Saturday, 11 April 2015

Pesa Anazopewa Za Ukimbizi Zinafaa Ajenge Msikiti Au Atoe Sadaka Kwa Waislamu?


SWALI:
 
Asalam aleykum warahmatulahi, mimi nauliza je inaswihi mtu kudanganya yeye ni mkimbizi kutoka nchi zenye vita hali ya kuwa si kweli na akapewa mahitaji yote kama kweli yeye ni mkimbizi nachotaka kujua ni kwamba akipewa hizo hela kwa matumizi yake ya chakula na mahitaji mengine itaswihi au itakuwa hela ni ya haramu kwa sababu amedanganya pia akitoa kiasi hicho cha fedha akajengea msikiti au akatoa sadaka kwa Waislamu wengine itaswihi?
 

JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu udanganyifu wa ukimbizi. Hakika hili leo limekuwa ni tatizo kubwa sana. Mara nyingi huwa tunafanya jambo bila kutizama hatima yake. Wapo wengi waliodanganya kuhusu suala hilo mpaka wakawa ni wenye kubadilisha majina ili wapate wasiyokuwa na haki nayo kuyapata.
 
Allaah Aliyetukuka Anasema:
Enyi Mlioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli” (9: 119).
Hapa tunaamriwa tuwe na wakweli kumaanisha kuwa nasi pia tunafaa tujipambe na tabia ya ukweli katika kila hali. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuhimiza kusema ukweli na Muumini hasemi uongo. Anatueleza (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa Muumini anaweza kuwa muoga, bakhili lakini hawezi kuwa muongo hasa kwa kupata kisichokuwa haki yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anayetudanganya si katika sisi (Waislamu)” (Muslim).
 
Hivyo, huko ni kama kuiba kutoka kwa serikali. Inatakiwa ufanye juhudi upate kazi ya halali ili uweze kujikimu kimaisha na kujenga Msikiti na kutoa sadaka kwa pesa zako na sio pesa za wizi ambazo unazipata kwa ulaghai na hila.
Misikiti haijengwi ila na pesa za halali hata Waarabu wakati wa ujahiliya kabla ya kutumilizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walijua hilo. Walipotaka kuijenga Ka‘bah baada kuvunjika kwa mvua kubwa walitoa masharti kuwa isiingie pesa ya haramu katika hilo.
 
Na Allaah Anajua zaidi

No comments: