Zaka

KUTOA ZAKAAH
 
Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y
 
 
Utangulizi
Kutoa Zakaah ni nguzo ya tatu ya Islam. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Nguzo za Islam ni tano. Shahada kuwa hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, na Kusimamisha Swalah, na Kutoa Zakaah, na Kufunga mwezi wa Ramadhaan na Kuhiji Makka kwa mwenye uwezo wa kufika huko".
 
Kufaridhishwa kwa Zakaah ni jambo muhimu na tukufu sana kwa Waislam kwa sababu ya wingi wa faida yake na kwa ajili ya haja kubwa ya kuwepo kwa jambo hilo, kutokana na masikini na mafakiri wanaohitajia sana msaada wa ndugu zao wenye uwezo, kwani katika Kutoa Zakaah uhusiano mzuri unajengeka baina ya Waislam matajiri na Waislam masikini, na hii ni kwa sababu siku zote moyo wa mtu huelekea na kumpenda yule anayemfanyia wema na ihsani. Zakaah inasaidia pia katika kuzisafisha na kuzitakasa nyoyo.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
"Chukuwa Sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao)".
At Tawba - 103
 
Katika kutoa Zakaah au Sadaka kunaizoesha nafsi katika kuwapendelea kheri watu wenye haja na katika kuwaonea huruma na pia kunaipatia nafsi baraka nyingi kutoka kwa Allaah Subhanahu wa Ta’ala.
Allaah ِAnasema:
وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ
"Na chochote mtakachotoa, basi Yeye Atakilipa; naye ni Mbora wa wanaoruzuku".
Saba-a - 39
 
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Allaah anasema: 'Ewe mwanadamu, toa na sisi tutakupa"
 
Anasema Ibni Uthaimiyn:
"Kutoa Zakaah ni jambo liliofaradhishwa katika Uislam, na ni nguzo muhimu sana baada ya Shahada mbili na Swalah, na dalili ya kuwajibika kwake imo ndani ya Qurani na pia katika mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), pamoja na ijmai ya Waislam, na yeyote anayeikanusha nguzo hii anakuwa Kafir aliyertadi katika Uislam, na hukumu yake ni kutubishwa, na akitubu anasamehewa. Ama akikataa kutubu na akaendelea kuikanusha basi hukmu yake ni kuuliwa.
Ama anayeifanyia ubakhili au akapunguza katika Zakaah yake, huyo anakuwa miongoni mwa madhalimu wanaostahiki adhabu ya Allaah.
Allaah Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Allaah, wape habari za adhabu inyoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyojilimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
At Tawba - 34 - 35
 
"Miongoni mwa faida za kutoa Zakaah anazozipata mtu katika dini yake" anaendelea kusema Sh. Ibin Uthaimiyn, "Ni kuitimiza nguzo katika nguzo za Kiislam, jambo litakalomletea mtu furaha katika dunia yake na katika akhera yake, na pia inazidi kumkaribisha mja kwa Mola wake na kumuongezea Imani, kama ilivyo katika mambo yote ya kumtii Allaah Subhanahu wa Ta’ala."
 
Maana ya Zakaah
Zakaah ni ile haki Aliyoifaradhisha Allaah kwa Muislam katika mali yake anayotakiwa kuwapa wanaostahiki. Neno Zakaah, katika lugha (katika kamusi ya lugha ya kiarabu) maana yake ni 'Kujitakasa', kwa sababu anayetoa Zakaah anataraji kuitakasa mali yake, nafsi yake na kupata baraka kutoka kwa Mola wake.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
"Chukuwa Sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao)".
At Tawba - 103
 
Zakaah ni nguzo ya tatu ya Uislam iliyofaradhishwa katika Qurani tukufu na katika mafundisho ya Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na kwa sababu ya umuhimu wake, Allaah ameitaja mara themanini na mbili katika Qurani kwa kuifuatanisha pamoja na Swalah.
 
Imepokelewa kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) kuwa amesema:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipomteua Muadh bin Jabal (Radhiya Allaahu anhu) kuwa gavana wa nchi ya Yemen na kadhi wao alimwambia:
"Unakwenda katika nchi ya watu wa Ahlul Kitab, kwa hivyo (kwanza) walinganie katika shahada ya Laa ilaaha illa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swalah tano mchana na usiku, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Sadaka (Zakaah) za mali zao, zichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurejeshewa masikini wao, na kama wakitii juu ya hilo, usije ukachukuwa mali zao zenye thamani, na uiogope dua ya aliyedhulumiwa, kwani hapana kizuizi baina yake (dua hiyo) na baina ya Allaah".
Imesimuliwa na Maimamu wote wa hadithi
 
Imesimuliwa pia na Attabarani kutoka kwa Aliy (Radhiya Allaahu anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Allaah amewafaradhishia matajiri wa Kiislam katika mali zao kiasi cha kuwatosha masikini wao. Na (masikini) wasingepata tabu ya njaa na mavazi isipokuwa kutokana na ubakhili wa matajiri wao. Jueni kuwa Allaah atawahesabia hesabu nzito sana na atawapa adhabu iumizayo".
 
Kufaradhishwa Zakaah
Zakaah imefaradhishwa wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa Makka katika siku za mwanzo za Uislam, lakini hapakuwekwa Nisaab, (kiwango cha mali ambacho mtu akiwa nacho kwa muda wa mwaka analazimika kuitolea Zakaah), wala kiasi cha kulipa, isipokuwa waliachiwa Waislam wenyewe kukisia kiasi cha kutoa.
Katika mwaka wa Pili baada ya Hijra, ilifaradhishwa kiasi chake katika kila aina ya mali na kubainishwa vizuri.
 
Umuhimu wake (katika Qur-aan)
Katika Qurani tukufu na katika Mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), yamo mafunzo mengi yanayopendekeza Kutoa Zakaah na yanayowakemea wale wasioitoa.
Katika Qurani Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
"(Ewe Mtume) Chukuwa Sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao)".
At Tawba - 103
 
Na maana yake ni "Chukuwa ewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Sadaka maalum kutoka katika mali za Waislam na uwape wanaostahiki ili wenye mali 'wasafike' kutokana na uchafu wa ubakhili na tamaa, na kutokana na ubaya wa kuwanyima masikini haki zao na pia 'uwatakase' nafsi zao kwa sadaka hizo na wapate baraka za Mola wao ili waweze kupata furaha za hapa duniani na za huko akhera.
 
Na Akasema:
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ. آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ. كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ. وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ. وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ
"Hakika wachamungu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
Wanapokea aliyo wapa Mola wao .
Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.
Walikuwa wakilala kidogo tu nyakati za usiku.
Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.
Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba".
Adhariyaat 15-19
 
Katika aya hizi Allaah anatuelezea juu ya wale atakaowaingiza katika bustani Zake na chemchem, kwa sababu walipokuwa huko duniani walikuwa wenye kulala muda mfupi sana nyakati za usiku, na sehemu kubwa ya usiku, walikuwa wakiswali, na nyakati za kabla ya kuingia alfajiri walikuwa wakiomba maghfira huku wakijikurubisha kwake Subhanahu wa Ta’ala.
 
Walikuwa pia watu wenye kutoa katika mali zao kuwapa fakiri na maskini, wenye kuomba na wasiyo omba huku wakiwaonea huruma.
Na Allaah Akasema pia:
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَـئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zakaah, na humtii Allaah na Mtume wake. Hao Allaah atawarehemu. Hakika Allaah ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima".
At Tawba – 71
 
Umuhimu wake (katika Sunnah)
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mambo matatu naapa juu yake na nakuhadithieni hadithi muihifadhi (vizuri).
Mali haipungui kwa kutoka sadaka, na mtu anapodhulumiwa akasubiri, basi Allaah humuongezea utukufu, na mtu anapojifungulia mlango wa kuombaomba, basi Allaah humfungulia mlango wa ufakiri".
Attirmidhy kutoka kwa Abi Kabsha al Anmaary (Radhiya Allaahu anhum)
 
Na kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Allaahu anhu) amesema kuwa; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Hakika Allaah anazikubali Sadaka na anazipokea kwa mkono wake wa kuume na anailea kama mmoja wenu anavyomlea nyumbu wake mpaka tonge (anayoitoa sadaka) inafikia ukubwa wa jabali Uhud".
Ahmed - Attirmidhiy na ameisahihisha
 
Hadithi hii inatujulisha kuwa mtu anapotoa Zakaah au Sadaka, basi Zakaah hiyo inaingia mikononi mwa Allaah Subhanahu wa Ta’ala kwanza, kabla haijaingia mikononi mwa masikini anayepewa, ikitufahamisha jinsi gani Allaah anavyoitukuza ibada hii ya Kutoa Zakaah na jinsi anavyompenda mja wake mwenye kutoa Zakaah au Sadaka hata akaipokea kwa mikono yake Mwenyewe Subhanahu wa Ta’ala kwanza, akaizidisha jaza yake na kuifanya iwe na ukubwa wa Jabali Uhud.
 
Anasema Waki’i:
"Hadithi hii pia inasadikisha kauli yake Subhanahu wa Ta’ala katika Qurani pale Aliposema:
يَعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ
"Je! Hawajui kwamba Allaah anapokea toba za waja Wake na kuzipokea Sadaka?"
At Tawba - 104
 
Na ِAliposema:
يَمْحَقُ اللّهُ الْرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ
"Allaah huyafutia (baraka mali ya) riba, na huyatia baraka (mali inayotolewa) Sadaka".
Al Baqarah - 276
 
Imepokelewa kuwa Anas (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Mtu mmoja kutoka katika kabila la Bani Tamim alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:
"Ewe Mtume wa Allaah, mimi nina mali nyingi na nina jamaa wengi na wageni huja kwangu kwa wingi. Kwa hivyo nijulishe nini nifanye na vipi nitowe?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Utoe Zakaah kutoka katika mali yako, kwa sababu hiyo ni tohara itakayokutahirisha, na uwaendee watu wako (ndugu zako wa nasaba), na uijue haki ya masikini na ya jirani na ya muombaji".
Ahmed
 
Na Kutoka kwa Bibi Aisha (Radhiya Allaahu anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mambo matatu naapa juu yake, Allaah hawezi kumfanya aliye na sehemu yake katika Uislam akawa sawa na yule asiye na sehemu. Na sehemu za Uislam ni tatu. Swalah, Funga na Zakaah. Na Allaah anapokuwa pamoja na mja wake hapa duniani, basi huko akhera hamuachi akawa na mwengine asiyekuwa Yeye. Na mtu anayewapenda watu hapa duniani, basi siku ya Qiyaamah Allaah Atamjaalie awe pamoja nao…."
Ahmed
 
Na kutoka kwa Jabir (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam);
"Ewe Mtume wa Allaah; Unasemaje juu ya mtu anayetoa Zakaah ya mali yake?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Atakayetoa Zakaah ya mali yake, keshaiondoa shari yake".
 
Wasiotoa Zakaah (katika Qur-aan)
Allaah Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Allaah, wape habari za adhabu inyoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyojilimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
At Tawba - 34 - 35
 
Na akasema:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُواْ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
"Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko). La, ni vibaya kwao. Watafungwa kongwa (madude ya kunasa shingoni) za yale waliyoyafanyia ubakhili - siku ya Kiyama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. Na Allaah ana khabari za yote mnayoyafanya."
Aali Imran - 180
 
Katika aya hii, Allaah amesema 'Sayutawwaquwna' na maana yake ni (Watafungwa kongwa) badala ya 'Sawfa yutawwaquna'. (Watakuja kufungwa kongwa).
Ameacha kutumia neno Sawfa’ akaiunganisha moja kwa moja kwa kusema: 'Sayutawwaquwna' kwa ajili ya kutujulisha ukaribu wa mtu kukumbana na adhabu hizo. Kwa sababu mtu akeshakufa tu Qiyaamah chake kishasimama, na kuanzia hapo mpaka siku ya Qiyaamah ataanza kukumbana na baadhi ya adhabu kutokana na yale maovu aliyoyatenda.
Wangapi wametoka majumbani mwao kwa miguu yao wenyewe, wakarudishwa wakiwa wamebebwa. Wangapi walifunga wenyewe vifungo vya suruali zao, wakaja kufunguliwa na waoshaji maiti.
Mwanadamu anapotafakari juu ya wale wanaobebwa juu ya majeneza kila siku na kupelekwa makaburini wakiacha mali zao nyingi nyuma yao, mali zitakazokuja kufaidiwa na warithi, ataona namna gani yeye alivyohangaika kuichuma mali hiyo na nani atakayekuja kufaidika nayo, na nani atakayehesabiwa juu ya mali hiyo.
Ikiwa mali imepatikana kwa njia zisizokuwa za halali au ikiwa mali hiyo haikutolewa ndani yake haki ya Allaah, basi mali hizo watasatarehe nayo warithi, na yule aliyechuma ndiye atakayeulizwa na Allaah na kuhesabiwa.
Allaah Subhanahu wa Ta’ala Akamaliza aya hii kwa kusema:
وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
"Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. Na Allaah ana khabari za yote mnayoyafanya."
 
Na maana yake ni kuwa hata kama utawaachia mali hiyo watu wako, wao pia watakuja kufa na watakaokuja baadaye nao watakufa, na mwisho kabisa hapana atakayebaki isipokuwa Allaah Subhanahu wa Ta’ala, siku atakayozirithi mbingu na ardhi na kila kilicho juu yake.
 
Wasiotoa Zakaah (katika Sunnah)
Imepokelewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Allaahu anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Atakayepewa mali kisha asitoe Zakaah yake, basi mali hiyo Siku ya Qiyaamah itageuzwa kuwa joka dume lenye upara, mwenye madoa mawili machoni pake (kutokana na wingi wa sumu aliyonayo), atajizungusha katika mwili wa mtu huyo, kisha atamkaba shingoni pake huku akimwambia:
"Mimi ndiyo hazina yako uliyokuwa ukiikusanya, mimi ndiyo mali yako", kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaisoma aya hii:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ
"Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko)".
Bukhari na Muslim
Na kutoka kwa AbdiAllaahi bin Umar bin Khattab - RadhiyAllaahu anhuma amesema kuwa; "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Enyi watu wa Madina, mambo matano mkija mkapewa mtihani juu yake na kuteremshiwa - Najikinga kwa Allaah yasije yakakukuteni - Hautoenea uzinzi katika kaumu mpaka wakafikia kujitangazia, (isipokuwa) yatakuja kuenea kwao maradhi (aina mpya) ambayo hayajakuwepo kwa waliowatangulia, na hawatopunjwa watu katika vipimo na katika mezani isipokuwa wataletewa umasikini na shida ya kupatikana vitu, na dhulma ya ufalme. Na watakapoacha (watu) kutoka Zakaah ya mali zao, watanyimwa mvua, na lau kama si kwa ajili ya wanyama, basi isingenyesha mvua. Na watakapovunja ahadi ya Allaah na ahadi ya Mtume wake, watasalitishiwa adui asiyekuwa mwenzao achukuwe baadhi ya vilivyo mikononi mwao. Na ikiwa viongozi wao hawatahukumu kwa kitabu cha Allaah, basi vitafanywa vita vyao viwe baina yao"
Ibni Majah - Al Bazaar na Al Bayhaqi
 
Hukmu ya asiyetowa Zakaah
Kutoa Zakaah ni fardhi, na ni katika mambo waliyokubaliana maulamaa wote kuwa yeyote anayeikanusha fardhi hii anakuwa kesha toka katika dini akiwa ni kafiri aliyertadi, isipokuwa kama mtu huyo ni Muislam mpya, na kwa ajili hiyo husameheka kutokana na kutoelewa kwake.
Ama yule anayeacha kutoa Zakaah lakini wakati huo huo hakanushi kuwajibika kwake, huyo anapata dhambi ya kuacha kuitoa, lakini kuacha huko hakumtoi katika dini, isipokuwa ikiwa anaishi katika nchi inayohukumiwa na sheria ya Kiislam, basi anayehukumu atatakiwa aichukuwe Zakaah hiyo kwa nguvu.
 
Ipo hitilafu baina ya maulamaa iwapo anayeacha kutoa Zakaah atozwe gharama kwa kuacha kwake huko kwa ajili ya kumtia adabu, na gharama yenyewe ni kuchukuliwa nusu ya mali yake, na hii inatokana na hadithi iliyotolewa na Imam Ahmad na Annasaiy na Abu Daud na Al Haakim na Al Bayhaqiy kutoka kwa Bahza bin Hakim kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kuwa amesema:
"Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:
"…Atakayekataa (kutoa Zakaah) tutaichukuwa (kwa nguvu, na pia tutachukua) pamoja na nusu ya mali yake haki katika haki ya Mola wetu Mtukufu na watu wa Aali Muhammad si halali kwao kuchukuwa chochote katika hiyo (Zakaah)".
Amesema Imam Ahmed kuwa isnadi ya hadithi hii ni sahihi na amesema Al Hakim kuwa hii ni hadithi sahihi.
 
Hata hivyo wapo baadhi ya maulamaa walioidhoofisha hadithi hii na wengine wakasema kuwa hukmu hii ilifutwa baadaye, wakiegemea baadhi ya hadithi zinazoelezea juu ya baadhi ya watu waliochelewa kulipa Zakaah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwachukulia nusu ya mali zao.
Ama ikiwa watu watakataa kutoa Zakaah wakiwa wanaelewa kuwa ni jambo la wajibu, na ikiwa zipo nguvu za kuweza kupambana nao, basi watapigwa vita mpaka wakubali kuitoa. Na hii inatokana na hadithi iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim kuwa AbdiAllaahi bin Umar (Radhiya Allaahu anhu) amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahad ya; Laa ilaaha illa Allaah Muhammadan Rasulu Allaah, na wasimamishe Swalah na watowe Zakaah. Wakishafanya hivyo, damu yao na mali zao zitakingika kwangu isipokuwa katika kulipa haki za Kiislam, na hesabu yao iko kwa Allaah".
 
Imeelezwa na Abu Huraira (Radhiya Allaahu anhu) kuwa; Alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Abubakar akawa (Khalifa), baadhi ya waarabu walikataa kutoa Zakaah, na Abubakar (Radhiya Allaahu anhu) alitayarisha jeshi akupambana nao.
Umar akasema (kumuuliza Abubakar):
"Vipi unataka kupigana vita na watu (Waislam), wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:
"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; Laa ilaaha illa Allaah na atakayetamka hayo itakingika kwangu mali yake na nafsi yake isipokuwa katika haki yake (anayodaiwa au kisasi kwa makosa aliyofanya), na hesabu yake iko kwa Allaah?”
Abubakar (Radhiya Allaahu anhu) akasema:
"WAllaahi nitampiga vita yeyote atakayetenganisha baina ya Swalah na Zakaah, kwa sababu Zakaah ni katika 'haki yake' (shahada hiyo). WAllaahi lau kama wataacha kunipa mbuzi mdogo (na katika riwaya nyingine 'Kamba') iliyokuwa ikilipwa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), ningewapiga vita kwa kukataa kwao kuitoa".
Umar (Radhiya Allaahu anhu) akasema:
"WAllaahi nilipoona kuwa Allaah amemfungulia Abubakar kifua chake aamue kuwapiga vita, nikajuwa kuwa yuko katika haki".
Muslim - Abu Daud - na Attirmidhy na maimamu wengine wa hadithi.
 
Wanaowajibika kutowa
  • Muislam anayemiliki Niswaab, nacho ni 'Kiwango maalum cha mali kilichowekwa na sheria katika aina yoyote ile ya mali inayowajibika kuitolea Zakaah.
  • Niswaab hiyo lazima iwe ishatolewa ndani yake mahitajio ya dharura ya lazima kama vile chakula, mavazi, makazi, vyombo vya nyumbani, chombo cha usafiri na vyombo vyake vya kufanyia kazi, madeni nk.
  • Lazima kiwango hicho kiwe kimemilikiwa kwa muda wa mwaka mzima (mwaka wa Kiislam) bila kupungua katika wakati wowote ule ndani ya mwaka huo, na kama kitapungua katika wakati wowote ule kabla ya kutimia mwaka, basi hesabu nyingine mpya itaanzwa kuanzia pale kinapokamilika tena Kiwango hicho.
Amesema Imam An Nawawiy:
"Madhehebu yetu na madhehebu ya Maimam Malik na Ahmad na ya maulamaa walio wengi ni kuwa; Mali inayotolewa Zakaah kwa ajili yake, kama vile dhahabu, fedha na wanyama wa kufugwa, lazima kiwango chake kibaki kwa muda wa mwaka mzima bila kupungua. Na wakati wowote ule kitakapopungua, basi mwaka wake unakatika, na wakati wowote ule kitakapotimia tena, unaanza kuhesabiwa mwaka mwingine".
 
Abu Hanifa anasema:
"Kinachotakiwa ni kuwepo kwa Kiwango (Niswaab) mwanzo wa mwaka na mwisho wake, na haidhuru iwapo kitapungua katikati ya mwaka, hata kama mtu alikuwa nazo Dirham mia mbili kisha zikapotea zote katikati ya mwaka na akabakiwa na dhirham moja tu, au kama alikuwa na kondoo arubaini wakapungua na akabaki mmoja tu, kisha mwisho wa mwaka akaweza kumiliki (Dirham) mia mbili kamili au (kondoo) arubaini kamili, basi itawajibika Zakaah kwa vyote".
 
Masharti haya hayahusiani na Zakaah za mazao na matunda, kwa sababu vitu hivyo Zakaah yake inatolewa siku ya mavuno.
Allaah anasema:
أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ
"Na toeni haki yake siku ya kuvuna kwake".
Al An-am – 141
 
Mtoto na mpungufu wa akili
Inamuwajibikia aliyekabidhiwa mali ya yatima au ya mtu mwenye upungufu wa akili kuitolea Zakaah mali hiyo ikifikia kiwango chake.
Kutoka kwa AbdiAllaahi bin Amru (Radhiya Allaahu anhu), anasema kuwa; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mwenye kumlea yatima mwenye mali, basi aifanyie biashara mali hiyo na asiiache mpaka ikamalizika kwa kuliwa na Sadaka (Zakaah)".
 
Anasema Sh. Sayed Sabeq katika Fiqhis Sunnah kuwa; Isnadi yake ina udhaifu ndani yake. Akaendelea kusema:
“Anasema Al Hafidh kuwa hadithi hii ina ushahidi kuwa ni 'Mursal' iliyorushwa moja kwa moja mpaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) bila ya kutaja isnadi. Ama Imam Shafi ameikubali (hadithi hii) kwa sababu zipo hadithi nyingi zinazoelezea juu ya kuwajibika kwa Zakaah katika mali yoyote ile.  Anasema Imam Attirmidhiy kuwa wanavyuoni wamekhitalifiana juu ya kuwajibika kuitolea Zakaah mali ya yatima,” amemaliza kusema Sh. Sayed Sabeq.
 
Mwenye deni
Mwenyezi kumiliki kiwango kinachomwajibisha kutoka Zakaah, na wakati huo huo anadaiwa, kwanza anatoa kiasi cha deni analodaiwa, kisha anailipia Zakaah mali iliyobaki ikiwa bado inafikia kiwango cha kutolewa Zakaah. Ama ikiwa mali iliyobaki haifikii kiwango, basi hatoi Zakaah, kwa sababu wakati huo anahesabiwa kuwa ni mtu fakiri, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anasema:
"Hatoi Sadaka (Zakaah) isipokuwa mtu tajiri".
Ahmad
 
Na amesema:
"Ichukuliwa (mali ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".
 
Aliyefariki
Anasema Sayyid Sabeq katika Fiqhis Sunnah kuwa, katika madhehebu ya Imam Shafi na Ahmad na Abu Thour, ni kuwa mtu akifarki na akaacha deni la Zakaah, basi inawajibika katika mali yake kwanza kutolewa deni la Zakaah hata kabla ya kutimizwa wasia aloacha na kabla ya kupewa warithi.
Allaah anasema:
مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ
"Baada ya kutoa aliyoyausia au kulipa deni".
An Nisaa - 11
 
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa".
Na Zakaah ni deni la Allaah.
 
Kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) kuwa amesema:
“Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Mama yangu amefariki na anadaiwa saumu ya mwezi mzima, je nimlipie?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuuliza:
"Mama yako angelikuwa na deni ungemlipia?"
Akasema:
"Naam, ningemlipia".
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Basi deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa".
Bukhari na Muslim
Nia
Zakaah ni ibada, na kwa ajili hiyo Kutia Nia ni jambo muhimu kama ilivyo katika ibada yoyote ile. Na nia ni kitu cha moyoni na hakina uhusiano na ulimi, na kusudi lake ni kuwa mtu anapotoa Zakaah akusudie kuitoa kwa ajili ya Allaah.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Hakika ya amali yoyote ni kutokana na nia, na mtu hulipwa kutokan na nia yake".
 
Kutowa panapowajibika
Inawajibika kuitoa Zakaah pale wakati wake unapowadia, na haijuzu kuichelewesha isipokuwa kwa dharura inayokubalika.
Kutoka kwa Bibi Aisha (Radhiya Allaahu anha) amesema kuwa; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Haichanganyiki mali pamoja na Zakaah isipokuwa itaiangamiza", na katika riwaya nyingine;
"Inakuwa ishakuwajibikia katika mali yako kuitolea Zakaah, kisha usiitoe, kwa hivyo (mali ya) haramu (isiyotolewa Zakaah) inaiangamiza (mali ya) halali".
Shafi na Bukhari katika 'Attariykh'
Kuitanguliza
Inajuzu kuitanguliza na kuitoa kabla ya kufikia wakati wake hata kabla ya miaka miwili.
Anasema Al Shoukani katika kitabu chake 'Naylu l Awtaar';
"Maulamaa wengi kama vile Azzuhriy na Al Hassan al Basriy na Maimam Shafi na Ahmad na Abu Hanifa wamejuzisha kuitanguliza Zakaah kabla ya kufikia wakati wake".
 
Ama Imam Malik na Sufyan al Thouriy na baadhi nyingine ya maulamaa wameona kuwa haijuzu kuitanguliza kabla ya wakati wake, wao wameziegemea zile hadithi zinazowajibisha kutoa Zakaah baada ya kukamilika mwaka.
 
Anasema Ibni Rushd:
"Hitilafu iliyopo baina ya maulamaa ni kuwa - Zakaah ni Ibada au haki iliyowajibishwa kupewa masikini. Wanaosema kuwa Zakaah ni Ibada, wao wameifananisha na Swalah na wakasema kuwa haiwezekani kutolewa kabla ya kufikia wakati wake.
Ama wale wenye kuona kuwa ni haki iliyowajibika, wamejuzisha kuitoa kabla ya kufikia wakati wake ikiwa mtu mwenyewe amejitolea kufanya hivyo".
 
Ama Imam Shafi ameegema madai yake katika hadithi inayosema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kuchukuwa katika mali ya Al ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) na kuitolea Zakaah kabla ya kufikia wakati wake.
 
Kuomba dua
Inapendeza kumuombea dua mtoaji Zakaah, pale anapoitoa.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ
"Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao) na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu. "
At Tawba - 103
 
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abi Aufiy amesema:
“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa pale anapoletewa mali ya Zakaah akisema: "Allaahumma salliy ‘alayhim". Na baba yangu siku moja alimpelekea mali ya Zakaah akasema: "Allaahumma salliy alaa aali Abi Aufiy".
Ahmad na wengineo.
 
Imepokelewa kutoka kwa Wail bin Hajar kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimuombea mtu mmoja aliyeleta ngamia wa Zakaah akasema:
"Allaahumma barik fiyhi wa fiy Ibilihi". (Allaah mbariki yeye na ngamia wake)
Anasema Imam Shafi:
"Ni Sunnah kwa Imam anapopokea mali ya Zakaah kumuombea dua mtoaji kwa kumwambia: "Aajaraka Allaahu fiyma aatayta, wa baarik laka fiyma abqayta".
(Allaah akupe ujira mwema katika ulichotoa na akubarikie katika kilichobaki).
 
Mali inayotolewa Zakaah
  1. Dhahabu na Fedha
  2. Mazao na Matunda
  3. Mali ya Biashara
  4. Wanayama wa kufugwa
  5. Dhahabu na Fesha
Dhahabu na  Fedha
Allaah Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Allaah, wape habari za adhabu inayoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyolimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
At Tawba - 34 - 35
 
Kwa hivyo mwenye kumiliki viwili hivyo (Dhahabu au Fedha) ikiwa ni katika mfumo wa pesa au mikufu au vipande (vinoo), ikitimia nisabu yake na kukamilisha mwaka na akawa hana deni, wala shida yoyote, anawajibika kuitolea Zakaah yake.
 
Wakati wa Mtume
Wakati wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), watu wa Bara Arabu walikuwa wakifanya biashara zao kwa njia ya kubadilishana bidhaa, na hawakuwa wakitumia pesa isipokuwa wachache sana walioweza kumiliki pesa za dhahabu na za fedha zilizokuwa zikitumika katika nchi za jirani.
Pesa zilizotengenezwa kwa dhahabu zilikuwa zikiitwa Dinari, na zilikuwa zikiletwa kutoka nchi za Warumi kama vile Byzantine na nyenginezo, na walikuwa pia wakitumia pesa zilizotengenezwa kwa fedha zilizokuwa zikiitwa Dirham na hizi zilikuwa zikitoka nchi ya Wafursi - Iran.
Kwa vile pesa hizo zilikuwa zikiwafikia zikiwa na uzito mbali mbali, na kiasi mbali mbali, nyengine ndogo ndogo na nyengine kubwa kubwa, na hazikuwa na kiasi maalum wala uzito maalum, kwa hivyo watu wa Makka hawakuwa wakizitumia kama zinavyotumiwa pesa za kawaida, bali walikuwa wakizipima na kuzipa thamani maalum waliyokubalina.
Miongoni mwa vipimo walivyokuwa wakitumia ilikuwa ratili, ambayo wakati huo ilikuwa na uzito wa wakia kumi na mbili na walikuwa pia wakitumia vipimo vya Mithqaal.
Kutokana na kipimo cha Mithqaal, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Haitolewi Zakaah ikiwa dhahabu haikutimia Mithqaal ishirini ".
 
Karatasi za benki (Bank notes) zinazopigwa chapa na serikali tofauti ulimwenguni, hupigwa chapa kulingana na Dhahabu na Fedha inayomiliki serikali hizo, ama sivyo serikali yoyote masikini au yenye madeni ingelipiga chapa idadi ya noti yenye thamani kubwa kuliko dhahabu waliyo nayo na kuweza kulipa madeni yao na kujitajirisha.
 
Nisabu yake
Dhahabu hailipiwi kitu mpaka ifikie Nisabu yake na imilikiwe (nisabu hiyo) kwa muda wa mwaka (Mwaka wa Kiislam).
Nisabu ya dhahabu ni mithqaal 20 au gramu 92 au Tola71/2 au wakia 3. (Baadhi ya maulamaa wanasema kuwa Nisabu yake ni gramu 85 au Tola 5 au wakia 2), na hii inatokana na ugumu wa kuweza kukisia bei ya vipimo vilivyokuwa vikitumika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na vinavyotumika wakati wetu huu. Hapana hitilafu juu ya kiwango cha Mithqaal 20 isipokuwa hitilafu ipo katika kuifasiri Mithqaal katika vipimo vya kisasa.
 
Inapofikia kiwango hicho, na kubaki muda wa mwaka, unaichukua na kuipeleka kuipima kwa sonara au kwa wajuzi, na baada ya kuijua thamani yake unailipia 2.5% (mbili unusu katika mia) ya thamani ya dhahabu yote.
Nisabu ya dhahabu ndiyo Nisabu ya pesa za kawaida.
Kwa mfano katika nchi ya UAE, bei ya gramu tisini na mbili ya dhahabu ni Dh. 2575/-
Kwa hivyo hicho ndicho kiwango cha kuanzia kulipia Zakaah. Na dhahabu yako inapofikia kiwango hicho unailipia Dh. 64 /- ambayo ni mbili unusu katika mia ya thamani hiyo. Dhabu inapozidi, na Zakaah yake inaongezeka.
Unailipia thamani ya dhahabu tu bila kuhesabu ujira wa mfuo au kazi ya mkono au thamani ya nakhshi zake. (Gharama za ufulishaji hazimo).
 
Fedha
Nisabu ya fedha ni mithqaal 140 au Tola 36 au wakia 141/2.
Ikifikia kiwango hicho na ikamilikiwa muda wa mwaka, inalipiwa moja katika arubaini au mbili unusu katika mia ya thamani yake.
Zakaah ya Deni (Mwenye kudai)
Maulamaa wameigawa deni katika hali mbili.
  1. Ikiwa anayedaiwa ni mtu tajiri au mtu muaminifu, deni hilo litachukuliwa mfano wa pesa zilizowekwa dhamana katika benki ambapo wakati wowote mtu anaweza kuzipata au ana uhakika wa kulipwa deni lake.
Katika hali hii zipo rai tatu.
  1. Ya kwanza ni kuwa mwenye kudai anatakiwa ailipie mali hiyo Zakaah yake, juu ya kuwa halazimiki kuilipia mpaka pale atakapozipata na wakati huo atailipia pamoja na Zakaah ya siku zote za nyuma.
  2. Ya pili ni kuwa analazimika kuilipia Zakaah yake kila unapotimia mwaka, kwa sababu pesa hizo zitahesabiwa mfano wa pesa zilizowekwa benki, na hii ni kwa sababu aliyekopeshwa ni mtu tajiri au muaminifu kiasi cha kuwa ana uhakika wa kulipwa au wa kuzipata pesa zake hizo wakati wowote ule anapozitaka.
  3. Rai ya tatu ni kuwa hazilipii mpaka pale atakapolipwa deni hilo, na hapo atazilipia Zakaah ya mwaka ule mmoja tu.
Anasema Sheikh Mohammad bin Uthaymiyn:
"Rai ya mwanzo, nayo ni kuilipia Zakaah ya miaka yote pale atakapozipata pesa zake ni bora zaidi na inakubalika zaidi".
 
  1. Ikiwa anayedaiwa ni mtu masikini au mtu asiyekuwa muaminifu, haimuwajibikii mwenye kudai kuzitolea Zakaah pesa hizo mpaka pake atakapozipata na kubaki nazo muda wa mwaka mzima kisha atazilipia Zakaah ya mwaka huo tu, ambao mali yake hiyo ilibaki kwake kama kawaida ya utoaji wa Zakaah.
Anasema Sheikh Bin Uthaimiyn:
"Haijuzu kumdai au kumlazimisha mtu masikini au kumshitaki na hatimaye kumuingiza jela na kumtenganisha na watu wake ikiwa mtu huyo hana kweli uwezo wa kulipa deni, na ikiwa mtu huyo hafanyi ujanja wa kuchelewesha makusudi, na badala yake tunatakiwa tumsitahamilie mpaka pale Allaah atakapomfariji.
Allaah Anasema:
وَاتَّقُواْ يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ
"Na kama (mkopi) ana dhiki, basi (mdai) angoje mpaka afarijike, na kama nyinyi (mnaodai mkizisamehe deni zenu) mkazifanya sadaka, basi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua haya (basi fanyeni).
Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Allaah, kisha viumbe wote watalipwa kwa ukamiliyote waliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa".
Al Baqarah - 280 - 281
Mtu akisema:
"Pesa zangu kwanini nisizidai?", Anaendelea kusema Sh. Bin Uthaimiyn,
"Tunamwamia:
Ni kweli pesa zako, lakini wewe mwenyewe ndiye uliyemkopesha pesa hizo. Pale alipokujia kutaka kukukopa ungelimtafutia udhuru wowote ule, kisha ukampa kiasi chochote cha mali ikiwa kama ni msaada tu kutoka kwako, basi yansingekukuta haya. Lakini umkopeshe na hali unajuwa kuwa mtu huyu ni masikini, kisha akishindwa kukulipa ukamshitaki, umtie jela na kumtenganisha na mke na watoto wake, jambo hilo ni haramu kabisa na haijuzu kwa Muislam kulitenda".
(Mwisho wa maneno ya Sheikh Ibni Uthaimiyn).
 
Zakaah ya Mapambo
Maulamaa wamekhitalifiana katika kuzitolea Zakaah dhahabu na fedha za mapambo.
Wapo waliosema kuwa dhahabu au fedha ya kujipamba inapofikia Nisabu yake lazima itolewe Zakaah yake, na hawa wameegemeza hadithi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema kumwambia mwanamke mmoja aliyemvisha mwanawe mkufu wa dhahabu akamwambia:
"Unailipia Zakaah yake?"
Akasema:
"La, hatuilipii"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Huogopi Allaah akakuvalisheni mikufu ya Moto? Zilipie Zakaah yake".
Imam Ahmad
 
Na pia hadithi iliyosimuliwa na Bibi Aisha (Radhiya Allaahu anha) aliposema:
"Aliingia chumbani kwangu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaniona nimevaa pete za fedha. Akaniuliza:
"Nini hiki Ewe Aisha?"
Nikamwambia:
"Nimezitengeneza ili nijipambe kwa ajili yako ewe Mtume wa Allaah".
Akasema:
"Unazilipia Zakaah yake?"
Nikasema:
"Hapana."
Akasema:
"Hiyo inatosha kwa (kukupatia adhabu ya) Moto".
Abu Daud - Addaraqutni na Al Baihaqi
 
Ama wale wanaosema kuwa Dhahabu ya mapambo hailipiwi Zakaah, wao wameegemeza hoja zao katika hadithi iliyosimuliwa na Al Baihaqiy inayosema:
"Jabir bin AbdiAllaah (Radhiya Allaahu anhu) aliulizwa juu ya mapambo:
"Yanatolewa Zakaah?
Akasema:
"La, hayatolewi"
Akaulizwa:
"Hata kama thamani yake itafikia Dinari elfu moja?'
Akasema:
"Zaidi" (hata kama zaidi ya thamani hiyo)
Na pia hadithi iliyomo katika Muwataa, kitabu cha Imam Malik inayosema:
"Bibi Aisha alikuwa akiwalea wana wa kaka yake mayatima na walikuwa na mapambo na hakuwa akiyatolea Zakaah.”
 
Atakayezichunguza hadithi hizi na zile, ataona kuwa zile zinazolazimisha kuitolea Zakaah dhahabu au fedha ya mapambo ndizo zenye nguvu zaidi na zenye uhakika zaidi kuliko zisizolazimisha - WAllaahu Ta’ala Aalam.
 
Zakaah ya Biashara
Hukmu yake
Wapo baadhi ya maulamaa ambao ni wachache sana wanaosema kuwa hapana dalili ya kuwa mali ya biashara inatolewa Zakaah, lakini dalili zilizomo ndani ya Qurani na Sunnah zinaleta maana kinyume na rai zao.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ
"Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao) na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu."
At Tawba - 103
Aya hii inaleta maana ya ujumla kuwa Zakaah inatakiwa itolewe kutoka katika mali zao (Matajiri), mali ya aina yoyote ile ikiwemo mali ya biashara, bila kufafanua aina ya mali hiyo.
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Ichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".
Kwa hivyo dalili hizi zinatujulisha kuwa mali yoyote ile, ikiwemo mali ya biashara, lazima itolewe Zakaah, na kwamba Zakaah hiyo ichukuliwe kutoka kwa matajiri, na bila shaka wafanya biashara ni matajiri, na kwamba irudishwe kwa masikini. Muhimu mali hiyo iwe imekifikia kile kiwango cha kutolewa Zakaah (Niswabu) na imekamilisha muda wa mwaka.
 
Namna ya kutoa Zakaah ya Biashara
Mwenye kumiliki mali ya biashara iliyofikia Niswabu, akishakamilisha mwaka anatakiwa ahesabu mali yake yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya biashara. Kama ni mfaya biashara wa nyumba, basi azihesabu nyumba zake (zile tu alizozitayarisha kwa ajili ya biashara), au ardhi au vyombo vya nyumbani, magari au nguo au biashara ya aina yoyote ile. Atavihesabu vitu alivyokuwa navyo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzihesabu pesa zote alizonazo kwa ajili ya biashara kisha atazitolea Zakaah yake, nayo ni mbili unusu katika mia au moja katika arubaini.
Atafanya hesabu hiyo bila kujali kama wakati wowote ule ndani ya mwaka ule pesa hizo zilipungua au kuongezeka.
 
Kumbuka
Ikumbukwe kuwa vitakavyohesabiwa ni vitu vilivyotayarishwa kwa ajili ya biashara tu.
Kwa mfano mtu anamiliki magari hata yakifikia idadi ya magari kumi au zaidi, au atataka kuuza gari lake mwenyewe kwa ajili ya kulibadilisha tu na kununua gari jengine au ardhi au nyumba au chochote kile, ikiwa anataka kuuza kwa ajili ya kutaka kununua kingine badala yake au kwa ajili ya mahitajio mengine yasiyokuwa ya kibiashara, basi mali hiyo haitolei Zakaah ya biashara, na hii ni kwa sababu nia ya kuviuza vitu hivyo si kwa ajili ya biashara.
Kumbuka pia kuwa Zakaah inatolewa kutokana na asili ya chochote kilichoongezeka kutokana mali hiyo wakati wowote ule katika mwaka. Ama kile kilichoongezeka kutokana na asili nyingine, basi mwaka wake unaanza kuhesabiwa kuanzia siku ile iliyoongezeka mali hiyo.
Kwa mfano;
Mfanya biashara alikuwa akiendela kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha Shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa mwisho au hata katika siku ya mwisho kabla ya kutimia mwaka, akapata faida kiasi cha Shilingi laki saba, pesa zote hizo ZITAHESABIWA pamoja na Zakaah ya biashara ya mwaka huo, kwa sababu asili yake (faida iliyopatikana) inatokana na biashara hiyo anayoitolea Zakaah.
Mfano mwingine:
Mfanya biashara alikuwa akiendelea kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa kumi na mbili au katika siku ya mwisho au siku yoyote ile ya mwaka huo kabla ya kuingia muda wa kulipa Zakaah ya mwaka ule, mtu huyo akarithi pesa kutoka kwa jamaa yake aliyefariki kiasi cha Shilingi milioni moja.
Pesa hizo alizorithi HAZITOHESABIWA katika Zakaah ya mwaka huo, bali ataanza kuzihesabia mwaka wake mpya kuanzia siku ile alizozipata pesa hizo. Kwa sababu asili ya pesa hizo hazitokani na biashara ile anayoitolea Zakaah, bali inatokana na asili nyingine, ambayo ni urithi.
 
Wenye kupokea mishahara
Kwa kawaida mwenye kupokea mshahara pesa zake huongezeka na kupungua katika miezi mbali mbali. Kwa vile itakuwa vigumu kwake kuweka hesabu ya kila mwezi pale zinapokamilisha Niswabu au kuongozeka pale zinapopungua, wanavyuoni wakasema kuwa mtu huyo ataanza kuuhesabu mwaka wake kuanzia siku ile aliyoweza kutimiza Nisabu, na kuanzia mwezi huo, atakuwa akiitolea Zakaah mali yake kila anapotimiza mwaka.
Zakaah ya Mazao
Allaah amewajibisha kuyatolea Zakaah mazao Aliposema:
وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ كُلُواْ مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ
"Naye (Allaah) ndiye alyeiumba miti inayoegemezwa na isiyoegemezwa, na mitende na mimea yenye matunda mbali mbaIi, na (akaumba) mizaituni na mikomamanga inayofananana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapotoa matunda na toeni haki yake siku ya kuvuna kwake".
Al An-am - 141
 
Katika kuifasiri aya hii amesema Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu):
'Haki yake, ni Zakaah yake iliyofaradhishwa".
 
Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Zakaah ya mazao ilikuwa ikitolewa katika Mahindi, Ngano, Mtama, Tende na Zabibu na wengine wakaongeza 'Mchele' na wengine wakasema kuwa Zakaah ya mazao inatolewa katika chakula chochote kile kinachoweza kubaki muda mrefu kama vile mwaka au zaidi bila kuharibika.
Matunda, hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa Tende na Zabibu. Matunda mengine hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa kama matunda hayo ni kwa ajili ya biashara, basi hapo itatolewa Zakaah ya biashara na si Zakaah ya Mazao.
Zakaah ya Mazao inatolewa siku ya kuvuna na kabla ya kuuzwa wala kuliwa na si lazima itimie mwaka.
 
Niswabu ya Mazao
Mazao hayatolewi Zakaah mpaka yatimie Wiski tano yakiwa safi bila magamba. Kama hayajasafishwa, basi lazima yatimie wiski kumi.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Chini ya Wiski tano haitolewi Zakaah".
Imam Ahmad na Al Bayhaqiy
 
Wiski 5 ni sawa na pishi 300, kwa sababu wiski moja ni sawa na pishi sitini kwa pishi iliyokuwa ikitumika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na pishi sitini mara tano ni sawa na pishi mia tatu.
Kwa vipimo vya kisasa, anasema Ustadh Said ‘Abdullaah Seif Al Hatimiy katika kitabu chake 'Kutoa Zakaah':
"Niswaab ya mazao ni Wisqi 5. Moja ni kilo 60 yaani kilo 300. Kilo moja ni ratili 13/4 (ratili mbili kasorobo) (300 mara 13/4 = ratili 525).
Kilo karibu ni sawa na pishi ya mbao (vibaba vinne)."
Mwisho wa maneno ya Ustadh Said Al Hatimiy.
 
Kwa hivyo mazao yakifikia pishi 300 au ratili 525 yanakuwa yamefikia Niswaab yake (kiwango chake) na yatatolewa Zakaah yake ambayo ni moja juu ya kumi (one tenth), hii ikiwa mazao hayo yanapata maji yake bila kuyahangaikia, yaani kama vile kunyeshewa na mvua au maji ya mito au chemchem nk.
Ama ikiwa mkulima anayatilia maji yeye mwenyewe kwa kuyahangaikia maji hayo, basi Zakaah yake itapungua na itakuwa ni nusu ya moja juu ya kumi.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Kilichonyeshewa na mvua au maji yanayopita (waadi) au yaliyotwama (Zakaah yake ni) moja katika kumi na kilichomiminiwa maji nusu ya moja katika kumi".
Bukhari na wengineo.
 
Allaah ameamrisha kuitoa Zakaah ya mazao; "Siku ya kuvuna kwake", na maana yake ni; kabla hakijaliwa wala kugawiwa chochote kile ndani yake, na ikiwa mtu amekwishafanya hivyo kwa kusahau, basi itambidi akisie kile alichotoa au alichouza na akitolee Zakaah yake.
Ama kile alichokula mkulima kabla ya kuvuna, hakimo katika hesabu.
Alipoulizwa Imam Ahmad juu ya wanachokula wenye ardhi kabla ya mavuno alisema:
"Hapana neno ikiwa atakula katika mazao yake kiasi anachohitajia".
Anasema Sh. Sayed Sabiq:
"Kauli hii pia imetamkwa na Imam Shafi na Allayth na Ibni Hazm'.
Ama Imam Malik na Imam Abu Hanifa wanasema:
"Anachokula mtu katika mazao yake kabla ya mavuno atahesabiwa katika Niswaab"
Mwisho wa maneno ya Sayed Sabiq.
 
Toeni katika vizuri
Baadhi ya wenye kumiliki mitende walikuwa wakitoa Zakaah yao ya mazao katika tende au zabibu au mazao yasiyokuwa mazuri. Walikuwa wakichagua mazao yasiyokuwa mazuri na kuyatolea Zakaah, na yale mazuri walikuwa wakichukua wenyewe.
Allaah Akasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَنفِقُواْ مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الأَرْضِ وَلاَ تَيَمَّمُواْ الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلاَّ أَن تُغْمِضُواْ فِيهِ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ
"Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma na katika vile tulivyokutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kutoviangalia (Basi Mungu atapokea vibaya?). Basi jueni kwamba Allaah ni Mkwasi na asifiwaye".
Al Baqarah - 267
 
Anasema Imam As Shoukani:
"Hii ni dalili kuwa, haijuzu mtu kuwapa watu Zakaah katika yale mazao mabovu na yasiyokuwa mazuri."
Zakaah ya wanyama wa kufugwa
Wanyama wanaofugwa wanalazimika kutolewa Zakaah kwa masharti yafuatayo:
  1. Lazima watimie Niswabu
  2. Wakamilishe mwaka
  3. Wawe wanyama wa kufugwa.
Wanyama wasiokuwa wa kufugwa kama vile wa kupandwa au wanaotumiwa kwa kubeba mizigo au kwa kilimo n.k. Hawa hawatolewi Zakaah.
Wanyama wanaotolewa Zakaah ni Ngamia, Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo.
 
Zakaah ya ngamia
Ngamia hawatolewi Zakaah mpaka watimie watano. Wakitimia watano wa kufugwa hadi tisa na kutimiza mwaka chini ya milki ya mtu, basi atawatolea mbuzi mmoja.
Wakitimia ngamia 10 mpaka 14 atawatolea mbuzi wawili.
Na hivyo hivyo kila wakizidi ngamia watano ataongeza mbuzi mmoja.
Wakitimia ngamia 25 mpaka 35 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha mwaka na kuingia mwaka wa pili au mtoto wa ngamia dume aliyekamilisha mwaka wa 2 na anaingia wa 3.
Kuanzia ngamia 36 mpaka 45 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 2 na keshaingia wa 3.
Kuanzia ngamia 46 mpaka 60 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 3 na kuingia wa 4.
Kuanzia ngamia 61 mpaka 75 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 4 na kuingia mwaka wa 5.
Kuanzia ngamia 76 mpaka 90 atatoa watoto wa ngamia wawili jike waliokamilisha miaka miwili na kuingia wa tatu.
Kuanzia ngamia 91 mpaka 120 atatoa watoto wa ngamia wa kike wawili waliotimia miaka 3 na kuingia mwaka wa 4.
Wakizidi kuliko hapo, basi katika kila ngamia 40 atatoa mtoto wa ngamia wa kike aliyekamilisha miaka 2 na kuingia wa 3. Na katika kila ngamia 50 waliozidi kuliko hapo atatoa mtoto wa ngami wa kike aliyekamilisha miaka 3 na kuingia wa nne.
Anasema Sayed Sabeq katika Fiqhis Sunnah:
"Hawatolewi Zakaah ngamia dume ikiwa wapo wa kike, lakini anatolewa mtoto wa ngamia wa kiume aliyetimia miaka miwili na kuingia wa tatu ikiwa hajapatikana wa kike aliyekamilisha mwaka na kuingia wa pili.
 
Zakaah ya ng’ombe
Ng'ombe hawatolewi Zakaah mpaka watimie 30 wa kufugwa. Wanapotimia 30 mpaka 39 wa kufugwa na kukamilisha mwaka, atatolewa ndama aliyekamilisha mwaka mmoja.
Wakitimia ng'ombe 40 mpaka 59 atatolewa ndama asiyepungua umri wa miaka miwili.
Wakitimia ng'ombe 60 mpaka 79 atatolewa ndama wawili wa mwaka mmoja.
Kutoka hapo, kila wakizidi ng'ombe 30, ataongeza kutoa ndama wa mwaka mmoja.
Na kila wakizidi ng'ombe 40 atawatolea ndama wa miaka miwili.
Zakaah ya mbuzi
Mbuzi hawatolewi Zakaah mpaka watimie 40, na wakitimia arubaini mpaka 120 wa kufugwa na kukamilisha mwaka kwa mwenye kuwamiliki, atawatolea mtoto wa mbuzi wa mwaka mmoja.
Hatowatolea tena mpaka wafikie idadi yao mbuzi 121.
Wakiongezeka na kutimia 121 mpaka 200, atawatolea mtoto wa miaka miwili.
Kuanzia mbuzi 201 mpaka 300 atawatolea kondoo watatu.
Wakizidi kuliko mbuzi 300, basi atawatolea kondoo mmoja katika kila mbuzi mia waliozidi.
Inaruhusiwa pia kutoa mbuzi badala ya kondoo.
 
Wanyama wengine
Wanyama wengine wasiokuwa hawa kama vile farasi, nyumbu, punda na wengineo, hawatolewi Zakaah isipokuwa kama ni kwa ajili ya biashara.
Zakaah ya madini ya kale
Madini inayotolewa ardhini kama vile petroli, gesi, shaba, chuma n.k, hivi vyote havitolewi Zakaah, isipokuwa dhahabu na fedha tu na tushaelezea hapo mwanzo namna ya kutoa Zakaah yake. Ama vilivyobaki vinatolewa Zakaah ya biashara baada ya kuchimbuliwa au kutolewa na kuuzwa.
Zakaahtul Fitri
Imefaridhishwa katika mwezi wa Shaabani mwaka wa 2 baada ya Hijra (baada ya kuhamia Madina). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifaridhisha Zakaahtul Fitr ili iitakase saumu kutokana na dhambi ndogo ndogo zilizopatikana ndani ya mazungumzo na matendo. Na wakati huo huo Zakaah hiyo iwe msaada kwa mafakiri na wasiojiweza katika kuisherehekea Sikukuu.
Imepokelewa kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) kuwa amesema:
"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifaridhisha Zakaah ya Fitri kwa ajili ya kumtakasa aliyefunga kutokana na dhambi ndogo ndogo za mazungumzo na matendo, na ili wafaidike masikini . Atakayeitoa kabla ya Swalah (ya Idi) inakubaliwa kama Zakaah ya Fitri na atakayeitoa baada ya Swalah inakubaliwa kama Sadaka ya kawaida."
Abu Daud – Ibni Majah na Addaraqutni
 
Alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akitoa Zakaah ya Fitri siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhaan kabla ya Swalah ya Idi kuswaliwa.
Abu Daud na Ibni Majah na Al Hakim
 
Kila aliyefunga Mwezi wa Ramadhaani mwenye kumiliki chakula cha kumtosha kwa muda wa siku moja, inamwajibikia kutoa Zakaahtul Fitri, nayo ni pishi ya tende au pishi ya ngano au pishi ya shaiyri. Anatakiwa atowe kwa ajili yake na kwa ajili ya kila anayemtegemea kama vile wanawe, wakeze nk. na kuwapa masikini ili nao wapate kufurahi katika Siku ya Sikukuu.
Kwa vipimo vya kisasa, pishi moja ya mbao iliyokuwa ikitumika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni kiasi cha kilo 2.
Zakaah hii ni wajibu kwa kila Muislam mdogo na mkubwa, mwanamume au mwanamke.
Ibni Umar (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amefaridhisha kwa kila mtu kutoa Zakaahtul Fitri katika mwezi wa Ramadhaani, pishi ya tende (au) pishi ya shaiyri, ikiwa yeye ni mtumwa au mtu aliye huru, mwanamume au mwanamke, mdogo au mkubwa miongoni mwa Waislam".
Bukhari na Muslim
 
Hikma yake
Zakaahtul Fitri ilifaridhishwa katika mwezi wa Shaabani mwaka wa pili baada ya Hijra kwa ajili ya kumtwahirisha aliyefunga kutokana na makosa yoyote yale aliyotenda katika mwezi wa Ramadhaani pale alipokuwa amefunga, kama vile mazungumzo ya upuuzi au madhambi, na wakati huo huo Zakaah hiyo itawafaa masikini na wahitaji ili nao wapate kufurahi pamoja na Waislam wenzao siku ya Sikukuu.
Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amefaridhisha Zakaahtul Fitri kwa ajili ya kumtahirisha aliyefunga kutokana na maneno ya upuuzi au madhambi madogo madogo na ili masikini nao wapate chakula. Atakayeitoa (Zakaah hiyo) kabla ya Swalah (ya Idi) inakubaliwa Zakaah yake, ama atakayeitoa baada ya Swalah (ya Idi), itahesabiwa kama ni Sadaka ya kawaida tu".
Abu Daud na Ibni Majah na Addaraqutniy
Mwenye kuitowa
Anayeitoa Zakaah hiyo ni mtu aliyefunga. Anajitolea yeye mwenyewe, mkewe na watoto wake wanaomtegemea na anawatolea pia wote wale wanaomtegemea wakiwemo watumishi wake.
Kiasi chake
Iliyowajibishwa katika Zakaahtul Fitri ni pishi ya ngano au ya shaiyri au ya tende au zabibu au mchele au mahindi na vinginevyo vilivyo na mfano huo katika vyakula.
Imam Abu Hanifa peke yake amejuzisha kutoa pesa zenye thamani hiyo badala ya kutoa nafaka panapo udhuru
 
Wakati wa kuitowa
Maulamaa wengi wamekubalina kuwa Zakaahtul Fitri itolewe katika Ramadhaani ya mwisho, lakini wamekhitalifiana juu ya wakati maalum unaowajibika kuitoa.
Wapo waliosema kuwa wakati unaowajibika kuitoa ni pale jua la Ramadhaani ya mwisho linapozama, na wengine wakasema kuwa wakati wake ni kuanzia baada ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu.
Kutokana na hitilafu hii tunapata faida ya kuwajibika kumtolea Zakaah hiyo mtoto aliyezaliwa kabla ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu na baada ya jua kuzama, je mtoto huyo anatolewa Zakaah?
Kwa wale wenye kufuata rai kuwa wakati wa kuitoa Zakaah hiyo ni pale jua la siku ya Ramadhaani ya mwisho kuzama, mtoto huyo hatolewi Zakaah kwa sababu amezaliwa baada ya kumalizika wakati wa kuwajibika, na kwa wenye kufuata rai ya pili, kwa sababu amezaliwa kabla ya wakati unaomwajibika.
Kuitanguliza
Maulamaa wengi wanakubali kuwa Zakaahtul Fitri inaweza kutangulizwa na kutolewa kabla ya wakati wake kwa siku moja au mbili.
Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibni Umar (Radhiya Allaahu anhu) inasema:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametuamrisha kuitoa Zakaahtul Fitri kabla ya watu kutoka msikitini (katika Sala ya Idi)".
 
Anasema Nafe-a (Radhiya Allaahu anhu):
"Ibni Umar (Radhiya Allaahu anhu) alikuwa akiitoa kwa siku moja au siku mbili kabla ya Siku ya Sikukuu".
 
Ama zaidi ya hapo, maulamaa wamekhitalifiana.
Imam Abu Hanifa amesema:
"Inaweza kutolewa wakati wowote ule katika mwezi wa Ramadhaani".
Imam Shafi amesema:
"Inajuzu kuitoa (hata) katika siku za mwanzo za mwezi wa Ramadhaani".
Imam Malik amesema:
"Inajuzu kutanguliza kwa siku moja au mbili kabla ya Sikukuu".
Lakini maulamaa wote wamekubaliana kuwa haijuzu kuiahirisha na kuitowa baada ya Idi.
 
Sadaka
Muislam anaipa mali yake mtazamo wa aina nyingine kabisa tofauti na asiyekuwa Muislam, kwani dini ya Kiislam inampa kila mtu haki ya kutafuta mali na kufanya biashara ya halali na kuwa tajiri anayeweza kumiliki mali nyingi. Isipokuwa baada ya kuimiliki mali hiyo, analazimika kuwapa maskini Zakaah, ambayo ni haki yao maalum waliyopangiwa na Mola wao Subhanahu wa Ta’ala.
Wakati huo huo Muislam anatakiwa ajipatie thawabu nyingi zaidi na ajiepushe na shari nyingi pamoja na kuwasaidia ndugu na jamaa zake, na masikini waislamu wenzake wenye kuhitaji, kwa kutowa kiasi kingine katika mali zao kwa hiari yao wenyewe na kwa kiasi anachokitaka mwenyewe, na hii inaitwa 'Sadaka'.
Kinyume na njia inayotumika katika nchi za kikoministi za kuwanyang'anya matajiri mali zao kwa nguvu na kuwapa masikini, kitendo cha dhulma na cha ufisadi, kwa sababu binadamu kwa kawaida wanakhitalifiana katika ujuzi na katika jitihada zao, na kwa ajili hiyo lazima wahitalifiane katika ujira na mapato yao, kwani katika kuwafanya watu wote wawe sawa katika mapato, utakuwa unamweka katika daraja moja mvivu na mwenye kujitahidi, hodari na asiyekuwa hodari, mTa’alamu na asiyekuwa mTa’alamu.
Hii ikiwa mali hiyo wanayonyang'anywa matajiri wanapewa kweli masikini na wale wanaostahiki, na ikiwa watu wote watakuwa sawa kweli, lakini uhakika wa mambo umethithibitisha kuwa yanayotendeka ni kinyume kabisa na maneno yao, kwani wao huwanyang'anya mali matajiri na kuwapa viongozi wa vyama vyao pamoja na vibaraka wao.
Allaah Anasema:
مَّا أَفَاء اللَّهُ عَلَى رَسُولِهِ مِنْ أَهْلِ الْقُرَى فَلِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاء مِنكُمْ
"Mali aliyoleta Allaah kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Allaah na kwa ajili ya Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri aliyeharibikiwa, ili isiwe kinyang'anyiro baina ya matajiri wenu tu."
Al Hashar - 7
 
Allaah katika aya hii anatujulisha kuwa jamaa na mayatima na masikini na wasafiri walioharibikiwa wana haki zao katika mali zetu, na anawakataza matajiri wasiifanye mali ikawa kinyang'anyiro baina yao tu na kusahau haki za wengine.
Muislam pia anatakiwa aitumie mali yake katika kuijenga akhera yake na kujitayarishia Pepo yake.
Allaah Anasema:
وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّهُ الدَّارَ الاخِرَةَ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الاَرْضِ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ
"Na utafute kwa yale aliyokupa Allaah - makazi mazuri ya akhera, wala usisahau sehemu yako ya dunia, na ufanye wema kama Allaah alivyokufanyia, wala usitafute kufanya ufisadi katika nchi, bila shaka Allaah hawapendi mafisadi".
Al Qasas - 77
 
Haya ndiyo mafundisho ya Kiislam yaliyo kinyume kabisa na mafundisho ya mafisadi wanaojishughulisha na kukusanya mali tu na kurimbika, na wakati huo huo yanatufundisha kuwa Musilam hatakiwi abaki msikitini tu akifanya ibada bila kujishughulisha na elimu pamoja na kufanya biashara, na kuwaachia makafiri peke yao katika uwanja wa elimu na biashara na viwanda, na kwa ajili hiyo wanapata nguvu ya kututawala kiuchumi na kielimu, bali Muislam anatakiwa asiisahau pia sehemu yake ya dunia.
Allaah Anasema:
وَلا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ
"Wala usisahau sehemu yako ya dunia, na ufanye wema kama Allaah alivyokufanyia".
Al Qasas - 77
 
Dini ya Kiislam inatutaka tuwe msitari wa mbele katika kutoa, na Allaah amewaahidi kheri nyingi wale wanaotoa katika njia Yake.
Allaah ِAnasema:
مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّئَةُ حَبَّةٍ وَاللّهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاء وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ
"Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja iliyotoa mashuke saba; ikawa katika kila shuke pana punje mia. Na Allaah humzidishia amtakaye, (zaidi kuliko hivi), na Allaah ni Mwenye wasaa mkubwa (na) Mwenye Kujua".
Al Baqarah - 261
 
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Hakika ya sadaka inazima ghadhabu ya Mola  na inamuondolea maiti adhabu"
Attirmidhiy
Na akasema:
"Haipiti asubuhi wanayoiamkia watu, ila Malaika wawili wanateremka. Mmoja wao anasema: "Allaah muongezee mtoaji badala ya kile anachokitoa".Na mwengine anasema: "Allaah mharibie mali yake (usiite baraka) aliyeacha kutoa ".
Muslim
 
Aina za Sadaka
Sadaka haina maana ya kutoa pesa tu au kumsaidia mtu, bali Sadaka ziko aina nyingi sana.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Kila Muislam anatakiwa atoe Sadaka".
Wakasema:
"Ewe Mtume wa Allaah, asiyekuwa na mali (je)?"
Akasema:
"Afanye kazi kwa mikono yake, ajisaidie nafsi yake kisha atoe Sadaka".
Wakasema:
"Ikiwa hajapata?"
Akasema:
"Amsaidie mwenye shida".
Wakasema:
"Asipompata?"
Akasema:
"Afanye mema na aache shari, kwani akifanya hivyo anaandikiwa (thawabu ya) Sadaka".
Bukhari na wengineo
 
Na katika riwaya nyingnem amesema:
"Kila siku jua linapochomoza nafsi inaandikiwa juu ya kila inachotenda (katika thawabu ya) Sadaka. Katika hayo ni kuwapatanisha wawili wanaogombana (anaandikiwa mtu thawabu ya kutoa) Sadaka. Akimsaidia mtu kumnyanyua ili aweze kumpanda mnyama wake, anaandikiwa Sadaka, akimnyanyulia mzigo wake, Sadaka, kuondoa udhia barabarani, Sadaka, neno jema, Sadaka, na kila hatua anayokwenda msikitini Sadaka".
Ahmad na wengineo
 
Na akasema:
"Kati yenu kama yupo mwenye kuuogopa moto, basi atoe Sadaka walau kwa nusu ya tende, na asiyepata, basi kwa neno jema”.
Ahmad na Muslim
 
Na akasema:
"Siku ya Qiyaamah Allaah Atasema:
"Ewe mwanadamu, niliumwa (kwa nini) hukunitembelea?"
Atasema (mwanadamu):
"Ewe Mola , vipi nitakutembelea na wewe ni Mola wa Ulimwengu?"
Atasema:
"Hukujuwa kuwa mja wangu fulani alikuwa akiumwa na hukumtembelea? Ama ungelimtembelea, ungelinikuta kwake. Ewe mwanadamu nimekuomba chakula na wewe hukunilisha?"
Atasema:
"Ewe Mola wangu, vipi nitakulisha na wewe ni Mola wa ulimwengu wote?"
Atasema:
"Hukujuwa kuwa fulani alikuomba chakula na hukumpa. Huelewe kuwa ungelimpa chakula, ungelikikuta kwangu?
Ewe mwanadamu, nilikuomba maji hukunipa".
Atasema:
"Ewe Mola wangu, vipi nitakunywesha nawe ni Mola wa Ulimwengu wote?'
Atasema:
"Mtu fulani alikuomba maji, na wewe hukumpa. Ama ungelimpa ungeyakuta hayo kwangu".
Muslim
 
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema pia:
"Mtu hapandi kitu au halimi kitu kisha mwanadamu akala katika mazao hayo au mnyama au chochote ila ataandikiwa kwa ajili yake Sadaka".
Ahmad na Attirmidhiy
 
Na akasema:
"Kila wema ni Sadaka, na katika wema ni kumkabili mwenzio kwa uso wa bashasha…(uso mkunjufu)."
Ahmad na Attirmidhiy
 
Wenye kustahiki zaidi
Watu wako, mkeo na watoto wako pamoja na ndugu zako wa nasaba ndio wanaoistahiki zaidi sadaka yako.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mmoja wenu akiwa fakiri, basi ajitosheleze nafsi yake, kinachozidi awape watoto wake, kinachozidi, awape ndugu zake wa nasaba, na kikizidi basi atoe huku na kule".
Ahmad na Muslim
 
Hukumu ya Sadaka inahitilafiana na ya Zakaah, kwani mali ya Zakaah haijuzu kupewa asiyekuwa Muislam, lakini Sadaka anaweza kupewa asiyekuwa Muislam.
 
Allaah Anasema:
وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا
"Na huwalisha chakula maskini na mayatima na wafungwa na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda".
Ad Dahar - 8
 
Neno lililotumika kwa 'wafungwa', katika aya hii ni 'Asiyran', na maana yake ni mateka wa kivita ambaye bila shaka ni kafiri aliyetekwa baada ya kupigana vita dhidi ya Waislam, lakini juu ya hivyo Allaah anawasifia Waislam wanaowalisha chakula wafungwa hao.
 
Kuiharibu sadaka
Haijuzu kumsimbulia au kumdharau anayepokea Sadaka kwa sababu kilichomfanya akubali kuipokea sadaka hiyo ni umasikini wake, na mtu kumtakabaria masikini ni dhambi kubwa sana, na anapofanya hivyo thawabu zake zinapotea bure.
Allaah Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تُبْطِلُواْ صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالأذَى كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاء النَّاسِ وَلاَ يُؤْمِنُ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ
"Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamwamini Allaah wala siku ya mwisho".
Al Baqarah – 264
 
 
 
Kutowa katika mali ya haramu
Allaah haikubali sadaka ikiwa inatokana na mali ya haramu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Enyi watu! Allaah ni mzuri na hakubali isipokuwa kizuri tu".
 
Imesimuliwa kuwa siku moja mtu mmoja aliiba tufaa kisha akaliuza, na pesa alizopata akawagawia masikini.
Habari zilipomfikia kadhi wa mji huo, akamwita na kumuuliza:
"Kwa nini umeiba kisha ukazigawa sadaka pesa za mali ya wizi?"
Yule mtu akajibu:
"Kwa sababu Allaah Anasema:
مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا
"Afanyae kitendo kizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na afanyae kitendo kibaya hatalipwa ila sawa nacho tu".
Al An am - 160
Kwa hivyo, akaendekelea kusema mtu Yule aliyeiba tufaa: ‘Kutokana na aya hii, mimi nilipoiba tufaa nilifanya kitendo kibaya nikalipwa dhambi moja tu sawa na tufaa moja nililoiba, lakini nilipowagawia masikini nilifanya kitendo chema nikalipwa mara kumi, na thawabu 10 nilizozipata kwa kuligawa tufaa lile,ukitoa ile dhambi moja ya kuiba, nitabakiwa na thawabu tisa"
Kadhi akamwambia:
"Lakini umesahau jambo moja ewe ndugu Muislam, (Allaah ni mwema, na hakubali isipokuwa chema tu).”
 
Kuwasaidia wanyama
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema kuwaambia Masahaba (Radhiya Allaahu anhum):
"Mtu mmoja aliyekuwa akitembea, alishikwa na kiu, akaona kisima mbele yake, akateremka na kunywa maji ndani yake kisha akatoka. Alipokuwa akitoka alimuona mbwa akihema kwa kiu. Yule mtu akasema; "Bila shaka mbwa huyu ameshikwa na kiu kama nilivyoshikwa mimi. Akateremka (tena) kisimani, akajaza maji kiatu chake, kisha akamshika kichwa chake mbwa yule na kumnywesha.
Akashukuriwa na Allaah na kughufuriwa".
Masahaba (Radhiya Allaahu anhu) wakasema:
"Hata katika wanyama tunapata thawabu?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Katika kila chenye uhai mna thawabu".
Bukhari
Sadakatuh jaariyah
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mwanadamu anapokufa, amali zake zote zinakatika isipokuwa tatu. Sadakatun jaariah (Sadaka inayoendela), au elimu yenye kunufaisha watu, au mtoto mwema anayemuombea".
Ahmad na Muslim
 
 
Kushukuru
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Atakayekufanyieni wema mlipeni, na ikiwa hamna cha kumlipa, basi muombeeni dua mpaka muhisi kuwa mumemlipa".
Abu Daud na Annasai
 
Imesimuliwa na Imam Ahmad kutoka kwa Al Ash-ath bin Qays kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Hamshukuru Allaah yule aisyewashukuru watu."
Ahmad
 
Na akasema:
"Alieyetendewa jema, akasema kumwambia aliyemtendea: “Jazaaka Allaahu khayran', (MwenyeziMungu akujaze kheri), huyo amekwisha shukuru kama inavyotakikana".
 
Wanaostahiki Zakaah
Sadaka ya kawaida, anapewa mtu yeyote hata akiwa si Muislam, ama Zakaahtul Fitri wanapewa watu wa aina mbili tu, nao ni masikini na mafakiri Waislam.
Zakaahtul Maal (Zakaah ya mali), hii wanapewa aina 8 tu ya Waislamu waliowataja na Allaah katika kitabu chake kitukufu Aliposema:
إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ
"Sadaka hupewa (watu hawa):-
  • Mafakiri na
  • Masikini na
  • Wanaozitumikia na
  • Wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislam) na
  • Katika kuwapa uungwana watumwa na
  • Katika kuwasaidia Wenye deni na
  • Katika (kutengeneza) Mambo aliyoamrisha Allaah na
  • Katika (kupewa) Wasafiri (walioharibikiwa).
Ni faradhi inayotoka kwa Allaah, na Allaah ni Mjuzi (na) Mwenye hikima".
At Tawaba - 60.
 
Ayakayeichunguza aya hii ataona kuwa Allaah ametumia neno 'Lil' katika kuwataja watu aina nne wa mwanzo wanaostahiki kupewa Zakaah. Na hii inaitwa Laam ya tamliyk, na maana yake ni kuwa lazima kuwamilikisha watu wa aina nne wa mwanzo (yaani kuwapa mikononi mwao) Zakaah yao.
Allaah ِAnasema:
إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ
Ama katika aina nne waliobaki, Allaah ametumia neno 'Fiy'. Na kwa kutumia neno hilo Allaah hatulazimishi, kuwamilikisha kwa kuwapa Zakaah yao mikononi mwao.
Allaah anasema:
وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ
Kwa hivyo katika aina nne za mwisho, kwa mfano kama unataka kumsaidia mwenye deni, hulazimiki kumpa pesa hizo mkononi mwake, bali unaweza kwenda kumlipia deni hilo moja kwa moja bila ya kumkabidhi mdaiwa huyo pesa hizo mkononi mwake. Hata hivyo, ukitaka unaweza pia kumkabidhi mweyewe mkononi mwake.
Ukitaka kuzitumia pesa za Zakaah katika njia ya Allaah, unaweza kununua kwa mfano silaha na kuwakabidhi wapiganaji 'Mujahidiin' au unaweza kuzitumia katika njia ya Allaah bila ya kumkabidhi mtu pesa hizo mkononi mwake, wakati huo huo unaweza ukitaka kuwakabidhi wanaohusika au wajuzi ili ipate kutumika kwa usahihi zaidi.
 
Mafakiri masikini
Juu ya kuwa watu wamehitalifiana juu ya nani masikini na nani fakiri, lakini kwa ujumla hawa ni watu ambao wanachokipata hakiwatoshi katika matumizi yao ya kila siku.
Mtu anaweza kuwa masikini hata kama anapata mshahara mkubwa lakini wakati huo huo ana watoto wengi au wazee na ndugu wanaomtegemea anaowajibika kuwatizama, au ana madeni kiasi ambapo juu ya kuwa anapata mshahara mkubwa, pesa hizo hazimtoshi kuwalisha watu wake hao.
Kwa ajili hiyo juu ya tofauti iliyopo baina ya masikini na fakiri katika sharhi yake, lakini katika kuhitajia kwao msaada, wote wawili wapo katika hali moja.
Zipo hadithi zinazotujulisha kuwa wapo baadhi ya masikini wenye kustahi kuombaomba juu ya shida kubwa walokuwa nazo. Waislam wanatakiwa wawachunguze watu wa aina hii na kuwasaidia na wasiwaache mpaka hali zao zikawa mbaya.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anasema:
"Masikini si yule anayeomba akapewa tende moja au mbili akaondoka, au tonge moja au mbili, lakini masikini wa kweli ni yule anayejizuwia. Someni mkitaka (kauli ya Mwenyezi Mung isemayo):
التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُم بِسِيمَاهُمْ لاَ يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا
"Utawafahamu kwa alama zao hawawaombi watu wakafanya ung'ang'anizi".
 
Anayepewa Zakaah ni Masikini au Fakiri Muislam tu, ama Masikini au Fakiri asiyekuwa Muislam hapewi katika mali ya Zakaah, na kama Fakiri asiyekuwa Muislam atahitajia msaada, basi atapewa katika mali ya Sadaka na si ya Zakaah.
 
Wenye kuzitumikia
Wanaozitumikia Zakaah ni wale waliopewa jukumu la kuipokea, kuikusanya kutoka kwa matajiri na wenye kazi ya kuihifadhi, waandishi, na wenye kuigawa, wakiwemo wachungaji wa wanyama wa Zakaah.
Ili waweze kupewa katika Mali ya Zakaah, watu hao lazima wawe Waislam, na wasiwe katika wale walioharamishwa kupokea Zakaah katika watu wa Ahlul Bayt ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika Banu Abdul Muttalib ambao tutawataja baadaye.
Katika wanaoitumikia Zakaah, hata akiwa mtu tajiri basi anastahiki kupewa katika mali hiyo, na ikiwa mtu wa aina hiyo amepewa na wakubwa wanaohusika na akawa hana haja nayo mali hiyo, basi aichukuwe na kuwagawia anaowataka au kumnunulia zawadi anayemtaka.
Imepokelewa kuwa Umar bin Khattab (Radhiya Allaahu anhu) alipokuwa akifanya kazi ya kukusanya mali ya Zakaah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimpa katika mali hiyo.
Umar (Radhiya Allaahu anhu) akasema:
"Mimi najitolea tu na sina haja ya kulipwa, mpe mwenye kuzihitajia zaidi kuliko mimi".
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Alichokupa Allaah katika mali hii bila ya wewe mwenyewe kuiomba, uichukuwe na uitumie au itolee Sadaka."
Bukhari na Annasai
 
Wenye kutiwa nguvu
Hawa ni watu wanaopewa katika mali ya Zakaah kwa ajili ya kulainishwa nyoyo zao na kutiwa nguvu kutokana na udhaifu wa nyoyo hizo, na wengine hupewa kwa ajili ya kuwaepusha Waislam na shari zao, au kuwavutia katika kuupenda Uislam na kuupa nguvu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa wakubwa wa makabila ya kiarabu na hasa makabila ya kibedui kwa ajili ya kuwapendekeza katika Uislam.
Imepokelewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimpa mtu mmoja aitwae Safwan bin Umayyah ngamia wengi sana katika ngamia wa ngawira waliopatikana katika vita vya Hunain, na Safwan huyu alikuwa mkubwa wa kabila lake.
Safwan alikuwa wakati huo bado hajasilimu, na alipopewa mali hiyo, akarudi kwa watu wake na kuwaambia:
"Enyi watu wangu, ingieni katika dini ya Kiislam, kwani Muhammad anatoa utoaji wa mtu asiyeogopa ufakiri".
(Mwenye kuchunguza, ataona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwatendea makabila ya Kibedui tofauti na anavyowatendea watu wa mijini. Alikuwa akiwachukulia kwa akili zao. Na hii ni kwa sababu Mabedui ni watu wagumu sana kufahamu. Hata katika kuuliza masuali, Mabedui walikuwa wakimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) masuali na kujibiwa, wakati masuali hayo hayo wangeuliza Masahaba wanaokaa mjini (Radhiya Allaahu anhum), basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) angekasirika nayo masuali hayo).
 
Wakati wa ukhalifa wake Abubakar (Radhiya Allaahu anhu) alikuwa akiendelea kuwapa watu wa aina hii, lakini Umar bin Khattab (Radhiya Allaahu anhu) siku moja alikataa kutoa, akawaambia:
"Hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akikupeni kwa ajili ya kuzizowesha nyoyo zenu na kuzilainisha, lakini sasa Allaah amekwishautukuza Uislam na hatuna haja nanyi tena, mkitaka ingieni katika Uislam, na kama hamtaki basi baina yetu na baina yenu ni panga. Allaah amesema:
وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاء فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاء فَلْيَكْفُرْ
"Na sema; 'Huu ni ukweli ulotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka na aamini na anayetaka na akufuru.”
Al Kahf - 29
 
Anasema Sayed Sabeq katika Fiqhis Sunnah:
"Abubakar (Radhiya Allaahu anhu) alikubaliana na Umar (Radhiya Allaahu anhu) katika uamuzi wake huo, na hapana hata Sahaba mmoja (Radhiya Allaahu anhum) aliyepinga. Na hii ni katika Ijtihadi zake Umar (Radhiya Allaahu anhu), na hata makhalifa waliokuja baada yake, Uthmaan na Aliy (Radhiya Allaahu anhum) hawakuwapa tena watu wa aina hii katika mali ya Zakaah.
Hata hivyo," anaendela kusema Sh. Sabeq, "hii haimaanishi kuwa watu wa aina hii wasipewe, na Imam yeyote yule atakayetawala na akaona kuwa ipo haja ya kuwapa watu wa aina hii, basi atawapa kwa sababu dalili ipo katika Qurani na Sunnah.”
 
Katika kugomboa
Uislam umeijaalia ibada hii ya kuwagomboa mateka na watumwa kuwa ni kitendo kinachompatia mtu thawabu nyingi sana na kumuingiza katika Pepo za Allaah Subhanahu wa Ta’ala.
Kutoka kwa Al Barra-a (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:
"Nijulishe juu ya amali (njema) itakayonikurubisha na Pepo na kunibaidisha na Moto".
Akasema:
"Waachie huru watu na wagomboe watumwa".
Akauliza (tena):
"Ewe Mtume wa Allaah, si yote hayo yanabeba maana moja tu?"
Akasema:
"La, (sivyo), 'kuwaachia huru' ni kujihusisha peke yako katika kuwaacha huru, na 'kuwagomboa' ni kusaidia katika kulipa thamani ya kuwagomboa".
Ahmed na Addaraqutniy.
 
Wakati ule ilikuwa mtumwa anaweza kuandikiana na kukubaliana kuwa atakapoweza kulipa malipo fulani katika muda fulani, ataachwa huru. Kwa hivyo Waislam walitakiwa wawasaidie watu wa aina hiyo kwa kuwalipia kiasi hicho ili waweze kujigomboa.
 
Kumsaidia mwenye deni
Hawa ni wale wenye madeni makubwa wakashindwa kuyalipa kutokana na kula hasara katika biashara zao nk. Sharti madeni hayo yawe katika mambo ya halali au yatokane na maasi aliyotubu nayo mtu huyo.
 
Imepokelewa kutoka kwa Maimam Ahmad na Abu Daud na Ibni Majah na Attirmidhiy, kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:
"Mas-ala (ya kuwasaidia wenye madeni), hayawi halali isipokuwa katika mambo matatu; aliye fakiri sana, au mwenye deni zito sana, au mwenye kudaiwa damu (ya diya - fidiya).”
(Huyu ni mtu aliyejikuta amebebeshwa deni la diya kutokana na ndugu yake au jamaa yake aliyeuwa kwa bahati mbaya. Ikiwa hajalipa diya hiyo, basi ndugu yake huyo au jamaa yake atauliwa kwa ajili ya kulipa kisasi)
 
Katika kutengeneza
(Fiy sabiyli Allaah), ni njia yoyote ile inayomfikisha mtu katika kumpatia radhi za Allaah Subhanahu wa Ta’ala, juu ya kuwa maulamaa wengi wanasema kuwa haya ni mambo yanayohusiana na vita vya Jihadi tu pamoja na watu wanaopigana vita hivyo.
Hawa wana sehemu yao katika mali ya Zakaah wanayopewa hata kama askari mpiganaji Jihadi ni tajiri anayejiweza.
Anasema Sayed Sabeq, katika Fiqhis Sunnah:
"Maulamaa wengine wamesema kuwa inajuzu kuzitumia pesa hizo katika kutengeneza njia inayowapeleka watu Makka kwa ajili ya Hija na katika kuwanunulia maji ya kunywa na chakula ikiwa hapana mali nyingine inayoweza kutumiwa katika kazi hiyo. Inajuzu pia kuzitumia katika kuwasomesha na kuwatayarisha walinganiaji wa dini kwa ajili ya kuwapeleka katika nchi zisizokuwa za Kiislam kwa ajili ya kufanya da-awa nk."
 
Vitu vinavyonunuliwa kutokana na pesa za Zakaah kwa ajili ya vita, kama vile farasi, panga, nk. lazima virudishwe katika nyumba ya hazina ya Waislam (Baytul maal) baada ya kumalizika kwa vita.
Katika kupewa wasafiri
Msafiri aliyeishiwa na pesa akawa hana njia nyingine ya kupata pesa za matumizi, huyu anapewa katika mali ya Zakaah, sharti safari yake hiyo iwe katika mambo ya twa-a na si katika kumuasi Mola wake, hata akiwa msafiri huyo huko kwao alikotoka ni mtu tajiri mwenye mali nyingi.
 
Walioharimishwa kupewa
  1. Kafiri
Katika hadithi iliyotangulia, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Zichukuliwe kutoka kwa matajiri Wao na kurejeshewa masikini Wao"
Na maana yake ni kuwa:-
Zichukuliwe kutoka kwa matajiri wa Kiislam na kupewa masikini wa Kiislam.
 
  1. Bani Hashim
Nao ni watoto wa Aliy na Aqiyl na Jaafar na Al ‘Abbaas na Al Harith (RadhiyAllaahu anhum).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Sadaka haijuzu kupewa kwa watu wa Muhammad".
Muslim
 
Maulamaa wamekhatalifiana juu ya ukoo wa Bani Al Muttalib, iwapo nao pia hawapewi katika mali ya Zakaah au wanapewa.
Imam Shafi amesema kuwa hawa nao wasipewe katika mali ya Zakaah, na hii inatokana na hadithi iliyotolewa na Imam Shafi na Imam Ahmad na Imam Bukhari kutoka kwa Jubair bin Mut-am aliposema:
"Siku ya Khaibar (baada ya kumalizika vita hivyo), Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliikusanya upande mmoja sehemu ya ngawira ya watu wa ukoo wake katika Bani Hashim na ya Bani Al Muttalib na akawaacha (watu wa kabila lake) katika Bani Nofel na Bani Abdu Shams. Tukamwendea mimi na Uthman bin Affan na kumuuliza:
"Ewe Mtume wa Allaah hawa ni Bani Hashim na sisi hatukanushi fadhila zao kutokana daraja yako mbele ya Allaah, lakini vipi hawa ndugu zetu katika Bani Al Muttalib, umewaingiza wao ukatuacha sisi wakati nasaba yao na yetu juu yako ni sawa sawa?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Sisi na Bani Muttalib hatujafarikiana katika ujahilia wala katika Uislam, bali sisi na wao ni kitu kimoja". Akaviingiza vidole vyake vya mkono wa kulia ndani ya vidole vya mkono wa kushoto na kuvichanganya."
 
Kutokana na ushahidi huu, baadhi ya maulamaa wakasema;
'Bani Muttalib nao pia wanaingia katika kuharamishiwa kupewa katika Mali ya Zakaah".
 
  1. Baba na watoto
Haijuzu mtu kumpa katika mali ya Zakaah baba yake, mama yake, watoto wake na babu zake, na hii ni kwa sababu mtoaji Zakaah anawajibika kuwatizama watu hao na kuwapa katika mali yake, na kwa ajili hiyo, watu hao wanalazimika kuwa matajiri kutokana na utajiri wake.
 
  1. Mke
Haijuzu mtu kumpa mkewe katika mali ya Zakaah, na jambo hili linakubaliwa na maulamaa wote na hii ni kwa sababu mtu anawajibika kumtizama na kumpa mkewe katika mali yake kama anavyowajibika kuwapa wazee wake wawili akiwa anao uwezo huo.
Anasema Ibnil Mundhir:
"Isipokuwa kama mke ana deni, basi hupewa Zakaah katika ile sehemu ya kuwasaidia wenye madeni kwa ajili ya kulipa deni hilo".
Ama ikiwa mke ni tajiri mwenye uwezo wa kutoa Zakaah, basi yeye anarushusiwa kumpa mumewe katika mali ya Zakaah kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:
"Amesema kweli Ibni Masaud, mumeo na mwanao wanastahiki zaidi kuwapa Sadaka".
Bukhari
 
  1. Haijuzu kuitumia mali ya Zakaah kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah kama vile kujenga misikiti, kununua misahafu, kununua vifaa vya kusaidia kuosha maiti nk. Na hii ni kwa sababu Allaah kwa hekima yake keshazitaja na kuzisherehesha njia za kutoka Zakaah katika aya iliyotangulia ya Surat At Tawba -60, na akaikamilisha aya hiyo kwa kusema;
 
"Na Allaah ni Mjuzi (na) Mwenye hikima".
 
Watu wema
Zakaah anapewa Muislam anayeistahiki akiwa Muislam huyo ni mtu mwema au mtu asi, isipokuwa mtu asi hapewi kaika mali ya Zakaah ikiwa itajulikana kwa uhakika kuwa atakuja kuitumia mali hiyo katika kuuendeleza uasi wake.
Ikijulikana kwa uhakika kuwa ataitumia mali hiyo katika kumuasi Allaah, basi mtu huyo atanyimwa, ama ikiwa hayajulikani hayo, au ikijulikana kuwa ataitumia mali hiyo katika shida zake, basi hapo atapewa.
Hata hivyo ni bora kwa mtoaji Zakaah aihusishe mali hiyo kwa kuwapa watu wema au maulamaa wanaostahiki wanaoifayia kazi elimu yao, kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Walisheni chakula chenu wachaMungu na mnaowajuwa katika walioamini (kweli)".
Ahmad
 
Anasema Ibni Taymiya:
"Asiyeswali hapewi katika mali ya Zakaah mpaka pale atakapotubu akawa anaswali."
 
Anasema Sayed Sabeq:
"Katika kundi hilo wanaingia pia wale wanaomuasi Allaah bila kujali wala kuona haya, na kuendelea kuzama katika maasi huku nyoyo zao zikiwa zishafisidika na dhamiri zao zimekwisha haribika".
 
Hawa hawapewi katika mali ya Zakaah isipokuwa kama Zakaah hiyo itawasaidia katika kuwaongoza mwongozo ulio sahihi au itawasaidia katika kutoka hali yao hiyo.
 
Kuinunua Zakaah
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amekataza mtu kuinunua Zakaah yake.
Kutoka kwa AbdiAllaahi bin Umar (Radhiya Allaahu anhu), amesema:
"Umar (Radhiya Allaahu anhu) alimtoa farasi wake Sadaka fiy sabiyli Allaah, kisha akamkuta farasi huyo anauzwa na akataka kumnunua. Akamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya jambo hilo, akamwambia:
"Usimnunue na wala usirudie (kutaka kuimiliki tena) Sadaka yako"
Bukhari, Muslim na wengineo
 
Baadhi ya maulamaa wakasema kuwa kukataza huko ni kwa ajili ya kujiepusha tu, na si kwa ajili ya kuharamisha, wakiegemea hadithi nyingine inayoruhusu mtu kuipokea sadaka yake kama zawadi itokayo kwa masikini aliyempa.
 
Kuisafirisha Zakaah
Mulamaa wengi wamekubali kuwa mali ya Zakaah (Zakaahtul Maal - si Zakaahtul Fitr) inaweza kusafirishwa na kutolewa katika nchi nyingine kwa wanaoistahiki zaidi ikiwa watu wa mji anaoishi mtoaji hawaihitajii zaidi mali hiyo. Ama ikiwa katika nchi hiyo wapo wanaoihitajia, basi zipo hadithi zinazotujulisha kuwa Zakaah ya kila nchi wanapewa masikini wake.
Katika madhehebu ya Imam Abu Hanifa, wao wanasema:
"Ni Makruh kuisafirisha mali ya Zakaah isipokuwa ikiwa kwa ajili ya kumsaidia ndugu wa nasaba mwenye kuihitajia, na hii inatokana na umuhimu wa kuunganisha undugu huo, au pia kwa ajili ya watu wenye shida sana katika watu wa nchi yake, au kwa ajili ya kuiondoa kutoka nchi ya kikafiri na kuipeleka katika nchi ya kiislam."
 
Madhehebu ya Imam Shafi yanasema:
"Haijuzu kuisafirisha mali ya Zakaah na inawajibika kutolewa katika nchi iliyochumwa mali hiyo isipokuwa pakikosekana wenye kuihitajia Zakaah hiyo katika nchi hiyo".
 
Muadh bin Jabal (Radhiya Allaahu anhu) alipewa ugavana wa nchi ya Yemen na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na alipotawala Umar bin Khattab (Radhiya Allaahu anhu) alimuacha Muadh aendelea kuwa gavana wa nchi hiyo. Lakini Muadh (Radhiya Allaahu anhu) alipompelekea Umar bin Khattab (Radhiya Allaahu anhu) theluthi ya mali ya Zakaah, Umar (Radhiya Allaahu anhu) alikataa kuzipokea akamwambia:
"Sikukupeleka uwe mchotaji (wa mali) wala mpokeaji wa kodi, bali nimekupeleka kwa ajili ya kuchukua mali (ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kuzirudisha kwa masikini wao".
Muadh (Radhiya Allaahu anhu) akasema:
"Nisingekuletea ila kwa sababu sikumpata (masikini) anayezistahiki kuzichukua".
 
Kuidhihirisha Zakaah
Inazuju kwa mtoaji kuidhihirisha au kuitoa kwa siri Zakaah yake, yote sawa ikiwa anachokitowa ni Sadaka ya kawaida au Zakaah ya mali, ingawaje kuitoa kwa siri ni bora zaidi.
Allaah Anasema:
إِن تُبْدُواْ الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاء فَهُوَ خَيْرٌ لُّكُمْ
"Kama mkitoa sadaka kwa dhahiri ni vizuri, na kama mkitoa kwa siri na kuwapa mafakiri, basi huo ni ubora zaidi kwenu".
Al Baqarah - 271
 
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"(Watu aina) Saba Allaah atawaweka chini ya kivuli chake siku ambayo hapatokuwa na kivuli isipokuwa kivuli chake:- Imamu muadilifu, na kijana aliyekulia katika kumuabudu Allaah, na mtu ambaye moyo wake umeshughulika na misikiti, na watu wawili waliopendana kwa ajili ya Allaah, walikutana kwa ajili Yake na wakafarikiana kwa ajili Yake, na mtu aliyetoa Sadaka kwa siri akaificha hata (mkono wake wa) kushoto usijuwe nini kimetolewa na wa kulia, na mtu aliyemtaja Allaah akiwa peke yake mpaka akatoka machozi, na mtu aliyeitwa na mwanamke aliye na cheo (kikubwa) na mali (nyingi) akimtaka kwa ajili ya nafsi yake (akimtaka azini naye), akasema (mtu huyo); "Mimi namuogopa Allaah".
Bukhari - Muslim na Imam Ahmad

1 comment:

kassimbayuu1@gmail.com said...

Mashaallah. Upo vyema kuliko