Tuesday 25 August 2015

 
Mola wetu Mtukufu Amemuumba mwanaadamu katika umbo bora lisilomithilika na kiumbe chochote. Naye ameumbwa kwa kutumia udongo uliopulizwa roho itokayo kwa Mola Mlezi.
 
Akamjaalia mwanaadamu ni mwenye kupata shida, mitihani, mtenda dhambi na mwenye kupata maradhi. Hakusita hapo Mola wetu Mtukufu, bali Akajaalia mlango wa pili wa kutokea kwenye mashaka ya dunia; Akajaalia kuwepo starehe, utulivu, toba na afya. Basi ni kwa neema zipi mwanaadamu anaweza kumlipa Mola wake!?
 
Tutambue kwamba hii roho tuliyokuwa nayo yatosha kuwa ni sababu ya kushukuru neema za Mola Mlezi kwa vitendo na kauli. Tusisahau wapi tulipotoka na wapi tunaelekea, hatukuwa chochote miaka 100 iliyopita. Basi ni nani kati yetu alikuwa na uhakika kwamba atadhihiri duniani kwa jina na umbo lake kabla ya kuzaliwa? Kuwa na adabu kwa kumcha Mola wako!
 
Muislamu yupo juu ya mgongo wa ardhi akiruzukiwa kila chenye manufaa na yeye, ni mwenye kula akapata njia ya kutolea uchafu, na siku uchafu unaposhindwa kutoka ndani ya tumbo ndio unaelewa umuhimu wa neema ya kuyeyusha chakula kwenye mwili. Ameumba kila kitu kwenye kiwango maalumu, kwani tumbo likiyeyusha kupita kiwango, mwanaadamu ataugua maradhi ya tumbo la kumuendesha. Hivyo, kumbuka na yazingatie maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{Na mkihesabu neema za Allaah hamtaweza kupata idadi yake. Hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.}} [An-Nahl: 18]
 
Basi elewa ndugu yangu, kwamba sisi si chochote si lolote zaidi ya tone la manii lililoengwa engwa hadi likafikia miezi tisa likaweza kutoka kwa sura ya mwanaadamu. Ndani ya tumbo, Mola wetu Mlezi Alitulinda na wala hatukuhitaji askari, jeshi, polisi, ultimate security au mwengineye. Ukatoka kwa ukenya wa kilio cha juu ukiomba msaada kwa mama yako. Ukafikia baleghe ukaweza kuoa/kuolewa na sasa kwa Qadar ya Mola unaweza nawe kupata mtoto. Aliyekuwa mbabe kati yetu azihesabu neema ngapi zimepita baina ya kuzaliwa kwake hadi hivi sasa, kisha aangalie ni kwa kiwango gani ataweza kuzishukuru neema hizo. SubhaanaLlaah! Yuko umbali gani mwanaadamu kwa kuzitilia maanani neema za Mola wake?
 
Ugeuze uso wako, uangalie mbingu ilivyotanda na ardhi ilivyotandikwa, kisha useme kwamba Mola wako amekutupa. Rizki zako Akazimimina kutoka mbinguni na Akazichimbua kutoka ardhini. Ni kipi basi katika chakula chako kitokacho nje ya mfumo huu? Basi kwa Kiburi Chake Mola Mlezi Anastahiki kuyaambia makundi ya wanaadamu na majini:
{{Enyi jamii ya majini na watu! Kama mtaweza kupenya katika mbingu na ardhi (ili mkimbie Nisikupateni), basi penyeni (Nikuoneni)! Hamtapenya ila kwa nguvu (Zangu. Nikikupeni nguvu hizo mtaweza).}} [Ar-Rahmaan: 33]
 
Tumcheni Mola wetu kwa kila kitu, kwa dogo na kubwa, kwa tunayoyajua na tusiyoyajua. Tutende mema kabla ya kutufika yale yasiyoweza kuhimili miili yetu. Wahenga wanatuambia: "Kijua ndi hichi usipouanika utaula mbichi."
 
 

No comments: