Thursday 30 October 2014

Mambo Ya Kufanya Siku Ya Ijumaa


Ijumaa hii tunaelezea utukufu wa siku hii kwa kujulisha mambo yanayotupasa kuyafanya yenye fadhila  na thawabu nyingi.

Kukoga (Ghuslu) Ni Wajibu

حديث أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ، عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: الْغُسْلُ يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَاجِبٌ عَلَى كُلِّ مُحْتَلِمٍ ( أخرجه البخاري)   
Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy ambaye alisema: Mtume صلى الله عليه وسلم  kasema  Ghuslu ( kukoga kwa kujitia twahara) siku ya Ijumaa ni wajibu kwa kila Muislamu aliyebaleghe.  [Al-Bukhaariy]

Inapendekezwa kwa kila anayekwenda kuswali kujisafisha, kupiga mswaki, kujitia mafuta mazuri (isipokuwa mwanamke) na kuvaa nguo iliyo nzuri kabisa. Muislamu akitimiza adabu ya Swalah ya Ijumaa hufutiwa madhambi yake ya wiki.

عن سلمان رضي الله عنه قال: قال رسول الله  صلى الله عليه  وسلم  لا يغتسل رجل يوم الجمعة، ويتطهر ما إستطاع من طهر، ويدّهن من دهنه، أو يمس من طيب بيته، ثم يخرج فلا يفرق بين إثنين، ثم يصلي ما كتب له، ثم ينصت إذا تكلم الإمام، إلا غفر له ما بينه وبين الجمعة الأخرى) رواه البخاري(

Kutoka kwa Salmaan رضي الله عنه  ambaye alisema:  Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم "Muislamu atakayekoga (Ghuslu)  siku ya Ijumaa, akajisafisha vizuri awezavyo, akatia rangi (nywele zake) (isiyo nyeusi),  au akajipaka mafuta mazuri  aliyonayo nyumbani kwake, kisha akaenda Msikitini bila ya kufarikisha (kuwapangua akipita) watu wawili (ambao wameshakaa kitako msikitini), akaswali aliyofaridhishwa, kisha akasikiliza  (khutbah) kimya, hufutiwa madhambi yake yaliyo baina ya Ijumaa hiyo na Ijumaa ijayo.  [Al-Bukhaariy na Ahmad]

Swalah Ya Ijumaa 

Allaah سبحانه وتعالى Ametuamrisha kwenda kuswali Swalah ya Ijumaa
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِي لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَى ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi mlioamini! Ikiadhiniwa Swalah siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Allaah, na acheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua” [Al-Jumu’ah 62: 9]

Ni wajibu kwa kila mwanamme Muislamu kwenda kuswali Ijumaa, na hatari ya  kutokwenda kuswali bila ya kuwa na sababu iliyoruhusu shari’ah ni kuwa  Allaah سبحانه وتعالى  humpiga muhuri mtu  moyoni  mwake, kama katika Hadiyth sahihi ifuatayo:

 قال رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: من ترك ثلاث جمع تهاونا طبع الله على قلبه (رواه أحمد وأصحاب السنن،)

Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم : Atakayeacha (kuswali Swalah ya) Ijumaa mara tatu bila ya sababu yeyote, Allaah سبحانه وتعالى humpiga muhuri katika moyo wake.” [Ahmad na wapokezi wa Hadiyth wengine wenye vitabu vya ‘Sunnan’]

Kupigwa muhuri huo inamaanisha kwamba Allaah سبحانه وتعالى Ameshampa chapa huyu mtu kuwa ni 'Aasi na amekwishatumbukia katika makemeo ya Allaah سبحانه وتعالى  kwamba   ni katika walioghafilika  kama alivyotutahadharisha Mtume صلى الله عليه وسلم :

حديث ابن عمر وأبي هريرة رضي الله عنهما المخرج في صحيح مسلم من أنهما سمعا رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول على أعواد منبره: لينتهين أقوام عن ودعهم الجمعات أو ليختمن الله على قلوبهم ثم ليكونن من الغافلين

Kutoka kwa Ibn 'Umar na Abu Hurayrah رضي الله عنهما kwamba wamemsikia Mtume صلى الله عليه وسلم akisema: “Wasiohudhuria  Swalah ya Ijumaa  wabadilishe  mtindo wao huo au sivyo Allaah سبحانه وتعالى Atawapiga mihuri katika nyoyo zao  na watakuwa  miongoni wa walioghafilika.” [Muslim]


Kufika Mapema Msikitini   

Kila atakapofika mtu mapema msikitini huwa amepata daraja Fulani na muhimu kabisa ni kufika kabla ya khutba kuanza, akichelewa mtu kufika akakosa khutba atakuwa amekosa Swala ya Ijumaa

حديث أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، أَنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ ثُمَّ رَاحَ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الرَّابِعَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ دَجَاجَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الْخَامِسَةِ فَكَأَنَّما قَرَّبَ بَيْضَةً، فَإِذَا خَرَجَ الإِمَامُ حَضَرَتِ الْمَلاَئِكَةُ يَسْتَمِعُونَ الذِّكْرَ (أخرجه البخاري )

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye alisema:  Mtume صلى الله عليه وسلم kasema: “Atakayekoga (Ghuslu) siku ya Ijumaa kisha akaenda Msikitini, itakuwa kama mfano ametoa (kafara ya) ngamia. Akienda  saa ya pili yake, itakuwa kama katoa (kafara ya) nġ’ombe.  Akienda saa ya tatu yake, itakuwa kama katoa (kafara ya) kondoo mwenye pembe. Akienda saa ya nne yake, itakuwa kama katoa   kuku. Akienda saa ya tano yake itakuwa kama katoa yai. Imaam akifika, Malaika watatoka kuja kusikiliza dhikr” [Al-Bukhaariy]


Surah Za Kusoma Siku Ya Ijumaa

·         Suratul Kahf

عن أبي سعيد الخدري رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه  وسلم  قال: من قرأ سورة الكهف يوم الجمعة أضاء له من النور ما بين الجمعتين ( رواه الترمذي)
Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy رضي الله عنه ambae alisema: Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم : “Atakayesoma Suratul-Kahf siku ya Ijumaa atakuwa katika mwangaza baina ya Ijumaa mbili.”  [At-Tirmidhiy]

Pamoja na kusemwa kuwa Hadiyth hiyo imetoka kwa Mtume صلى الله عليه وسلم, lakini Wanachuoni wa Hadiyth wengi wamesema ni Hadiyth 'Mawquuf' ambayo haijaelezwa na Mtume bali ni kutoka kwa Maswahaba, na kwa nyongeza ya neno 'atakayeisoma Ijumaa' haikuthibiti kwa Mtume, na maelezo hayo hapo juu ni ya kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy na yeye ndiye aliyekuwa akiisoma Surah hiyo katika siku ya Ijumaa, na Wanachuoni wanasema kuwa maadam Maswahaba walikuwa wakiisoma Surah hiyo siku ya Ijumaa, basi hakuna neno kuisoma Ijumaa, japo kuisoma siku yoyote ni sawa na mtu atapata fadhila zilizotajwa kwenye Hadiyth hiyo. Ama kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وسلم, Wanachuoni wamesema haikuja na lafdhi ya 'kuisoma Ijumaa', bali imekuja kwa ujumla wake wa kuisoma Surah hiyo siku yoyote ile kama ilivyokuja hapa chini:

((وقال صلى الله عليه وسلم : من قرأ سورة الكهف كما أنزلت كانت له نورا يوم القيامة ، من مقامه إلى مكة ، و من قرأ عشر آيات من آخرها ثم خرج الدجال لم يضره ....))  صححه الألباني في سلسلة الأحاديث الصحيح 
((Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم atakayesoma Suratul-Kahf kama ilivyoteremshwa, atakuwa na mwangaza siku ya Qiyaamah pale alipo mpaka Makkah, na atakayesoma Aya kumi za mwisho kisha akitokea Dajjaal hatomdhuru)) [Swahiyh kama alivyoeleza Shaykh Al-Albaaniy katika Silsilatul-Ahaadiyth As-Swahiyhah]

·         Swalah ya Alfajiri

حديث أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، قَالَ: كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ، فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ، آلَم تَنْزيلُ، السَّجْدَةَ، وَ هَلْ أَتَى عَلَى الإِنْسَانِ ( أخرجه البخاري)

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye alisema:  Alikuwa Mtume صلى الله عليه وسلم  akisoma surah ya Alif-Laam-Tanziylu (Suratus Sajdah) na Hal-Ataa 'Alal-Insaan (Suratul Insaan)”  [Al-Bukhaariy]

·         Kumswalia Mtume صلى الله عليه وسلم

عن أوس بن أوس رضي الله عنه قال: قال رسول الله  صلى الله عليه  وسلم  إن من أفضل أيامكم يوم الجمعة، فأكثروا علي من الصلاة فيه، فإن صلاتكم معروضة علي  ) رواه أبو داود)
Kutoka kwa Aws Ibn Aws رضي الله عنه ambaye alisema:  Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم : “Siku bora kabisa kwenu ni siku ya Ijumaa, kwa hiyo zidisheni kuniswalia,  kwani Swalah (kuniombea) zenu zinaonyeshwa (zinaletwa mbele yangu) kwangu.” [Abu Daawuud]
 

No comments: