Nani Aliyepanga Surah, Aayah Na Nani Aliyetoa Majina ya Surah?
SWALI:
Swali La Kwanza:
Asslaam aleykum,
Ni
nani aliezipanga sura za Qur-an katika mpango tunaouona sasa. Ni kwa
nini na kuna hikma gani. Ikiwa Suratul Baqra imeteremshwa Madina kwa
nini iwe ya pili katika msahafu na isiwe ya 86, kwani za mwanzo zilianza
kuteremshwa Makkah?
Swali La Pili:
Shekh,
naomba tafadhali maelezo nani aliyetoa majina ya sura za qurani? Vipi
zimepangwa aya ikiwa Qurani imeteremshwa kidogo kidogo kuanzia iqra hadi
aya za mwisho kabla kufa Mtume maana naona imeanza Alhamdu na
kumalizikia Qul-audhu.
JIBU:
Sifa
zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote,
Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani
zetu za dhati kwa swali lako kuhusu upangaji wa surah za Qur-aan. Ni
jambo linaloeleweka kuwa hakuna jambo lolote la Uislamu isipokuwa lina
hekima kubwa ni sawa tunazijua hizo hekima au la.
Mpangilio
wa Qur-aan na majina yake yamepangwa na Yeye Mwenyewe Allaah Mwenye
hekima na busara kubwa. Tufahamu kuwa Qur-aan yote ilikuwa imehifadhiwa
na Allaah Aliyetukuka katika sehemu inayoitwa Lawhul Mahfuudh na kisha
kuteremshwa yote usiku wa al-Qadr katika mwezi wa Ramadhaan hadi wingu
wa duniani. Kutoka hapo Jibriyl ('Alayhis Salaam) akawa ni mwenye
kupatiwa amri na Aliyetukuka kumteremshia Mtume wa Allaah (Swalla
Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) kidogo kidogo kwa miaka 23
kulingana na mahitajio.
Kila
ilipokuwa inateremshwa Surah au baadhi ya Aayah Jibriyl ('Alayhis
Salaam) kwa maagizo kutoka kwa Allaah Aliyetukuka alikuwa akimuamuru
Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) aiweke mahali kadhaa
na jina la Surah liwe kadhaa. Baada ya kuhama Madiynah, Jibriyl alikuwa
akija kila Ramadhaan kumsikiliza Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi
wa sallam) kisomo cha Qur-aan. Na ule mwaka aliokufa, Jibriyl alikuja
mara mbili na mara ya mwisho Zayd bin Thaabit (Radhiya Allaahu 'anhu)
alikuwepo.
Hivyo, alivyoaga dunia (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) waliandika Qur-aan kama
walivyofundishwa na kuagiziwa na Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa
aalihi wa sallam). Hata wale waandishi wa Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi
wa aalihi wa sallam) walikuwa wakipatiwa maagizo hayo.
Ama kuhusu Suratul Baqarah kuwa ni ya 86 si kweli na huenda kuwa ndugu yetu akawa amekosea katika ubinaadamu wake. Na hilo
si la ajabu. Hakika ni kuwa Suratul Baqarah ni Surah ya 87 kuteremshwa
na ya kwanza kuteremka Madiynah. Surah ya mwisho kuteremshwa Makkah
ilikuwa ni ya 86 nayo ni Suratul Mutwaffifiyn (83).
Na Allaah Anajua zaidi
No comments:
Post a Comment