Thursday, 30 October 2014

Wasiya Kumi Wa Allaah - Wasiya Wa 2 Kuwafanyia Wema Wazazi



Wasia wa pili wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama tulivyosoma katika Aayah zilizotangulia ni, kuwafanyia wema wazazi wawili:
 ((...وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا...)) 
((…Na wazazi wenu wafanyieni wema…))
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesisitiza sana kuwafanyia wazazi ihsaan (wema). Wema huo unaweza kuwafanyia wangali bado wahai au hata baada ya kufariki kwao. Tunaona kwamba Swahaba alipoumuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kitendo bora kabisa, akajulishwa kuwa mojawapo ni kuwafanyia wazazi wema:
  ((عَنْ اِبْن مَسْعُود رَضِيَ اللَّه عَنْهُ أَنَّهُ قَالَ : سَأَلْت رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَيّ الْعَمَل أَفْضَل ؟ قَالَ الصَّلَاة عَلَى وَقْتهَا قُلْت ثُمَّ أَيّ ؟ قُلْ بِرّ الْوَالِدَيْنِ قُلْت ثُمَّ أَيّ ؟ قَالَ الْجِهَاد فِي سَبِيل اللَّه)) البخاري و مسلم
Kutoka kwa Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nilimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Kitendo gani bora kabisa? Akasema: ((Swalah kwa wakati wake)) Kisha nikasema: Kisha kipi? Akasema: ((Kuwafanyia wema wazazi wawili)): Kisha nikasema: Kisha kipi? Akasema: ((Jihaadi katika njia ya Allaah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwa umuhimu wake kitendo hiki hata ikiwa ni wazazi makafiri basi tunapaswa kuwatendea wema, ila tu watakapomuamrisha Muislamu kumshirikisha Allaah au maovu mengineyo hapo hawapaswi kutiiwa:
((وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ))
((Na Tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyokuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na Nitakwambieni mliyokuwa mkiyatenda)) Al-‘Ankabuut: 8]
Utakuta Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) mara Anapotaja kumuabudu Yeye, Hutaja na kuwafanyia wema wazazi wawili. Hii ni dhahiri jinsi gani jambo hili lilivyokuwa zito mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَ بَنِي إِسْرَائِيلَ لاَ تَعْبُدُونَ إِلاَّ اللّهَ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَاناً))
((Na Tulipofunga agano na Wana wa Israaiyl Hamtamuabudu yeyote ila Allaah na muwafanyie wema wazazi)) [Al-Baqarah: 83]
Maelezo zaidi kwa upana kuhusa mas-ala haya tumeshayatoa katika Nasiha za Ijumaa wiki zilizopita na yote yanapatikana katika viungo vifuatavyo:


Itaendelea InshaAllaah…
 

1 comment:

Anonymous said...

sijaelewa