kutoa kiapo kama hicho.
 
Kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kiapo cha Muislamu kinaelekezwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na nini maana ya kiapo? Kiapo ni kuweka dhamana ya lile unalosema kwa Yule Unayemwapia. Kwamba hayo unayoyaapia ni ya kweli unahitaji kusadikiwa na wanaadamu wenzio. Basi ole wake yule ambaye anaweka kwa Muumba wake kiapo cha uongo.
 
Hivyo, kiapo ni chenye kuchungwa mno na wala sio kukifanya kuwa ni dhikri ya ulimi ukataka kila kitu kukifanyia kiapo hadi kuwa ni sababu ya kutumbukia kwenye dimbwi la moto. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuambia tusimtii yule mwenye kuapa kila wakati:
{{Wala usimtii kila muapaji sana, aliye dhalili.}} [Suratul-Qalam: 10]
 
Kitu ambacho kimejaa ndani ya maisha yetu Waislamu ni viapo visivyokuwa na kichwa wala mguu. Na kila wanapokumbushwa wao wanaufanyia kazi ule msemo: "Kelele za mlango hazimughasi mwenye nyumba". Wanakuwa hawajali wala hawakubali maneno ya Qur-aan au Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
 
 
Mtume wetu amekataza mno Muislamu kula kiapo ovyo ovyo. Kinyume chake Muislamu anakula kiapo cha uongo katika biashara ingawa Mtume wetu amesema kwamba Allaah Hatamuangalia (kwa jicho la huruma) mtu namna hiyo Siku ya Qiyaamah. [Imesimuliwa na Abu Dharr na kupokelewa na Muslim].
 
Lililo kubwa ndani ya jamii zetu ni kufikishana mbele ya vyombo vya sheria kwa namna za udanganyifu, utapeli na uongo mtupu. Muislamu anadiriki kuweka kiapo cha uongo kwa Mola wake ili apate mali ya mwengine bila ya halali. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesimuliwa akisema kama ilivyopokewa na Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘Anha):
 
((Mimi ni binaadamu tu na nyinyi mnaleta migogoro yenu kwangu mimi, mukiwa wenye fasaha katika viapo vyenu kuliko wengine, ili ya kwamba nitoe hukumu kwa niaba yenu kwa mujibu wa ninayoyasikia kutoka kwenu. Hivyo, vyovyote nitakavyoamua kwa yeyote, ambapo kwa haki ni ya ndugu yake, asichukue kwani simpatii chochote ila kipande cha moto.))
[Imepokewa na Al-Bukhaariy].
 
Tunawanasihi wale waliochukua viapo vya uongo wakamilikishwa mali kwa njia za haramu wazirejeshe amana hizo haraka iwezekanavyo. Ya Ar-Rahmaan! Na wapo miongoni mwa viumbe Vyako waliokula kiapo kwa kudhulumu mayatima na wakala kiapo kwa lengo la kuzini na wake za watu. Umetakasika! Shingo zao zipo mikononi Mwako!
 
Ya Allaah! Tunategemea kwako, na tunageuka kuja Kwako, na Kwako tu ndiko marejeo yetu. Basi tunakuomba Mola wetu! Tutimizie nuru yetu, na Utughufirie, hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
 

Toa Swadaqah Kwa Ajili Ya Allaah

 
Naaswir Haamid
 
 
Ihsaan ni kinyume cha ufisadi, na miongoni mwa Ihsaan ni kufanya wema bila ya kujali mipaka ya Kaskazi wala Kusi, na kutoa kwa ajili ya Allaah ni wema na Ihsaan kwa mwanaadamu.
 
Hakuna shaka yoyote kwamba Swadaqah ni katika tabia njema, na iwapo tutafungua kurasa za Siyrah za wema waliotangulia, tutaona kwamba walikuwa wakikithiri mno kwenye kutoa Swadaqah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
{{Chukua Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao).}} [At-Tawbah: 103]
 
Kupitia Tamko hilo hapo juu, tunafahamu kwamba kumbe kuisafisha nafsi kutokana na takataka za upungufu na kuiinua jamii mpaka kuifikisha kwenye daraja tukufu kabisa, ndio hekima ya juu. Ni kwa ajili hii ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanua wigo katika kuelezea maana ya neno “Swadaqah” ambayo Muislamu anatakiwa kuitoa, akasema:
((Tabasamu lako usoni kwa nduguyo (Muislamu mwenzio) ni Swadaqah, kuamrisha kwako mema na kukataza kwako maovu ni Swadaqah. Na kumuongoza kwako njia mtu katika ardhi (nchi) ya upotevu, hilo kwako ni Swadaqah. Na kuondosha kwako njiani udhia, mwiba na mfupa, hilo kwako (nalo) ni Swadaqah. Na kumtekea kwako maji nduguyo, kwako ni Swadaqah na kumsaidia kwako mtu dhaifu wa uoni kuongoza njia, (hilo nalo) kwako ni Swadaqah)). [Al-Bukhaariy]
 
Swadaqah huanza kwa kuuzoesha mkono kutoa kila mara bila ya kinyongo wala manuuniko. Mkono una dhima kuu ya kukulingania kutoa Swadaqah katika vile ulivyoruzukiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama Alivyosema:
{{Yule anayetoa (Zakaah, Swadaqah na vinginevyo) na kumcha Allaah. Na kusadiki jambo jema (akalifuata). Tutamsahilishia njia ya kwenda Peponi.}} [Al-Layl: 5-7]
 
Hiyo ndio faida na jazaa ya aliyeutumia vyema mkono wake katika kutoa Swadaqah. Akautumia mkono wake katika kutoa vile Alivyoruzukiwa na Allaah Ar-Razzaaq, katika kuisadia jamii na kuupeleka mbele Uislamu.
 
Ni vyema ukakumbuka kwamba kutoa katika mambo ya khayr ni katika kuishukuru neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ambako hakumaanishi ila kuzidishiwa neema, tusome kwa mazingatio:
{{Na (kumbukeni) Alipotangaza Mola wenu (kuwa): "Kama mkishukuru, Nitakuzidishieni; na kama mkikufuru, (jueni) kuwa adhabu Yangu ni kali sana.}} [Ibraahiym: 7]
 
"Mtenda wema hutendea nafsi yake na mtenda ovu humrejea mwenyewe". Hivyo elewa kamba kuishukuru neema kikweli kweli na kuitumia vile inavyostahiki sio tu kusema au kuandika kwenye milango kwa mbwembwe: ‘AlhamduliLlaah’ au ‘Hadha Min Fadhli Rabiy’! Na ni ubaya ulioje kuzitumia neema hizi kinyume na vile Alivyoamrisha Ar-Razzaaq.
Dunia ni tamu na kawaida ya mwanaadamu kupenda mazuri mno. Hujitahidi kadiri ya juhudi zake kukusanya yale ayaonayo kuwa ni yenye kufurahisha nafsi yake. Hutafuta yale yenye laghai na anasa - 'material world'.
 
Hilo halina shaka na hata Qur-aan na Sunnah yatuthibitishia kwamba dunia imeumbwa kuunganishwa na matamanio ya mwanaadamu. Lakini sio yote ambayo Muislamu anatakiwa kuyatilia mkazo kwa kuyavamia. Ndio lengo la kuwepo halali na haramu ndani ya Uislamu ili kumtofautisha mwanaadamu na Muislamu.
 
Waislamu walio wengi kabisa wanatamka shahaadah ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni Mmoja na Ndiye Apaswaye kuabudiwa pamoja na kutiiwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kikomo cha wengi kinamalizia hapa kwenye kauli tu. Matendo yao yanakuwa kinyume na kauli hii. Hivyo, hufanya ibada kwa kudanganya macho ya waumini, kwani wanatenda mbele ya kadamnasi, wanapokuwa peke yao huingia kwenye hiyo 'material world' kwa mapana na marefu. Hiyo sio iymaan inayopigiwa mfano na Mola Mlezi:
 
{{Ambao wanamuogopa Mola wao (hata) wanapokuwa faraghani, na pia hukiogopa Qiyaamah.}} [21:49]
 
Taariykh yatufunza kwamba Waislamu hapo kale walilelewa kwenye Tawhiyd ya kumuamini Allaah pamoja na Malaika, Mitume, Vitabu, Siku ya Mwisho, Qadar kheri na shari. Kwa wakati wa sasa ni Kitabu cha Qur-aan pekee ndicho kilicho mbele ya macho yetu. Vilivyobaki vyote vinabaki kuwa nyuma ya pazia 'ghayb'.
 
Imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu): amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba:
"Iymaan ni kumuamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Kukutana Kwake (Siku ya Qiyaamah), na Mitume Wake na kuamini ufufuo wa Siku ya Mwisho." (Imepokewa na Shaykhaan)
 
Kukosa kuamini moja ya nguzo za iymaan, kunapelekea kutoamini ghayb. Hivyo, kuanguka kwa iymaan ya ghayb kutasababisha kuondoka iymaan ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Yupo.
 
Ni ghayb hii inayomfanya mwanaadamu na hata Muislamu kutotilia mkazo kuutafuta ukweli halisi wa Uislamu, ghayb ndiko kunakomfanya Muislamu kutotenda mema kwa lengo la kupata ridhaa ya Allaah. Thawabu wala dhambi hazioni mtu, Malaika wanaoandika mema na maovu nani anayewaona? Haya yote yapo kwenye ghayb. Muislamu anatakiwa kuamini hii ghayb bila ya mjadala. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuambia:
 
{{Tendeni mambo (mazuri). Allaah Atayaona mambo yenu hayo na Mtume Wake na Waislamu. Na mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri; Naye Atakwambieni (yote) mliyokuwa mkiyatenda.}} [9:105]
 
Apambanue Muislamu juu ya kukosa kwake iymaan ya ghayb na kuirudisha nyuma akili kabla ya kuwepo kwake; yeye alikuwa ni nani? Nani aliyemhifadhi ndani ya tumbo la mama kwa miezi tisa? Hivyo, ghayb ni wajibu kuiamini na kwamba yapo mambo nyuma ya macho yetu yanatokea au yapo tayari kutokea.
 
Kukosekana kwa iymaan ya ghayb ndani ya nafsi ya Muislamu ndio kwamfanya awache himma ya kutenda mema. Ni sababu hii inayowafanya vijana walio wengi kujishughulisha mno na ratiba za mipira inayokula muda wa Waislamu. Nao kina dada kutilia mkazo urembo, mikusanyiko ya haramu na kutembea kwao utupu kunatokana na kukosa kwao kuamini ghayb.
 
Basi na aangalie Muislamu alivyoumbwa, chakula chake kinavyoyayushwa na kugaiwa sehemu mbali mbali. Vitamini, damu, madini, sukari, chumvi, mafuta na vyengineo; vyote vinapelekwa na kuhifadhiwa sehemu zake maalum. Atupe jicho lake kwa kuangalia linapotoka na kuzama jua, tofauti ya usiku na mchana, hali ya uzima na ugonjwa, maisha na mauti na mengineyo:
 
{{Naye ndiye Aliyeziumba mbingu na ardhi kwa haki. Na wakati Anaposema (kuliambia jambo): "Kuwa," basi huwa… Mjuzi wa ya siri na dhahiri…}} [6:73]
 
Basi ni mengi yaliyopo Mkononi Mwako yaa Allaah! Namna tutakavyojifunza katu hatutafikia chembe ya 'ilmu Yako. Hivyo, tunatamka kama ambavyo Umetufunza:
 
{{Wewe Umetakasika na kuwa na mshirika. Hainijuzii mimi kusema ambayo si haki yangu. Kama ningalisema bila shaka Ungalijua; Unayajua yaliyomo nafsini mwangu, lakini mimi siyajui yaliyomo nafsini Mwako; hakika Wewe Ndiye Ujuaye mambo ya ghayb.}} [5:116]

Wasiya Wa Pili Wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – Swalaah Ya Adhw-Dhwuhaa.

Imetajwa pia katika Hadiyth ya Abu Ad-Dardaai kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemuusia naye mambo matatu kama aliyomuusia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), nayo ni: Swiyaam (kufunga) siku tatu, kuswali Swalaah ya adhw-dhwuhaa na kuswali Swalaah ya Witr kabla ya kulala,
وعَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ رضي الله عنه قَالَ : "أَوْصَانِي حَبِيبِي صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِثَلَاثٍ لَنْ أَدَعَهُنَّ مَا عِشْتُ : بِصِيَامِ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ، وَصَلَاةِ الضُّحَى  وَبِأَنْ لَا أَنَامَ حَتَّى أُوتِرَ"   رواه مسلم  
Imepokelewa kutoka kwa Abu Ad-Dardaai (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: “Ameniusia mpenzi wangu Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam [mambo] matatu nisiyaache maishani mwangu; Swiyaam (kufunga) siku tatu kila mwezi na Swalaah ya Adhw-Dhwuhaa na nisilale mpaka niswali Witr” [Muslim]

Swalaah ya Adhw-Dhwuhaa – Fadhila zake, idadi ya raka’ah zake na wakati wake:

Ukumbusho Wa Swiyaam (Funga) za Ayyaamul-biydhw (Masiku meupe) Dhul-Qa'dah 1436H

SWIYAAM (FUNGA) SIKU TATU KILA MWEZI THAWABU ZAKE NI SAWA NA THAWABU ZA SWIYAAM YA MWAKA!
Tunapenda kuwakumbusha Swiyaam (funga) za Ayyaamul-biydhw (masiku meupe) ambayo ni tarehe 13, 14, 15 katika kila mwezi wa Kiislaam (Hijriyyah). Masiku hayo mwezi huu wa Dhul-Qa’dah 1436H, yataangukia tarehe 28, 29, 30 August (Ijumaa, Jumamosi, Jumapili). Bonyeza 'Endelea' upate fadhila kadhaa za Ayyaamul-biydhw na fadhila za Swiyaam siku tatu kila mwezi, pamoja na fadhila za Swiyaam kwa ujumla.  Soma  na utekeleze ili ufaidike na ujichumie thawabu tele In Shaa Allaah.  Na hakuna tawfiyq isipokuwa ya Allaah ‘Azza wa Jalla, Kwake tunatawakali na Kwake tunarudia kutubia.

Nasiha Za Minasaba Mbali Mbali

Tumeingia Katika Miezi Mitukufu Inatupasa Kuitakasa Kwa Kuacha Maovu Na Kuzidisha Mema

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُم))

((Hakika idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allaah, tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo)) [At-Tawbah: 36].

Miezi minne hiyo imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:
  عَنْ أَبَى بَكْرَة أَنَّ رَسُول اللَّه - صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - قَالَ فِي حَجَّة الْوَدَاع : ((إِنَّ الزَّمَان قَدْ اِسْتَدَارَ كَهَيْئَتِهِ يَوْم خَلَقَ اللَّه السَّمَوَات وَالْأَرْض السَّنَة اِثْنَا عَشَر شَهْرًا مِنْهَا أَرْبَعَة حُرُم : ثَلَاث مُتَوَالِيَات ذُو الْقَعْدَة وَذُو الْحِجَّة وَالْمُحَرَّم وَرَجَب مُضَر الَّذِي بَيْن جُمَادَى وَشَعْبَان)) صَحِيح الْبُخَارِيّ

491- Hakuna Mjinga Mkubwa Katika Dini Kama Huyu! - ´Allaamah al-Luhaydaan

Wednesday 29 July 2015

Complete Mp3 Al Qur'an 30 Juz - Syeikh Maher Al Muaiqly

Rudi Tena Ukaswali, Kwani Hukuswali


Imefasiriwa na Ilyaasa Mawlaana


Kwa jina la Allaah, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu.


Sehemu Ya Kwanza

Katika usiku wa giza, Abu Lu’lu’ Al-Majuusi (kipenzi cha Mashia) alijificha katika vivuli akijiandaa kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri, wakati ambapo ataendesha mipango yake ya kishetani kumuua Amiyr wa waumini – ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allahu ‘anhu).

‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) alikuwa (na kawaida) ya kuongoza Swalah ya Alfajiri huku akisoma surah ndefu, akiwapa wafuasi wa jamii, muda wa kuhudhuria mkusanyiko (wa Swalaah). Katika siku hii, wakati (‘Umar) akisoma (Qur-aan), Abuu Lu’Lu’ akachukua hatua kutoka kwenye nguzo inayofifia, hali ya kuwa ana kisu cha sumu katika mkono wa vazi lake. Akaruka mbele ya ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) na akamkata tumbo wazi kwa (kile) kisu. Baada ya hapo, akajaribu kuukimbia mkusanyiko. Akiwa ana chana chana mbele na nyuma, akiwauwa watu wengi zaidi ambao walikuwepo katika njia yake. Swahaabah mmoja akamtupia nguo juu yake na alipo tahayari kwamba keshakamatwa Abu Lu’lu’ akajiua. 
‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allahu ‘anhu) akaikamilisha Swalaah ya Alfajiri ambayo aliianza ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu). ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) alikamilisha Swalaah yake hali ya kuwa ni miongoni mwa watu (maamuma) katika Jama’ah na akafariki dunia baadaye katika kitanda chake, (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Umuhimu wa Swalaah katika Uislamu hauwezi kudharauliwa. Ni nguzo ya kwanza ya Uislamu iliyotajwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya tamko la Imani (shahaadah), ambayo kutokana nayo mtu huwa Muislamu.

Swalaah imefaradhishwa kwa Manabii na watu wote. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alitangaza hadhi yake ya kuwa ni faradhi katika tukio Tukufu. Kwa mfano, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipozungumza na Muusa (‘Alayhis Salaam), Amesema:

{{Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayofunuliwa. Hakika Mimi ndiye Allaah. Hapana muabudiwa wa haki ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Swalah kwa ajili ya kunikumbuka Mimi}} [Twaaha: 13-14]

Hivyo hivyo, Swalaah imefaradhishwa kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipopelekwa mbinguni. Zaidi, wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anawasifu waumini kama katika Suratul-Al-Mu-uminuun, moja katika sifa ambazo Anazitaja kuhusiana nao ni kule kushikana kwao na Swalaah:
{{Hakika wamefanikiwa Waumini. Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao}} [Al-Mu’minuun: 1-2]

Umuhimu wa Swalaah unaendelea kuonyeshwa katika kauli nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mfano, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

“Jambo la kwanza ambalo mja atahukumiwa katika Siku ya Hisabu ni Swalaah. Kama ikiwa ni nzuri basi amali zake zilizobakia zitakuwa nzuri. Na ikiwa ni mbaya, basi amali zake zilizobakia zitakuwa mbaya.” [At-Twabaraaniy].
Kwa kweli, ikiwa Swalaah imeswaliwa vizuri ikiambatana na ukumbusho  wa kweli wa kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na kumgeukia Yeye kutaka msamaha, itakuwa na athari kubwa juu ya mtu kwa kipindi  kirefu. Mtu anapokamilisha Swalaah yake, moyo wake utajaa ukumbusho wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Atakuwa ana hofu na pia vilevile matarajio juu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Baada ya tukio hilo, hatotaka tena kuondoka kutoka katika sehemu hiyo ya fakhari kuelekea kwa ile ambayo ndani yake atamuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anaitaja hali hii ya Swalaah katika Qur-aan:  

{{Hakika Swalah inazuilia mambo machafu na maovu}} [Al-‘Ankabuut: 45].

Lakini katika wale ambao wanaoswali, utakuta kuna vitendo vya kivivu ambavyo vinahitaji kumulikwa. Kwa mfano:

·         Wengine hawazingatii kile ambacho wanakisema.
·         Wengine wanafanya haraka katika Swalah zao
·         Wengine wanaachilia nadhari yao ya macho izurure wakati wa Swalah
·         Wengine mara kwa mara husahau nambari ya rakaa zilizotimizwa.
·         Dunia inakumbatia mioyo ya baadhi ya watu wakati wa Swalah na inafunika akili zao.
·         Na watu wengine katika Jamaa’ah wanaanza kusujudu kabla hata ya Imaam kusema “Allaahu Akbar”

Linganisha hii (hali yetu katika Swalaah) na Swalaah za watu ambao walikuja kabla yetu. Watu walikuwa wanafikiria ya kwamba Ar-Rabiy’ bin Khaytham alikuwa ni kipofu kwa sababu ya kuinamisha macho yake mara kwa mara. Alikuwa akiishi nyumbani kwa Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allahu ‘anhu) kwa miaka ishirini na mtumwa wake wa kike akimuona alikuwa akisema: “Rafiki yako kipofu anakuja” na Abdullaah alikuwa akimcheka kwa kauli yake.

Ndani ya Al-Bukhaariy na Muslim, Abuu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) anatueleza ya kwamba, kuna mtu aliingia msikitini, ambao Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa. Akaswali rakaa mbili na kisha akaja kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu salamu yake na halafu akasema, “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.” Hivyo, yule mtu akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara ya kwanza, akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu salamu na akasema “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.” Hivyo, yule mtu akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara ya kwanza akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu salamu kwa mara nyingine tena na kwa mara nyingine tena akasema: “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali”. Hadi kufikia mara hii ya tatu, mtu huyo alisema: “Naapa kwa Yule ambaye alikutuma wewe na ukweli, Ewe Mtume wa Allaah, sijui vyovyote isipokuwa hivi, Nifundishe.” Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Ikiwa unasimama kwa ajili ya Swalaah sema “Allaahu Akbar”. Halafu soma ambacho kitakujia kwa wepesi katika Qur-aan. Kisha rukuu mpaka utakapohisi kwamba umetulia katika rukuu yako. Kisha, simama mpaka uwe umesimama wima kisawa sawa. Kisha, sujudu mpaka uwe umetulia katika sujudu yako. Kisha keti mpaka uwe umetulia katika juluus yako. Kisha sujudu mpaka uwe umetulia katika sujudu yako. Na uwe unafanya hivi ndani ya Swalaah yako yote”.


(Kwahiyo turudi tukarudie Swalah zetu)

Kwanini tunakuja msikitini; nini sababu yetu ya kutekeleza Swalah? Tunafanya hivyo kwa kufuata amri ya Muumba wetu (Subhaanahu wa Ta’ala). Kwanini hasa tupoteze baraka na thawabu kwa sababu ya moyo usiotulia na mkono unaowasha. Khushuu ni kiini cha Swalaah zetu. Khushuu ni matunda ya imani yetu. Lakini, hata baada ya kujua haya, watu hawafanyi juhudi kukamilisha Swalah zao na kwa hiyo huandikiwa sehemu ndogo tu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;

“Kwa hakika, mtu ataondoka (katika Swalaah yake) na ataandikiwa (thawabu) kumi za Swalaah yake; tisa, nane, saba, sita, tano, nne, tatu, nusu.” [Abu Daawuud na at-Tirmidhiy]


‘Uthmaan bin Abii Dahshah (Radhiya Allahu ‘anhu) alisema: “Sijawahi kuswali Swalah ambayo baada yake nilikosa kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anisamehe kwa upungufu wangu katika Swalah ile.”

Mtu ambaye anaharakisha Swalah yake ni mwizi.  Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema katika Hadiyth sahihi, “Mwizi muovu kuliko wote ni yule ambaye anaiba katika Swalaah yake”. Swahaaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakauliza: “Ewe Mjumbe wa Allaah, anaibaje katika Swalah yake?” Naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakamilishi rukuu na sujudu zake”


Kwa sababu ya kasi ya jinsi ya watu wanavyoswali, wanaonekana kama ndege, wanaodonoa juu na chini. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza  mtu kudonoa (katika Swalah) kama kunguru.


‘Umar (Radhiya Allahu  ‘anhu) wakati mmoja alisimama katika Minbari akiuhutubia umati wa watu kwa sauti ya nguvu akisema, “Mtu anaweza akakulia mpaka utu uzima katika Uislamu na asiweze kamwe kukamilisha kwa ajili ya Allaah hata Swalah moja!” (Watu) wakasema, “Vipi hali hii?” (‘Umar) (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema: “Hakamilishi khushuu yake, hata unyenyekevu wake, hata nadhari yake juu ya Allaah ‘Azza wa Jalla.”

Wakati mmoja, Ma’aruuf Al-Karkhiy (Rahimahu Allaah) aliposimama miongoni mwa wanafunzi wake, mmoja wao akamwambia mwenziwe, “Tafadhali swalisha Swalaah ya ‘Ishaa”. Mwanafunzi wa kwanza akakubali lakini akasema “Nitaswalisha Swalaah ya ‘Ishaa kwa sharti ya kwamba wewe utaswalisha Swalaah ya Alfajiri sio mie” Ma’aruuf Al-Karkhiy alishtushwa na kauli aliyoisema na akasema, “Naapa kwa Allaah, ikiwa unafikiria ya kwamba utakuwa hai wakati wa Alfajiri, basi naapa kwa Allaah, hujakamilisha Swalah yako”.


Sehemu Ya Pili

Jinsi ya kuwa na Khushuu ndani ya Swalah
Al-Qaasim bin Muhammad (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilikwenda nje siku moja, na kila nilipotoka ni lazima nipite kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha) na kumsalimia. Siku hiyo nilitoka na nilipomkuta mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha) akiswali Swalah ya Dhwuhaa, akisoma tena na tena Aayah ya Allaah:
 
{{Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa (adhabu ya Allaah). Basi Allaah Akatufanyia hisani na Akatulinda na adhabu ya Moto.}} [Atw-Twuur: 26-27]

Alikuwa analia na akimwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na huku akirudia Aayah hiyo. Nilisimama pale mpaka nikachoka, hali ya kuwa yeye amebaki kama nilivyomkuta. Nilipoona haya nilijiambia, “Hebu niende sokoni, nifanye ninachotakiwa kufanya, halafu nije tena”. Kwa hiyo, baada ya kumaliza kufanya nilichotaka kufanya sokoni, nilirudi kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha). Alikuwa kama nilivyomuacha, akirudia Ayaah, akimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na akilia”.
 

Vipi tuwe na khushuu katika Swalaah?

Katika Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)tunafundishwa yafuatayo:


1.     Njoo mapema kwa ajili ya Swalaah na jitayarishe kuwa na khushuu.
Fuatiliza adhana pamoja na Mu’adhin na baada ya adhana, sema dua iliyoamriwa. Omba dua baina ya Adhaana na Iqaamah. Tia wudhuu vizuri, hali ukisukutuwa mdomo wako, na vaa nguo zako nzuri kabisa.

2.     Nuia kupata dhawabu zote za Swalaah yako.
Abu Bakr bin ‘Iyaash alisema, “Nilimuona Habiyb bin Thaabit katika sujudu. Ukimuona utadhania kwamba kashakufa (kwa urefu wa sujudu zake).”


3.     Zingatia Aayah na adhkaar ambayo inasomwa ndani ya Swalaah.
Fikiria kuhusu maana za Aayah ambazo unazisoma. Je haivunji moyo ya kwamba mtu anaweza kuswali miaka kumi baada ya kumi, siku baada ya siku na pia bado hajui anasema nini? Qur-aan iliteremshwa ili itafakariwe! Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kateremsha (katika Qur-aan Ayaah inayosema):

{{Na hiki Kitabu, Tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.}} [Swaad: 29].


4.     Swali Jama’ah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaamrisha:

{{Na simamisheni Swalah, na toeni Zakaah, na rukuuni pamoja na wenye kurukuu.}} [Al-Baqarah: 43].


5.     Usikose kamwe kuswali Swalah zako za nawaafil (Sunnah zilizotiliwa mkazo), hasa zile ambazo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali siku zote, kama vile Witri na Sunnah ya Alfajiri.


6.     Usiharakishe Swalah yako.

Chukua muda wako na usikubali kuifanya Swalah yako kuwa kitendo kilichokuwa hakina thamani katika siku yako. Ibn Wahb (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilimuona Ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) kwenye Kaa’bah.  Baada ya Swalah ya Magharibi, alinyanyuka kuswali na kisha akasujudu. Hakunyanyuka katika ile sujudu mpaka adhana ya ‘Ishaa ilipoadhiniwa.”


7.     Jua ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajibu Swalah yako. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

“Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyetukuka alisema: “Nimeigawa Swalah kati Yangu na mja Wangu  katika nusu mbili, na mja Wangu atapata alichokiomba” [Kutoka katika Surat ul- Faatiha ] Wakati mja anaposema, “Sifa njema zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), Mola wa viumbe vyote,” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Mja Wangu Amenihimidi” . Wakati mja anaposema “Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Mja wangu Amenisifu.” Wakati mja anaposema, “Mwenye Kumiliki Siku ya Malipo”, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema mja Wangu Amenitukuza”.  Wakati mja anaposema, “Wewe tu tunakuabudu na wewe tu tunakuomba msaada.” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema, Hii ni kati Yangu Mimi na mja Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba”. Wakati mja anaposema “Tuongoze katika njia iliyonyooka, njia ya  uliowaneemesha, sio ya wale uliowakasirikia, wala ya wale waliopotea,” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)  Anasema, “Hivi vyote ni kwa ajili ya mja Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba” [Muslim]


8.     Swali pamoja na kizuizi (weka sutrah) mbele yako na swali karibu yake.

Kitu chengine ambacho kitakusaidia kuwa na khushuu’ [utulivu] ni kushughulika (au kuwa makini) katika suala la kuwa na kizuizi (sutrah) na kuswali karibu yake. Kuwa na sutrah kutazuia uoni wako, kutakulinda juu ya Shaytwaan, na kutazuia watu kupita mbele yako, kitu ambacho husababisha wasiwasi na hupunguza thawabu za Swalah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: 

“Ikiwa mmoja wenu ataswali basi na aswali akielekea kwenye sutrah, na awe karibu nayo” [Abuu Daawuud].


9.     Tafuta ulinzi] kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na Shaytwaan.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha vipi tupambane na wasi wasi wa Shaytwaan. Abul- ‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu) kasimulia ya kwamba alisema, “Ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Shaytwaan ananisumbua wakati ninaswali, na hupata wasiwasi katika kisomo changu.” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Huyo ni Shaytwaan  ambaye jina lake ni Khanzab. Ikiwa utahisi kwamba yupo, jilinde kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana naye, na tema mate (makavu) katika upande wako wa kushoto mara tatu”. Abu’l –‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu) alisema: “nilifanya hivyo na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akaniondoshea.” [Muslim].

10.            Swali kama kwamba umeambiwa kuwa baada kumaliza Swalah utarudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Abu Bakr Al-Muzaniy (Rahimahu Allaah) alisema, “Kama unataka Swalah yako ikufae, basi sema: “Nitakufa baada tu ya Swalah hii!”  

Kumuoa Mkristo Atakayesilimu Siku Ya Ndoa



SWALI:
 Je inakubalika kumuoa Mkiristo atakaesilimu siku ya ndoa?
 

 
 
JIBU:
 
 
Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakuna tatizo lolote endapo atasilimu kidhati, Imepokewa kutoka kwa Anas amesema: Abu Twalha alipomuoa Ummu Sulaym, mahari yao ilikuwa ni kusilimu, Ummu Sulaym alisilimu mwanzo kabla ya Abu Twalha, alipomchumbia, akasema kwa hakika mimi nimeshasilimu, ikiwa utasilimu utanioa, akasilimu na ikawa kusilimu ndiyo mahari yao" (An-Nasaaiy 6/114).
Lakini Muislamu mwanamume awe makini na mwanamke mwenye kutaka kusilimu siku ya ndoa, isijekuwa ni mwenye kumdanganya akawa anasubiri siku hiyo wakati ameshatayrisha mambo ya harusi kisha amgeukie. Ikiwa hili ndilo sharti aliloliweka huyo mwanamke basi nasiha yetu ni kuwa uwe makini na ujaribu kuchunguza kwanza dhamira yake.
 
Na Allaah Anajua zaidi
 
 

Yajue Mambo Anayopaswa Kufanyiwa Mtu Akifariki


Yampasa Muislam ajiandae kufikiwa na mauti kwa kukithirisha (kufanya sana) matendo mema na kujiepusha na makatazo (vilivyoharamishwa). Vilevile mauti yawe akilini mwake, kwa maneno ya Mtume صلي الله عليه وآله وسلم:
“Zidisheni kukumbuka kiondoshacho ladha (yaani mauti)”. Hadiyth hii imepokewa na Imaam at-Tirmidhiy na akaithibitisha usahihi wake Imaam al-Albaaniy katika kitabu chake Irwaaul-Ghaliyl uk. 682.

Anapofariki Muislam yampasa yule au wale waliopo pale karibu na maiti kumfanyia mambo yafuatayo:
1.     Kuyafumba macho ya maiti huyo kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliyafumba macho ya Abu Salamah alipofariki kisha akasema: “Hakika macho yanafuata roho inapotolewa”. Imesimuliwa na Imaam Muslim.

2.     Avilainishe viungo vya maiti ili visikakamae.

3.     Aifunike maiti hiyo kwa nguo ambayo itasitiri mwili mzima kwa kauli ya mama wa waumini ‘Aaishah:“Hakika alipofariki Mtume صلي الله عليه وآله وسلم alifunikwa kwa nguo iliyomsitiri kote.” Imesimuliwa na Imaam al-Bukhaariy na Imaam Muslim.

4.     Waharakishe kuiandaa maiti, kuiosha, kuikafini, kuiswalia na kuizika. Kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم amesema: “Liharakisheni jeneza…” Imesimuliwa na Imaam al-Bukhaariy na Imaam Muslim.

5.     Waizike katika mji au eneo alilofia kwa vile katika vita vya Uhud “Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliamrisha mashahidi wa vita wazikwe pahala pale walipofia wala wasihamishwe”. Imepokewa na Ahlus Sunan (Ma-Imaam Abu Daawuud, an-Nasaaiy, at-Tirmidhiy, Ibnu Maajah) na ameithibitisha usahihi wa Hadiyth hiyo Imaam al-Albaaniy katika kitabu chake cha Ahkaamul Janaaiz uk. 14.