Thursday 30 October 2014

Usimuombe Muhammad, Bali Muombe Allaah

 
Waislamu sote tunakiri na kutamka kwa ndimi zetu kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mtume wa mwisho, naye ni mbora wa viumbe, mwenye tabia bora za kupigiwa mfano na sisi tunawajibika kuzifanyia kazi.
 
Hata hivyo, juu ya hikmah zake, cheo na daraja alichonacho, hatustahiki hata kidogo kumuomba Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika lolote tunalohitajia kuliomba. Wala hatuwajibiki kuamini kwamba du’aa isiyopita transit kwake, haikubaliwi. Hilo sio sahihi katu, kwani Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa malaaikah wala jamii isiyokuwa yetu sisi. Ni mwenzetu, mwenye maumbile sawa na sisi, kilichobadilika kutoka kwake ni kupokea wahyi tu.
 
Mola wetu, Anasema kwamba tumuombe Yeye, kwani Ndiye Anayezisikia du’aa zetu na malalamiko yetu:
 
{{Na waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi Nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.)) [Al-Baqarah:186]
 
Pia Amesema:
 
{{Na Mola wenu Anasema: Niombeni nitakuitikieni.}} [Suratul-Ghaafir: 60]
 
Kwa upande wake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba tusimtukuze kama walivyomtukuza Manasara kwa Nabii ‘Iysaa hadi kumpa daraja na cheo sawa cha Uungu:
 
((Msinitukuze (kwa kunipandisha cheo kama cha Allaah) kama walivyomtukuza Manasara ‘Iysaa mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja, kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Mjumbe Wake.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
 
Wala hawa Manasara hawakuishia hapo, nao pia wakajitukuza na kujipachika vyeo vya Unabii na Utume, na kujidai kuweza kuombwa na wanaadamu wenzao pamoja na kusamehe madhambi. Hayo kwetu yatabakia ni uzushi mkubwa na ni shirki iliyo wazi.
 
Kwa hapa, tunaomba tuzingatie kwamba du’aa yoyote inatakiwa kuelekezwa moja kwa moja, kiroho na kimatamshi kwake Muumba wala sio kwa Mtume. Tunaona ndani ya jamii zetu za Kiswahili, mtu anapojitoka, anapotokewa na tatizo la ghafla au mfano wa hayo; basi kauli ya mwanzo linalomjia mdomoni ni la kishirikina: Mtume! na mfano wa hayo.
 
Ewe ndugu yangu Muislamu, umesahau ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti. Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti, asiyeweza hata kusikia maombi yetu, seuze kuweza kutuombea kwa Mola. Sasa iweje leo neno lako la mwanzo unapotokezewa na shida liwe Mtume!?
 
Na wengine wapo waliochupa mipaka, wakawapatia vyeo wanaowaita masharifu, mashekhe, mamufti, maqadhi, mawalii na kadhalika, wakawatumia kuzipitisha du’aa zao kwao. Ni ushirikina na uzushi ulioje. Utakuta kwenye du’aa zao wakisema: Kwa kuhudhuria Sayyiduna Muhammad, mawlaana, sharful-anbiyaa, wa shuyukhina, al-faatihah! Ujahili ulioje huu, Mola wetu yupo karibu kuliko mapigo ya mioyo yetu, ya nini kupata taabu kuzipitisha du’aa kupitia kwa viumbe vinavyotegemea rahmah zake?
 
Tunamalizia kwa kuzinasihi nyoyo zetu na za Waislamu wote, kuachana na aina hii ya shirki, kwani tutakuwa tunamuomba kiumbe badala ya kumuomba Muumba.
 

1 comment:

Anonymous said...

1- A.alykum mimi nauliza kuhusu tawasul sheikh
2- Allah ameahidi kulitukuza jina la Mtume SAW hadi kuwekwa kuwa swala bila kumswalia Mtume haikubaliki. Pia inasemekana dua unapoianza na kumswalia Mtume SAW ni maqbul.
Hili unasemaje sheikh