Saturday 1 November 2014

Hukmu Ya Kufunga Ijumaa Ikiwa Ni Siku Ya 'Arafah Au 'Aashuraa


SWALI LA KWANZA:
Assalaam 'Alaykum,
Shukurani zetu kwa kutujuilisha muandamo wa mwezi,
Pia nilikuwa nina masuala machache kuhusu  mwezi huu.  Jee tunaweza kufunga Arafa Ijumaa peke yake? au ni vizuri tufunge na Alhamis ili tuepuka kufunga siku ya Ijumaa pekee na kupata fadhila za Alhamis??
Pia kuna ushahidi wowote wa kufunga siku tisa za mwanzo za mfungo tatu (Hijja) kama ilivyozoeleka na wengi
Jazaka Allah Khayra
SWALI LA PILI:
Je inafaa kufunga Ijumaa ikiwa itaangukia ni siku ya tarehe 10 Muharram (Ashura)?
 




JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Mas-ala ya kufunga siku ya Ijumaa pekee au Jumamosi pekee zinapoangukia siku zilizotajwa kuwa ni siku za kufunga kama 'Arafah na 'Ashuraa, yana ikhtilaaf baina ya Maulamaa. Kuna waliosema kuwa inafaa kutokana na fadhila zilizotajwa katika kufunga siku hizo na kuna waliopinga kabisa kutokana na Hadiyth za Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 
Makatazo ya Kufunga siku ya Ijumaa:

 عن أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ : (( لا يَصُومَنَّ أَحَدُكُمْ يَوْمَ الْجُمُعَةِ إِلا يَوْمًا قَبْلَهُ أَوْ بَعْدَهُ )) رواه البخاري   ومسلم
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) ambaye amesema: 'Nimemsikia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Asifunge yeyote siku ya Ijumaa ila ikiwa (akiunganisha) siku kabla yake au baada yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Vile vile,
  عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : (( لا تَخْتَصُّوا لَيْلَةَ الْجُمُعَةِ بِقِيَامٍ مِنْ بَيْنِ اللَّيَالِي وَلَا تَخُصُّوا يَوْمَ الْجُمُعَةِ بِصِيَامٍ مِنْ بَيْنِ الْأَيَّامِ إِلا أَنْ يَكُونَ فِي صَوْمٍ يَصُومُهُ أَحَدُكُمْ ))  مسلم
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msiufanye usiku wa Ijumaa kuwa ni mahsusi kwa Qiyaam (Kisimamcho cha kuswali usiku) baina ya nyusiku nyingine na wala msiifanye siku ya Ijumaa ni makhsusi kwa kufunga baina ya siku nyingine isipokuwa ikiwa ni miongoni mwa siku anazofunga mmoja wenu)) [Muslim]

عَنْ جُوَيْرِيَةَ بِنْتِ الْحَارِثِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ دَخَلَ عَلَيْهَا يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَهِيَ صَائِمَةٌ فَقَالَ ((أَصُمْتِ أَمْسِ)) قَالَتْ لا قَالَ ((تُرِيدِينَ أَنْ تَصُومِي غَدًا)) قَالَتْ لا قَالَ ((فَأَفْطِرِي)) وَقَالَ حَمَّادُ بْنُ الْجَعْدِ سَمِعَ قَتَادَةَ حَدَّثَنِي أَبُو أَيُّوبَ أَنَّ جُوَيْرِيَةَ حَدَّثَتْهُ فَأَمَرَهَا فَأَفْطَرَتْ   رواه البخاري
Kutoka kwa Juwariyah bin Al-Haarith (Radhiya Allahu 'anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwake siku ya Ijumaa naye akiwa amefunga akasema: ((Je ulifunga jana?)) Akasema: "Hapana". Akasema: ((Je unataka kufunga kesho?)) Akasema: "Hapana". Akasema: ((Basi fungua)) [yaani usifunge] Na kasema Hammad bin Al-Ja'd 'Nimemsikia Qataadah akisema, Abu Ayyuub kaniambia kuwa  Juwayriyah alimhadithia  (alivyozungumza na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ) akamuamrisha afungue . [Al-Bukhaariy]

Makatazo ya kufunga siku ya Jumamosi
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ بُسْرٍ عَنْ أُخْتِهِ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : (( لا تَصُومُوا يَوْمَ السَّبْتِ إِلا فِيمَا افْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ ، فَإِنْ لَمْ يَجِدْ أَحَدُكُمْ إِلا لِحَاءَ عِنَبَةٍ ، أَوْ عُودَ شَجَرَةٍ فَلْيَمْضُغْهُ))      وأبو داود  وابن ماجه صححه الألباني في "الإروا
Kutoka kwa 'Abdullahi bin Busr kutoka kwa kaka yake kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Msifunge siku ya Jumamosi isipokuwa ikiwa mmefaridhiwa na Allah kwenu. Ikiwa mtu hakupata chochote cha kula isipokuwa jani la zabibu au gome la mti, basi alitafune)) [Abu Daawuud na Ibn Maajah na kaipa daraja ya sahiyh Shaykh Al-Albaaniy katika Al-Irwaa]
Bonyeza katika kiungo kifuatacho chenye maelezo zaidi kuhusu hukmu ya funga ya Jumamosi:
 Hukumu Ya Kufunga Siku Ya Jumamosi Pekee

Kauli za Maulamaa kuhusu mas-ala haya:
Ibn Qudaamah kasema: "Ni makruuh kuipwekesha siku ya kufunga Ijumaa ila ikiwa imeangukia katika siku ambayo ni kawaida yake mtu kufunga kama vile Swawm ya siku moja na ya pili kuacha (Swawm ya Nabii Daawuud) ikaangukia Swawm kama hiyo katika siku ya Ijumaa, au kwa mwenye tabia ya kufunga siku ya mwanzo au ya mwisho au ya katikati katika mwezi" [Al-Mughni, Mjadala 3 Uk. 53]
An-Nawawy kasema: "Wafuasi wetu (yaani Mashaafi'iy) wamesema: Ni makruuh kuipwekesha siku ya Jumamosi kufunga. Lakini mtu anaweza kuunga siku kabla yake au baada yake. Au ikiwa imeangukia katika siku za kawaida yake kufunga, au kama kaweka nadhiri mfano; ni siku ambayo mpenzi wake amepona, au siku 'fulani' atakayorudi, na ikatokea kuwa siku hiyo ni Ijumaa basi sio makruuh kufunga" [Al-Majmuu-sharh al Muhadhadhab, Mjadala 6, Uk. 479]
Shaykhul-Islaam amesema: "Sunnah inasema kuwa ni makruuh kupwekesha (mwezi wa ) Rajab kwa kufunga na ni makruuh kuipwekesha Ijumaa (kwa kufunga)" [Al-Fataawa al-Kubra, Mjadala 6, Uk. 180]
Shaykh Ibn 'Uthaymiyn kasema: "Ama Ijumaa, sio Sunnah kufunga siku hii, na ni makruuh kuipwekesha kwa ajili ya kufunga" [Ash-Sharh al-Mumti', Mjadala 6, Uk.465]
Tukiacha makatazo hayo ya kuipwekesha siku ya Ijumaa kufunga, mtu anaweza kufunga ikiwa ni siku ya kawaida yake mtu kama mwenye kufunga Ayyaamul-Biydhw (tarehe 13, 14, 15 ya kila mwezi wa Kiislam) mwenye kutaka kufunga 'Arafah na ikaangukia kuwa ni Ijumaa.
Vile vile ikiwa mtu anataka kulipa deni lake la Ramadhaan anaweza kufunga Ijumaa peke yake. Hii ni kutokana na Fataawa inayosema: "Inaruhusiwa Muislamu afunge Ijumaa peke yake ikiwa ni funga ya deni la Ramadhaan" [Fatwa al-Lajnah ad-Daaimah, Mjadala 10, Uk. 347] 
Kwa hiyo ikiwa ni 'Arafah au 'Ashuraa imeangukia kuwa ni Ijumaa inaruhusiwa kufunga kwa sababu nia ni ya kufunga 'Arafah au 'Ashuraa na sio kufunga Ijumaa. Vilevile ikiwa mtu atafunga na siku ya Alkhamiys, itakuwa ni jambo jema zaidi kwani atakuwa amepata fadhila zaidi ya moja;
  1. Fadhila ya kutekeleza Sunnah ya kuifunga siku hiyo kama alivyokuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufunga Jumatatu na Alkhamiys.
  2. Fadhila ya kufunga siku ya kabla ya siku ya Ijumaa, na hivyo ni kuondosha shaka yoyote inayohusiana na kuipwekesha Ijumaa kwa Swawm.
  3. Fadhila ya kutenda kitendo kizuri katika masiku kumi ya Dhul-Hijjah kama ilivyosisitizwa katika Sunnah. 
Alhidaaya inawasisitiza sana ndugu Waislam mfunge siku ya Alkhamiys na Ijumaa .
Ama kuhusu swali lako la pili kuhusu kufunga siku 9 za Dhul-Hijjah, jibu lake liko tayari kwenye kiungo kifuatacho:
Inafaa Kufunga Siku 9 Za Dhul-Hijjah?
Tunawakumbusha tena waulizaji, muwe mnatembelea kitengo cha maswali na majibu kwenye tovuti kabla hamjauliza maswali yenu. Kufanya hivyo kunawasaidia kupata majibu ya maswali mnayotaka kuuliza ambayo tayari yashajibiwa, na kadhalika kutatuwepesishia sisi na kazi za ziada In Shaa Allaah.
Yanayohusiana na Swawm ya Jumamosi yanapatikana katika kiungo kifuatacho:
Hukumu Ya Kufunga Siku Ya Jumamosi Pekee Na Inapoangukiwa Siku Ya 'Arafah Au 'Aashuraa

Na Allaah Anajua zaidi

No comments: