Saturday 28 February 2015

Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika Ramadhaan


Nyakati tatu hizi ni muhimu sana za kufanya ibada kutokana na fadhila zake kuu. Mwenye kupenda kuchuma thawabu nyingi asizikose khaswa katika mwezi huu Mtukufu Wa Ramadhaan ambao ni mwezi wenye malipo maradufu

1-Wakati wa mwanzo:  Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:

Usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) aliomba: 

((اللهم بارك لأمتي في بكورها))  الترمذي, أحمد, أبي داود, ابن ماجه 
((Ee Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]

Usimulizi huu umetoka kwa Maswahaba kadhaa ambao wameelezea kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alipotaka kupeleka kikosi au jeshi aliwapeleka mwanzo wa asubuhi". Vile vile wamesimulia kwamba: "Swakhar alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea biashara zake mwanzo wa asubuhi na matokeo yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata faida kubwa sana".

Wamesimulia Salafus-Swaalih kwamba Ibn 'Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo alipomwambia:

   "قُم، أتنام في الساعة التي تقسَّم فيه الأرزاق؟"
"Inuka! Je, unalala katika saa ambayo rizki inagaiwa?"
Ikiwa wakati huo ni kama hivyo ilivyoelezwa juu, basi vipi Muislamu aache wakati huu umpite hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhaan?
Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake 'Zaad Al-Ma'aad' amesema: "Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…"  


Faida nyingine kubwa ya kubakia macho ukimdhukuru Allaah wakati huu:  

Kwa muda wa saaa moja na nusu takriban utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah zikiwa kamilifu:
عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال  (( من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله  حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة) ) أخرج الترمذي  صححه الألباني .
Imetoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha akakaa anamdhukuru  Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]

Pindi ukifanya hivyo kwa mwezi mzima utakuwa umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah za muda wa mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa Ramadhaan? Jitahidi ndugu Muislamu kadiri uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo zingelikukalifu mali, tabu za safari na mashaka ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini kwa Rehma ya Allaah Amejaalia thawabu hizo ziweze kuchumwa tukiwa majumbani mwetu tena kwa wepesi kabisa. Wanaume inawapasa waswali msikitini kuzipata thawabu hizo kwa kuwa Hadiyth imetaja atakayeswali jamaa’ah. Ama wanawake, wanazipata fadhila hizo hata wakiswali majumbani mwao. Hata hivyo, juu ya kuweko fadhila kama hiyo, tusisahau kuwa haivunji wala haifuti fardh ya kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa kumetengua wajibu wake wa kuhiji au kufanya ‘Umrah.


2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi):

Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du'aa yake anayoiomba hairudi:

 قال صلى الله عليه وسلم: ((ثَلاثةٌ لا تُرَدُّ دعوتُهم: الصَّائم حتَّى يُفْطِر، والإمام العادِل، ودعْوة المظْلوم)) وروى الترمذي  بسند حسن
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du'aa zao hazirudi; mwenye kufunga Swawm hadi afuturu. Kiongozi muadilifu na aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]

Ni fursa kwa Muislamu atumie wakati huo kuomba du'aa wakati huu hasa kwa vile ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:
 وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ  
 ... na msabbih kwa kumsifu Mola wako  kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa  [Qaaf: 39]
  
 وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا وَمِنْ آنَاء اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَى  
 …Na msabbih Mola wako kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umsabbih na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha  [Twaahaa: 130].

  وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَار
Na omba maghfirah kwa dhambi zako, na umsabbih Mola wako  kwa kumsifu jioni na asubuhi)) [Ghaafir: 55]
   
3- Wakati wa tatu: Suhuur - Kabla ya Alfajiri

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaaahidi wenye taqwa Pepo kwa sababu miongoni mwa sifa zao ni  kuomba maghfira kabla ya Alfajiri: 

 إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُون. آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ.   كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ.    وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُون.

Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchem. Wanapokea Aliyowapa Mola wao. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira. [Adh-Dhaariyaat: 15-18]



Kisha wamesifiwa tena kwa sifa kama hiyo pamoja na nyinginezo:

 الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالأَسْحَارِ   
Wanaosubiri, wanaosema kweli, na watiifu, na wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira kabla ya Alfajiri. [Al-'Imraan: 17]

Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba na kuweko mbingu ya ardhi kututakabalia maombi ya anayemuomba: 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم  
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Mola wake kumtakabalia haja zake au kumuondeshea shida zake? Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache wakati huu ukakupita hasa kwa vile ni mwezi wa Ramadhaan ambao kila jambo ulifanyalo lina fadhila na thawabu marudufu.

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na nyingine, tuwe katika ibada katika mwezi huu wa Ramadhaan na miezi yote mingineyo na Atujaalie kheri na Baraka nyingi, Atutakabalie haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie madhambi yetu yote. Aamiyn.

No comments: