Thursday 30 October 2014

Kutafuta Elimu Ni Wajibu

Jibriyl (‘Alayhis Salaam) aliposhuka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtikisha na kumbana barabara akimuamuru kusoma kwa jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Mola Ambaye Amemuumba mwanadamu kwa tone la damu na kumfunza kwa kutumia kalamu.
 
Iwapo kipenzi cha Mola Mlezi asiyejua kusoma wala kuandika ametikishwa namna hiyo, je sisi tutarajie nini katika kutafuta elimu? Wengi wa Waislamu ni wenye kwenda na kurudi bila ya kutilia mkazo elimu ya Kiislamu. Na kama Waislamu watasimama kihaki liLlaahi kuitafuta elimu, basi ndio itakuwa sababu ya kuondoka udhalilifu walionao Waislamu hivi sasa.
 
Katika baadhi ya miji ya Waislamu, utakuta kuna Misikiti chungu nzima lakini Madrasah zikiwa kidogo kweli kweli. Sasa hiyo Misikiti ikaswalishwe na kusomeshwa darsa na nani? Ingawa hizo Madrasah pia zipo na zimejaa taa na mazulia mazuri mazuri, lakini wanafunzi wake ni wachache kabisa. Kwanza Waislamu watilie mkazo kusoma na kusomesha, badaye ndio wasambazwe hao waliosoma ndani ya Misikiti. Na kwa bahati mbaya, hivi sasa Misikiti na Madrasah ni vitu viwili tofauti. Misikiti mingi inajengwa kwa ajili ya kuswalia tu, na Madrasah kwa ajili ya kusoma tu. Tumesahau ya kwamba Mtume aliujenga Msikiti ambao ndio kiini cha elimu ya Kiislamu na hivi sasa unatoa shahada za juu kabisa kwa wanafunzi.
 
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa utume kwa kauli ya "Iqraa" iliyomo ndani ya Suratul-'Alaq na akaamrishwa kulingania kupitia aya za mwanzo za Suratul-Muddathir. Tunachojifunza hapa ni kwamba amri ya kusoma imekuja mwanzo kabla ya kulingania. Na bila ya shaka Mola Amemuamuru mwanaadamu kutafuta elimu kabla ya kumuamuru kumuelewa Mola Mwenyezi (elimu ya tawhiyd). Kwani kupitia elimu ndio atapata wepesi wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema ndani ya Qur-aan:
 
{{Jua ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Mwenyezi Mungu.}} [Suratu-Muhammad: 19]
 
Amri ya Mola inayosema "jua" ina maana sawa na "soma". Kilichopo hapo ni kwamba kwanza tusome na ndani ya hiyo elimu tutaelewa kuwa hakuna aabudiwaye kwa haki ila Mwenyezi Mungu. Hii inatutambulisha kwamba amri ya kumtambua Mola ipo chini kulinganisha na amri ya kutafuta elimu.
 
Tuzingatie na tuelewe ule msemo wa Waarabu unaosema: "العلم من المعهد إلى العهد"
wenye maana kwamba elimu ni ya kutafutwa milele kuanzia chuoni hadi mwisho wa maisha yake mtu. Tusikate tamaa katika kutafuta elimu. Kwani elimu ni ngumu kuipata na ndio silaha yako hapa duniani na kesho Akhera iwapo utaitumia vyema. Hata unapofariki, warithi wako hawataipata kwani unaondoka nayo kama vile unavyoondoka na ‘amali zako. Watabaki kurithi hizo pumbao za dunia. Na kama umeisoma kisha ukaisomesha na kuwapatia manufaa watu, basi thawabu zake utaendelea kuzichuma hadi kaburini insha Allaah.
 
Tunamuomba Mola Atupatie fahamu ya Manabii na nyoyo zenye kuelewa mambo kwa wepesi kabisa. Atufunulie akili zetu kwa mambo yenye manufaa na kuzifunga akili zetu zisifahamu wala kuelewa hata kidogo yale yasiyo na manufaa. Aamiyn!

No comments: