Maswahaba wa mtume

WAJUWE MASWAHABA WA MTUME (S.A.W)
Huyu ndiye Ibni Abbas (Radhiya Llah anhuma), mchaMungu wa umma huu na Aalimu wao na Bahri ya elimu. Juu ya udogo wa umri wake, siku ile Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alipokuwa akiwasifia Masahaba wake na kumpa kila mmoja sifa yake, alisema:
"Mwenye huruma kupita wote katika umati wangu - Abubakar
Mkali wao kwa kufuata amri za Mwenyezi Mungu – Umar
Mwingi wa kuona haya kupita wote – Uthman
Msomaji wao bora wa Qurani – Ubay bin Kaab, (na katika riwaya nyingine Abdillahi Ibni Masaood)
Mtoaji hukmu bora – Ali bin Abi Talib
Mjuzi wao katika halali na haramu – Muadh bin Jabal
Mwaminifu wao – Abu Ubaidah bin Jarah
Na aalim wa umma huu ni Abdillahi bin Abbas."
(Radhiya Llahu anhum Jamiyan)
Wakati akipewa daraja hii, Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) alikuwa bado hajatimia umri wa miaka kumi na mitatu.
Abdullah bin Abbas (Radhiya Llahu anhuma)
mtoto wa Al Abbas bin Abdul Muttalib bin Hashim ambaye ni ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam).
Abdullah bin Abdul Muttalib baba yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na Al Abbas bin Abdul Muttalib baba yake Abdullah bin Abbas (Radhiya Llahu anhuma) ni ndugu kwa baba na mama.
Kwa hivyo Abdullah bin Abbas ambaye anajulikana zaidi kwa jina la 'Ibni Abbas' na maana yake ni mtoto wa Abbas anakuwa mtoto wa ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) .
Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) alipohama kutoka Makka kwenda Madina, umri wa Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) ulikuwa miaka mitatu tu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) alipofariki dunia, Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) alikuwa akipendezwa sana na wingi wa masuali ya hekima aliyokuwa akipenda kuyauliza Sahaba huyu mtukufu aliyekuwa pia hambanduki, na mwenye kupenda kumtumikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) kwa kumsogezea maji ya kutawadhia na kumsogezea viatu nk.
Siku moja Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alipomuona (Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) anataka kutawadha, kama kawaida yake alimsogezea maji kwa haraka sana na kumtawadhisha.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) alifurahi sana na alipoinuka kuswali alimuashiria Ibni Abbas asimame sawa nae ili wasali pamoja.
Ibni Abbas alifanya kama alivyoamrishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) lakini mara baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) kufunga swala, Ibni Abbas alijirudisha nyuma na kukamilisha swala akiwa nyuma kidogo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam).
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alipomaliza kuswali akamuuliza:
“Kwa nini umerudi nyuma wakati nilikuambia usimame sawa nami?”
Ibni Abbas (Radhiya Llah anhuma) akasema:
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nilikuwa kila ninapokutazama, utukufu wako unanijaa machoni mwangu, nikaona kuwa sistahiki kabisa kusimama sawa nawe”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alifurahishwa sana na maneno yale, akainama na kumbusu kipaji chake kisha akamwekea mkono kifuani pake na kumuombea dua ifuatayo:
“Mola wangu mpe elimu ya fiq-hi katika dini na muelimishe elimu ya kujuwa uhakika wa mambo)."
Bukhari na Muslim
Kwa baraka za dua hiyo, Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) alikuwa aalim mkubwa aliyechota sehemu kubwa ya elimu yake kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam), na hakupata hata siku moja kukosa kuhudhuria darsa zake, na baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) kufariki dunia Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alikuwa akienda kuitafuta elimu kwa Masahaba wakubwa waliokuwa wakijulikana kwa elimu wakati huo.
Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma):
"Alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam)
niliwaambia vijana wenzangu:
“Tuwaendee Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) na kuwauliza, kwani leo bado wapo wengi”.
Wakawa wananiambia:
“Ama wewe unastaajabisha! Huoni kuwa watu wote wanakuja kutafuta elimu kwako wakiwemo hao Masahaba wakubwa?”
“Lakini mimi”, anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma), “nilikuwa ninaposikia kuwa Sahaba fulani anahifadhi hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam), humuendea nyumbani kwake wakati wa mchana na kumsubiri nje ya mlango wake mpaka atoke.
Hukaa hapo huku nikiwa nimeutandaza upanga wangu nikijuwa kuwa wakati huo atakuwa amelala, na nikijuwa pia kuwa ningelimgongea mlango angelinifungulia kwa furaha yake, lakini nilikuwa nikimuacha apumzike, na pale anapotoka na kuniona katika hali ile huniambia:
“Ewe bin ami wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) kipi kilichokuleta mpaka hapa, si ungelimtuma mtu tu aniite na mimi ningekuja mpaka nyumbani kwako?”
Na mimi humjibu:
“Mimi ndiye ninayestahiki kukufuata, kwani elimu inafuatwa na haifuati”.
Kisha humuuliza juu ya hadithi ninayotaka kumuuliza”.
Alikuwa aalim wa tafsiri ya Qurani na Sunnah, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) alimpa jina la “Hibri haadhihil ummah”, na maana yake ni ‘Aalim wa umma huu’, na alikuwa akijulikana pia kama ni “Turjumaan al Qu-aan”, na maana yake ni ‘Mfasiri wa Qurani’.
Anasema Abdullah bin Masaud (Radhiya Llahu anhu):
“Mbora wa kufasiri Qurani ni Abdullahi bin Abbas”
Alikuwa mcha Mungu sana, mwingi wa kufunga na kuswali nyakati za usiku, na zimepokelewa kutoka kwake hadithi sahihi zipatazo elfu moja mia sita na sitini zilizofanyiwa tahakiki na Maimam Bukhari na Muslim na kuandikwa katika vitabu vyao,
juu ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) alipohama kutoka Makka kwenda Madina, Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alikuwa na umri wa miaka mitatu tu.
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alipofariki dunia, Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alikuwa bado kijana mdogo asiyebaleghe mwenye umri wa miaka kumi na mitatu
Hebu tumsikilize mmoja katika maulamaa wakubwa wa wakati wake akizungumza juu Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma):
Anasema Masrooq bin Al Ajda-a ambaye ni miongoni mwa maulamaa wakubwa
wa Al Tabiiyn:[1][1]
“Nilikuwa ninapomuona tu Ibni Abbas nikisema:
“Ni mzuri kupita wote”,
Na anapoanza kutamka neno, nikisema:
“Ni mfasihi kupita wote”.
Na anapozungumza, nikisema:
“Ni aalim kupita wote”.
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) aliulizwa siku moja:
“Uliwezaje kukusanya elimu kiasi hicho?”
Akasema;
“Kwa ulimi unaouliza na kwa moyo unaotafakari”.
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) hakuwa akimiliki elimu na ucha Mungu peke yake, bali alikuwa mkarimu na mwenye moyo wa kusamehe unaolingana na elimu yake.
Walioishi wakati wake walikuwa wakisema:
“Hatukupata kuona nyumba iliyokuwa ikiwagawia watu vyakula na vinywaji na matunda na elimu kuliko nyumba ya Ibni Abbas.”
Alikuwa akimpendelea kheri kila mtu. Anayemjuwa na asiyemjuwa. Alikuwa akisema:
“Ninapoifikia aya katika kitabu cha Mwenyezi Mungu nikaifahamu maana yake, basi hutamani kila mtu aifahamu kama nilivyoifahamu mimi.
Na ninaposikia juu ya gavana katika magavana wa Kiislamu akihukumu kwa uadilifu, hufurahi na kumuombea dua hata kama sina kadhia yoyote kwake.
Na ninaposikia juu ya mvua inayonyesha juu ya ardhi ya Waislamu, mimi hufurahi hata kama sina maslahi yoyote katika ardhi hiyo”.
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alikuwa shujaa, mwaminifu na mpenda amani.
Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi ya Aly bin Abu Talib na Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiyallahu anhum), Ibni Abbas alikuwa upande wa Aly bin Abu Talib, hata hivyo alikuwa akipendelea zaidi amani kuliko vita, na upole kuliko ukali, na nguvu ya mantiki kuliko kulazimisha.
Wakati Al Hussein (Radhiya Llahu anhu) alipoamua kwenda Karballa – Iraq, kupambana na majeshi ya Ubeidullah bin Ziad, Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alimshikila huku akimng’ang’ania na kumuomba asiende huko, lakini bila mafanikio.
Juu ya shughuli zake nyingi za kuelimisha watu, Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alishiriki katika vita vingi vya Jihadi.
Na wakati wa utawala wa Muawiya bin Abu Sufyan, Ibni Abbas alikuwemo ndani ya jeshi la Waislamu lililoiteka nchi ya Constantinople ambalo ndani yake walikuwemo Masahaba wengi (Radhiya Llahu anhum) chini ya uongozi wa Yazid mwana wa Muawiya bin Abu Sufyan.
Constantinople ilikuwa ikitawaliwa na Ceaser ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) aliwahi kusema juu yake:
“Jeshi la mwanzo litakaloiteka nchi ya Ceaser limeghufuriwa madhambi yao”.
Bukhari
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) hakuwa mwenye kuwaita watu katika njia ya Mwenyezi Mungu kisha yeye asifanya anayoyasema, bali alikuwa mcha Mungu, mwingi wa kufunga na kuswali nyakati za usiku.
Anasema Abdullah bin Malika:
“Nilifuatana na Ibni Abbas katika safari kutoka Makka kwenda Madina, na pale msafara unaposimama nyakati za usiku kwa ajili ya kupumzika, na watu wanapokikimbilia kulala, nilikuwa nikimuona akiinuka nyakati hizo na kuswali.
Nilimuona pia usiku moja akiisoma kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
“Na kutoka roho kutakapomjia kwa haki. (Hapo ataambiwa):
“Hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.”
Qaf – 19
Akawa anaendelea kuisoma na kuikariri aya hiyo huku akilia mpaka alfajiri ilipoingia”.
Baadhi ya wafuasi wa Aly bin Abu Talib (Radhiya Llahu anhu) walijitenga naye baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi yake na majeshi ya Muawiyah (Radhiya Llahu anhu) kwa hoja kuwa Aly (Radhiya Llahu anhu) alikwenda kinyume na mafundisho ya Qurani kwa kukubali kuundwa tume ya watu watakaohukumu baina yao.
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alimuomba Aly (Radhiya Llahu anhu) amruhusu aende kujadiliana na waliojitenga.
Aly (Radhiya Llahu anhu) alimruhusu huku akimuambia:
"Lakini nakuogopea."
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) akasema:
"Hapana hofu yoyote Inshaallah".
Ibni Abbas alipowaendea akawakuta kuwa ni watu wenye kufanya ibada sana, na walipomuona wakamuambia:
"Karibu ewe Ibni Abbas, kipi kilichokuleta?"
Akasema:
"Nimekuja kuzungumza nanyi".
Wengine kati yao wakasema:
"Msizungumze naye".
Wengine wakasema:
"Sema tutakusikiliza".
Akasema:
"Hebu niambieni, mnamlaumu kwa makosa gani Aly ambaye ni bin ami wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), mume wa mwanawe, na wa mwanzo kumuamini?"
Wakasema:
"Mambo matatu".
"Yepi hayo?"
Wakasema:
"La mwanzo ni kukubali kwake kufuata hukmu ya wanadamu katika dini ya Mwenyezi Mungu. La pili ni kuwa amepigana vita na Aysha na Muawiya bila kuchukuwa ngawira wala kuwateka, na la tatu amekubali kujiondolea mwenyewe cheo chake cha Amiri wa Waumini juu ya kuwa Waislamu wamefungamana naye na kumkubali kuwa yeye ni Amiri wao".
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhua) akawauliza:
"Mnaonaje nikikupeni dalili kutoka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na kutoka katika mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) juu ya haya mnayomlaumu, mtarudi kwake na kuyaacha haya mliyo ndani yake?"
Wakasema:
"Ndiyo".
Akasema:
"Ama ile kauli yenu katika kumlaumu kukubali kwake kuhukumiwa na watu katika dini ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu anasema:
"Enyi mlioamini! Msiuwe mawindo na hali mumo katika Hija au Umra. Na miongoni mwenu atakayemuua kwa kusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa (kuchinja) kilicho sawa na alichokiuwa katika wanyama wanaofugwa, kama watakavyohukumu waadilifu wawili miongoni mwenu."
Al Maidah - 95
Semeni ukweli wenu. Hivyo kuhukumiwa na wanadamu katika kusimamisha umwagaji wa damu na upotezaji wa nafsi na kupatanisha baina yenu ni bora, au kuhukumiwa na wanadamu juu ya sungura (aliyeuliwa na mtu anayehiji) ambaye thamani yake ni sawa na robo dirham?"
Wakasema:
"Bali katika kusimamisha umwagaji wa damu na kupatanisha baina ya watu".
Akasema:
"Hilo tushalimaliza?'
Wakasema:
"Ndiyo".
Akasema:
"Ama ile kauli yenu kuwa Aly alipigana vita na hakuwateka ngawira wanawake kama vile Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alivyofanya.
Hivyo nyinyi mlikuwa mkimtaka Aly amteke ngawira mama yenu Bibi Aysha na awe halali kwenu kama wanavyohalalishwa wanawake wanaotekwa katika vita?
Mkijibu 'ndiyo', mtakuwa mumekufuru, na mkisema kuwa yeye si mama yenu, pia mtakuwa mumekufuru, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:
"Na wakeze ni mama zao"
Ahzab - 6
Kwa hivyo jichagulieni mnachotaka".
Wakasema:
"Na hili pia tushalimaliza".
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) akasema:
"Ama kauli yenu kuwa Aly alijifutia mwenyewe cheo chake cha Amiri wa waumini, basi hata Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alifanya hivyo siku ya mapatano ya Hudaibia, pale washirikina walipomtaka aandike mkataba, na alipoandika:
"Haya ni makubaliano baina ya Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu…."
Makafiri wakasema:
"Ingekuwa sisi tunaamini kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, tusingelikuzuwia kwenda kutufu katika Al Kaaba, na wala tusingekupiga vita, lakini andika:
"Muhammd bin Abdillah".
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akalikubali sharti lao huku akisema:
"Wallahi mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu hata mkinikadhibisha".
Wakasema:
"Na hili pia nalo tushalimaliza.
Ikawa katika matunda ya majadiliano hayo yenye hoja zilizo wazi, watu wapatao elfu tano walirudi katika kambi ya Aly bin Abi Talib (Radhiya Llahu anhu) na riwaya nyingine zinasema kuwa idadi kubwa kuliko hiyo walirudi
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma) alifariki dunia katika mji wa Taif katika mwaka 68 Hijri akiwa na umri wa miaka 71, na miongoni mwa waliohudhuria maziko yake na kuteremka kaburini alikuwa Aly bin Abdullah (mwanawe) na Muhammad bin Al Hanafiyah (mtoto wa Aly bin Abu Talib) na Al Abbas bin Muhammad bin Abdullah bin Abbas na Safwan na Kuraib na Ikrimah na Abu Said na watu wengi sana.

2 comments:

Anonymous said...

Mashaalah

Muharrami Mng'ombe said...

Maashaallah! Nimependa jina alotoa Mtume (S.W) kwa Abdullah bin Abbas. Nami nimeweka nia nafsini mwangu kuwa Allah akinijaalia mtoto wa kiume basi nitamwita HIBRI inshaallah. Nashauri tuwekee pia ktk mfumo wa PDF.